Notification texts go here Contact Us Buy Now!

DEREVA TAXI SEHEMU YA KUMI NA TATU (13)

TAXI DRIVER SEHEMU YA 13
Saa 2: 00

vijana wale waliwatikisa wakuu wa usalama baada ya kushika sehemu muhimu kama kutishia kuilipua kambi ya jeshi ya Pande, Bandari pamoja na kuharibu kiwanja cha ndege. Kitu kinachonifanya niwe makini zaidi hata sasa ni kuhusu utendaji kazi wake wa kiusalama wa nchi hii. Pamoja na kitisho kile lakini Jeshi halikujibu chochote na badala yake wakatumwa watu wawili tu ambao hawakuwa vijana lakini uwezo wao ulikuwa mkubwa sana. Wakawapelekesha vijana wetu na kuwadhoofisha kwa vile walivyokuwa wakivitegemea, wakawashambulia kwa risasi na kufanikiwa kumjeruhi mmoja na mwingine kukamatwa akiwa na hali mbaya. Baada ya hapo wakawasafirisha kwa siri na kuanzia hapo haikujulikana walipelekwa wapi hadi pale fununu ziliposikika kuwa wamehifadhiwa kwenye gereza la Maweni. Othman amelia sana kwani Habibu Suleiman ni binamu yake na alikuwa akimpenda sana. Hasara kubwa waliyoipata hawatakuja kuisahau. Nisiwadanganye, mnaweza kuona hili ni jambo dogo tu la mzahamzaha lakini madhara yake ni makubwa sana. Ni lazima tuuwe, tufanye kila namna hadi watu hao wawe huru, ikishindikana basi ni kufanya maangamizi hadi kieleweke. Watu hao wapo na walikuwa wakisubiri hukumu ili wahukumiwe kwa makosa hayo ya kigaidi na usafirishaji silaha kinyume na utaratibu. Mashahidi waliokuwa wakitegemewa ni wale wazee ambao ndio walihusika kwenye kuwakamata baada ya mapambano mazito. Hao wakawekwa maalumu kwa ulinzi maalumu lakini finyu. Sasa hakuna shahidi aliye hai japo hatukukamata ushahidi wowote kutoka kwao lakini hilo linatosha kuwaumiza kichwa. Tunachokisubiri ni nini kitasemwa na mahakama kuu juu ya uwepo wa vijana hao wakati siku ya kutajwa kwa kesi ikiwa imewadia. Kuna mafanikio makubwa nimeahidiwa pindi jambo hili litakapofanikiwa na kwa hili ni lazima mjue kuwa mafanikio yangu ni mafanikio yenu, najua kuwa Tanzania ilinilea na kua mtu mkubwa lakini nadhani mnajua kuwa asili yetu nini?" Aliuliza swali Hasheem baada ya maelezo marefu kasha akameza mate huku akiwatazama watu wale kwa awamu. "Asili yetu sisi ni pesa na mali!" Alijibu mzee mwingine pale ambaye naye alikuwa ni mwenye asili ya kiarabu kama wengine walivyo. "Ewaaa! Umenena wallah! Asili ya mwarabu si cheo abadani, asili ya mwarabu ni pesa na mali ili aishi kifalme. Hata baadhi ya manabii walikuwa hivyo kama nabii Suleiman aliyekuwa anamiliki utajiri wa madini na milki nyingine kubwa kubwa sambamba na wanawake wengi. Hivi kuna nini kingine sasa ambacho ninakitafuta? kama sio pesa na Mali? Kama heshima ya cheo walishanipa wazanzibar sasa ni pesa na mali ndiyo niiwazayo na hawa wasomali hasa huyu Othman, ameniahidi utajiri endapo nitafanikiwa kumsaidia katika harakati za kumuacha nduguye na mwenziwe huru," alimaliza kuongea Hasheem, akachukua tena gilasi iliyo na maji ndanimwe akapiga funda moja kasha akatulia.

Kilichobakia ni nini kuanzia sasa?" Akahoji yule ambaye alikuwa kimya muda wote. "Kilichobakia ni kusubiri tarehe ya kesi tu hapa ndiyo tutakapowaonesha maajabu. Tayari kwa sasa ninapata kila kitu kutoka gerezani kuhusu maandalizi ya jinsi ya kuwasafirisha watuhumiwa hao ambao watasafirishwa kwenda Dar es salaam kwa ajili ya kwenda kusikilizwa kesi yao kwa mara nyingine maana kesi hii ni kubwa na haiwezi kusikilizwa sehemu yoyote ile zaidi ya mahakama kuu," Alijibu Hasheem. "Hivi kutakuwa na hukumu kweli kama hao mashahidi wote wawili wameuawa?" Aliuliza mzee mwingine, Hasheem kabla ya kujibu akamtazama mzee huyo kwa tabasamu lililozuiwa na kofia ile aliyoivaa kasha akasema. "Kila kitu ni akili tu Abas, hawa walikuwa ni lazima waondolewe ili hata kama mchezo wetu ukifeli kule mahakamani kuwe hakuna jipya, tambueni pia kuwa siku ya kesi Othman mwenyewe atakuwapo mahakani lakini anaamini fika sisi tutakuwa tumefanya ya kueleweka kabla ya siku hiyo husika kufika," akajibu Hasheem.
"Sawa nimekupata vizuri nadhani kila kitu kiko kwenye usawa na hakuna shaka" Akasema huyo mzee aliyetambulishwa hapo kwa jina la Abas. "Yaa kila kitu kiko sawa hapa jibu linalosubiriwa ni la kutoka bandarini kwa mkurugenzi wa kampuni ya upakuaji na upakiaji mizigo, tumeshatuma vijana na natumai kama sio leo basi ni kesho, tunaweza pata majibu ya zana za kazi kama zipo na usalama wake maana tulitumia ofisi yake kuhifadhia vyombo vyetu," alijibu Hasheem, wale wazee wawili wakaamka na kupanga siku ya kukutana kwa ajili ya kwenda bandarini kutazama na kuhakiki silaha zao.

Saa 06:04 jioni. Mkurugenzi wa kampuni ya Upakiaji na upakuaji mizigo bandarini aliingia ofisini kwake lakini kabla ya hapo alipitia kwenye ofisi ya katibu muhtasi wake ili kujua kama kwa muda huo angeweza kuwepo kazini, hakuwepo. Aliamini hivyo kwa asilimia mia moja kuwa asingeweza kumkuta na hata ujio wake mahala hapo pia ulitaka asimkute ofisini hapo hivyo kwenda huko ni kutaka kujihakikishia tu. Muda ambao alirudi kutoka safarini bwana huyo ambaye alifahamika kwa jina moja tu la Gambe, haukuwa muda ambao alitakiwa kufika mahali hapo hata kidogo lakini kuna jambo la msingi sana lilimfanya yeye kuweza kufika mahali hapo. Ahadi ya kukutana na watu fulani kwa ajili ya mipango ya kazi au maongezi fulani, vilikuwa vikimtaka kuwa hapo kazini kwake Masaa ishirini na nne. Sasa kutokuwepo kwake kazini kwa muda wa siku tatu zote hizo, kulipelekea aamini kuwa kungeweza kuwa na ujumbe wowote ule ulioachwa ofisini kwake na hicho ndicho pekee kilichomfanya kufika mahala hapo wanguwangu.

Jina Gambe hakupewa na kabila lake wala koo yake tukiachana na wazazi wake waliomleta duniani, jina lake halisi alifahamika kama Gabriel Musamba mzaliwa wa huko nyanda za juu kusini japo kuna tetesi na uvumi kuwa bwana huyu hakuwa raia wa Tanzania kuokana na jinsi alivyo. Alikuwa mweusi tii! Mkubwa aliyebarikiwa kitambi kilichoonesha kuridhishwa na maisha lakini hakuwa akiweza kuongea lugha ya kiswahili vizuri, kama ukipata bahati ya kumuona akiongea, kiswahili chake kilikuwa kibovu waweza sema ametokea nchini Kongo. Jina la Gambe alipewa na vijana aliowahi kufanya nao kazi mbalimbali nchini hapa na hasa lilitokana na kupenda sana ulabu. Akikaa vizuri baa anaondoka na Creti nzima ya bia bila kupoteza 
kumbukumbu zake kichwani. Bora nyama za kushushia kinywaji hicho zisiwe mbali. Wengi walijiuliza sijui ni kwanini huwa halewi lakini wala yeye hakuwa na muda wa kuwasikiliza alizidi kufanya yake vile apendavyo. Alipoingia ofisini kwake bwana huyo, alijikalisha kitini halafu bila kupoteza muda akaanza na kuzunguusha macho yake mekundu juu ya meza ile, alipoona hakukuwa na kitu akavuta mtoto wa meza. Hapo akakutana na bahasha ya khaki juu ikiwa imepambwa na maandishi makubwa, MKURUGENZI. Akaitazama kwa muda kabla hajaichana na kuingia ndani. Aliipitishia macho kwa haraka haraka kasha akaitupia mezani na kuitazama kwa muda kidogo kabla ya kuinyakua na kuirudishia kwenye ile bahasha lakini hakutaka kuicha tena pale, alitoka nayo na kuelekea nayo hadi nje akaitupia kwenye dash board ya gari yake na kutulia. Alikumbuka mengi sana yaliyopita kuanzia jinsi alivyokutana na watu wale hadi kufikia hapo. Usiku alipokuwa akipata ulabu maeneo ya Tanga pazuri, jinsi watu hao walivyomuibukia na kujenga naye ukaribu hadi kuzoena na hatimaye wakampa dili hilo ambalo kwayo lilikuwa likimpa pesa nyingi kila baada ya muda fulani, pesa hizi zikamfanya kubadili kabisa mfumo wa maisha yake lakini pamoja na kuwa alibadilika kimaisha, kuna kitu woga kilikuwa kikiusumbua sana moyo wake na hiki ndicho kilichompa mawazo kila mara. Nilijua tu watakuwa ni wao, wanataka kuja kuukagua mzigo wao siku yoyote kuanzia sasa kabla ya kuamua kuuchukua lakini mbona si mzigo wote ambao wanataka kuuchukua pia? Wanataka kuzidi kuniweka roho juu hawa lakini aaaghr! Acha tu waendelee kuweka, kinachotakiwa ni umakini kwani kupitia dili hili nimejikuta nikibadili maisha yangu kwa kiasi kikubwa sana. Nitawataka wawe makini zaidi kwani sitapenda kuwa mikononi mwa wanausalama. Alijiwazia akiwa hapo garini kwake baada ya kuamua kuisoma ile barua. Akaondoka na kuingia mitaani huku akiwa na ujumbe uliomtaka siku mbili zinazofuata awe maeneo ya kazi yake nyakati za usiku mkubwa kwani jamaa hao walitaka kukagua mzigo ili wajihakikishie uwepo wa kazi yao kwa uhakika.

Muziki ulikuwa ukirindima maeneo ya Tanga pazuri, hapa palikuwa kweli ni Tanga pazuri, hapakuwa kwa daraja la juu sana lakini jinsi palivyotegwa na kupangiliwa ilikuwa ni lazima upapende. Muziki huo ulikuwa ukipigwa kwa sauti ya taratibu sana na ulipata kusindikizwa na burudani za kawaida za macho kwa watazamaji wazuri, wahudumu wa hapo walivyo warembo, vyakula vya kutosha pamoja na vinywaji mbalimbali. Siku hii ilikuwa ni ya kipekee sana kwa watu waliofika mahali hapo kwani kulipata kuwa na michezo midogomidogo pamoja na ofa za hapa na pale. Wakati mambo yote hayo yakiwa yanatendeka, kwenye kona moja ya sehemu ya kujipatia chakula kulikuwa na binti mmoja aliyekuwa amevaa mawani ya giza na kofia ya chepeo iliyoweza kumtoa vizuri, alikuwa akipeleka kinywaji kinywani mwake kwa madaha makubwa na hakuonekana kuwa na papara sana kwani aliweza kumaliza hata dakika nzima bila kunyanyua kinywaji na kupeleka tena kinywani. Macho yake yalionekana kutazama michezo hiyo iliyokuwa ikiendelea mahala hapo lakini akili yake ilikuwa maili nyingi kimawazo. Hii huwenda pengine ndiyo iliyopelekea kupoa sana na kupoteza muda mrefu katika kutafuna kinywaji kile. Si huyo tu, kwa upande mwingine eneo hilo hilo kuna kijana alikuwa akichukua nafasi na alionekana si muda mrefu tangu kuingia eneo hilo. Baada ya kuketi muhudumu alifika na kumtaka aseme hitaji lake. Huyu alifahamika vema na hakuwa mwingine isipokuwa Tom au dereva Taxi kwa lugha nyingine ambayo wengi hupenda kuitumia hasa wanaomfahamu ama kumuhitaji kwa biashara hiyo. Japo wenzake wanaomjua zaidi walimpachika jina la mzee wa matukio.

Alipokuwa anaagiza, macho ya yule binti yakatua machoni mwa kijana yule na alimuangalia kwa kitambo kingi hadi pale muhudumu alipoondoka na kumuacha kijana yule akigeuka huku na huko akishangaa eneo lile ndipo binti yule asiyejulikana alipoangusha macho yake kilipo kinywaji chake na kukinyanyua na kukipeleka kinywani huku jicho likirudi tena kwa kijana yule. Kabla muhudumu yule hajaleta kinywaji au vile alivyoagizwa na Tom, shindo kubwa likasikika kutokea barabarani na sauti ya pikipiki kubwa ikiunguruma na kupiga misele huku sauti za misuguano ya magurudumu ya gari nyingine zikisikika mara baada ya madereva wa gari hizo kuzitafuta breki zilipo ili kujinusuru na dhahma hiyo. Kishindo kingine kidogo kikasika kisha kimya na kelele za mashuhuda walioacha shughuli zao na kukimbilia huko zikichukua hatamu. Tom alisharuka ukuta mdogo wa eneo hilo siku nyingi na kuwahi mahala kuliposikika kelele hizo za kishindo. Alipofika kwenye kibanda kidogo cha wakala wa mitandao ya simu akasimama, ndipo alipoona pikipiki kubwa likiwa limekamata barabara ndogo ya vumbi ya bustani ya maua nyuma ya kituo cha mafuta cha Lake Oil likatokea kwenye makutano ya reli na barabara likakunja kuume kwa kasi hiyohiyo na kuchukua barabara ya kwenda kwa mkuu wa mkoa. Tom pamoja na mashuhuda wengine wakaruka mtaroni kulipokuwapo na gari ndogo ya kukodi/Taxi, ambayo ilikuwa bado ikitweta huku honi zikirindima kwa wingi.

"Unajua huyu jamaa wa hii gari alikuwa mbio sana na lile pikipiki likawa kama linamfukuza huyu jamaa, baada ya dereva wa lile pikipiki kuwa sawa na hii gari cha kwanza mlipuko wa kama gurudumu lililopata pancha kasha tukaona damu zikiruka kwenye kioo cha mbele huku gari hii ikiacha njia aisee!" Alikuwa ni dereva mmoja wa bodaboda akitoa ushuhuda juu ya kile alichopata kukishuhudia yeye. "Ameumia?" Sauti za watu zilizokuwa zikiuliza zilisikika. "Daah! Ameumia kichwani aisee! Na inaonekana ni risasi hii. Amepigwa risasi jamaa!" Alisema kwa sauti Tom ambaye alilitilia mashaka hilo tukio baada ya kuona ni Taxi. Baadhi ya watu waliposikia ni risasi wakaanza kujiondoa hilo eneo taratibu wakiogopa kuingizwa kwenye ushahidi wa kuisaidia polisi. 

"Wanazidi kuendelea kufanya mauaji ya ndugu zangu, sasa ni muda wa kula nao sahani moja" Akasema kwa sauti ndogo Tom huku akiondoka na kuielekea gari yake lakini hakujua wakati anaongea yale nyuma yake kulikuwapo yule binti mwenye mawani ya jua na kapelo kichwani. Jicho alilotazamwa Tom na yule dada lilikuwa la kipekee sana na kulionekana kuna kitu huyu binti alikihitaji kwa kijana huyo na hayo maneno ni kama yalimjengea picha nyingine zaidi. Tom alipoondoka naye alichukua usafiri wa bodaboda na kutoweka kabisa eneo hilo akielekea kituo cha daladala mjini. Binti yule mwenye kapelo baadae alikuja kushushwa maeneo ya barabra ya Tanga beach kituo kimoja kinachoitwa maduka manne. Aliposhuka kutokea ndani ya dalala hiyo iliyokuwa ikifanya safari zake maeneo hayo ya kutokea mjini kasha likatisha Msambweni, Makorola, Share kasha kuibukia na barabara hiyo ya Tanga beach. Binti huyo aliingia mitaani na kupotelea huko na kuja kuibukia kwenye jengo moja la kawaida lakini lililo na huduma muhimu za kimakazi. Hakuwa na mashaka hata kidogo aliingia ndani baada ya kuufungua mlango wa nyumba hiyo akaingia ndani kisha kuurudishia na kuufunga kabisa akaenda kufungua mlango wa nyuma maana nyumba hiyo ilitengenezwa kwa muundo wa milango miwili kama zile nyumba zenye mabanda ya uwani. Baada ya kuufungua mlango huo alijikalisha kizingitini na kuingia katika tafakuri nzito. Aliwaza mengi sana, kila alichopishana nacho ama kilichomtokea kama siyo kupitia, alikikumbuka ipasavyo. Hiyo ya siku hiyo aliona huwenda ndiyo ikawa ni njia moja wapo ya kuwakaribia anaowataka lakini pia ajue ni akina nani hao anaowataka? Kwanza yeye mwenyewe ni nani? Kwanini alikuwa akimtazama Tom kwa macho ya pekee sana je, anamfahamu au ni nini ilikuwa sababu ya kumtazama kijana yule namna ile. Kizunguzungu. "Halafu ni dereva Taxi pia" akajisemea huyo dada na kunyanyuka hapo kasha akaufunga na huo mlango kwa ndani na kujitokomeza chumbani akatulia kimya.

ITAENDELEA.

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.