Notification texts go here Contact Us Buy Now!

NISAMEHE RATIFA SEHEMU YA 22

NISAMEHE RATIFA EP 22*


“Ibrahi…nime…kus…ame..he..” alisema Latifa huku akilia.
Walichukua dakika kumi njiani ndipo walipofika alipokuwa akiishi Ibrahim. Kwa kuwa nyumba ilizungushiwa ukuta huku ikiwa na geti kubwa, Ibrahim akateremka na kwenda kulifungua geti lile ili gari liingizwe ndani.
Kitu cha ajabu alipofika katika eneo la nyumba hiyo, akapiga uyowe mkubwa, mbele yake alikuwepo mzee Deo, alikuwa hoi chini, kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma, muda huo napo damu zilikuwa zikimtoka katika kipande cha mguu wake, Nusrat alikuwa amemtoa ndani ya nyumba yake.
Latifa na watu wengine waliposikia uyowe huo, wakahomoka kutoka garini, wakajua kwamba kulikuwa na kitu ndani ya nyumba hiyo, walipolifungua geti dogo na kuingia ndani, wakamkuta Ibrahim akiwa amemshika mzee Deo aliyekuwa chini huku akilia, mzee huyo alikuwa hoi, damu ziliendelea kumtoka katika kipande chake cha mguu na alikuwa akilia kwa maumivu makali.
Wote wakamfuata, kila mtu aliyemwangalia, sura yake ilifanana na Latifa kwa mbali, hakukuwa na mtu aliyekuwa na ubishi kwamba mzee yule alikuwa mzazi wa Latifa.
Latifa akajikuta akianza kulia, hasira ikamkaba kooni dhidi ya Nusrat, alionekana kuwa na hasira mno.
“Hanijui, yaani pamoja na kuniumiza bado ananiumizia baba yangu! Atanitambua mimi ni nani,” alisema Latifa huku kwa kumwangalia tu ungegundua ni jinsi gani alikuwa na hasira.
Walichokifanya ni kumchukua na kumpeleka hospitalini huku Latifa akiahidi kwamba ni lazima angemuonyesha Nusrat yeye alikuwa nani.
****
Latifa alikuwa akilia tu, kila alipomwangalia baba yake, moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama alikuwa kwenye hali ile. Watu wengine walimbembeleza anyamaze lakini hakunyamaza, hasira kali dhidi ya Nusrat ilimkamata mpaka kufikia kiasi cha kukunya ngumi.
Kitendo cha kupigwa baba yake na kuumizwa namna ile kulimuongezea hasira ya kumchukia Nusrat ambaye miaka michache nyuma alimuumiza kwa kumchukulia mwanaume wake, hakuonekana kuridhika, leo hii alimpigia baba yake.
“Nitamuonyesha,” alisema Latifa huku akionekana kuwa na hasira kali.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Japokuwa kipindi cha nyuma alisema kwamba baba yake alikuwa miongoni mwa watu aliokuwa akiwachukia kwa kuwa tu alkimfukuza mama yake lakini wakati alipokuwa akimwangalia, mateso aliyoyapata, chuki yote dhidi yake aliyokuwa nayo ikaondoka na huruma kumuingia.
Manesi waliokuwa na machela wakasogea lilipokuwa gari lile na kumpajndisha mzee Deo juu ya machela ile na kuanza kusukumwa kwenda kwenye chumba kimoja kilichoandikwa Theatre. Walipofika nje ya chumba kile, wakazuiliwa.
Watu waliokuwa wamegundua kwamba msichana aliyekuwa mbele yao alikuwa Latifa walibaki wakishangaa, hawakuamini kama kweli yule aliyesimama mbele yao alikuwa ndiye au alikuwa msichana mwingine aliyefanana naye.
“Inawezekana ndiyo yeye,” alisema jamaa mmoja huku akimwangalia Latifa ambaye machozi yalikuwa yakimbubujika tu.
“Labda! Ila awe hapa anafanya nini?”
“Sijui, hebu tusogee karibu zaidi tumuone.”
Kila aliyepita, hakuacha kumshangaa Latifa aliyekuwa akilia tu. Ibrahim alikuwa kimya, moyo wake ulimuuma, alimzoea sana mzee Deo, alikuwa rafiki yake mkubwa, alimpenda pasipo kujua kwamba mzee huyo alikuwa mzazi wa msichana aliyemuacha kipindi cha nyuma, Latifa.
Madaktari wakawa wanapishana mlangoni, wengine waliingia na wengine kutoka. Mgonjwa aliyeletwa kwao alionekana kuwa wa maana sana, ilikuwa ni bora kuleta utani kwa mgonjwa mwingine lakini baba yake Latifa.
Baada ya msaa mawili, mlango ukafunguliwa na daktari kutoka, akawaita watu hao ofisini kwake kwa lengo la kuzungumza nao. Walipofika huko, akawaweka chini.
“Hali ya mgonjwa si mbaya, alitoneshwa tu kidonda chake,” alisema Dk. Mimi, mwanamke mzuri mwenye umbo la kuvutia.
“Ila ninataka kuzungumza naye, naweza kufanya hivyo?”
“Hakuna tatizo, unaweza ila kama baada ya saa moja hivi, atahitaji muda wa kupumzika,” alisema Dk. Mimi.
“Sawa!”
Kusubiri halikuwa tatizo kabisa, alitaka kumsikia baba yake akizungumza kile alichokuwa akitaka kuzungumza. Alitaka kusikia kile ambacho hakuwa amekisikia kuhusu mama yake, kile alichosema Ibrahim kwamba mzee huyo alikuwa na la ziada.
“Nyamaza Latifa,” alisema Dominick huku akimvuta Latifa upande wake.
Walitulia kwa muda wa saa moja na ndipo walipoambiwa kwamba wangeweza kumuona mgonjwa wao. Wakainuka na kuingia ndani. Latifa alipomuona baba yake kitandani pale, uso wake ukajawa na tabasamu pana na kuanza kumsogelea.
Moyo wake ukaingiwa na hisia kali, ukapatwa na furaha kubwa kiasi kwamba alishindwa kuliuia tabasamu lake kutawala usoni mwake.
“Baba…”
“Naam mwanangu.”
“Nini kilitokea?”
“Maisha, maisha yalinipiga na ndiyo maana nipo hivi,” alijibu mzee Deo.
Latifa akanyamaza, akamsogelea baba yake kitandani pale na kumbusu katika shavu la uso huku machozi ya furaha yakimbubujika mashavuni mwake.
“Umefanana sana na mama yako,” alisema mzee Deo.
“Nani? Mimi?”
“Ndiyo! Mama yako alikuwa mrembo kama ulivyo,” alisema mzee Deo.
“Sasa kwa nini ulimfukuza wakati alipokuwa na mimba yako?”
“Nilimpenda sana mama yako, nilijitolea kwa kila kitu, nilitaka niishi naye japokuwa nyumbani kwao hawakuwa wakinipenda kisa tu nilikuwa mtu mweusi. Alipofukuzwa kwao, akakosa pa kwenda, alichoamua ni kuja nyumbani kwangu.
“Hata kabla hajafika, tayari wazazi wake waliwatuma watu wawili, walikuja huku wakiwa na bunduki, waliniambia kwamba endapo ningempokea mama yako na kuishi naye, hakika wangeniua, na waliniambia kabisa kwamba walitumwa na wazazi wake,” alisema mzee Deo na kuendelea:
“Niliogopa sana, niliona kweli ningeuawa, nilichokifanya ni kumfukuza Nahra huku nikiumia moyoni. Sikufanya vile kwa kuwa sikuwa nikimpenda, la hasha! Nilifanya vile kwa kuwa nyuma yangu niliwekewa bunduki. Alipoondoka, sikukaa nyumbani, niliondoka kwenda kumtafuta, usiku mzima nilimtafuta kila kona, ila sikufanikiwa kumpata, huo ukawa mwisho wa kuonana naye,” alisema mzee Deo, tayari naye machozi yalianza kumbubujika.
Watu wote waliokuwa mahali pale walikuwa kimya wakimsikiliza, mzee huyo alitia huruma kitandani pale, alionekana kukosa nguvu na alikuwa mtu aliyekosa tumaini kabisa.
“Nisamehe Latifa,” alisema mzee Deo.
“Nimekusamehe baba! Kila kitu kilichopita, kimepita, ni lazima tugange yajayo,” alisema Latifa, hapohapo akayapeleka macho yake usoni mwa Ibrahim aliyekuwa kimya.
“Ulimfahamu vipi Ibrahim?”
“Ni mtu ambaye amenisaidia sana, bila yeye nafikiri leo hii nisingekutana na wewe. Alinionyeshea upendo mkubwa sana, sikuamini kama kuna watu wenye roho nzuri kama alivyokuwa yeye. Nimekuwa naye kipindi chote, nilipopata tatizo, alinisaidia kwa fedha kidogo aliyokuwa nayo.
“Hakujua kama mimi ni baba yako, alinionyeshea upendo kwa kuwa aliona nastahili kufanyiwa hivyo japokuwa mke wake alikuwa ni tatizo kubwa. Binti yangu! Ibrahim alinihadithia kila kitu kuhusu wewe hata kabla hajajua kama mimi ni mzazi wako, naomba umsamehe, inawezekana mambo yote anayopitia, shida zote anazozipata ni kwa ajili ya laana yako, msamehe na sahau kila kitu,” alisema mzee Deo.
Latifa akayapeleka tena macho yake kwa Ibrahim, alipanga kutokusamehe katika maisha yake lakini kila alipokuwa akimwangalia, bado mwanaume huyo alionekana kuhitaji msamaha.
Alionekana kupigika katika maisha yake, alitia huruma lakini pamoja na hayo yote, alifanya kazi kubwa sana kumlea baba yake. Hakuwa na fedha za kutosha lakini nkiasi hichohicho kidogo alikitumia kwa ajili ya kumtibu baba yake, hakika alifganya jambo kubwa lililohitaji sifa kubwa kutoka kwake.
Hakuongea kitu, alichokifanya ni kumsogelea na kumkumbatia. Wote wawili walikuwa wakibubujikwa na machozi. Latifa hakuwa na jinsi, aliukana moyo wake na kumsamehe mwanaume huyo aliyeonekana kuhitaji sana msamaha.
“Nisamehe Latifa.”
“Nimekusamehe Ibrahim, Ahsante kwa yote uliyomfanyia baba yangu,” alisema Latifa huku akijifuta machozi.
“Naomba umsamehe Nusrat pia! Ni mwanamke mpumbavu asiyejua lile analolifanya. Naomba umsamehe.”
“Nimsamehe Nusrat?”
“Ndiyo!”
“Kwa hivi alivyomfanyia baba yangu?”
“Latifa! Hebu sahau kwanza. Wewe ni mtu mkubwa na mwenye heshima, tazama dunia nzima inakutazama wewe, usiposamehe, vipi wale vijana wanaotaka kuwa kama wewe? Nao watakapokosewa hawatakiwi kukosea kisa wewe haukusamehe? Vipi kuhusu wale watoto wanaotaka kuwa kama Latifa, kweli nao hawatakiwi kusamehe? Samahe saba mara sabini, au umesahau hilo?” aliuliza Ibrahim.
“Nakumbuka.”
“Basi naomba umsamehe!”
“Nimemsamehe!”
“Nashukuru!”
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa maisha mapya, Latifa hakuwa na kinyongo, moyo wake ulilainika na hakutaka kuwa na kingo na mtu yeyote yule, alichokiamua ni kumsahmehe kila mtu aliyewahi kumfanyia ubaya kwa makusudi au bahati mbaya.
Alikuwa mtu mwenye mafanikio, bilionea, alichokifanya ni kumsafirisha baba yake nchini Marekani, alitaka akatibiwe huko na kuishi naye hukohuko. Kwa Ibrahim, japokuwa alimfanyia mambo mabaya nyuma hakutaka kumuacha hivihivi, aliamua kumsaidia kama alivyomsaidia baba yake.
Akamnunulia nyumba kubwa Mbezi Beach na kumgawia kiasi cha shilingi milioni mia tatu kwa ajili ya kufanya biashara zake kitu ambacho kwa Ibrahim kilikuwa kitu kikubwa, baada ya wiki moja, akaamua kumpa talaka Nusrat na kumuoa mwanamke mwingine na kuishi naye nyumbani kwake huku akifungua biashara kubwa.
Kwa Latifa, akaamua kufunga ndoa ya kishria Dominick na watu hao kuishi pamoja kwa amani ni na upendo ambapo baada ya miaka miwili, wakafanikiwa kupata mtoto wa kiume waliyemuita kwa jina la Godlove.
Dawa yake ya kansa ya Morphimousis iliendelea kutikisa duniani, watu waliokuwa na magonjwa ya aina hiyo waliendelea kutibiwa na kupona. Aliendelea kuingiza kiasi kikubwa cha fedha, utajiri wake ukazidi kuongezeka maradufu.
Baada ya miaka mitano kupita, wakapata mtoto wa pili wa kike waliyempa jina la Cecilia. Latifa alikuwa na furaha tele, moyo wake ulikuwa na amani, hakuwa na kinyongo na mtu yeyote, maisha yake yalikuwa ya furaha tele.

MWISHO….

*Nashukuruni sana kwa kuifuatilia simulizi hii. Mungu awabariki*

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.