SIMULIZI FUPI jibu sehemu 2.
MWISHO
Mtunze DJ wait
MWEZI WA NNE tangu waanze kuishi pamoja Ben aliyekuwa na pesa za kutosha katika akaunti yake akaanza visa, mara achelewe kurudi nyumbani. Mara alalae kwa rafiki zake ambao Caro hakuwajua. Caro alipouliza majibu yakawa ya mkato.
“Mpenzi leo ni siku ya ibada…”
“Wewe ndo Yesu ama?” Ben alijibu bila kujali lolote.
Zamani simu ya Ben ilikuwa simu ya Caro lakini sasa aliweka ‘password’ na hakutaka kujibu kwanini amefanya hivyo. Zamani simu zilizopigwa alizipokea bila shaka lakini sasa akawa anachagua simu za kupokea.
“Mbona simu inaita unakata.” Caro alihoji.
“Simu yako imekushinda unahamia kwenye simu yangu.” Alijibu kwa jeuri. Kisha akatoweka sebuleni
Caro aliugundua mchezo ule jinsi ulivyokuwa unaenda lakini alijiweka katika upande wa mwanamke mstaarabu hakutaka shari. Akauliza kistaarabu sana na hata alipojibiwa kwa shari hakuacha kumwekea mpenzi wake maji bafuni.
Siku moja alihoji……
“Baba Caro….kuna jambo nahitaji kuzungumza nawe.”
“Nakusikiliza.”
“Ni kuhusu kuoana…” Caro alisema. Ben akashtuka hakutegemea hoja ile…
“Bado mapema Caro….yaani hata mwaka hatujafikisha aisee.”
“Umeniitaje?” Caro alishtuka kwa mara ya kwanza katika uhusiano wao Ben anamuita kwa jina lake la kuzaliwa wakati walizoea kuitana, ‘mama Ben’ na ‘baba Caro’.
“Nimepitiwa tu…” alijibu bila hofu. Caro akakaa kimya.
Caro akajikunyata kama kuku aliyemwagiwa maji ya baridi. Lakini kichwani akitafakari mengi, alikuwa akimtafakari Ben huku akitafakari na swali alilotoka nalo Uganda. Aliona kama jibu linakaribia.
“Maana nina mimba kwa sasa…” Caro alimweleza baada ya kunyanyua kichwa.
“Car…aah mama Ben,,una mimba…mimba ya nini kwa sasa, unataka tupate mtoto nje ya ndoa….” Aling’aka Ben. Caro hakusema neno kwanza akatulia.
“Mara yetu ya mwisho kutumia kinga ni lini unakumbuka.” Caro aliweka msumari. Ben akagundua kuwa tangu wapime na kujikuta hawana virusi hawajawahi kutumia kinga. Soni ikamshika.
KITENDO cha Ben kusikia Caro ana mimba ndo kilimuhamisha kabisa nyumbani. Akawa hakosi kuhudhuria kwa Zulfa, msichana kigoli aliyekuwa amemdatisha. Kila alichokuwa anasema Ben alitii, karibia kila siku alipomtembelea alimwachia shilingi lakini moja hadi moja na nusu. Pesa ilikuwepo kwa nini asimwachie. Alifanya yote haya kwa jeuri ya pesa. Pesa ambayo amesahau chanzo chake.
MWEZI WA TANO wa mahusiano hali ilizidi kuwa tete. Ben akawa na sauti kuu zaidi katika nyumba, Caro akakosa amani, kila mara alikuwa anagombezwa bila kujalisha ni katika simu ama ana kwa ana. Ben alikuwa kama kichaa. Mara akagundulika kuanza kutumia pombe, akawa muhudhuriaji mzuri wa kumbi za starehe zinazosadikika kuwakamua watu wengi pesa hapa mjini. Huko kwenye hizo kumbi Ben akawa mpenda sifa aliwatuza wacheza shoo na waimbaji. Kibaya zaidi Ben akakumbwa na tamaa ya kutembea na wasichana warembo, hakuwakosa kwa sababu alikuwa na pesa wakajikosha akafanya nao mapenzi. Maisha yakaendelea.
Caro alipogundua hili akaamua kuwa makini. Hakuna mapenzi bila kinga la sivyo hakuna kufanya kabisa. Hali hii ikamkera Ben akazidi kujikita kwa kimada wake. Hilo nalo Caro aliligundua kupitia kwa marafiki wa Ben wenye tabia za kishakunaku. Ilimuuma sana lakini alifurahi kwa sababu alikuwa analipata jibu.
MWEZI WA SITA alimbadilikia Ben, akaanza kuwa mkali na muulizaji wa kila kitu kinavyoendelea. Ben hakutaka kutoa ushirikiano alikuwa jeuri na asiyeshaurika. Hata Rapha alikuwa amegombana naye tayari na Ben hakujali lolote kwa sababu alikuwa na pesa. Aliamini kuwa pesa ni kila kitu kwake…
Caro alipohoji juu ya ugomvi wake na Rapha kwa mara ya kwanza akajikuta akipokea kipigo kutoka kwa Ben, kipigo kitakatifu. Masikio yake yalisikia akiitwa jina baya ‘MALAYA’, Caro amekuwa Malaya?
Hakika aliumia lakini bado alitabasamu moyoni maana alikuwa anazidi kulipamba jibu lake…
Zilikuwa zimebaki siku kadhaa mkataba wake wa mkiezi sita katika nyumba ile uweze kumalizika na hakuwa na mpango wowote wa kuongeza muda wa kuishi pale na mwenye nyumba alitambua hilo. Kila kitu ndani ya nyumba ile kilikuwa mali ya mwenye nyumba. Ni nguo pekee na vitu vingine vidogo vya ziada ndo vilikuwa vya wapangaji.
Hizo ni aina ya nyumba za kupanga jijini ambazo malipo yake huwa makubwa sana na mara nyingi familia za kitajiri humudu…..
Ni nyumba ambazo huna haja ya kuhangaika kuhamisha mizigo mingi wakati wa kuhamia na kuhama.
CARO alijikusanyia kilicho chake. Kwa sababu lilikuwa jambo la kawaida sana Ben kuacha kurudi nyumbani hata kwa siku tatu bila taarifa….Caro hakuhangaika. Alifurahi kuyakuta magari yote mawili yakiwa uani. Ben hakuondoka na gari siku hiyo….
Caro akapiga simu kwa watu aliofahamiana nao. Wakayaondosha magari na mizigo yake kidogo pamoja na nguo nyingi za Ben. Akamuaga mwenye nyumba na kumkabidhi funguo zake.
SIKU iliyofuata ndege ikatua katika uwanja wa kimataifa nchini Uganda.
Caro akapokelewa na marafiki zake waliokuwa na shauku ya kuonana naye tena. Wote walingoja majibu kutoka kwa binti huyu.
Caro hakuwa na papara. Walipofika mahali tulivu alianza kuwasimulia. Walianza wao kumkumbusha swali aliloondoka nalo.
“UTAITAMBUA VIPI TABIA HALISI YA MWANADAMU?”
Caro Mduma akatabasamu. Kisha akatoa majibu kwa utaratibu.
“Ukitaka kumjua vyema mwanadamu tabia zake mpe pesa, pesa za kutosha utamfahamu vyema. Mngemuona huyo Ben wallah msingeweza kumdhania kama anaweza kubadilika…alikuwa mshamba hajui kuvaa na mtaratibu tena mnyenyekevu mno. Sijui nilivutika nini kuamua kumtumia katika kulijibu swali langu lakini niliamua kuwa naye. Mwanzoni alikuwa ana mapenzi ya kweli hauwezi amini kidogo mwenzenu nishawishike kuwa awe mpenzi wangu wa maisha kwa jinsi alivynicare, yaani alikuwa ni husband kweli lakini mambo yakabadilika baadaye. Akageuka mbogo baada ya pesa kumzoea…mshenzi sana kumbe. Nilimzuga nina mimba akaonekana kama anataka kuikataa…..nikamdanganya tuoane yote hayo akakataa, nilikuwa namfuatilia sana viwanja zake. Hakuna mtu anapenda sifa kwa wasichana kama Ben, Ben alinyanyua mikono akanibamiza baada ya kumuuliza kwanini amegombana na rafiki yake…, hakuna mwanaume limbukeni kama yule, alitekwa na manzi mmoja hata Yule msichana alikuwa mbaya class kwetu anamzidi. Akawa anampatia pesa kila leo….eti akagombana na rafiki yake aliyekuwa anamuhifadhi kwa room yake. Akadhani mimi mjinga kumbe nipo katika kutafuta jibu. Nimemwacha solemba. Sijui atachanganyikiwaje tu….amebaki na biashara yake hiyo ndo zawadi kwa kunisaidia kupata jibu. Yaani ningekuwa nimempenda kweli sijui nini kingehappen….” Caro alimaliza. Kila mmoja alikuwa akimtazama katika namna ya kumshangaa. Lakini wakaelewa azma yake. Hakika alikuwa amelipata jibu kwa vitendo.
MPE MASIKINI PESA UMJUE TABIA ZAKE VIZURI….
SEMA LOLOTE KUHUSIANA NA SIMULIZI HII FUPI…..
MWISHO