Notification texts go here Contact Us Buy Now!

DEREVA TAXI SEHEMU YA KUMI NA SABA (17)

TAXI DRIVER SEHEMU YA 17
Saa 8:30 Asubuh

Akaitoa usalama ile bastola kisha akamwambia kuwa katika kazi yao wanaogopa sana shahidi, hivyo kila anayeshuhudia wanachokifanya huyo huwa hana maisha mazuri ya kuishi, ni lazima wamuuwe sasa kwa kuwa yeye amejileta kwenye kifo basi haina budi kumuua. Akajiandaa kumshuti kwa risasi lakini ghafula tu mlipuko mkubwa wa bunduki ulisikika kisha kimya kikatanda huku kila mmoja kati ya moni na Hudah macho yakiwatoka wasielewe nini kimejiri mahala hapo.

_______________________________

"Nataka majibu ya kazi niliyokupeni isizidi masaa mawili kwani nataka kujua kati ya uchunguzi wetu na wa hawa polisi ni upi uko sahihi na nataka kupata ufumbuzi yakinifu juu ya hilo," alikuwa ni Roi akiwa ameiweka simu yake masikioni na hiyo ni mara baada ya kutoka kutuma vile vielelezo alivyovipata kutoka kwa SP Asna. "Ok, brother ni muda mfupi kuanzia sasa nitakuwa nimeshapata majibu ya kukupa," upande wa pili wa simu hiyo ulijibu. "Fanya hima Amiri, fanya hima sana hii kazi naona inamkanganyiko sana sasa nataka kujua nini uhalisia wake," akasisitiza Roi, upande wa pili ukamhakikishia uharaka wa jambo hilo jinsi utakavyofanyika. Simu ikakatwa na akaamua kufungua friji na kutoka na kinywaji baridi kasha akakiweka kinywani.

"Mko maeneo gani kwa sasa mnasema?" akauliza mtu mmoja simuni. "Tupo hatua tano kutokea kwenye nyumba hiyo ambayo tuliitilia mashaka mkuu," alijibu mtu mmoja mwenye kofia kubwa kichwani mwake. "Ok, sawa nini mnadhani sasa maana maelezo yanasema kuwa kati ya nyumba mbili walizokuwa wanakaa wale wazee ambao hadi sasa hatujui wako wapi, hiyo pekee ndiyo inayoonesha kuwa kuna mtu anaishi," Ilisema sauti simuni. "Nje kuna gari ndogo imepaki na lango la nyumba yenyewe linaonekana kuwa limefungwa lakini mlango mdogo kama umerudishiwa tu," alijibu mtu huyo mwenye kofia kubwa. "Hakikisheni mnauwa kila mnachokutana nacho nataka mnipe taarifa ya kuwa kila kitu kiko sawa bila shaka yupo mtu hapo," Mtu huyo simuni akasema kasha akakata simu. Mtu huyo mwenye kofia kubwa kichwani akawaamrisha vijana wake kuwa sasa walitakiwa kulivamia lile eneo kwa akili nyingi sana na kwa uangalifu mkubwa. Wakatawanyika, walipata kuwa kama vijana sita hivi kwa idadi yao na yule mwenye kofia kubwa akawa ameongeza idadi ya watu saba Wakalikaribia lile gari na kulitazama ndani lilikuwa tupu, wakajaribu kusukuma mlango mdogo wakaona ukiwa unasukumika bila shida. Wakapeana ishara kuwa njia nzuri ya kupita ilikuwa ni hiyo, wakapita wote mahala hapo na kutawanyika tena walipofika ndani ya uzio ule. Walipokelewa na nyasi ambazo hazikuwa katika mpangilio mzuri sana na zilikuwa ndefu kiasi kuonesha kuwa zina muda kidogo hazijafanyiwa usafi wa aina yoyote. Maua yaliyopandwa kufuata kuta yakiwa marefu zaidi, wakatazama mahali mlango ulipo lakini pia wakatazama kwenye maegesho ya magari wakaona kuna gari mbili. Land Rover Deffender toleo la zamani na nyingine ambayo ilikuwa imefunikwa na turubai. "Kunaweza kuwa na mtu kweli mbona mazingira yanakataa?" akaonesha wasiwasi mmoja wao. "Inaonekana hivyo lakini ni lazima tujihakikishie kwa kuingia ndani...wataanza wawili kuingia kasha sisi wengine tutafuatia kwa kila baada ya sekunde tano ili kuepuka kuvamia pasipo utaratibu," yule bwana mwenye kofia kubwa akajibu na kutoa maelekezo kasha akateuwa watu wa kuingia.

Ndani mule, chupa ya pombe ilikuwa imesalia kidogo sana kuisha na mnywaji ni kama kuna mawazo yalikuwa yakimsumbua kichwani mwake, alikuwa yupo kwenye kisima kirefu sana cha mawazo. Akaikamata chupa ile na kuiweka kinywani mwake lakini kabla hajaruhusu kinywaji kiingie kinywani mwake, akaona kitasa cha mlango kikiguswa. Wageni. Akawaza lakini akaendelea. Utaratibu mbovu huu sasa wa wageni hawa wa digitali, hawaji na taarifa. Alipomaliza kuwaza hivyo, akajirusha kando huku ile chupa ya kinywaji akiwa ameiweka kwenye mgongo wa kiti alichokuwa amekalia ili kuficha muonekano wa kuwa kulikuwa na mtu mule ndani kwa majira hayo. Alipiga hatua za bila sauti hadi kwenye kona moja yenye giza kasha akachomoa bastola yake kutokea kiunoni na kuingiza mkono kwenye mfuko wa suruali na kutoka na bomba moja dogo sana kasha akalifunga mbele ya bastola ile. Akaanza kuwahesabia wageni wale kwa jinsi walivyokuwa wakiingia kwa kunyata hadi idadi yao ilipofikia saba kasha mlango ukarudishwa. Akawaona jinsi walivyokuwa wakiishangaa ile sebule ilivyokosa utaratibu wa kimpangilio wakatikisa vichwa vyao. Bila shaka walikuwa wakipingana juu ya uwepo wa binadamu anayeshi akiwa hai ndani ya nyumba hiyo. Akamuona mtu mwenye kofia akiwagawa wale vijana wawili wawili kuingia kwenye kila chumba kasha yeye kuanza kuelekea kwenye chumba cha kuhifadhia makablasha mbalimbali. Baada ya kama dakika moja kila chumba kikaanza kufunguliwa na waliponusa tu pua zao kwenye sebule hiyo walipokelewa na risasi bila sauti, vijana wane wakawa wamepoteza maisha. wakabakia watatu ambao wawili ndiyo walikuwa wanatoka kwenye chumba walichotakiwa kukifanyia upekuzi. Risasi mbili zikatumwa kwenda kuwapoke na kuwapa hifadhi sebuleni hapo lakini yule bwana mwenye kofia kubwa akaona muanguko wa watu wake mara tu baada ya kuchungulia sebuleni hapo, akaona mahali ambapo risasi zilitokea akapeleka risasi zake ambazo zilimkosa Roi kwa sentimita chake kijana huyo akajibana zaidi kwenye kona ya ukuta huo aliopo na kwa kuwa alikaa mahali ambapo palikuwa ni karibu na swichi ya kuwashia taa, akazima taa ghafula akasikia mguno wa mfadhaiko kutoka kwa jamaa huyo lakini kabla hata hajafanya maamuzi, mvua ya risasi ikawa inamiminika kumuelekea yeye. Roi akawa kwenye wakati mgumu kidogo maana jamaa huyo alikuwa akimkosa kwa uchache sana na hakuweza kutoka hapo mahala. Jamaa huyo alichokuwa akikifanya ni kumimina risasi huku akiufuata mlango wa kumtoa humo ndani ili aweze kujiokoa. Wakati anaukaribia mlango, taa ikawashwa kasha kitasa cha mlango kuchanguliwa kwa risasi kutoka kwa Roi na kuufanya mlago huo kujifunga. Bwana huyo akageuka na kupiga risasi mbili ambazo ndizo pekee zilizikuwa zimesalia kwenye silaha yake, Roi akajirudisha nyuma kwa nguvu na kuifanya bastola yake kujigonga kwenye ukuta ikamtoka na kudondokea kwa mbele, akajitoa kwa kasi kubwa na kuruka kasha akakanyaga ukuta na kujigeuza juu akamzawadia jamaa huyo mateke mawili ambayo jamaa huyo aliyapokea vema maana yalimrusha kwenye meza ya hapo sebuleni na kuivunja. Akanyanyuka kwa nguvu na kuja huku akipiga kelele, akarusha mikono ambayo ilikuwa na lengo fulani kwa mrushiwaji Roi akawa na kazi ya kukinga mapigo yale lakini hakuweza kukinga yote kwani moja ama mawili yalimgusa mahali na kumpotezea malengo. Jamaa huyo alikuwa anapiga kama mtu aliyechanganyikiwa kwani pigo lake moja lilikuwa zito na endapo likitua mwilini mwako basi huwenda likakuletea madhara. Akazidi kuleta mashambulizi hayo huku Roi akiwa anamsoma ujaji wake na upigaji wake. Ngumi moja kali sana ikampata Roi kwenye pembe ya jicho na kumfanya ahisi kama jicho lake linataka kutoka, akapoteza muhimili wa kazi yake, akaruhusu mapigo kumshukia kwa nguvu kubwa hadi akaenda chini. Jamaa huyo akaja kwa kasi sana lakini Roi akanyanyuka kwa kujirusha kidogo kasha akampisha huyo jamaa na kumpiga ngumi moja ya mgongo iliyomfanya bwana huyo kujikunja kwa mbele kama kuku aliyebanikwa, Roi akaruka tena kwa mbele na kumtandika ngumi safi ya shingo jamaa akaenda chini mate yakiwa yanamtoka.

"Nani aliyekutuma kuja kuichunguza hii nyumba?" akauliza Roi akiwa amemkanyaga jamaa huyo kifuani. "Aaaaghr! Sijui mjinga wewe...aaah!" alijibu jamaa huyo huku akionekana kupitia maumivu lakini kutokana na jeuri zake, alijikuta akichezea pigo moja la mbavu lililomfanya apige kelele za maumivu zaidi. "Sema wewe ukiepuke kifo la sivyo huwenda ukafa kabla hujaamua kunijibu maana sitavumilia ucheleweshwaji wa majibu ya maswali niliyouliza," akasema Roi. Kimya kikakita lakini jamaa huyo alijigeuza na kujifanya kama atakaye kulala ubavu ubavu kasha akaupiga mguu wa Roi uliokuwa umekikanyaga kifua chake, Roi akayumba lakini hakufika chini na kabla jamaa hajafanya maamuzi mengine, kijana Roi alikuwa tayari ameshachomoa kisu na kumchoma kijana huyo kwenye paja. Kelele za maumivu zikamtoka zaidi. "Haya sema basi maana hukutaka kujibu kwa urafiki," akamwambia Roi huku akikitembeza kile kisu mbele nyuma. Jamaa akapiga kelele nyingi huku akimtaka kijana huyo aache hilo zoezi na kumwambia kuwa atasema, kijana huyo akasitisha na kumtazama usoni. "Janga," akasema huyo jamaa. "Anapatikana wapi huyo Janga?" akahoji zaidi Roi. "Majani mapana nyumba namba 113,"Asante kwa kuwa na ushirikiano mzuri nami," akasema Roi kasha akanyanyua guu lake na kulishusha shingoni mwa huyo jamaa na kutoa sauti ya mvunjiko kasha akajikalisha palepale kitini na kuchukua kinywaji chake akakimalizia. Akiwa hapo anaendelea kujiburudisha na kinywaji hicho, simu yake ndogo ya mkononi ikaita, akatazama mpigaji alikuwa ni mzee Kasa. Akaipokea na kuiweka sikioni. 

"Nimeona, nimeona na nilijua tu ni lazima wafike hapo, najua kuna kitu utakuwa umeng'amua kutoka kwao, njoo Shule ya msingi Masiwani hapa Chuma muda huu ikibidi," aliongea Kasa kasha akakata simu. Roi akajiuliza, ameona, ameona nini? Inamaana alijua kuwa nitavamiwa hapa siyo? Akaliacha hivyohivyo swali hilo bila kulitafutia ufumbuzi wa majibu. Akatazama saa ilikuwa ni saa kumi za jioni. Akaicheki simu yake ya kuwasiliana na vijana wake wa kazi akaona haikuwa na kitu chochote kilichoashiria kuwepo kwa mawasiliano. Akanyanyua ile simu ndogo na kupiga kwa Kasa lakini kabla simu haijaleta majibu kuwa inaita, simu ile nyingine ikatoa sauti ya mlio wa kuashiria ujumbe ulikukuwa ukiingia. Akakata ile aliyokuwa akimpigia Kasa na kuutazama ujumbe uliokuwa umeingia. 'Jina kamili ni Amos Amos Tumbo. Alizaliwa tarehe 06-08-1974. Mweusi rangi yake, anaishi Magomeni Kondoa mtaa wa karibu na msikiti nyumba no. 63 na mwingine ni Janga Dominic, huyu anapatikana Majani mapana nyumba no. 113; Ujumbe huo ulisomeka hivyo. Akaunganisha na majibu ya mtu mwenye kofia kubwa aliyemlaza milele, akaiweka simu ile mfukoni huku ile ndogo akiwa ameishika mkononi, moja kwa moja hadi lilipo gari akalichunguza kwa umakini mkubwa, alipohakikisha usalama, akaingia na kuondoka kwa kasi kubwa.

************
Silaha ilimtoka Hudah mikononi kasha damu kuanza kumchuruzika kutokea pajini mwa uso wake taratibu akianza kubonyea chini bila kupenda. Risasi kutokea kwenye bastola aliyoikamata Tom barabara iliweza kuyakatisha majigambo ya Hudah kwa ghafula tu pia maisha yake kukomea hapo. Moni aliichukua ile bastola kutokea chini baada ya kuachiwa na Hudah kasha akamfuata Tom na kuingia garini bila kumsemesha. "Sasa nikupeleke wapi?" akauliza Tom akiwa anaingurumisha injini ya gari yake huku bado akili yake ikimfikiria huyo binti ambaye yeye anasema kuwa anamfahamu lakini akili yake bado ilikuwa ikigoma kumfunulia kuwa ni wapi aliwahi kukutana na binti huyo. "Sina makazi maalumu," akajibu Moni kasha akatulia kimya. Tom alimtazama binti huyo kupitia kioo cha mbele pale na kumuona jinsi alivyojiinamia chini hana habari naye. Akaliwasha gari na kuligeuza kulirudisha lilipotoka hadi walipokuja kuikama barabara ndipo walibadili muelekeo na kuelekea mjini.

Roi alifika Masiwani shule ya msingi kwa muda mfupi tu na kuteremka garini kasha akachukua uelekeo wa mti mmoja wa Muarobaini ambao kwa chini ya mti huo kulikuwa na mzee aliyekuwa amechutama. Akafika hadi hapo na kusimama nyuma yake akatulia kimya bila kusema jambo. Mzee huyo akanyanyuka na kusimama wima akasema baada ya kujikohoza kidogo. "Ilikuwa ni vigumu sana kujua ni nani wanaotuchanganya kwenye hili au haya yanayotokea kila leo. Kutokana na kile kilichotokea uwanja wa ndege, nikajua na wao watafanya kila namna kututafuta mimi na mwenzangu. Mwenzangu nikamwambia aondoke kabisa pale lakini mimi nikataka nikupe pa kuanzia. Najua kuna ushahidi aliouacha Kichambua mikononi mwa polisi unao. Kwa sasa unatakiwa uishi mbali kabisa na mishemishe za watu yaani utakaa nje kidogo ya mji. Kuna nyumba iko Majengo nyuma kidogo kabla hujafika msikitini, nyumba hiyo inatazamana na soko dogo la hapo Majengo," akaongea mzee Kasa na kutoa ramani ya nyumba na eneo nyumba ilipo kasha akampa pamoja na ufunguo kijana huyo. Akaendelea. "Hakuna mtu ambaye anayajua makazi hayo na nyumba hiyo licha ya kuwa na mlango wa mbele unaotazamana na soko lakini pia kuna mlango wa nyuma ambao unauwanja mkubwa utakaokuwezesha kuegesha gari na pia haina uzio wowote. Utaishi kienyeji kabisa kutokana na kuweza kuwachanganya hawa watu. Gari niliyokuja nayo mimi ndiyo utakayoondoka nayo mahala hapa na uliyokuja nayo wewe nitaondoka nayo mimi na uendako utakutana na gari yako kutokea kitengoni kwako ni vijana wenzako wamekuletea gari hiyo ikiwa na maana kuwa sasa kila kitu kinaanza rasmi," baada ya kusema hayo akapiga hatua kuondoka eneo hilo huku akimwambia kuwa atazidi kuwa naye kwani kila kazi ipo chini yake na yeye ndiye aliye naye kwenye kazi hiyo kwani Kichambua, Zubery na Ezekiel wao wamepangiwa majukumu mengine hivyo hawatakuwepo tena kwenye kazi hiyo. Roi aliondoka hapo na kuingia kwenye gari aliyokuja nayo Kasa kasha akaichunguza kwa vifaa vyake kwani hakutaka kumuamini mtu hata mmoja kwa muda huo. Alipoona kuwa kila kitu kiko sawa akafikiria kazi mbili zilizopo mbele yake moja ya Majani mapana na ile ya Magomeni Kondoa. Akaona muda mzuri ni siku inayofuata kwani alitakiwa kuzifanya zote kwa pamoja ndani ya siku moja. Akawasha gari lakini hakuondoka akatoa kadi kazi na kuchukua simu yake na kuingiza namba kwenye simu hiyo

Shemeji amekubana nini naona kimya?" alianza hivyo Roi mara baada ya simu hiyo kupokelewa. "Hapana sina mtu wa kunibana kwanza sijakufahamu ni nani mwenzangu?" ukajibu upande wa pili wa simu. "Roi hapa naongea," "waoh! Samahani bwana, unajua kazi zetu hizi ukirudi nyumbani nako nyumba inakutazama uifanyie usafi, ukimaliza vyote vinavyokuhusu uko hoi,"
"Pole sana, kwa hiyo utakuwa umechoka sana hadi sasa?" akatupa chambo.

Itaendelea.

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.