TAXI DRIVER SEHEMU YA 19
Inamaana Roi baada ya kutoa kichapo, Kasa akaibuka na vijana wakasafisha nyumba na kuacha maiti kama zilivyo. Ngoma nzito.
"Mbona mapema hivi inamaana huyo mtu au watu hakuna hata mmoja aliyekufa?" akauliza kwa sauti ndogo kiasi cha upande wa pili kutokusikia vizuri mtu huyo anachokiongea. Hadi kupelekea kuuliza ili apate kusikia vema. Hasheem akauliza vilevile na jibu lilikuwa ni kama maelezo ya awali kuwa hakuna aliyekutwa amepoteza maisha wala kujeruhiwa wa upande wa waliovamiwa. "Ok, ifikapo kesho nitakutaarifuni nini cha kufanya nadhani usiku wa leo nitaita kikao kwa ajili ya kujua hatima pia kuna mjadala muhimu ambao tutatakiwa kuujadili," akahitisha mzee huyo na kubung'aza macho kama anafundisha uchawi wa Pemba.
%%%%%%%%%%%%
Ilikuwa yapata saa 11:30 mchana. Jopo kubwa la wajumbe mbalimbali kutoka kwenye ngazi mbalimbali za kiusalama walikuwa wakimalizia malizia mjadala wa kuhusu hukumu ya watu wawili kutokea Somalia ambao walikamatwa kwa makosa ya upitishaji wa silaha kwenye pwani ya Tanga pasipo utaratibu maalumu pia walifunguliwa kesi ya mauaji makubwa yaliyotokea miaka miwili nyuma wakati wa mapambano makali dhidi yao. "Hili la mauaji nadhani tungeliondoa kwani wanaweza kulipinga tena na kesi hii ikaahirishwa na kuzidi kuchukua muda mwingine?" aliongea mjumbe mmoja katika harakati za uchangiaji hoja kuhusiana na suala hilo. Alikuwa ni kamanda wa jeshi la polisi kanda ya kaskazini. "Hatuwezi kubadilisha maamuzi hata kidogo, kile tulichoanza nacho ndicho ambacho kitaendelea ni lazima watu hao wapande kizimbani kwa ajili ya kujibu tuhuma hizo mbili, hatuwezi kuonekana wadhaifu hata kidogo na tutakapotoa kosa moja na kusimama na moja hata waendesha mashtaka watatudharau na kutuona hatuna msimamo thabiti. Hatuwezi kubadilisha katu," alifoka mjumbe mwingine akipingana na wazo la mjumbe wa kwanza na wengi walionekana kumuunga mkono yeye kuliko yule mwingine. Mjadala ule ulichukua muda mrefu katika kuujadili ukachukua sura mpya mara baada ya mjumbe mmoja kutaka kujua afya za watuhumiwa hao ziko katika hali gani. Hilo lilikuwa ni kama kosa kwake kuweza kuuliza hivyo kwani walimjia juu na kumuuliza ni kwanini yeye anauliza hivyo na wakati aliyetakiwa kuuliza hivyo ni mwanasheria au wanasheria ambao wanasimamia watuhumiwa hao wa ugaidi. Aliangukiwa na maneno kutoka kila kona na asipate muda wa kupumua hata kidogo hadi pale alipotoa utetezi wake kuwa hakuwa na maana mbaya kwani aliona jinsi uhatari ulivyo kama watu hao wakiwa kwenye matatizo kwani ndugu zake huwenda wakataka fidia kubwa ambayo inaweza kuligharimu taifa. Wachache wakaelewa lakini wengi walikuwa na mashaka juu ya hoja za mjumbe huyo. Kuna waliotaka kuongezewa ulinzi mkali majaji ambao wataendesha kesi hiyo kwani mfano mzuri umetokea Tanga kwa kuuawa kwa jaji mstaafu aliwahi kuiendesha kesi hiyo huko Tanga kabla ya kuhamishiwa kwenye mahakama kuu. Hili na mengine mengi yaliyo na tija kwa maslahi ya taifa na uzalendo wa taifa, yakapewa kipaumbele na yale yaliyohitaji mjadala zaidi yalijadiliwa hadi pale makubaliano ya pamoja yaliposimama ndipo kikao hicho kikafungwa kwa maazimio kuwa ifikapo tarehe kenda mwezi unaofuata yani mwezi wa pili mwaka huo wa 2016, watuhumiwa hao ni lazima wapandishwe kizimbani kama mahakama ilivyotangaza, hivyo siku mbili kabla ya tarehe husika watuhumiwa hao walitakiwa kutolewa kwenye gereza la siri walilopo huko jijini Tanga na kusafirishwa kwa siri na ulinzi mkali hadi Dar es salaam ili ikifika siku ya kusomwa kwa kesi kuwe na utaratibu mzuri na wa kueleweka. Tarehe ya msafara ikapangwa na Kamishina mkuu wa jeshi la magereza nchini akapewa hiyo kazi huku akitakiwa kupanga vijana makini ambao wataweza kutekeleza hilo kwa ubora zaidi. Jibu likawa kuwa tarehe saba ndiyo siku pangwa hivyo kila mtu hapo kikaoni akaondoka na jibu kuwa ifikapo siku hiyo kila kitu kinafanyika kikamilifu kabisa na kwa usiri mkubwa. Na kila mtu alijua kuwa tayari mawakili na wanasheria ambao wanawasimamia watu hao, walishaingia nchini muda mrefu hivyo kwa siku hizo ilikuwa ni lazima kuwe na ushahidi wa kutosha wa kuweza kuwabana watu hao hadi wakose pa kutokea. Wanasheria wa serikali mahili katika kazi hiyo ya kusimamia sheria walikuwa tayari na walizidi kukusanya shahidi mbalimbali ili kusiwe na mlolongo usio na mantiki siku ya siku. Baada ya kikao hicho kikuu kufika tamati, wazee watatu akiwepo mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP, kiongozi mkuu wa usalama wa taifa na kiongozi wa kitengo cha kupambana na ujasusi Hussein Babu. Walivutana faragha na kuteta jambo. Hapa kulikuwa na jambo kuu moja nalo ni kuhusiana na ushahidi wa mwisho ambao haukuweza kupatikana na hadi muda huo haukujulikana ulipo na anao nani. Hili walikubalina kuwa watalitafuta kwa udi na uvumba hadi watakapofanikiwa kulipata lakini wakawa na shida hasa na ushahidi ambao wangeweza kuanza nao ili waweze kusimama vema katika kesi hiyo. Karatasi kadhaa zilikuwapo lakini pia kuliwapo na shahidi mmoja huyu hawakumtilia maanani sana kama angeweza kuwa na nguvu sana na pia ingekuwa ni vigumu kuaminika kwani alitokea upande wa jeshi la polisi. Baada ya kupata ushahidi muhimu ambao ulikabidhiwa kwa mkuu wa masuala ya sheria kwa ajili ya kuwakabidhi vijana watakaofanya kazi hiyo vema, kikao hicho nacho kikafunga mbawa zake na kuhitimishwa huku wakihimizana kuharakisha ushahidi uliokuwa kwa marehemu Dao utafutwe haraka sana kwani ni muhimu kuanzia huku shahidi nyingine zikitafutwa taratibu kwa sababu hazijulikani zilipo kabisa.
"Hivi unadhani hili jambo tutalimaliza kwa namna gani, maana kuanzia sasa hadi kufikia siku ya tukio ni siku ishirini na nne tu zimesalia?" Aliuliza IGP alipokuwa na Mkuu wa kitengo cha kupambana na ujasusi Tanzania bwana Hussein Babu. Walikuwa wakipiga hatua ndogo ndogo kuelekea maegeshoni. "Inabidi kuwa na mkakati mzuri wa kuweza kuhakikisha hili linakwenda kikamilifu, hakuna budi kuandaa vijana makini na mahodari wa kutumia silaha ambao watatumika kuweka ulinzi wakati wa kuwasafirisha watuhumiwa au kama ikibidi basi itumike hata Helkopta basi," akashauri Babu. "Hapana, hatuwezi kutumia gharama kubwa kiasi hicho kwa kazi ndogo kama hiyo lakini huwenda ikawa inatija zaidi kwa ajili ya usalama....lakini ni watuhumiwa wangapi hadi sasa tumewasafirisha kutoka gereza moja kwenda jingine na hakukuwa na shida yoyote,"
Ni wengi lakini walikuwa tofauti na hawa, hawa wa sasa ni wasomali na nadhani unaijua vizuri rekodi ya watu hawa, ubishi, kiburi na roho mbaya na kunauwezekano wakawa wameweza kuandaa hata watu wa kuweza kuleta shambulio wakati wa kuwasafirisha,"
"Yatupasa kuwa makini zaidi. Kuanzia sasa nadhani hilo litatekelezwa na ninaimani na mkuu wa magereza katika hili, atalitenda kwa weledi mkubwa lakini hata wewe inabidi ufanye juu chini ujue ni vipi tunaweza kuupata ushahidi kamili ambao haukujulikana umekwenda wapi baada ya shahidi kuuawa na unajua hadi sasa sijajua ni kwanini huyu shahidi mkubwa namna hii hakuwekewa ulinzi wa kutosha na mnajua fika lilihitajika hilo?" Aliuliza IGP baada ya kuona kuwa kulikuwa na umuhimu mkubwa sana wa ulinzi kwa mtu huyo na pengine hali isingefikia huko. Babu akatulia kidogo na kutazama chini kabla ya kunyanyua kichwa chake juu huku akiwa ameshika nyuma ya gari ikiwa ni baada ya kufika maegeshoni. "Hili suala lilipitishwa na wengi sana IGP, na lilikaliwa kikao na wanausalama wa usalama wa taifa hili mwishoe tukapata wazo hilo ambalo leo limeleta majibu haya. Tulipanga hivyo ikiwa na maana ya kuwa iwe siri na mtu yeyote yule asijue uwepo wa mtu yule kule porini," alieleza Hussein Babu. "Kwanini sasa imekuwa kinyume chake tena mapema kabisa bila hata kufika kwenye kilele husika?" akauliza IGP. "Ipo sababu na sababu hii si nyingine bali ni usaliti. Kwenye baadhi ya wale tuliowaamini wapo waliovunja uwaminifu na wakaamua kutugeuka bila shaka kuna maslahi wameahidiwa kwenye hili," akajibu Hussein. IGP akatikisa kichwa kuelewa jambo, hapo akakubali kuwa isingeweza kuwa kirahisi hivyo. Wakakubaliana kuwa jambo hilo lifanyiwe kazi na wabaya wajulikane lakini pia walikuwa na imani na vijana ambao hadi muda huo walikuwa kazini. Wakaachana hapo IGP akapanda gari yake na kuondoka huku yeye akichukua usafiri pia na kuondoka kwa ajili ya kwenda kupanga mipango mingine ya kikazi zaidi. Kikao hicho kilipokuwa kimekwisha, kwa upande wa pili wa shilingi kulikuwa na kikao kingine kilichokuwa kimekaliwa na watu wane tu na watu hao kati yao, watatu wakiwa ni wale wazee wa kiarabu na Mzee Hasheem mwenyewe lakini kukiwa na kijana mwingine mdogo huyu alikuwa ana asili ya uzungu uzungu ndani ya damu yake. Alikodiwa maalumu kwa mauaji. Kikao hicho kilikuwa ni majadiliano kuhusiana na vifo walivyovipokea vya vijana wao lakini pia ikiwa ni kama nafasi au wasaa wa kumkaribisha huyo kijana kazini mara baada ya kuuawa kwa Hudah vilevile kuwakaribisha wageni ambao walikuwa wakiingia jijini hapo usiku huo na wao ndiwo watakao kuwa wapokezi wakubwa. Kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Leod Jackpol, alitambulishwa mbele ya wazee hao pia akapewa sifa za mtu ambaye ndiye anayeichukua nafasi yake na mwisho akapewa majukumu ya kutwaa nafasi hiyo. Wazee wale wawili ambao walifahamika kwa jina la pamoja 'wasuka mipango' hawakuwa na mashaka na kijana huyo hata chembe kwani walijua uwezo wake. Mara baada ya kupewa kazi ya kuhakikisha askari aliyehusika na upelelezi wa mauaji yale ya Jaji mstaafu anauawa ili kusiwe na muendelezo wowote wa mambo ya ufuatiliwaji wa kesi hiyo. Kijana huyo wa kizungu ndiye aliyetengeneza mpango wa kuigiza sauti ya OCD na kumtaka askari yule wa kike anayefahamika kwa jina la SP Asna afike mahala fulani kwa lengo fulani kumbe haikuwa hivyo bali alikuwa akiuziwa mbuzi kwenye gunia. Kazi ilikuwa ndogo sana kwani ndani ya kituo cha polisi alikuwepo mtu ambaye wao walimuweka maalumu kwa ajili ya kuhakikisha anawavujishia baadhi ya siri na hata kuvamia mawasiliano ya mtu fulani hasa wanapomtaka. Hivyo kijana huyo Leod alipewa nafasi ya pekee sana katika kuhakikisha roho za wanaotakiwa kufa zinakufa kwa wakati pangwa. Wakamaliza kikao chao kwa makubaliano kuwa ifikapo usiku wa saa sita, ugeni huo wa Hasheem unapokelewa.
Kifo cha SP Asna kinawachanganya askari polisi kwa kiwango kikubwa sana, haikujulikana muuwaji ni nani na aliuwa kwa muda gani. Kila mmoja alisema kuwa ni jioni ya jana tulikuwa naye na kuagana kuwa anarudi nyumbani huku akiahidi kuonana kesho yaani leo. Sasa habari ya kuwa mwanadada huyo mpole ila mchapakazi, amepoteza maisha kwa kunyongwa shingo yake garini, ilikuwa ya kushtusha sana. Hakukuwa na mambo mengi sana ya kujadili kilichotakiwa kutekelezwa mahala hapo ilikuwa ni uchunguzi wa kina dhidi ya muuaji au mauaji hayo. Mkuu wa kituo kikuu cha polisi Chumbageni alimuita askari wake ambaye ndiye aliyemkabidhi jalada linalohusu ufuatiliaji wa kesi hizo za mauaji na kumkabidhi mzigo huo mwingine ambao alitaka amkabidhi majibu ya upelelezi huo ndani ya siku tano tu za mwanzoni. "Naona wanataka kutubandika viraka vya uzembe tutembee navyo kwa mashaka mitaani, tusiwape vichwa wajinga tu na werevu wakaonekana si lolote si chochote, ni wakati wa kuonesha makucha sasa, ni wakati wa kusimama kwa msimamo kuwaonesha kuwa sisi si wapuuzi tuliokalia nafasi hizi. Nataka majibu ya kazi hiyo kwa muda pangwa. Panga muda wako na nafasi yako lakini unifikishie kwa wakati," ndivyo alivyokuwa akitoa maagizo mkuu huyo wa kituo kwa Insp. Musa. "Ndiyo, mkuu," aliitikia kwa utii kijana huyo kasha akachukua jalada hilo na kukakamaa ishara ya heshima kwa kiongozi wake wa kazi na kujitoa humo ofisini. Alijua ni wapi pa kuanzia hivyo haikumpa tabu kujua nini afanye kwa majira hayo. Kituo cha kwanza kilikuwa ni kwenye ofisi ya vijana wa mawasiliano, alipofika huko akauliza kuhusiana na kazi ambayo aliiacha mikononi mwa vijana hao. Kijana mmoja akasema kuwa kazi wameifanya kikamilifu na kugundua mahali mtu huyo alipopiga simu lakini tatizo lililopo ambalo limechukua muda kuling'amua ni kuhusu namba iliyotumika. Na hayo yote vijana hao walifanya kupitia simu ya marehemu Asna ilimjua aliyekuwa akiwasiliana naye ni nani. Kwani namba iliyotumika ilionekana ni ya mkuu lakini tulipofanya uchunguzi wa kina zaidi tukagundua kuwa wakati simu hiyo ikiwa inapigwa au wakati mpigaji alipokuwa akiongea na SP Asna, mkuu alikuwa pia akiitumia simu yake muda huohuo akiongea na mtu mwingine. Ilitubidi kukaa na simu ya mkuu kwa muda wa masaa si chini ya mawili kwa uchunguzi wa kina zaidi. Mtu aliyekuwa akiongea na SP hakuwa mkuu hata kidogo kwani namba iliyotumika kuongea naye ni hii hapa," akasontesha kidole kijana huyo mahali ilipo kompyuta na kuonesha hiyo namba. "Zaidi ya hapo nini mlifanya sasa?" akahoji tena Inspekta Musa. "Tulianza kazi ya kuifuatilia hii namba na kujua kama bado inatumika. Ilitusumbua kidogo, hawa watu wanaonekana ni wajuzi wa mambo na walifanya hili kwa kujua kuwa hatutaweza kulichimbua hadi kupata ung'amuzi. Namba hii inatumika na kwa sasa inapatikana katikati ya mji barabara ya jamaa karibu kabisa na msikiti wa ijumaa," akaweka kituo hapo kijana huyo. "Ok, hongereni kwa kazi nzuri hakikisheni mnanipa kila kitakacho kuwa kikiendelea kwani naamini kabisa naweza kumkamata kwa urahisi mtu huyo," akasema Insp. Musa na kutoka ndani humo. Akachukua vijana watano wenye silaha na wanaojua kuishika na kuitumia silaha vema. Wakachukua gari na kuingia nayo barabarani. Kutoka hapo kituoni hadi kufika barabara ya jamaa si mbali. Alipofika barabara ya nane akaingia kushoto na kupanda taratibu hadi alipoikamata barabara ya jamaa.
Niambie mahala ambapo anasomeka mtu huyo lakini pia unipe na namba ya nyumba ili iwe rahisi kumvami," akaagiza Musa. "Ok, bado inasomeka mahala hapo na ni ndani ya nyumba ya ghorofa maana inaoneka kwa juu ni jingo lenye namba BJ 38." akatoa maelekezo kijana huyo huku akisisitiza zaidi kuwa akifika karibu na msikiti wa ijumaa atamuelekeza zaidi. Safari ikawa inazidi kusonga huku ukimya ukichukua nafasi kwa asilimia kubwa. walipokuwa wakiukaribia msikiti huo, radio Call ikaunguruma, maneno kadhaa yasiyoeleweka yakawa yanasikika kasha sauti ikasikika ikisema. "Kiongozi alama fuatiliwaji imepotea machoni mwetu hatuioni kabisa.
ITAENDELEA