NAJUTA KUUTUNZA USICHANA WANGU -33
“ Tuliaaaa…” Aliniambia kwa ukali.
Alinishika na kunikandamiza chini,nilijitutumua na kumsukuma. Kama mzigo alianguka chini. Nilisimama na kutimua mbio, kabla sijafika mlangoni aliniwahi. Alinishika tena na kuniangusha chini.
“ Kwanini unakuwa msumbufu? “ Aliniuliza.
Sikumjibu, badala yake nilijitutumua na kumuangusha tena.Tofauti na Baba Hans, Martini hakuwa na nguvu sana. Ilikuwa ni rahisi kiasi kupambana naye. Tuliendelea kuangushana na kusumbuana pale chini.
“ Emmaaaa….Tulia basiiii….” Alinisihi.
“ niacheeeee…..”
“ Sawa, nakuacha ila usikimbie. Usikimbie ili tuzungumze.” Aliniambia.
Aliniacha. Nilirudi nyuma kwa tahadhari.
“ Naomba usinifanyie hivyo , mimi nipo tofauti na Baba Hans na mtoto wake. Mimi ni mtu mzuri tu. Hata kuhusu mauaji ya James wamenisingizia. Muuaji ni Hans, sio mimi.” Aliongea Martini.
“ Kwanini upo hapa? Jela umetokaje?”
“ Badala ya kushukuru nimekuja kukuokoa unauliza nimetokaje tena?”
“ Nahitaji kujua.”
“Sina kesi, imegundulika ushahidi wote uliopatikana ulitengenezwa. Kwanza mkuu wa kituo aliyesimamia nikamate kahamishwa, alikuwa anatumiwa na baba Hans. Huyu wa sasa hana utani, yeye ndiye aliyeamuru niachiwe baaada yakuwa na mashaka mengi kwenye ushahidi.”
“ mmmmh!”
“ Usigune! Ukweli ndio huo, “ Aliongea Martini huku akinisogelea. Kila aliponisogelea, nilirudi nyuma. Aliniwahi na kunishika mkono.Nilimsukuma, alinidaka tena.
“ kwanini unataka nitumie nguvu? Mbona Baba Hans haukumsumbua hivi?” Aliniuliza.
Sikumjibu, Nilipata mbinu ya kumtoroka. Nilitulia na kumsubiri anisogelee.Bila kujua alinisogelea, nilimpisha kwa kasi na kumsukumia kwa mbele, kama mzigo alienda kuanguka . Sikushangaa, niligeuka na kutimua mbio kutoka mle ndani.
Nilitokea kwenye varanda, nyumba ilikuwa kubwa sana, nilianza kuifata varanda.
“ Emmaaaa…Emmaaa…” Nilimsikia Martini akiniita kwa mbali.
Nilitembelesha, varanda ilikuwa ndefu sana, nikiwa katikati, nyuma yangu alitokea Martini na kunisihi nisimame .
“Nyumba kubwa hii . hauwezi kutoka wala kukimbia.” Aliniambia.
Niliongeza mwendo. Niliuona mlango pembeni ya kivaranda, niliusukuma na kuingia. Niliubamiza kwa nguvu. Martini alifika na kuugonga kwa nguvu.Haukufunguka.
“ Emmaaaa……” Aliniita.
Sikuitika, nilikitazama kile chumba. Kilikuwa na giza totoro. Vitu vya ndani havikuonekana vizuri. Nilipapasa ukutani nikaukuta mlango mwingine. Niliufungua ukafunguka. Nilichungulia na kukiona kivaranda kingine.
“ mmmmh!” Niliguna. Kivaranda kile kilinichanganya . Kilikuwa kinafanana na kile cha kwanza. Uwepo wa kivaranda cha pili ulitoa tafsiri kuwa ile nyumba ni kubwa .
“ Hili jengo gani?” Nilijiuliza. Nilipiga hatua kwenda mbele.
Niliwaza hali ya baba yangu huko aliko. “ Bila shaka baba amenitafuta sana, sijui mpaka sasa wanafikiria nini kuhusu mimi. MUNGU awasaidie waje eneo hili, nahitaji msaada wao niweze kupona.” Nilijiambia.
Nilipiga magoti chini na kumuomba MUNGU anisaidie. Sikuwa tayari kurudi tena mikono mwa Martini. Nilimuomba MUNGU anitoe kwenye kisanga nilichomo. Niliahidi kumtumikia maisha yangu yote kama atanisaidia.
“ Sina ubaya nililokutendea kustahili haya . Naomba nisaidie mwanao. Naomba nisaidie hiki kikombe kiniepuke.” Niliomba.
Baada ya kuomba sana, moyo wangu ulihisi amani, hofu na mshaka havikuwepo tena. Niliona kama nimeshaishida vita. Nilisimama na kuelekea mbele kwenye ile korido.
Nikiwa katikati, nilihisi kama kuna mtu ananifata nyuma.
Niligeuka kutazama, macho yangu yalikutana uso kwa uso na macho ya Mama Hans.
“ eeeeeh!” Nilistaajabu. Kabla sijafanya lolote mama Hans alinisogelea na kunipiga kibao cha nguvu.
“ paaaaaaaah!” Kilitua shavuni kwangu
NAJUTA KUUTUNZA USICHANA WANGU -34
“ Paah” Kilitua shavuni.
Alinishika mkono na kunivuta.
“ Mumeo sijampiga mimi? Mumeo alipigwa na Martini.” Nilimwambia.
“Kelele kengeeeeee wewe ….” Aliniambia kwa ukali. Nilimtoa mkono na kumsukuma. Alijiweka sawa na kunishika tena. Alinivuta kuelekea nilikotoka.
“ una nini na mimi?” Nilimuuliza.
Hakujibu, alinishika vizuri na kunivuta. Nilijaribu kujitoa nilishindwa. Nilimsukuma kwa nguvu nilishindwa pia. Alikuwa imara sana.
‘ Hauna hujanja hapa, ni bora ukubali yaisheeee.” Aliniambia.
Maneno yake yalinimaliza nguvu. Kiasi Fulani nilikubalina naye. Sikuona sababu ya kuendela kupambana naye.
“ Nilimuomba MUNGU anisaidie lakini hajanisaidia. Nilitunza usichana wangu kufata maagizo ya dini yangu, badala ya kubarikiwa nakuja kupata matatizo makubwa. Hakuna haja ya kuishi.” Niliwaza.
Nilikata shauri, kama mjinga niliamua kumfata Mama Hans. Kila alikonivuta nilienda bila kuleta upinzani wa aina yeyote . Tuliingia kile chumba kisha tukatokea kwenye korido nyingine.
Kichwani kwangu niliona ni bora nijitoe uhai. Niliona kitu pekee chakufanya ni kutoa uhai wangu. Tukiwa tunatembea niliangalia kila sehemu kutafuta kitu ambacho kingeweza kunitoa uhai kwa haraka.
“ Ahsante sana , Nashukuru sana.” Aliongea Martini akiwa mbele yetu.
“ Usifanye makosa tena. Tulipofikia hakuna kurudi nyuma.” Aliongea mama Hans. Alinisukumia kwa Martini.
“ Usijali..nitafanya haraka na kwa uhakika.”
“ Lakini ulichomfanya mwanangu Hans na Mume wangu sio sawa . Haukupaswa kuwafanya vile. Japokuwa nakupenda na nina malengo na wewe lakini kumbuka yule ni mume wangu wa ndoa, na Hans ni mwanangu pia.” Aliongea Mama Hans.
“ Ukisema hivyo unakosea! Hivi unadhani naweza kumfanya Hans vile? Naanzaje? Hans sio mwanao tu, ni mwanangu pia.”
“ Shiiiii….” Mama Hans alimpa ishara Martini ya kutoongea zaidi.
“Unanizuia nini? Kuna kitu gani cha ajabu kwanza? Kwani hata huyu akijua atafanya nini?. Hans ni mwanangu, na siku sio nyingi watu wote watajua ukweli. Hans sio mtoto wa Mumeo, ni mwanangu.”
“ Halafu aliyemjeruhi vile ni Mumeo” Aliongea Martini.
Maneno yake yaliniacha kinywa wazi, pia yalinipa mwanga kuhusu kile kilichotokea.
“ Ndio mana Baba Hans alimfanya vile Hans. Kumbe anajua kuwa Hans sio mwanaye ndio mana alitaka kumuua.” Niliwaza.
“ Haya mambo hayakupaswa kufika huku, hii njia sio sahihi. Hii njia inaweza kutuletea matatizo baadae.” Aliongea mama Hans.
“ Kuhusu hilo mlaamu mumeo. Yeye ndiye aliyesababisha haya, alimuua James na kunisingizia mimi. Alitaka niozee jela. Sasa jela nimetoka na Bikra ya Emma naitoa mimi.”
“ Unaongea hayo utafikiri hujawahi kumtendea ubaya .”
“ Ndio, mimi sijawahi kumtendea ubaya, ubaya alianza yeye. Alikuoa wakati akijua wewe ni mpenzi wangu. Bila yeye ,mimi na wewe tungekuwa mke na mume. Bila shaka saizi tungekuwa tunaishi kwa amani. Sema na wewe kipindi kile ulizuzuka na Vihela vyake .”
“ Ukiongea hivyo unanikosea? Tena unanivunjia heshima mbele ya Emma.”
“ Heshima gani ninayoivunja kwako Malaya mkubwa wewe.” Aliongea Martini..
Mananeo yake makali yalimchefua Mama Hans, hakukubali, naye alijibu mashambulizi. Walianza kuzozana wenyewe kwa wenyewe. Wakiwa wanazozana niliokota kipande cha nondo na kukificha mgongoni.
“ Unaniita Malaya! Upendo wote nilioutoa kwako unaniita Malaya? Wewe wa kunifanyia hivi mimi?” Aliuliza kwa uchungu Mama Hans.
“ Kosa lako kubwa ni kumpa Mumeo mtoto asiyekuwa wake, Hans ni mtoto wangu kwa tamaa zako na ujinga wako mimba ulimpa Mumeo.” Aliongea Martini huku akimsogelea, sikushangaaa, pale pale nilimpiga na kile chuma kichwani.
“ Nakufaaaaa…” Alipiga kelele, kama mzigo alianguka chini.
“ Umefanya nini?” Aliniuliza Mama Hans. Naye sikumchelewesha, nilimlamba chuma cha kichwa. Kama mzigo alianguka chini.
Sikushangaa, Nilikimbia kuelekea nje, nilipita kwenye kile chumba na kutokea kwenye ile varanda, niliangaza kila pande huku nikikimbia. Kwa mbali niliona Madambala chini, niliyaokota na kuyavaaa. Nilinyosha na ile korido mpaka nikafika nje.
Nilitoka na kukimbilia mtaani. Watu walinishangaa, nilisimama na kuomba msaada, niliwaeleza kilichotokea. Walipiga simu polisi. Polisi walifika, kwa pamoja, polisi na wananchi tuliongozana kwenda kwenye ile nyumba.
Kwa tahadhari kubwa polisi waliingia ndani, walinitaka niingie nikawaonyeshe, niliingia nao hadi kwenye maeneo ambayo matukio yalitokea, Ajabu, hatukukuta mtu ndani. Chumba nilichowaacha Hans na baba yake kilikuwa tupu hakukuwa na mtu, na pale kwenye korido nilipowaacha mama Hans na Martini nako palikuwa tupu, hapakuwa na kitu.
“ Inawezekana vipi? Hawa watu niliwaacha hapa.” Niliwaambia polisi.
NAJUTA KUUTUNZA USICHANA WANGU – 35
“ Acha kuendelea kutudanganya , unanitia hasira ujue.” Aliongea Askari.
“ Nawadanganya? Naanzaje kuwadanganya, hivi kwa hali yangu hii naanzaje kuwadanganya? Hawa watu walikuwepo hapa, Martini, Baba Hans , Mama Hans na Hans.Wote walikuwepo hapa.”
“ mmmmh! Hans? Hans yupi?”
“ Yule aliyekuwa mume wangu, aliyejinyonga usiku wa fungate .”
“ ahahaha…ahahaha…ahahaah…” Alicheka Askari.
“Daaaaah.. leo tumepatikana. Tumetoka kituoni mkuku mkuku, na nyie wananchi hata kuchambua mambo mnashindwa. Kitu kidogo tu mmetukimbiza bila kujua mtu mwenyewe kichaaa.”
“ Kichaaa? Hapana mimi sio kichaaa.”
“ Kichaaa ndio, unamzungumziaje Hans? Mtu ambaye alishakufa siku nyingi na akazikwa?” Aliniuliza.
Kauli yake iliungwa mkono na wenzake pamoja na wale wananchi.
“ Lakini mimi toka mwanzo nilihisi hivyo. Kwa jinsi alivyokuwa amevaa matambala na jinsi alivyokuwa anakimbia nilijua atakuwa kichaaa.” Aliongea kaka mmoja ambaye sikumjua.
“ Daaha namuonea huruma sana, bila shaka vifo vya Hans na James vimemchanganya.” Aliongea dada mwingine.
“ Mimi sio kichaaaa, nina akili zangu. Watu niliowataja walikuwa hapa! Walikuwa wanataka kunibaka.” Niliwaambia. Hakuna aliyenisikiliza. Polisi waliondoka na kuniacha pale, niliongozana na wananchi kutoka . Nikiwa nje ya Jengo nilikutana na mama pamoja na baba.
“ Ulikuwa wapi mwanangu?” Aliuliza baba. Kabla sijamjibu alinisogelea na kunikumbatia kwa nguvu.
“ Pole sana mwanangu..” Aliongea mama.
Walinifariji , kwapamoja tuliongozana kurudi nyumbani.Tukiwa nyumbani waliniandalia maji nikaenda kuoga , baada ya kujisafisha na kujiweka sawa, waliniita barazani niwaeleze kila kitu kilivyokuwa. Niliwaeleza, niliwaeleza yote, A to Z.
“ Inaonekana ishu hapa ni hiyo bikra yako, kabla hatujaamua kupambana nao, ni busara kutafuta ukweli wake. Kwanini hawa watu wapo tayari kufanya yote haya kwa ajili ya bikra tu.” Aliongea baba.
Kauli yake iliungwa mkono na mama.
“ Lakini kabla hatujaanza kufatilia naomba Emma kwanza twende hospital. Inabidi tukacheki afya yako. Uzima wako ni kitu muhimu kuliko kitu chochote kile. “ Aliongea baba.
“ Kuna kitu nakiwaza hapa! Emma uliwahi kuniambia kuhusu mdogo wake Hans, huyo mtu anyejifanya hans sio mdogo wake kweli?” Aliuliza Mama.
“ Hata sielewi mama, lakini yeye mwenyewe anasema ni hans. Na anasema hakufa.”
“ Atakuwa Hans. Hans hana mdogo wake, angekuwepo ningemjua. Hata yule dereva yebo alimuona Hans, hakuwa mdogo wake Hans. Nazani baada ya kuonwa hans alimdanganya kuwa yeye ni mdogo wake wakati sio kweli.” Aliongea Baba.
“ Inawezekana , Hans aliniambia baada ya tuko la maigizo yao ya kujinyonga alienda mtwara, na yule dereva yebo alisema amemuona mdogo wake hans mtwara. Bila shaka alikuwa mtu mmoja.” Niliwaambia
……………….
Siku ya pili , Asubuhi na mapema tulienda Hospital. Nilikuwa nimeongozana na baba. Tulipokelewa vizuri, walinifanyia uchunguzi na kunitoa wasiwasi. Hakukuwa na shida yeyote kwenye mwili wangu.
“ Ahsante sana! “ Baba alimshukuru Daktari.
Kabla hatujaaga , gafla, mlango ulifunguliwa waliingia polisi wakiwa na silaha.
“ Utaratibu gani wa kuingia ofisini kwangu na silaha?” Aliuliza Daktari.
“ Unahitajika kituoni” Askari waliniambia. Kabla sijaongea lolote walinishika mikono na kunitaka nifatane nao. Sikubisha , niliongozana nao mpaka kituoni. Moja kwa moja walinipeleka kwa mkuu wa kituo.
“ kuna mambo nimesikia umeyaongea. Nahitaji ufafanuzi kutoka kwako.” Aliniambia.
“ Mambo gani?” Nilimuuliza.
“ Ni kuhusu mtu aliyekufa! Anaitwa Hans. Alijinyonga usiku wa harusi yenu. Nasikia uliwaambia askari wangu yupo hai?”
“ Ndio, yupo hai”
“ Unaweza kuthibitisha?” Aliniuliza.
“ Njia pekee ya kuthibitisha ni kulifukua kaburi lake. Kama kweli alikufa na kuzikwa kwenye kaburi lake kutakuwa na maiti.” Nilimwambia.
“ Ok safi,” Aliongea. Alichukua simu yake ya mezani na kupiga. Alitoa maelekezo kwa mtu aliyeongea naye . Alimwambia anahitaji kibari cha kwenda kufukua kaburi. Nilimsikia kwa mbali mtu aliyekuwa anaongea naye akimjibu kibali kitakuwa tayari baada ya nusu saa.
Alikata simu na kuniambia nisubiri nje. Nilitoka na kukaa kwenye benchi kusubiri. Nikiwa pale kwenye benchi, macho yangu yalikutana na macho ya askari ambaye siku hans anajinyonga afika hotelini na kuthibitisha. Aliniangalia kwa jicho kali sana.
“ Habari..” Nilimsalimia.
Hakunijibu, alinipita na kuingia ndani.
…………………
Baada ya masaa kadhaaa kupita, kibali kilipatikana, mkuu wa kituo aliita watu kadhaa, pia alipiga simu hospital kumwita daktari, kwa pamoja tuliongozana kuelekea kwenye kaburi la hans. Kufika tu, kaburi lilianza kufukuliwa.
Sanduku lilitolewa nje ya kaburi.
“ Fungueni tuangalie.” Aliongea mkuu wa kituo.
Askari walifungua, ajabu, sanduku lilikuwa na maiti ya hans.
“ aaaaah!” nilistaajabu.
NAJUTA KUUTUNZA USICHANA WANGU -36
Ajabu, jeneza lilikuwa na maiti ya hans.
“ Hapana..hapana…haiwezekani…” Niliwaambia.
“ Utakuwa kichaa kweli! Haiwezakani nini? Maiti ya marehemu mumeo si hii hapa. Kitu gani ambacho hakiwezekani?” Aliniuliza .
“ Hans nimekutana naye. Nimemuona kwa macho yangu. Tena hadi kumshika nimeshika, na yeye mwenyewe kanithibitishia hajafa. Huu mwili sio wake.” Niliwaambia.
“ Inawezekana labda sisi hatumjui vizuri hans, naomba vijana fanyeni taratibu muwalete ndugu wa Hans hapa.” Aliongea Mkuu wa kituo. Askari kadhaa waliniingia kwenye gari na kuondoka.
Walituacha eneo la makaburini, niliendelea kuwabishia kuwa yule sio hans.Pamoja na kuwabishia, nafsi yangu nayo ilianza kuingia mashaka. Nilihisi uenda mtu niliyemuona hakuwa Hans.
“ Au ni kweli yule mtu niliyekutana naye sio Hans? Hans alikuwa ananipenda sana, lakini yule mtu alikataa kunipenda. Alisema hanipendi na alinioa kwa ajili ya baba yake? Inawezekana yule sio hans?” Nilijiuliza.
“ Lakini kama huyu ni Hans, kwanini baba yake alikuwa hataki kufanya buriani, kwanini marehemu hakuagwa? Na kwanini nilipotaka kulifungua alikuja haraka kunizuia? kwanini pia hata mochwari wafanyakazi wengine waliondolewa siku ya kwenda kuuchukua mwili?” Nilijiuliza moyoni.
“ Kama ndugu zake watathibitisha huyu ni Hans itabidi tukupeleke Hospital, inawezekana ukawa unachanganyikiwa.” Aliongea Mkuu wa kituo. Sikumjibu, kiasi Fulani nilianza kuhisi uenda ni kweli nachanganyikiwa..
………………………
Nusu saa mbele, askari walioondoka walirudi wakiwa wameongozana na Baba Hans na mkewe. Baba Hans alikuwa na jeraha kichwani.
“ Hawa walitokaje mle ndani?” Nilijiuliza.
Walitusogelea, waliniangalia kwa jicho kali sana. Chuki ya wazi ilionekana machoni pao.
“ Mtafukuaje kaburi la mwanangu bila ruhusa yangu! Mimi ni mzazi wa huyu mtoto, hili kaburi ni mali yetu. Hata kama nyie ni polisi, ilibidi kwanza mtushirikishe.” Aliongea Baba Hans.
Mkuu wa kituo kwa busara sana, alimuomba Baba Hans samahani. Alimweleza jinsi jambo lenyewe lilivyokuwa la haraka. Baba Hans alitulia. Alimuuliza sababu ya kumwita pale.
“ Naomba niambie kama huu mwili ni mwili wa mwanao au lah?” Aliuliza Mkuu wa kituo.
“ Sasa kama sio wa mwanangu ni mwili wa nani? Mbona ipo wazi kabisa, huyu ni mwanangu.”
“ Nashukuru kwa majibu yako, nadhani kazi imeisha. Tulifanya hivi kutaka kuthibitisha maneno aliyokuwa anayongea huyu aliyekuwa mkamwana wenu. Alisema amemuona Hans kwa macho yake.”
“ Mmmmh! yaani na nyie mlimsikiliza Emma? Mbona huyu alishachanganyikiwa . Huyu inabidi apelekwe hospitali ya vichaaa, mtu aliyekufa atamuonaje? Labda alikuwa mzuka wake?” Aliongea baba Hans.
“ Nazani kesi imeisha.” Aliongea Mkuu wa kituo. Aliwataka vijana wafukie kaburi. Walilifukia na kulirudishia kama lilivyokuwa. Tuliondoa eneo lile. Kila mmoja alienda na njia yake, mimi nilirudi nyumbani, polisi walielekea kituoni.
Nikiwa nyumbani nilikumbuka kitu. Kuna kitu ambacho hakikuwa cha kawaida nilikiona kwenye maiti ya hans. “ Inawezekana vipi maiti iliyozikwa miezi kadhaa nyuma ikawa vile vile tu. Yaani hata kuoza kidogo hamna?” Nilijiuliza .
Kitendo cha maiti ya Hans kuwa kama maiti ya mtu aliyekufa jana kilinipa maswali zaidi. Nilihisi kuna kitu kisicho cha kawaida kinaendelea.
“ Hivi inachukua muda gani maiti kuoza?” Nilimuuliza Baba.
“ Siku chache sana, nazani ndani ya wiki moja mwili unakuwa umeshaoza na kuanza kunuka.” Alinijibu.
“ Sasa inawezekanaje mwili wa Hans uwe vile vile? Miezi zaidi ya sita mwili upo vile vile hata dalili za kuanza kuoza hamna?”
“ Mmmmh hio sio kawaida! Kuna kitu hakipo sawa.” Aliniambia baba.
“ Kwahiyo tunafanyaje?”
“ Chakufanya ni kuwaeleza polisi wasiwasi wako, Mkuu wa kituo wa sasa yuko makini sana. Tofauti na yule wa nyuma aliyekuwa anatumiwa na Baba Hans.” Aliniambia.
“ Itabidi nimfate ofisni kwake nikamweleze wasiwasi wangu.” Nilimwambia baba.
………………………………
Majira ya saa nane usiku, nilishtuka kitandani. Moyo wangu ulikuwa mzito sana. Nilijaribu kulala nilishindwa. Niliamua kukaa kitandani. Nikiwa nimekaa , gafla, alitokea mtu uvunguni, niliruka na kukimbilia mlangoni, kabla sijafungua mlango aliniwahi na kuniziba mdomo.
“ ..ni…a….cheee…….” Nilitamka kwa shida.