Notification texts go here Contact Us Buy Now!

HADITHI- BINTI MFALME LEGITA SEHEMU YA 01

HADITHI- BINTI MFALME (Legita)
SEHEMU - 1

MTUNZI- LISSA WA MARIAM
Ilikuwa ni jioni Legita alikuwa chumbani kwake akijiandaa kwenda matembezi, baada ya kuhakikisha amependeza, alitoka huku kijakazi wake akiwa anamfuata nyuma, alipofika kwenye ukumbuki mkubwa, alikutana na mama yake aitwae malkia Gwanta, alimpita pasipo kutoa salamu yoyote

"Legita?" malkia aliita

Hapo hapo Legita akasimama pasipo kugeuka na kumuangalia, malkia Gwanta aliamua kumsogelea hadi mbele yake

"Ina maana hujaniona?" Malkia aliuliza

"Kwani vipi? Nikuone au nisikuone itanisaidia nini mimi?" Legita alijibu kwa jeuli

"Unapaswa unisalimie"

"Alafu nikishakusalimia ndo inakuwaje? sioni umuhimu wa kuanza kuhangaikia salam yangu, mbona kuna mambo mengi ya kufanya"

"Haya hakuna shida, naomba kujua unaenda wapi?"
"Naenda kutembea, haya kuna lingine?"

"Huwezi kutoka jioni hii" malkia Gwanta alisema

"Kwani wewe unanitafuta nini lakini? Unanizuia kutoka wewe kama nani labda?"

"Mimi kama malkia Gwanta wa himaya hii ya Kwembeo, pia mimi kama mama yako, japo unaniona mdogo ila nimetangulia kuzaliwa" Gwanta alijibu kwa kujiamini

"Hahahaha unanichekesha sana, sasa tutaona kama sitoki, hakuna mpuuzi yoyote anayeweza kunizuia kutoka nje ya hapa, isipokuwa mfalme tu, tofauti na huyo nitaamua vyovyote vile nitakavyo, wewe sio mama yangu na wala huwezi kunizaa mimi hata ardhi ipinduke" Legita nae alijibu kwa kujiamini

Kweli Gwanta hakuwa mama yake wa kumzaa, baada ya mama Legita kufariki, mfalme aliamua kutafuta mwanamke mwingine na kumuoa, alikuwa ni binti mdogo kwake, kama angewahi kuzaa basi Gwanta angekuwa mtoto wa kwanza na Legita angekuwa wapili, tangu hapo Legita hakumpenda mama yake wa kambo, alimuona ni mwanamke asiyestahili kuwa na baba yake, ila hakuwa na jinsi, aliishi kwa kutomuheshim siku zote, malkia nae alikuwa jeuli haswa hakutaka kushindwa hata kidogo, aliweza kutumia cheo chake vilivyo

"Wewe Jema rudi ndani haraka sana, mimi ndio malkia unapaswa utii amri yangu" malkia alimuamrisha kijakazi wa Legita kwa hasira,

Jema alikubali na kutaka kuondoka, lakini Legita alimsimamisha 

"Unakwenda wapi? Na uliona wapi tamaduni kama hii? Umechoka kazi hapa unataka nikutimue? Tambua kuwa sitokutimua tu bali nitakupatia na adhabu pia"

"Samahani ewe mtoto wa mfalme, napaswa kumsikiliza malkia kwanza" alijibu Jema huku akibinya binya mikono yake na kuinamisha kichwa chini kwa hofu

"Vizuri sana, ondoka mbele yangu, kuanzia sasa sitaki unitumikie tena, nitatafuta kijakazi mwingine, pia tambua sijakuacha hivi hivi" Legita aliongea kwa hasira na kuingia ndani kwake

"Safi sana binti, ungekaidi amri yangu hakika ungejutia maisha yako yote, kwasasa hutakiwi kumsikiliza Legita kitu chochote, umenielewa?"

"Ndio malkia wangu"
"Haya mlikuwa mnaenda wapi jioni hii niambie"
"Aliniambia nimpeleke mtoni mara moja"

Malkia alipoambiwa hivyo alitoka haraka nje akiwa na kijakazi wake aitwae Zamo,

********
Anaonekana mwanaume mmoja akiwa pembezoni mwa mto akirusha rusha mawe madogo madogo ndani ya mto ule, umri wake ulikuwa miaka isiyopungua 32, mara ghafla alihisi mtu akimziba macho

"Aah nishakuona Legita embu niache bana" alisema huku akitabasam,

Yule mtu aliyemziba macho alimuachia na kwenda mbele yake, hapo yule mwanaume aitwae Chansa alishtuka baada ya kumuona malkia

"Naona ulikuwa na ahadi ya kukutana na Legita hapa, kwa bahati mbaya hawezi kutoka na kuja huku leo, nimemzuia" 

alisema malkia Gwanta kisha akamgeukia kijakazi wake na kumpa ishara awapishe, Zamo akasogea mbali

"Kwanini umekuja huku?" Chansa akauliza

"Kwasababu nataka nikae na wewe, au wewe hupendi kuwa karibu na mimi?"

"Tangu ulipoamua kuolewa na mfalme na kuniacha mimi, nilijikuta sitamani tena kuwa karibu na wewe, hivi huwezi kuniacha kwa amani ili nikabaki na Legita?"

"Kwahiyo sasa hivi unampenda sana Legita kuliko mimi? Umesahau ulivyokuwa ukiniambia unanipenda kipindi cha nyuma? Ina maana maneno yote yale ulikuwa ukinidanganya?" Malkia Gwanta aliongea kwa hasira

"Kila kitu nilichokwambia kwa wakati ule kilitoka moyoni, nilikupenda sana Gwanta, lakini unasahau kabisa kama ni wewe mwenyewe uliamua kuniacha mimi na kwenda kuolewa na mfalme? Kosa la nani? Ulitaka mimi nisiwe na mtu mwingine tena ili niteseke na mapenzi yako? Hilo lisingewezekana"

"Sasa Chansa ulitaka mimi nifanyaje? Isingewezekana kukaidi amri ya mfalme, pia kama angejua namkataa sababu yako ni lazima mmoja wetu angepata matatizo au hata wote"

"Kwahiyo sasa hivi unavyo nifuata huogopi matatizo au? Gwanta naomba usiniponze tafadhali, hivi una lengo gani na mimi? unataka niangamie?"

"Hapana sipo tayari kuona unapatwa tatizo, bado nakupenda Chansa, ninachoomba usikatili penzi langu, mapenzi yangu yote yapo kwako na sio kwa mfalme, siwezi kukubali nikukose, nitajitahidi kuishi na wewe kwa siri" Gwanta aliongea kwa hisia 
ITAENDELEA

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.