Notification texts go here Contact Us Buy Now!

Baba Kiumbe Wa Ajabu sehemu ya 15

Simulizi: BABA KIUMBE CHA AJABU
EPISODE:15
ILIPOISHIA.
“Leo usiende, nenda keshokutwa ila kuna kitu kitatokea si cha kawaida, kuwa tayari kukabiliana nacho.”
“Kitu gani hicho?”
“Wee nenda, ila majibu utayapata kujua kinga niliyokukinga inafanya kazi kiasi gani.”
“Niambie ili nijue ikiwezekana nisiende.”
“Lazima uende ili kuwaumbua wabaya wako.”
“Mmh! Sawa.”
“Baada ya kesho kwenda rudi tumalizie tiba, kwa vile hawatakubali kuona umewashinda.”
“Sawa nimekuelewa.”
“Nilitaka kusahau kitu kimoja, leo usioge wala kukutana na mwanamke kimwili ikiwezekana leo kila mmoja alale chumba chake au kitanda chake.”
“Sawa nimekuelewa.”
“Ndoto utakayoiota ndilo jibu la safari yako.”
“Nashukuru kwa msaada wako.”
SASA ENDELEA KUSISIMKA KIVYAKOVYAKO.
Baada ya mazungumzo, tulirudi hoteli tuliyokuwa tumepanga kwa ajili ya mapumziko, siku ile sikukaa kutokana na kuwa na alama nyeusi za kuchanjwa na mganga.
Kwa vile hatukuruhusiwa kulala pamoja, tulichukua chumba cha vitanda viwili na kila mtu alilala kitanda chake. Usiku niliota ndoto nafukuzwa na kichaa mmoja ambaye katika kunifukuza aligongwa na gari, hapohapo nilishtuka usingizini na kujiuliza kichaa yule ni nani na ndoto ile inaashiria kitu gani.
Siku ya pili nilimueleza mpenzi wangu ambaye alinishauri heri nisiende nyumbani ili kuepusha nilichokiota.
“Masalu kama mganga alikuambia utakachokiota ndicho kitakachotokea, kwa nini uende?”
“Hilo wazo hata mimi nilikuwa nalo lakini mganga alisema lazima niende, ili nirudi na kupata dawa ya mwisho.”
“Kwa nini asikupe hiyo dawa?”
“Alisema lazima niende ili kuonesha uwezo wa kile alichokifanya jana.”
“Mmh! Mtihani mzito kweli.”
“Lakini kwetu hatuna kichaa.”
“Basi inawezekana utakutana naye njiani.”
“Kama ni hivyo bora nikodi gari mpaka mlangoni.”
“Bora ufanye hivyo.”
“Sawa, basi tuongozane, wewe uende kwenu najua wamekutafuta sana.”
“Hata wakinitafuta mimi mtu mzima, kuna mdogo wangu anajua kila kitu sidhani kama watasumbuka sana. Mbona tuliishasafiri zaidi ya wiki hakuna kilichoharibika?”
“Si uliaga?”
“Basi taarifa zangu watazipata kwa mdogo wangu na leo nikifika watapata jibu.”
“Mmh! Haya.”
Niliongozana na mpenzi wangu hadi kwao, nilimteresha na mimi kuendelea na safari yangu. Nilikwenda na gari hadi mlangoni na kuteremka, wote waliokuwepo walishtuka. Baba aliyekuwa amelazwa sebuleni aliponiona alipiga kelele.
“Mtoeni...mtoeni ataniua...ataniua.”
“Baba siwezi kukuua, utajiua mwenyewe,” nilimjibu baba.
“Jamani mtoeni ataniua,” baba alizidi kupiga kelele.
“Masalu hebu toka nje,” dada alinifokea.
Niligeuka kutoka nje, kaka yangu alikuja kwa nyuma na kunishika kisogoni, mara alianza kupiga kelele kama mtu aliyepagawa, akachukua jembe na kutaka kunipiga nalo, alinikosakosa mara mbili, nilipoona hatanii nilitimua mbio, alinikimbiza mpaka barabarani huku akidhamiria kuniumiza.
Ilinibidi nivuke barabara bila kuangalia baada ya kuona nakufa najiona, baada ya kuvuka nilisikia kishindo nyuma yangu na kelele za watu. Nilipogeuka nilimuona kaka yangu akiwa chini akivuja damu kichwani.
Japo ajali ile ilifanya moyo uume na kupatwa na huruma, lakini sikutaka kurudi kuangalia, wakati huo watu walikuwa wakijaa kwenye tukio la ajali na kumzunguka kaka. Nilikodi teksi iliyokuwa ikipita kuwahi nyumbani. Nilipofika nyumbani nilimpigia simu mpenzi wangu.
“Vipi Masalu mbona kama kuna tatizo?”
“Ndiyo.”
“Tatizo gani?”
“Si la kulizungumzia kwenye simu.”
“Upo wapi?”
“Nyumbani.”
“Nakuja sasa hivi.”
Baada ya kukata simu nilibaki nimejilaza kwenye kochi nilijiuliza vita nzito niliyoelezwa na mganga ndani ya familia yangu nini hatima yake. Nilijiuliza kaka yangu bila kugongwa na gari alitaka kunifanya nini. Au alikusudia kuniua?
Njozi ile baada ya kuuona ukweli nilijuliza nini kitafuata.
Niliamini kama vita ya nguvu za giza itashindikana basi watatumia nguvu za kawaida ili kunitokomeza duniani. Nilijiuliza kama itakuwa hivyo nitawezaje kuwaepuka? Nilipanga kuukimbia Mji wa Mwanza ili kuokoa maisha yangu kwa kuliuza duka langu.
Wazo lile nilitaka nishauriane na mwenzangu kabla ya kutoa uamuzi, nilipanga akija nitamgusia suala lile ambalo kwa upande wangu lilichukua sura mpya ya kutishia maisha yangu. Wakati nikiwa kwenye dimbwi la mawazo mpenzi wangu aliingia kwa hali aliyonikuta nayo ya kujilaza mikono kichwani ilimshtua sana.
“Vipi?”
“Masalu?”
“Mambo mazito.”
“Kivipi?”
Nilimueleza niliyokutana nayo nyumbani, alibakia mdomo wazi asiamini nilichomueleza.
“Sasa bila kugongwa na gari ingekuwaje?”
“Hata sijui.”
“Sasa kwa nini mganga hakukuambia?”
“Aniambie nini wakati aliniambia nitakayoyaota ndotoni ndiyo nitakutana nayo?”
“Sawa, lakini alitakiwa akupe tahadhari.”
“Mganga hawezi kukuambia kitu kijacho kabla ya kutokea ili usije sema uongo.”
“Pole sana mpenzi wangu sasa tutafanya nini?”
Mara simu yangu iliita nilipoangalia nilikuta ni dada, niliitazama bila kupokea kitu kilichomfanya mpenzi wangu kuuliza.
“Mbona hupokei ni nani?”
“Dada”
“Anataka nini si alikufukuza?”
“Hata mimi nashangaa.”
“Usipokee.”
Kweli sikuipokea, iliita mpaka ikakatika, baada ya kukatika haukupita muda iliita tena. Vilevile sikuipokea, ikaita mpaka ikakatika. Nilitaka kuizima lakini mpenzi wangu alikataa kwa kuniambia:
“Simu za ndugu zako usipokee, lakini zingine ziache ziingie.”
“Kutokana na vita hii nzito nilikuwa nimepanga kuuza duka langu niondoke Mwanza, ulikuwa na wazo gani?”
“Mmh! Ni haraka sana kwa nini tusirudi kwa mganga tumsikilize atasema nini?”
“Mganga kazi yake ni kunizindika ili nisidhurike na nguvu za wachawi, lakini si kuwazuia kunidhuru kwa silaha za kawaida.”
“Sawa, lakini kabla ya kufanya hayo tukamsikilize mganga, si alikuambia urudi.”
“Mmh! Kweli, kuna umuhimu wa kwenda muda huu.”
“Hakuna tatizo ni muda mzuri.”
Nilikubaliana na mwenzangu kurudi kwa mganga, tuliongozana hadi kwa mganga, tulimkuta akihudumia wagonjwa. Ilitupasa kusuburi kwa zaidi ya saa nne. Ilipofika zamu yangu niliingia kwa mganga, aliponiona alitabasamu na kusema:
“Umeona?”
“Ndiyo.”
“Sasa ule ndiyo ubaya uliokuwa umekuzunguka, bila kupitia hapa alipokushika ungeanguka chini na kupooza, kuanzia muda ule ungewekwa kwenye chumba chenye mwanga hafifu na hayo ndiyo yangekuwa maisha yako mpaka unakufa.”
“Mmh! Na kaka yangu aliyegongwa na gari hakufa?”
“Hakufa.”
“Atapona?”
“Atapona, lakini itachukua muda mrefu sana kupona, alipogongwa hakuumia. Lile halikuwa gari la ukweli kama ulivyodhania ni kinga yako mwilini hakuna wa kukuchezea. Atakayetaka kukuchezea atapatwa na mazito kuliko yaliyompata kaka yako.
“Kila tatizo litakalokutokea utaliota usingizini kabla ya kukutokea.”
“Kwa hilo nashukuru, lakini wakitumia silaha?”
“Zindiko nililokuwekea hawawezi kukudhuru kwa kitu chochote.”
“Nilikuwa na wazo la kuuza duka ili nitoroke.”
“Wala usiende popote, hakuna wa kukugusa, watakuogopa kama ukoma, ila inabidi duka lako lifanyiwe zindiko bila hivyo mali zako zote zitamomonyoka na kukufanya ubaki kuwa maskini wa kutupwa.”
“Na ndugu zangu?”
“Nao wana wakati mgumu, si muda mrefu watakuwa na maisha magumu, labda wahangaike tena la sivyo kwa kutegemea ndagu ya kidonda wataadhirika.”
“Kwa hiyo unataka kuniambia kaka hakupata ajali?”
“Hakupata ajali ila amepata kichaa baada ya kutaka kukudhuru na kumrudia mwenyewe.”
“Lile gari na watu waliokuja walitokea wapi?”
Kile ni kiini macho tu lakini ile ndiyo kinga inayokulinda, baada ya kumzuia ulipata nafasi ya kukimbia na kurudi kwako.”
“Na hali ya baba?”
“Mmh! Hali ya baba yako ndiyo hivyo imeshikiliwa na uhai wako, kubali uteseke baba yako apone.”
“Sipo tayari wacha afe, siwezi kuwaonea huruma tena ni watu wabaya wasionitakia mema.”
“Basi leo nitamalizia kazi yangu, ukitoka hapa fanya mambo yako bila hofu, atakayekugusa atapotea.”
Mganga baada ya kusema vile alichukua dawa nyeusi iliyokuwa kwenye chupa na kuichanganya na asali kisha alisema niachame mdomo, akanichanja kwenye ulimi na kunipaka dawa kwa kutumia simbi. Chale zingine alinichanja katikati ya utosi, kifuani na mgongoni na sehemu zote za maungio ya mwili kisha alinipa ruhusa ya kurudi nyumbani na kunipa masharti yaleyale ya kutolala na mwanamke kwa siku ile.
“Kijana kazi imekwisha, unaweza kuendelea na shughuli zako kama kawaida.”
“Asante, na kuhusu hali ya baba?”
“Yangu nimemaliza, utaamua mwenyewe.”
“Hawezi kupona tena?”
“Akipona ujue unakufa wewe.”
“Hata akipelekwa kwa mtaalamu mwingine?”
“Kwangu nimemaliza na kazi yangu naiamini haijawahi kutokea kama itatokea basi ujue ndiyo kifo chako.”
“Na asipopona?”
“Utakufa.”
“Sasa itakuwaje, ndugu si watajua mimi ndiye niliyemuua?”
“Kijana niondolee upumbavu, niambie unataka nifanye nini, ufe baba yako apone au afe baba yako wewe upone?” Mganga alikasirishwa na maswali yangu.
“Basi mzee nisamehe,” niliomba msamaha baada ya kuona nimemuudhi mganga.
“Sjawahi kuona mtu mpumbavu kama wewe, unanipotezea wakati wangu nakuomba uondoke,” mganga alikuja juu na kunifukuza.
“Samahani mzee wangu,” nilijikuta nikichanganyikiwa baada ya kumuudhi mamba kabla sijavuka mto.
“Samahani nini, nilikuita hapa nikutibu?”
“Hapana.”
“Nilikuomba nikusaidie?”
“Hapana.”
“Sasa kwa nini unanitia ujinga kwa kazi nzito niliyoifanya ya kuokoa maisha yako?”
“Nisamehe mzee wangu nipo chini ya miguu yako sitakuuliza tena swali lolote kuhusiana na familia yangu.”
“Kazi nimemaliza nipe changu kilichobaki kisha uende zako utaamua chochote kwenda kwa mganga yeyote akusaidie. Ila ukiondoa mguu wako hapa usije tena.”
“Mzee wangu najua nimekukosea naomba usifike huko,” nilizidi kumuomba msamaha mganga baada ya kubaini kosa langu.
“Lazima nifike nimekufafanulia mangapi yaliyotaka kukupata na leo umepata jibu bado unajitoa akili nikufanye nini? Wewe mtoto?”
“Hapana, nimekosa mzee wangu nipe adhabu yoyoye lakini usinikataze kuja hapa,” nilipiga magoti mbele ya mganga kuomba msamaha.
“Nimekuelewa kijana lakini usirudie tena kuingilia kazi za watu.”
“Nashukuru mzee wangu.”
******
Baada ya kusamehewa na mganga, tuliagana na kunieleza ninapotokewa na tatizo niende kwake bila tatizo. Baada ya kutoka pale sikutaka kurudi nyumbani ambako niliamini lazima ndugu zangu watanitafuta.
Kama kawaida tulirudi kwenye hoteli yetu tuliyolala jana yake, tulilala pale mpaka siku ya pili. Usiku wa siku ile mpenzi wangu alitaka kujua nini hatima ya maisha yangu baada ya kutoka kwa mganga.
“Mh, Masalu mganga amesemaje juu ya uamuzi wako wa kukimbia mji?”
“Amesema hakuna kitakachonitokea nikae hapahapa.”
“Na kuhusu ile ajali?”
“Anasema haikuwa ajali bali kinga aliyoniwekea ndiyo iliyonilinda nisidhuliwe na kaka.”
“Masalu! Unataka kuniambia kaka yako hakugongwa na gari?”
“Mganga ndivyo alivyonieleza.”
“Mmh! Makubwa, lakini mganga huyu kiboko, sifa zake ni kubwa.”
“Lakini alitaka kunitimua.”
“He! Kivipi?”
“Nilitaka kumuulizia hatima ya hali ya baba yangu.”
“Akakujibu nini?”
“Wewe, kumbe niliwasha moto wacha anifukuze kama mbwa aliyeiba mayai.”
“Ehe! Ikawaje?”
“Mmh! Ilibidi nimuombe msamaha huku ninalia.”
“Mkaishiaje?”
“Alinisamehe na kunionya nisirudie tena kuuliza maswali ya kijinga.”
“Lakini nawe umeyataka, unamuombea dhamana mtu uliyemfunga mwenyewe?”
“Pamoja na hayo, lakini yule ni mzazi wangu.”
“Haya sasa, chagua mzazi apone uumie wewe.”
“Japo inaniuma lakini kisu kimegusa mfupa, kungekuwa na njia mbadala nisingekubali kuona baba yangu anateseka kwa ajili yangu.”
“Lakini ningekuwa ni mimi nisingekuwa na huruma na mtu anayenitoa kafara kwa tamaa zake. Tena ningemuulia mbali hata kwa sumu.”
“Lakini kumbuka pamoja na yote ni mzazi wako.”
“Siwezi kumuonea huruma mzazi mwenye nia mbaya na mimi, akitaka kuniua nikigundua na mimi namfanyia kitu kibaya.”
“Lakini si kila baya lazima ulipe baya kuna lingine unatakiwa kulisamehe.”
“Kwa upande wako utasamehe vipi, ili kupona lazima mtu aumie, kibaya zaidi pamoja na yote waliyokufanyia bado wanataka kukupoteza kwenye sura ya dunia bado watu kama hao unawaonea huruma?”
“Kwa kweli nimechanganyikiwa.”
“Sikiliza Masalu, unapofanya kitu kibaya kisha ukaona huruma basi lazima litakurudia na halitapata tiba mpaka unakufa.”
“Wewe nani kakwambia?”
“Masalu mpaka nakupeleka kwa yule mganga nayajua mengi kwa hiyo jiepushe kukingia kifua unayoyafanya, bora ungeacha kabisa kuliko kuingilia kazi ya mganga hasa wakikusaidia katika matatizo yako.”
“Kwa hiyo nikiendelea kusikitika itakuwaje?”
“Usishangae ugonjwa wa baba yako ukakurudia.”
“Lakini sasa hivi si nimeachana nao.”
“Basi ndiyo hivyo, siku zote usioneshe huruma pale unapoamua kutenda jambo zito, huruma yako hugeuka sumu na kukurudia mwenyewe.”
“Nimekuelewa.”
Kwa vile muda ulikuwa umekwenda tulikubaliana tulale ili mengine tuzungumze kesho yake kwa vile bado tulipanga kuendelea kuwa pale kwa siku moja zaidi. Kila mtu alilala kitanda chake kama tulivyoelezwa na mganga, ilionesha wazi kabisa mpenzi wangu alikuwa akiumia kutokana na kumnyima haki yake ya msingi.
Lakini bado sikuwa tayari kumuua baba yangu kwa kulifanya tendo lile, hata hali aliyokuwa nayo ilitokana na kuyaokoa maisha yangu yaliyofikia hatua mbaya. Pia hakukuwa na njia mbadala ya kuweza mimi kupona bila baba yangu kuguswa.
Japo mpenzi wangu alionekana hana huruma na familia yangu na kuwa tayari kuiona inapotea baada ya kugundua walikuwa na mpango mbaya kwangu lakini nilijitahidi kutafuta njia ya kumueleza kwa makini ili anielewe, sikupenda hata siku moja kifo cha baba yangu kitokane na mimi kwa kufanya tendo la ndoa nikijua kabisa ndilo litalalomaliza uhai wake.
Je nini kitaendelea.

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.