BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati (Ewura CCC) limewatahadharisha watumiaji wa jiko la gesi kuwa wasitumie simu za mikononi wakati wakipika, kwa vile linaweza kulipuka kwa kuwa simu zinatumia mionzi.
Mjumbe wa Kamati ya Huduma kwa Watumiaji wa Maji na Nishati Ewura CCC Mkoa, Potamia Buretta ametoa tahadhari hiyo wakati wa kikao cha utoaji wa elimu kwa watumiaji wa huduma hizo kilichofanyika mjini hapa juzi.
Katika kikao hicho cha utoaji wa elimu kwa watumishi wa huduma hizo, kiliwashirikisha walimu wakuu wa shule za msingi wakuu wa shule za sekondari na waratibu wa elimu kata wa Manispaa ya Morogoro.
Buretta alisema mara nyingi watumiaji wa majiko ya gesi nyumbani, hawatambui athari ya kutumia simu za mkononi wakati wakipika, kwani kitendo hicho ni cha hatari kwa kulipuka simu ambazo zinatumia mionzi.
“Ninashauri usitumie simu eneo unalopika na jiko la gesi kwa vile simu zinatumia mionzi na zinaweza kulipuka pale unapotikea uvujaji, hili ni kwa usalama wetu na tahadhari kwa maisha yetu,” alisema Buretta.
Pia aliwataka watumishi wa nishati ya gesi, kununua mitungi kwenye kampuni husika na ikiwa imefungwa lakiri kwa ajili ya kujihakikishia ujazo na usalama wa mitungi.
Kwa upande wa wanunuzi wa mafuta ya dizeli na petroli zinazouzwa barabarani kwenye madumu na chupa za plastiki, alisema mafuta hayo yanaweza kusababisha madhara kwenye magari kutokana na kukosa ubora, ujazo usio sahihi na kuchakachuliwa na uchafu.
Amewashauri wenye magari, kujaza mafuta asubuhi kwa vile yanakuwa na uzito kwa kutoa ujazo sahihi, badala ya kujaza nyakati za mchana kwani muda huo ni wa joto na mafuta yanakuwa mepesi, hivyo kukosa ujazo sahihi.
Amesema ujazaji mzuri wa mafuta wakati wote ni tangi linapokuwa na mafuta nusu na hiyo huepusha hewa kuingia ambayo inachangia kuchukua sehemu ya ujazo wa mafuta yanapojazwa yakiwa chini ya hapo.
Aliwashauri wenye magari wanapojaza mafuta, kudai risiti ili wanapobaini mafuta yamechakachuliwa, iwe ni rahisi kuwasilisha malalamiko ya mtoa huduma kwa baraza hilo kwa hatua zaidi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Morogoro ya Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Ewura CCC, Abdul Dachi amesema elimu hiyo imetolewa kwa makundi mengine na awamu hiyo ni walimu na viongozi ambao ni rahisi kwao kuifikisha kwa jamii inayowazunguka.
Amesema jukumu la baraza hilo ni kupokea malalamiko dhidi ya watoa huduma za maji, nishati na petroli ili hatua mbalimbali zichukuliwe kwa ajili ya kuona maslahi yao yanalindwa.