MTUNZI: Saad Salum Mzola.
MWANDISHI: Saad Salum Mzola.
SIMU: 0716-197066.
NIMEKOSEA NAMBA SEHEMU YA 01.
UTANGULIZI:
Hivi hujawahi kukosea namba? Yaani namaanisha unataka kumpigia simu mtu fulani badala yake anapokea mtu mwingine kabisa tofauti na matarajio yako? Kama hujawahi, basi suala hili ni la kawaida sana katika mitandao. Na hii hutokea pale unapokosea namba moja ama zaidi ya moja, hivyo simu itaenda kwa mtu mwingine. Unaweza ukajiuliza kwa nini nimesema hivi? Ungana na mimi katika simulizi hii tamu sana ili kujua.
SONGA NAYO:
Kwa nini unanifanyia hivyo? Yaani kukupenda kote malipo yangu ni hayo? Huo ulikuwa ni ujumbe mfupi wa maneno kutoka katika namba ngeni kabisa uliongia katika simu ya kijana mmoja aitwaye Chibe. Hivi unamjua Chibe? Huyu ni mshikaji mmoja hivi machachari sana katika kutunga simulizi na hadithi tamu mitandaoni. Huyu jamaa hutunga simulizi nzuri sana kiasi cha kufanya simulizi zake kupendwa na watu wengi sana. Ujumbe huu mfupi ulimshtua sana kwani hakujua ni nani aliyeutuma? Alikuwa anajiuliza maswali mwenyewe bila kupata majibu. Ndio, alikuwa hajui kabisa kinachoendelea.
Unajua nini? Kipindi hiko Chibe alitoka kuachana na mpenzi wake wa siku nyingi sana aitwaye Edina. Hivyo hakutegemea kabisa kupata ujumbe kama ule kwa kuwa alikuwa hana mpenzi kwa kipindi kile. Wakati ujumbe huu unaingia katika simu yake, Chibe alikuwa anaandika simulizi moja iitwayo "PIGO LA KIGAIDI" Ni simulizi iliowafanya wasomaji wengi sana kumwaga machozi. Huwezi kusoma hadithi hii bila ya kuwa na kitambaa mkononi kwa ajili ya kufuta machozi. Kama hukuwahi kuisoma, nakushauri itafute. Ni simulizi iliyojaa simanzi na majonzi. Tuachane na hayo, Ujumbe ule haukumfanya asitishe zoezi lake, yeye aliendelea tu kuandika simulizi ile. Mara ukaingia ujumbe mwingine mfupi wa maneno. Na huu ulisomeka hivi:
"Ukimya wako ni maumivu kwangu"
"Hivi ni nani huyu aliyetuma ujumbe huu?
Chibe alijiuliza sana, lakini alikosa majibu.
"Bila shaka atakuwa amekosea namba. Alikuwa anawaza kichwani kwake"
Ndipo alipoamua kuchukua simu yake ya mkononi na kupiga namba ile. Mara namba ile ikapokelewa na binti mmoja mwenye sauti nyororo utadhani mtoto mdogo. Ndio, ni ile sauti ya kumtoa nyoka pangoni. Sauti yenye mvuto wa kimapenzi. Ni sauti ya kuombea mkopo benki. Sauti ile ilipenya katika ngoma za masikio ya Chibe. Asikwambie mtu bwana, kuna wanawake wamejaaliwa sauti. Yaani unaweza kuhisi ni Malaika.
"Hallow, nani mwenzangu? Ni muda mfupi tu umenitumia ujumbe mfupi"
Chibe alimuuliza yule binti.
"Jamani mpenzi, ina maana umeamua kufuta na namba yangu ya simu?
Ilisikika ile sauti nyororo ikisema.
"Kwani wewe ni nani? Mbona mimi sikujui? Chibe alimuuliza swali yule binti"
"Mimi ni yule mpenzi wako wa siku nyingi sana. Kwa jina naitwa Sofia"
"Utakuwa umekosea namba. Hivi unajua unaongea na nani? Chibe alimuuliza"
"Najua..! Hivi kwa nini umekuwa msaliti?
Sofia alimuuliza swali Chibe. Ukweli ni kwamba Chibe alikuwa hamjui kabisa binti yule. Katika historia yake ya mapenzi hakuwa kuwa binti mwenye jina kama lile.
"Sikiliza binti, nahisi utakuwa umekosea namba. Hebu jaribu kuitazama upya"
Hayo yalikuwa ni maneno ya Chibe. Baada ya kumwambia maneno yale, Chibe aliamua kukata simu na kuendelea kuandika ile simulizi yake.
Dakika mbili mbele, Sofia aliamua kupiga simu kwa Chibe. Safari hii haukuwa tena ujumbe mfupi wa maneno.
"Hallow, samahani sana kaka. Nimekosea namba. Alisikika yule binti akisema"
"Hakuna tatizo dada. Chibe alimjibu"
"Kama sauti tu iko hivi, sijui yeye mwenyewe atakuaje? Chibe alijiuliza"
Akiwa katika tafakuri nzito, mara ukaingia ujumbe mwingine mfupi wa maneno.
"Samahani kaka. Tunaweza tukawa marafiki? Ujumbe ulisomeka hivyo"
"Ni urafiki gani huo? Chibe alimuuliza"
"Ni urafiki wa kawaida tu. Kwa nini umeuliza hivyo? Yule binti aliuliza swali"
"Usijali, nilikuwa nataka tu kujua"
"Basi sawa. Alisikika Sofia akisema.
Ilikuwa hivyo yaani, baada ya muda mfupi Chibe alimaliza kuandika ile simulizi yake na kuituma mitandaoni. Simulizi ilikuwa imewashika watu pabaya, maana kila mtu alikuwa anamwaga machozi kutokana na ile simulizi. Ni simulizi inayosikitisha sana na kutia majonzi. Huwezi kuisoma simulizi hii bila ya kuwa na kitambaa cha kufutia machozi mkononi maana inaumiza sana. Wakati huo Chibe alikuwa anajaribu kufuatilia maoni ya watu wanaosoma simulizi ile. Mara akakutana na komenti ya binti mmoja aitwaye Sofia. Komenti yake ilisomeka hivi.
"Hiki ndicho kitu ninachokupendea kaka Chibe. Yaani simulizi zako ni tamu?
Chibe alianza kujiuliza maswali mwenyewe bila kupata majibu.
"Hivi, huyu ni Sofia yule ambaye nimetoka kuzungumza nae hivi punde?
Maswali yake yalikosa majibu. Akiwa anaendelea kufuatilia maoni ya wasomaji wake, mara ukaingia ujumbe mwingine. Hakuwa mtu mwingine bali ni yule yule binti aitwaye Sofia. Aliandika hivi,
"Kaka tuchart, ndio. Ulikuwa hivyo yaani"
Kabla Chibe hajajibu ujumbe ule alianza kuhisi jambo. Akaamua kuingia katika akaunti ya yule binti aitwaye Sofia na kuanza kutazama picha zake. Wakati huo alikuwa hajui wala hana uhakika kwamba meseji zile zilikuwa zinatumwa na yule binti anayezitazama picha zake kwa kipindi kile. Naam, kama kweli alikuwa ni yeye basi Mwenyezi apewe sifa zake. Ndio, maana kama kuumbwa basi Mwenyezi Mungu aliifanya kazi hii akiwa katika utulivu wa hali ya juu sana. Asikwambie mtu bwana, Sofia ni msichana mrembo sana kupita maelezo. Nashindwa hata kumfananisha na mtu mwingine maana hakuna kama yeye hapa duniani. Ninaposema hivyo, ujue namaanisha. Ndio, hakuna kama yeye.
Ghafla breki za Chibe zilifeli baada ya kuona picha za yule binti. Bila kufanya ajizi aliamua kumjibu ule ujumbe wake.
"Nambie Sofia. Uko poa?
"Niko poa kabisa. Pande gani? Sofia alimuuliza swali yule kijana Chibe.
"Niko Dar-es-salaam. Chibe alimjibu"
"Dar-es-salaam ni kubwa sana. Unapatikana maeneo gani?
"Mimi niko Magomeni. Chibe alimjibu"
"Nafurahi kusikia hivyo. Je, unataka kujua mengi kuhusu mimi? Sofia alimuuliza"
"Itakuwa vizuri sana. Nae alimjibu"
"Mimi naishi Masaki jijini Dar-es-salaam"
"Ahsante sana. Sijui nikuulize swali?
Chibe alimuuliza yule binti Sofia.
"Bila shaka, wewe uliza tu. Alimjibu"
"Hivi, una akaunti ya facebook? Na kama unayo unatumia jina gani?
"Niko nayo. Natumia jina la Sofia Msodoki. Kwa nini umeuliza hivyo?
Mara ukimya ukachukua nafasi. Kumbe Chibe aliamua kuingia facebook na kufuatilia jina lile. Huwezi amini, kumbe ni yule binti mrembo sana aliyeandika comment katika ile simulizi ya "Pigo la kigaidi" Ni yule binti mrembo mwenye viwango vya kimataifa. Wakati anaendelea kumfuatilia, mara Sofia alinitumia ujumbe mwingine.
"Mbona uko kimya sana? Si ulitaka kujua kama nina akaunti ya facebook?
Chibe hakuweza kabisa kujibu ujumbe ule kwa alikuwa haamini kama ana chart na binti mrembo kama yule. Alijikuta amechanganyikiwa ghafla. Ndipo Sofia alipochukua simu yake ya mkononi na kuamua kumpiga.
"Hallow, mbona uko kimya sana?
"Daaah..! Hivi ni wewe kweli? Alisikika Chibe akimuuliza swali yule binti"
"Una maana gani kusema hivyo? Mbona nashindwa kukuelewa? Kwani umegundua nini? Sofia alimuuliza"
Unajua ni kitu gani kiliendelea? Hii si ya kukosa kabisa. Ni bonge la simulizi. Haijawahi kutokea kabisa. Najua una shauku ya kutaka kujua. Ungana na mimi katika sehemu ya pili ya simulizi hii tamu sana. Simulizi inakwenda kwa jina la "NIMEKOSEA NAMBA" Ili kupata simulizi hii tamu na nyingine nyingi usisahau ku-like page yangu inayokwenda kwa jina la Saad Salum Mzola-Chibe.
********** ENDELEA NA SEHEMU YA 02 YA SIMULIZI HII YA NIMEKOSEA NAMBA *********
NIMEKOSEA NAMBA SEHEMU YA 02.
"Aaaah, basi tu. Chibe alijibu kwa kifupi"
Ukweli ni kwamba Chibe alijikuta amepatwa na kigugumizi na kushindwa kabisa kusema chochote. Kichwani kwake alikuwa anawaza vitu vingi sana.
"Naona kama Mbuzi kafia kwa muuza supu vile, ni bahati ilioje kwangu"
"Nahisi kama kajileta mwenyewe vile"
"Huu ni wakati sasa wa kutupa ndoano yangu. Siku zote samaki hakiishi chombo"
Chibe alikuwa anawaza ni jinsi gani anaweza kumuingilia Sofia na kumweleza lile lililo moyoni mwake. Baada ya ukimya wa muda mrefu Sofia aliamua kupiga simu kwa Chibe.
"Hallow, nikuulize swali? Alimuuliza"
"Uliza tu Sofia. Nae alimjibu"
"Au unaona ni kero kuchart na mimi?
"Hapana Sofia. Mbona shwari tu"
"Kama ni hivyo, mbona uko kimya sana?
"Usijali, kimya kingi kina mshindo mkuu.
Alisikika Chibe akimwambia Sofia"
Waliendelea kuchart kwa muda mrefu sana, Chibe akajikuta anasitisha zoezi zima la kuendelea kuandika simulizi. Muda wote huo alikuwa ana chart tu.
"Nahisi kama nina usingizi. Tutaongea vizuri siku inayofuata. Sofia aliamua kumtumia Chibe ujumbe mfupi (sms)
"Kwa nini unanifanyia hivyo Sofia?
"Hapana bwana, nimechoka sana my"
"Okay, sio kesi. Kwa hiyo unaniachaje?
Sofia aliamua kumtumia Chibe picha moja nzuri sana. Hakika Sofia alijuwa kumtega Chibe. Yaani hiyo picha ilikuwa ni balaa, mtoto kaumbika hasa. Huko nyuma sasa, utadhani anachambia hamira. Chibe akajikuta yuko hoi bin taaban. Jicho lilimtoka utadhani anachambua mchele. Alijisemea moyoni.
"Kumkosa binti kama huyu ni kesi ya jinai"
"Nitahakikisha anakuwa chini ya himaya yangu. Liwe jua ama mvua kitaeleweka"
Chibe aliamua kuchukua simu yake na kumpigia Sofia. Alitaka tu kusikia japo sauti yake ili aweze kulala unono.
"Namba unayopiga kwa sasa haipatikani"
Ndio, kumbe muda huo Sofia aliamua kupanda kitandani na kulala.
"Daaah..! Usiku wa leo utakuwa mrefu sana kwangu. Maana si kadhia hii"
Ilimchukua Chibe muda mrefu sana kupata usingizi maana muda wote alikuwa anaweweseka tu. Mara ikafika saa sita za usiku. Ndipo alipoamua kupanda kitandani kwake tayari kwa kulala. Ni kama alikuwa anamuona vile. Pale pale ukaingia ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwa Sofia.
"Ukilala lala salama, kumbatia picha yangu. Ujumbe ulikuwa unasomeka hivi"
Ghafla Chibe akajikuta usingizi unakatika. Aliamka ghafla na kuanza kuusoma ule uje tena kwa kurudia rudia. Alikuwa katika wakati mgumu sana.
"Ukisikia majaribu ndio haya. Sio bure huyu binti kuna kitu ananitafuta"
Chibe alijisemea mwenyewe moyoni. Hakuweza kabisa kuujibu ule ujumbe wake kwa kuwa alikuwa anaweweseka tu.
"Hakuna namna, kesho nitaanza na yeye. Ni lazima nijue kinachoendelea"
Chibe alikuwa anawaza kichwani kwake. Kwa kuwa ilikuwa ni usiku sana, Chibe aliamua kulala. Ilimchukua muda mrefu sana kupata usingizi. Hatimaye alifanikiwa kupata usingizi. Kwa kuwa alikuwa amechoka sana usiku wa jana yake, Chibe alijikuta anapitiwa na usingizi mpaka inafika saa moja asubuhi. Alishtuka kutoka usingizi baada ya kuingia ujumbe mfupi wa maneno katika simu yake, alianza kujiuliza maswali.
"Ni nani tena huyu? Anataka nini?
Akachukua simu yake na kuanza kuusoma ule ujumbe mfupi wa maneno. Kumbe ujumbe ule ulitumwa na Sofia.
"Umeamka salama? Ulisomeka hivi"
"Niko poa tu. Nilitaka kujua hali yako"
"Njema tu. Nambie Sofia. Alimjibu"
"Namshukuru Mungu. Ahsante sana Sofia. Chibe aliamua kumjibu"
"Basi sawa, nakutakia siku njema Chibe"
Sofia alimaliza kwa kusema vile.
"Nawe pia. Chibe alimjibu"
"Yaani huyu binti asubuhi yote hii ameanza kuichanganya akili yangu"
"Ni muda mfupi sana tangu niachane na Edina, nahisi kama nimepata mfariji"
"Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuonana nae. Hakuna namna"
Hayo yalikuwa ni mawazo ya Chibe. Kichwani kwake alikuwa anawaza ni jinsi gani anaweza kuonana na yule binti aitwaye Sofia. Ndani ya muda mfupi alikuwa amemshika pabaya. Baada ya kumaliza kufanya kazi zake za siku ile, Chibe aliamua kuchukua simu yake ya mkononi na kumpigia simu Sofia.
"Hallow, nambie. Uko poa?
"Niko poa Chibe. Umeshindaje?
"Njema tu, sijui wewe?
"Mimi niko poa tu. Alisikika akisema"
Sauti ya Sofia ilizidi kumchanganya Chibe, ilisikika kama mtu mwenye ugonjwa wa mafua. Ndio, ni kama alikuwa anaongea kwa kubana ile pua yake. Ni hatari sana huyu binti.
"Samahani sana Sofia, tunaweza kuonana? Chibe alimuuliza swali"
"Daaah...! Itakuwa ngumu sana Chibe"
"Kwa nini unasema hivyo Sofia?
"Niko chini ya himaya ya wazazi. Hivi hujui kama mimi ni mtoto wa geti kali?
"Hapana Sofia, mimi sijui. Alimjibu"
"Ndio hivyo, hata mimi napenda sana
kuonana na wewe. Tatizo sina muda"
"Basi sawa. Nikwambie kitu Sofia?
"Nambie tu Chibe. Mimi nakusikiliza"
"Nitakuwa katika wakati mgumu sana iwapo sitakutia machoni. Alimwambia"
"Jamani Chibe, unasemaje wewe?
"Ndio hivyo tena Sofia. We acha tu"
"Kunitia machoni hiyo veepe? Kuna usalama kweli. Sofia alimuuliza Chibe"
"Ndio. Namaanisha kuonana wewe"
"Anhaa..! Kumbe kuniona? Ujue mawazo yangu yalienda mbali sana. Alisema"
"Kwani wewe ulidhani nini? Chibe aliamua kumuuliza swali yule binti Sofia"
"Daaah..! Nilikuwa nawaza ujinga tu"
Chibe alicheka sana baada ya kusikia maneno yale. Kumbe Sofia alikuwa na mawazo mengi kabisa. Ama kweli kiswahili ni kijana sana, neno moja linaweza kuwa na maana nyingi sana.
"Sikiliza Chibe, mimi nitafanya kitu kwa ajili yako. Sipendi kuona ukiumia"
"Unasema kweli Sofia?
"Hivyo yaani, huwezi amini Chibe"
"Basi sawa, nakusikiliza wewe Sofia"
"Okay, lakini kuwa na subra maana natafuta sababu ya kutaka kutoka"
"Usijali Sofia. Mimi sina haraka kabisa"
Hayo yalikuwa ni mazungumzo kati ya Chibe na yule binti aitwaye Sofia. Masiku yalizidi kusonga huku Chibe akiendelea kuwasiliana na yule binti aitwaye Sofia. Lakini kulikuwa hakuna dalili yoyote ya Sofia kutaka kuonana na Chibe.
"Sikiliza Sofia, nimeanza kukata tamaa"
"Kwa nini iwe hivyo? Mbona umekosa subra? Naomba usiwe na wasi wasi"
"Hapana Sofia. Nimechoka kusubiri"
"Enheee..! Kuna wazo nimelipata. Nahisi hii itakuwa sababu ya mimi kutoka nyumbani. Hebu nipe muda kidogo"
"Bado unataka nikupe muda tena? Hivi Sofia uko serious kweli? Alimuuliza swali"
"Ni jioni ya leo tu nitakupa jibu"
"Unahisi litakuwa ni jibu zuri kwangu?
"Hivyo yaani. Nina imani hata wewe mwenyewe utafurahi sana. Niamini"
Ilipofika jioni, Sofia alimwambia Chibe kitu ambacho kilimfanya afurahie sana.
Je, ni kitu gani hiko? Kwa nini Chibe awe na furaha? Majibu ya haya maswali tutayapa kwenye kipande kijacho. Bila shaka una shauku ya kutaka kujua, ungana na mimi katika sehemu ya tatu ya simulizi hii tamu sana. Simulizi inakwenda kwa jina la "NIMEKOSEA NAMBA" Ili kupata simulizi hii tamu na nyingine nyingi usisahau ku-like page yangu inayokwenda kwa jina la Saad Salum Mzola-Chibe.
********** ENDELEA NA SEHEMU YA 03 YA SIMULIZI HII YA NIMEKOSEA NAMBA *********
NIMEKOSEA NAMBA SEHEMU YA 03.
Mchana wa siku ile ulionekana mrefu sana kwa Chibe. Alikuwa ana shauku kubwa sana ya kutaka kujua, ni kitu gani Sofia atamwambia? Kwa kifupi Chibe alijikuta kama mtumwa wa mapenzi kwa Sofia. Muda wote alikuwa anamuwaza yeye tu. Hivi, haya mapenzi ni kitu gani? Unajua nini? Kuna wakati mapenzi yanaweza kumfanya mtu kuonekana mjinga hata kama alikuwa na akili timamu. Na sio hivyo tu, mapenzi haya haya yanaweza kumfanya mtu mzima kuonekana kama mtoto mdogo.
Neno mapenzi ni neno lenye herufi chache lakini lina tafsiri kubwa sana. Akiwa katika tafakuri nzito, mida hiyo ilikuwa kama saa kumi na mbili za jioni hivi mara simu ya Chibe iliita.
"Hallow, Nambie Chibe. Ilikuwa ni simu kutoka kwa yule binti aitwaye Sofia"
"Poa tu Sofia. Haya nambie. Kuna jipya?
"Yeah..! Niko nalo. Hii inaweza ikawa ni taarifa njema sana kwako. Alimwambia"
"Waooh..! Ningependa kusikia hivyo"
"Siku ya kesho tunaweza kuonana pale Msasani Club? Alisikika Sofia akisema"
"Kwa nini isiwezekane? Niko tayari"
"Basi sawa. Naomba tuonane pale kwenye mida kama ya saa nane?
"Usijali Sofia, mimi nitakuwa pale mapema sana. Huwezi amini yaani"
"Kama ni hivyo itakuwa poa maana nitakuwa na muda mchache sana"
"Daaah..! Kwa nini iwe muda mchache?
"Nitakwambia kitu siku ya kesho. Nina imani tutapata muda mwingi sana wa kutosha katika siku zijazo. Usijali"
"Sio kesi, kitendo cha kuonana na wewe tu kitakuwa ni faraja kubwa sana kwangu"
"Basi sawa. Naomba kabla ya kulala jioni ya leo nitafute tuongee vizuri"
"Hakuna tatizo. Nitafanya hivyo Sofia"
Lile shinikizo la damu (presha) aliyokuwa nayo Chibe ilishuka kwa kiasi fulani baada ya kusikia taarifa zile njema kwake. Ndio, naweza kusema ni taarifa njema kwake. Kama kawaida, ilipofika kwenye mida kama ya saa tatu za usiku Chibe aliamua kumpigia simu Sofia. Waliongea mambo mengi sana, kwa kiasi fulani Chibe aliona kama kuna mwelekeo fulani hivi mbele yake japokuwa hawakuongea ya ndani zaidi.
Kama kawaida yake Chibe kuupata usingizi siku ile ilikuwa ni shida. Huyu jamaa huwaga ni mchovu sana kwa mabinti, historia inaonyesha kwenye mtihani wa mapenzi hakuwahi kufauru kabisa. Huwezi amini, sijui huwa anakwama wapi? Ilikuwa hivyo yaani. Wahenga wanasema, usiku wa deni hauchelewi kucha. Mara ikafika ile siku ambayo Chibe alikuwa na miadi ya kukutana na mtu wa ndoto yake aitwaye Sofia. Ni binti aliyekuwa anatembea na moyo wake japokuwa walikuwa hawajahi kuonana hata siku moja. Na sijui itakuaje baada ya kuonana nae? Ngoja tuone.
Asubuhi ya siku ile Chibe aliamka mapema sana. Alijitahidi kufanya kazi zake pale nyumbani kwa haraka sana ili asije akachelewa kwenda kwenye sehemu ya tukio. Huwezi amini, mpaka kufikia mpaka kwenye saa tatu asubuhi alikuwa ameshamaliza shughuli zake zote. Mara akaanza safari ya kuelekea Msasani Club ili kukutana na Sofia. Kijana Chibe si mgeni sana katika eneo lile kwani sio mara yake ya kwanza kufika. Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, mara akajikuta yuko katika eneo la tukio.
Alitafuta mahali pazuri sana na kukaa, dakika mbili mbele alikuja mhudumu ili kutaka kumhudumia. Ndio, alijua kabisa kuna kitu anahitaji kwa muda ule.
"Habari yako kaka, sijui nikusaidie nini?
"Niko poa tu. Naweza kupata maji ya Kilimanjaro? Alisikika akisema"
"Bila shaka, ni maji tu au kuna kitu kingine unahitaji? Mhudumu alimuuliza swali"
"Kwa sasa nipatie maji tu. Kama kuna kitu kingine nitakwambia baadae"
Yule binti mhudumu alienda mahali husika na kumletea maji ya kunywa. Muda huo Sofia alikuwa bado hajafika kabisa katika eneo la tukio. Na kuhusu wakati ilikuwa kama saa sita za mchana hivi. Akiwa katika lindi la mawazo kichwani kwake, mara akasikia simu yake inaita. Hakuwa mtu mwingine bali alikuwa ni Sofia. Ndio, ni yule ambaye alikuwa na miadi ya kuonana nae siku ile.
"Hallow Chibe, ndio natoka nyumbani. Nipe kama dakika kumi hivi nakuja"
"Usijali Sofia, Mimi nimefika tayari"
"Daaah..! Uko makini sana, napenda sana watu kama wewe. Uko vizuri sana"
"Naam, huwaga nazingatia sana muda"
Chibe alimjibu yule binti aitwaye Sofia. Ni kama alivyosema, ndani ya muda mfupi Sofia alifika pale Msasani Club. Muda huo Chibe alikuwa hajui kinachoendelea. Mara Sofia alichukua simu yake ya mkononi na kumpigia Chibe.
"Hallow Chibe, ndio nimefika hapa Msasani Club. Je, uko wapi?
Ilisikika sauti nyororo sana yenye mvuto wa kimapenzi kama sio huba kutoka kwa Sofia. Sauti yenye vionjo fulani hivi kwa kumpandisha mtu hisia za kimapenzi.
"Niko hapa karibu na kaunta. Nimevalia t-shirt nyeusi na kofia nyekundu"
"Ohooo..! Nimekuona. Haya nakuja"
"Mama yangu we..! Hakika huyu binti si wa mchezo mchezo kabisa. Yaani"
Unaambiwa Sofia alipigilia vitu hatari sana. Kila mtu pale Msasani Club alikuwa anamtupia jicho yeye. Achana na huo uzuri wake, gumzo lilikuwa huko nyuma utadhani kabeba furushi la mwizi. Nazungumzia yale makalio yake, utadhani mtoto haendi chooni. Alikuwa na kifurushi cha kutosha tu, bila shaka ni kile cha mitandao yote. Hivyo yaani. Kwa mwendo wake wa madaha kama mnyama Twiga akiwa katika mbuga ya wanyama ya Serengeti, alikuwa anaelekea mahali ambapo Chibe alikuwa amekaa. Unaambiwa huko nyuma ni mwendo wa Singida..! Dodoma..!
"Daaah..! Huyu binti avae dera ama kimini. Kwa hii rojo rojo yake ni noma"
Chibe alikuwa anajisemea mwenyewe moyoni. Hatari sana huyu mtu. Iwapo utakutana nae njiani anatembea, unaweza ukasema hawezi kufika mbali anaweza kujinyea kama sio kuangusha kipande kimoja cha tako. Asikwambie mtu bwana, Mwenyezi Mungu anajua kuumba. Si wanasema binadamu ameumbwa kwa udongo? Nina imani huyu Sofia wakati anaumbwa basi kulikuwa na kiasi fulani cha udongo kilibaki ambacho kisingeweza kuumba kiumbe chochote kile, hivyo Mwenyezi Mungu aliamua kumuwekea Sofia katika yale makalio yake. Hivyo yaani.
"Karibu sana Sofia. Ilisikika sauti yenye mikwaruzo kutoka kwa Chibe"
Mikwaruzo ile haikuwa ya kawaida kabisa. Yaani muda huo alikuwa anahema pasipokuwa na mpangalio. Joto la mwili wake lilikuwa liko juu sana, minara ya simu ilikuwa imesimama lakini network ilikuwa haifanyi kazi. Naam, asikwambie mtu bwana, Huyu binti ni kisanga.
"Ahsante sana Chibe, hivi ni wewe?
"Ni mimi Sofia. Haya nambie"
"Hata siamini macho yangu. Yaani kukutana na mtunzi mahiri wa simulizi"
"Unasema kweli Sofia? Mbona mimi ni mtu wa kawaida sana. Alimwambia"
"Nalijua hilo, lakini ilikuwa ni ndoto yangu kutaka kuonana na wewe. Huwezi amini"
"Okay, nami najisikia faraja sana kuonana na wewe. Ujue hata mimi siamini?
"Jamani Chibe..! Huamini nini sasa?
"Siamini kuonana na Sofia Msodoki. Uko vizuri sana wewe mtu. We acha tu"
"Mh..! Sina maajabu yoyote. Nashangaa unavyonimwagia hiyo misifa"
"Kaa chini basi Sofia. Utasimama hivyo mpaka muda gani? Chibe alimuuliza"
"Ujue mwenzio nimeishiwa pozi hivyo? Hivi Chibe una nini? Nashindwa kuelewa?
Hayo yalikuwa ni mazungumzo kati ya Chibe na yule binti aitwaye Sofia.
Mara akaja mhudumu mpaka mahali ambapo Chibe alikuwa amekaa na yule binti bomba sana aitwaye Sofia.
"Karibuni sana jamani, sijui niwahudumie nini? Alisikika yule binti akisema"
"Hebu msikilize kwanza huyu dada. Chibe alimwambia yule mhudumu.
"Enheee..! Nambie dada. Unataka nini?
"Jamani Chibe, si unichagulie tu kinywaji cha kunywa? Sofia alimwambia Chibe"
"Kutokana na rangi ya mwili wake, Hebu mpatie Fanta orange. Sijui itakufaa?
"Daaah..! Ulijuaje? Yaani hiki ndicho kinywaji ninachokipenda sana"
"Nilijua tu. Nina uzoefu mkubwa na watu kama nyinyi. Alisikika Chibe akisema"
"Unasemaje Chibe? Uzoefu huo umeipata wapi? Naanza kupatwa na mashaka"
"Hapana Sofia. Ni utani tu. Alimwambia"
"Nilitaka kushangaaa...! Alimjibu"
Baada ya mhudumu kumaliza kufanya kazi yake alitoweka katika eneo lile.
Mara ukafika wakati wa Chibe na Sofia kuanza mazungumzo yao muhimu.
Je, ni mazungumzo gani hayo? Kale kautamu ka hadithi hii kanaanzia hapa. Si unataka kujua? Basi ungana na mimi katika sehemu ya nne ya simulizi hii tamu sana. Ni simulizi ya mapenzi ambayo utaufurahia. Simulizi inakwenda kwa jina la "NIMEKOSEA NAMBA" Ili kupata simulizi hii tamu na nyingine nyingi usisahau ku-like page yangu inayokwenda kwa jina la Saad Salum Mzola-Chibe.
********** USIKOSE **********