Kwa majina naitwa Rajabu Milinga,nina miaka 33, ni Baba wa familia. Mke wangu anaitwa Maimuna Rashidi, tunamtoto mmoja, jina lake Ashura. Wengi mtaani wamezoea kuniita baba Ashura,Tunaishi wilaya ya Songea ,kata ya Msamala, Mtaa wa Joshoni.
Hakika,Waliosema Dunia ina mambo hawakukosea, ndio, hawakukosea . Dunia inamambo, inamambo haswaaaaaa. Ungana nami mwanzo mwisho kwenye hiki kisa cha kweli, ujifunze na uelimike.
.........
SITASAHAU MAZIWA YA MKE WANGU YALIVYOLETA KIZAA ZAA SEHEMU YA 01.
Ilikuwa jumatatu, nilikuwa Hospitali, mbele ya mlango wa Wodi. Akili yangu haikuwa sawa, nilikuwa na hofu kubwa. Nilienda mbele na kurudi nyuma, niliingiza mikono mfukoni na kuitoa, nilishika kichwa na kukiacha. Kifupi sikutulia hata kidogo.
“ Atakuwa salama ….yaaaah!....atakuwa salama ……” Nilijiambia. Nilijipa moyo.
Gafla, mlango ulisukumwa, alitoka Daktari na Nesi, mikononi Nesi alimshika mtoto Mchanga.
“ Hongera, Mkeo kajifungua mtoto wa kiume” Nesi aliniambia.
“ Mke wangu yupo salama?’ Niliwauliza. Akili yangu ilimuwaza Mke wangu,usalama wake ulikuwa muhimu kuliko mtoto. Mtoto hakuwa akilini mwangu hata lepe.
“ Ndio, yupo salama, ingia ukamuone” Aliongea Daktari. Haraka, niliusukuma mlango wa wodi na kuingia, ajabu, hakukuwa na mtu ndani, kitanda kilikuwa kimetandikwa vizuri, hakuwepo Mama Ashura wala hakukuwa na dalili ya mtu kuzalishwa mle ndani.
“ Mmmmmh!” Niliguna.Nilitoka nje ,kwa mbali nilimuona yule Daktari akikata kona. Nilitimua mbio kumfata.
“..Doktaaa… Doktaaaa….” Nilimwita. Daktari aligeuka.
“ Vipi mbona mkuku mkuku? Umemuona mkeo?” Aliniuliza.
“ Ha..yu.po…..mle ndani hayupo…” Nilimwambia.
“ Acha masihara, hayupo kaenda wapi?” Daktari aliniuliza.
“ Sijui”
Alinishika mkono tukaelekea wodini.
“ Kwanza wewe umeingia wodi gani?”
“ Namba kumi na mbili ”
“ Kama ni hiyo sahihi, mkeo yupo mle ndani, kwanza ametoka kujifungua, bado nguvu za kutembea hana” Aliongea Daktari.
Tulifika. Dokta aliusukuma mlango, kwa pamoja tukaingia ndani.
“ Si unaona, hakuna mtu” Nilimwambia.
“ Aaaah! Hiki kitanda katandika nani? Na saa ngapi? Mbona mkeo alikuwa humu ndani, na kwenye sakafu kulikuwa na damu , Nani kazifuta?” Maswali mfululizo yalitoka kinywani mwa Daktari..
“ Mke wangu…mke wangu….Mama Ashura mke wangu…” Nilijikuta natamka.
“ Au tumechanganya chumba? Lakini hapana, chumba ni hiki hiki” Aliongea Daktari. Alitoa simu yake na kumpigia Mganga Mkuu. Alimpa taarifa ya kilichotokea. Dakika tatu mbele walinzi wa Hospital walifika, waliongozana na Mganga Mkuu.
“ Taaarifa yako imenishtua, hebu nifafanulie” Aliongea Mganga Mkuu.
Daktari alimuelezea tukio nzima.
“ Hapana, mnachokisema hakiwezekani, hii wodi inamlango mmoja tu, kama nyie mlipotoka mumewe aliingia, huyo mwanamke amepotea vipi?” Aliuliza Mganga Mkuu.
“ Ni kweli haiwezekani, ndio mana tumechanganyikiwa, mbaya zaidi tumekuta kitanda kimetandikwa, pia matone ya damu yaliyokuwa sakafuni hayapo” Aliongea Daktari.
“ Bado nashindwa kuamini” Aliongea Mganga Mkuu.
“ Na kama ametoka kuzaa, basi kuna mtu amemchukua. Kutembea mwenyewe mpaka nje haiwezekani” Aliongea Mganga Mkuu. Alitoa amri ya ulinzi kuimarishwa Hospital nzima.Tulianza kumtafuta, tulipita chumba kimoja hadi kingine, wodi moja hadi nyingine. tulipekua kila kona ya Hospitali bila mfanikio.
“Huyu mtu hayupo hapa, bila shaka atakuwa katoroshwa” Aliongea Mganga Mkuu.
“ Katoroshwa? Hapana, nani amtoreshe mke wangu? Hatuna adui sisi.” Niliwaambia.
“ Sasa kama hajatoroshwa yuko wapi?” Aliniuliza Mganga Mkuu.
“ Sijui..”
“ Kama haujui basi kubali ninachokuambia, mkeo katoroshwa.”
“Kwahiyo…mnanisaidiaje?” Niliwauliza.
“ Hakuna la kukusaidia zaidi ya kwenda kutoa taarifa polisi” Aliongea Mganga Mkuu.
………………..
Niliongozana na Mganga Mkuu kwenda Polisi.
Tulifika, tuliandika maelezo.
“ Mmmmh! Mbona tukio lenu linafanana na tukio lilitokea Hospital ya St Benjamini muda sio mrefu.” Aliongea Polisi.
“ Eeeh! Na huko Mama aliyejifungua kapotea?” Niliuliza.
“ Ndio, kapotea, tena maelezo yao yanafanana na yenu, kapotea kiutata kama ilivyokuwa kwenu. Tena naye amepotea baada ya kujifungua.” Aliongea Polisi.
Tuliangaliana na Mganga Mkuu kwa mshangao. Kabla hatujasema lolote, simu ya Mganga Mkuu iliita. Aliipokea na kuiweka sikioni. Akiwa anasikiliza, Sura yake ilibadilika.Taaarifa aliyopewa inaonekana haikuwa nzuri.
“ Kuna nini?” Nilimuuliza.
Hakujibu, alikata simu,alionekana kuishiwa nguvu. Alichuchumaa chini.Alijishika kichwa kwa mikono miwili. “ Mmmmmmh!” Aliguna.
“ Umeambiwa nini?” Askari alimuuliza.
Alitoa macho kutuangalia bila kusema lolote.
SITASAHAU MAZIWA YA MKE WANGU YALIPOZUA KIZAZAA SEHEMU YA 02.
Askari alizunguka kutoka kaunta. Alimshika mabega na kumtikisa.
“ Doktaa….Dokta…” Alimwita. Mganga Mkuu hakujibu kitu. Alikuwa mbali kwa mawazo. Askari alizidi kumtikisa. “ Oyaaaaa….oyaaaaaaa….” Alimwita.
“ Hiii dunia hiiii……acha tu” Mganga Mkuu aliongea.
“ Umeambiwa nini?” Nilimuuliza.
“ ..Mama mwingine kapotea” Alituambia. Nilimwangalia kama mzuka, sikuelewa kamaanisha nini. “ Unasemaje?” Nilimuuliza.
“ Mama mwingine kapotea” Alituambia.
“ Naye amezaa kama hawa wengine waliyopotea?” Aliuliza Askari.
“ Ndio, naye kapotea mara baada ya kujifungua tu” Aliongea.
“ Mmmmmmh” Aliguna Askari. Binafsi, sikuamini nilichosikia.Nilihisi naota. “ huyu ni watatu sasa,wanapoteaje? Au kuna mtu kawachukua? Kama amewachukua yeye wakazi gani?” Nilijiuliza. “ Hapana, nitakuwa naota” Nilijiambia. Nilijishika kichwa na kukipiga piga.
“ Eeeeh! Tulieni, tulieni, naona wote mnataka kuchanganyikiwa. Nisubirini hapa hapa” Aliongea yule Askari na kuondoka.
“ Unauhakika mwingine tena kapotea?” Nilimuuliza Mganga Mkuu.
Mganga Mkuu alitikisa tu kichwa, alisimama, alienda mbele na kurudi nyuma. Alikaa kwenye Benchi , alisimama tena, alisogea Kaunta na kuegemea. “ Mmmmmh” Aliguna. Alitoka na kwenda kukaa kwenye Benchi. Hakukaa sana, alisimama na kunifata.
“ Hivi nini kinataka kutokea? Mbona sielewi?” Aliniuliza.
“ Mwenyewe sielewi, nahisi naota”
“ Lakini Baba Ashura! Hebu niambie ukweli. Mkeo hakukuambia lolote ambalo linaweza kutusaidia?”
“ Hakuniambia.”
“ Usiseme hakukuambia kwa here, tafadhali jaribu kukumbuka nyakati za mwisho. Ukute kuna maneno alikuambia” Aliniambia.Nilijaribu kukumbuka. Kila nilipovuta kumbukumbu za nyuma niliona giza. Hakuna lolote la maana nililolikumbuka.
“ Naumiza kichwa bila sababu, hakuna lolote ninalo kumbuka” Nilimwambia.
Yule Askari aliyeondoka alikuja,aliongozana na mwenzake, bila shaka alikuwa Mkuu wa kituo. Walisogea mpaka tulipo. “ Taarifa zenu zinaogofya na kuchanganya sana, twendeni tukashuhudie wenyewe” Aliongea Mkuu wa Kituo.
Tuliongozana mpaka nje ya kituo. Tuliingia kwenye gari na safari ya kuelekea Hospitali ilianza. Njia nzima, akili yangu ilikuwa inaniambia naota. Muda wote nilikuwa najifinya ili niweze kuzinduka, lakini Sikuzinduka mpaka tunafika Hospitali. Hii ilinithibitishia sikuwa naota.
…………………………
“ Kuna nini kingine kimetokea hapa” Mkuu wa kituo alimuuliza Daktari aliyetupokea. Alikuwa ni yule aliyemzalisha Mke wangu, Dokta Komba.
“ Mama mwingine amepotea baada ya kujifungua” Aliongea Dokta Komba.
“Nyie ni wazembe, mmeruhusi vipi apotee” Alifoka Mganga Mkuu.
“ Ukali na hasira hazitatusaidia ,punguza hasira ili Daktari wako atueleze vizuri” Aliongea Mkuu wa kituo. Dokta Komba alipewa nafasi ya kueleza, alieleza kila kitu kama kilivyotokea.
“ Maelezo yako hayana tofauti na tukio la kupotea Mama Ashura, pia hayana tofauti na tukio lilitokea St Benjamin” Aliongea Mkuu wa kituo. Alichukua simu yake na kusogea pembeni. Alipiga na kuongea . Baada ya dakika kadhaa alirudi tulipokuwa tumesimama.
“ Kwa maelezo yenu, bila shaka mtu anayetekeleza haya matukio ni mmoja, na bila shaka alijipanga kwa muda mrefu. Nimempigia Mkuu wangu wa kazi, naye amempigia mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ambaye ni Mkuu wa wilaya.Muda wowote kuanzia sasa watafika, sasa wakati tunawasubiri, naomba nikague eneo la Hospitali vizuri” Aliongea Mkuu wa kituo.
“ Lakini Mkuu, kwanini mtu awaibe au kuwatorosha wanawake waliotoka kujifungua? Yeye wa nini?” Nilimuuliza.
“ Dunia inamengi sana, tutajua baada ya kuchunguza” Aliongea. Alimpa ishara Mganga Mkuu aongoze njia,aliongoza.Tukiwa hatujafika popote, Mkuu wa wilaya alifika akiongozana na viongozi wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama. Walipokelewa na kupewa maelezo ya matukio yote.
“ Wakati vyombo vya ulinzi vinaendelea na uchunguzi, naomba Madaktari mtulie na muendelee na kazi yenu kama kawaida.” Aliongea Mkuu wa Wilaya.
“ Pia nawaomba jeshi la polisi muimarishe ulinzi kwenye hii Hospital na ile ya St Benjamin, wodi zote za wajawazito zilindwe na askari muda wote. Ulinzi uwe mkali .” Aliongea Mkuu wa wilaya. OCD alitikisa kichwa kukubaliana naye.
Walinipa Pole, waliniomba nitulie na kuahidi mke wangu kupatikana. Hawakuchukua muda mrefu wakaondoka. Nikiwa na mawazo mengi, niliondoka kuelekea nyumbani .
“ Labda atakuwa nyumbani” Nilijiambia.
Nilifika Nyumbani, sikumkuta , nilimkuta mwanangu Ashura akiwa anatazama Tv. “ Mama Yuko wapi?” Aliniuliza.
“ Yupo Hospital, atakuja baada ya kupona ” Nilimdanganya.
Nilijaribu kuchangamka ili kutoonesha tofauti yoyote. Sikutaka Ashura ajue mama yake kapotea katika mazingira tata. Nilipika chakula tukala. Nilimsaidia kazi zake za shule . Nilimwandalia maji akaoga na kwenda kulala.
Niliingia chumbani kwangu kulala.
Nikiwa kitandani, usingizi ulinipitia kushoto, Sikuwa na usingizi hata lepe. Nilijifunika shuka gubi gubi kuhamasisha usingizi lakini ilikuwa sifuri, sikupata usingizi. Usiku kucha, macho yangu yalitazama dari.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Majira ya saa tisa usiku, dirisha la chumba changu liligongwa. Nilikurupuka kitandani, niliinama uvunguni na kuchukua panga.Nilisogea na kujibanza pembeni ya dirisha. “ Akivunja dirisha namuuwa hapa hapa.” Nilijiambia. Akili yangu iliniambia ni mwizi.
“ Baba Ashuraa…Baba Ashura…..” Sauti ilisikika dirishani.
“ Mmmh! Mwizi gani ananiita jina? Au sio wezi?, wakina nani sasa? Au ni watu waliompoteza mke wangu?” Nilijiuliza. Nikiwa najiuliza na kujaribu kuikumbuka ile sauti kama naijua, yalisikika maneno yaliyoniacha mdomo wazi.
“ Baba Ashura amka tuzungumze kuhusu mkeo” Ilisikika sauti kutoka dirishani.
SITASAHAU JINSI MAZIWA YA MKE WANGU YALIVYOZUA KIZAAZAA- 03
Wakati mdomo wangu ukiwa wazi kwa mshangao, maswali mfululizo yalikuja kichwani kwangu. “ Kujadili habari za mke wangu? Usiku huu?” Atakuwa nani huyu? Ni polisi? Hapana , haiwezekani, sio polisi. Hawa ni watu waliomtorosha mke wangu.”Nilijiambia.
“ Nifanyeje sasa?” Nilijiuliza.” Hakuna chakufanya zaidi ya kupambana nao” Niliwaza. Nililishika panga vizuri na kuuliza.
“Wewe ni nani?”
“ Toka nje tuongee, utanijua baada ya kuniona” Aliniambia. Niliwaza na kuwazua.Upande mmoja wa nafsi yangu ulikubali na mwingine ulikataa. “ Vipi kama wanataka kukuchukua na wewe? Mwanao Ashura ataishi vipi?” upande mmoja wa nafsi yangu uliniuliza.
“ Acha uwoga, ni vyema ukatoka kuwasikiliza. Huwezi kuwajua kama hautatoka nje” Upande mwingine wa nafsi yangu uliniambia.Niliamua kuusikiliza upande huu. Niliamua kutoka nje. Nikiwa mlangoni, niliwasha tochi na kumulika nje. Kwa tahadhari kubwa nikawa nasogea upande aliokuwepo.
“ Mmmmh!” Niliguna baada ya kuwaona wakiwa wawili.
“ Huu ujasiri wangu unaweza kuniponza, kama ni swala la kupotea mke wangu kwanini hawakuja mchana? Kwanini waje saa tisa usiku?” Nilijiuliza. Ni kama walijua ninachokiwaza, walinisogelea.
“ Punguza woga Baba Ashura, sisi ni wenzako, na sisi tumepotelewa na wake zetu kama wewe” Aliongea mmoja wao huku wakija nilipo. “ Mmmmh! Hata kama na wao wamepotelewa na wake zao, kwanini waje saa tisa usiku? Kwanini hawakuja mchana?” Nilijiuliza. Ni kama walijua nilichokuwa najiuliza.
“ Najua unaweza kuwa na maswali mengi sana kwasababu tumekuja usiku.Tusamehe kwa hilo, samahani sana” Waliniambia.
“ Bila samahani ,Lakini ……” Nilitaka kuongea nikasita.
“ Lakini nini?” Waliniuliza.
“Nawaamini vipi kama na nyie wake zenu wamepotea hospitali?” Niliwauliza.
“ Hakuna namna,yakupasa utuamini.”Waliniambia.Sikuwa na jinsi zaidi ya kukaa kwa tahadhari. Niliamua kuwasikiliza. “ Tumefika hapa ili tuongee hatma ya wake zetu. Ila kabla ya kuongea lolote,naomba tujuane kwanza. Mimi naitwa Husein, jina nililozoeleka mtaani ni Baba Hans.” Aliambia aliyekuwa mbele yangu, bila shaka ndiye aliyeniita dirishani.
“ Na mimi naitwa Hamadi, jina nililozoeleka mtaaani ni baba Saida” Alijitambulisha yule mwingine.
“Naitwa Rajabu Milinga, ila jina maarufu ni Baba Ashura kama ambavyo mliniita dirishani” Niliwaambia huku nikiwatazama kwa tahadhari, bado sikuwaamini kabisa. Miguu yangu niliiweka katika utayari wa kutimua mbio.Nilipanga pale nitakapoona dalili isiyonjema, basi nitimue mbio.
Baaada ya wote kujitambulisha, yule aliyejitambulisha kama Baba Hans,alinitazama na kuongea. “ Kama tulivyokuambia Baba Ashura, tumefika tujadiliane Hatma ya wake zetu, tungekutana Asubuhi, lakini kiukweli wenzako usingizi hatukupata kabisa, hivyo tukaona usiku huu huu tukutane .”
“Baaada ya utambulisho huu bila shaka wote mtakuwa mmegundua kitu, ila kabla sijasema nilichogundua mimi. Naomba kwanza tumchague kiongozi, ambaye ataongoza hiki kikao na pia atatusaidia katika kuwapata wake zetu” Aliongea yule mwingine, ambaye alijitambulisha kama Baba Saida.
“ Sidhani kama kuna haja ya kupoteza muda katika hilo, nadhani Baba Hans hapa anatufaa sana” Niliwaambia.
“ Ni kweli hata mimi nilitaka kusema hivyo hivyo” Aliongea Baba Saida.
“ Kama wote mmeridhia sina shida” Alituambia Baba Hans. Alitutazama kisha akaendelea. “ Lengo la kuja hapa ni kujadili tunafanyaje kuwapata wake zetu. Mpaka sasa jitihada za polisi kiukweli hazifurahishi hata kidogo. Polisi wamekuwa wasanii sana” Aliongea Baba Hans.
“ Ni kweli, nakubaliana na wewe. Yaaani toka tukio litokeee sioni jitihada zozote za Polisi” Aliongea Baba Saida.
“ Kutokana na Polisi kuwa wasanii,nawaomba kwa pamoja tuanze kuwatafuta wake zetu wenyewe. Tuachane na habari za polisi.” Aliongea Baba Hans.
Wote tulikubalina na wazo la Baba Hans.Muda ulivyokuwa unaenda, nilijikuta nawaamini.Mawazo ya kukimbia nitakapoona dalili mbaya yalipotea. Nilijikuta naongea nao kama watu ninaowajua kwa muda mrefu.
“ Kwakuwa wote tumekubaliana, naomba wote tuanze kuumiza kichwa na kudadavua kila kitu kinachohusiana na kupotea wake zetu.” Aliongea Baba Hans.
“ Lakini tulipojitambulisha Baba Saida alisema kuna kitu amegundua, naomba atuambe ili tujue tunaanzia wapi?” Niliwaambia.
“ Nilichogundua ni hiki, katika utambulisho wetu ,kila mmoja wetu amesema anaitwa baba flani. Hii maana yake anamtoto mwingine” Aliongea baba Saida. Alitutazama , Sura zetu zilionesha bado tulikuwa njia panda.
“ Hii maana yake wanawake wote walipotea ni wale ambao walishazaa mara moja tayari. Kwenye mzao wao wa pili ndio wamepotea” Aliongea Baba Saida. Wote tulitikisa kichwa kukubaliana naye.
“ Ni kweli..” Nilimwambia.
“ Lakini hilo peke yake haliwezi kutusaidia kuwapata wake zetu, ili kazi iwe rahisi naomba kila mmoja wetu atupe taarifa za mkewe . Yaani kazaliwa wapi? Kasoma wapi? Rafiki zake ni wakina nani? Wazazi wake , ndugu zake, kiujumla ni taarifa zote kumuhusu Mkeo” Aliongea Baba Hans.
“ Kama ni taarifa zote, naomba tupe nafasi ya kuziandaaa, kila mmoja wetu atoke aende kuzitafuta. Kesho jioni tukutane tukiwa na hizo taarifa” Nilimwambia..
“ Ni sahihi” Alijibu Baba Saida. Tulipanga sehemu ya kukutana siku ya pili.Waliniaga , wakiwa wanaondoka niliwasindikiza kwa macho. Jinsi walivyokuwa wanatembea, na jinsi walivyokuwa wanaongea, walionekana wanajuana , tena ni marafiki.
“ Hawa ni marafiki? Ilikuwaje wake zao wakajifungua siku moja? Au mimba waliwapa siku moja?” Nilijiuliza. Urafiki wao ulianza kunipa mashaka.
“ au ni waongo, wake zao hawajapotea” Nilijiuliza huku nikiingia ndani.
…………………..
Siku ya pili. Kabla hatujakutana. Niliamua kuwachunguza wenzangu. Nilienda kwenye nyumba walizoniambia wanaishi , niliwadadisi majirani zao.Baada ya kuwadadisi sana, niligundua mambo mawili. Moja , niligundua ni kweli wake zao walipotea siku ile hospitali, na mbili niligundua walikuwa marafiki wakubwa sana.Urafiki wao mkubwa ulinipa maswali yasiyokuwa na majibu.
Mida ya jioni, nilienda eneo tulilopanga kukutana. Wote tulifika. Kila mmoja aliwasilisha taarifa kumuhusu mkewe. Baada ya kuzichambua.Nilibaki mdomo wazi. “ Mmmmh! Hivi ni macho yangu au? Mbona ni ajabu sana?’
“ Umeona nini baba Ashura?” Aliniuliza baba Hans
“ Tazameni hapa” Niliwaambia .
“ Eeeeeeeh!” Walistaajabu.