Notification texts go here Contact Us Buy Now!

DEREVA TAXI SEHEMU YA KUMI NA SITA (16)

TAXI DRIVER SEHEMU YA 16
Extra...

Dereva wa Moni alizidi kufuata bila kusema kitu yeye kazi yake kuu ilikuwa ni kufuata kile anachoamriwa na mteja wake. "Fuata hukohuko naona amepunguza kasi bila shaka anakaribia kufika," alisema Moni baada ya gari ya Tom kuingia Amtico na kuchukua barabara iliyokuwa ikielekea Amani lakini baada ya mwendo mfupi mbele, ikaiacha barabara ya Amani na kuchukua ile inayokwenda kwenye Hospitali ya wilaya hiyo, Hospitali ya Mt. Augustino/Teule au ni kama alikuwa akielekea Genge. Baada ya kushusha kwenye mteremko mdogo, ikasimama kwenye mti mmoja ndani ya soko la Samaki. Moni alipoona vile akamzuia dereva wa gari aliyomo asiingize gari kule bali alimtaka asimame. Akalipa ujira wa watu kasha akamuamuru dereva huyo aondoke, baada ya gari hiyo kuondoka, Moni akavaa mzula uliofunika kabisa paji lake la uso kasha akatundika na mawani ya jua machoni mwake. Akapiga hatua ndogondogo binti huyo hadi alipoivuka reli kama anayekwenda Mapana, akasimama pembezoni mwa barabara baada ya kuona gari ya Tom ikiwa inarudi upande ule. Ilipofika alipo, akaipiga mkono ikasimama kasha kijana huyo akashusha kioo. "Labda kama unakwenda mjini isiwe safari nyingine," akasema Tom kabla dada Huyo hajasema hitaji lake. "Hukohuko," akajibu Moni akiwa anakaa kwenye siti mara baada ya kujifungulia mlango. Tom akaweka sawa kioo cha kutazama nyuma kwa abiria wake akamtazama huyo binti ambaye alikuwa akitazama chini, akamtazama kwa muda kidogo huku akiondoka eneo hilo taratibu. "Elfu kumi hadi mjini kwa sababu safari yangu ni huko sijui unakwenda sehemu gani?" akauliza Tom akiwa anamtazama abiria wake kupitia kioo. "Zaidi ya elfu kumi nitakupa na nakwenda mjini," alijibu Moni huku naye akimtazama dereva wa Taxi hiyo kupitia kile kioo. Tom akapiga kimya lakini moyoni akiwa anajiuliza majibu ya binti huyo yalivyo ya mkato na alikuwa akitabasamu, alifikiri sana na asipate jibu lakini akaona ni vema amnyuke swali jingine ili aone jibu litakalo rudi kwake litakuwaje. "Tanga mjini ndiyo nyumbani au unakwenda kikazi, miadi au matembezi, samahani lakini," akauliza Tom huku naye akilirudisha tabasamu usoni mwake. "Hivi yule bwana uliyemuacha pale kwenye soko la samaki ni nani?" akauliza Moni badala ya kujibu alichoulizwa. Swali hili likamtoa macho muulizwaji. Lilikuwa ni swali asilolitarajia mahala hapo hata kidogo na lilimpa picha kuwa binti huyo alikuwa akimfuatilia pengine kuanzia mjini hadi hapo au alimuona wakati anamshusha mtu huyo ndipo akamsubiri. Yote hayo aliyapa nafasi ubongoni mwake lakini asijue ni lipi linaweza kuwa ndilo. Akiwa bado anajiuliza Moni akamkumbusha kuhusu jibu la swali lake. Tom akashusha munkari na kujibu kuwa alikuwa ni mfanya biashara tu na alimkodisha kutokea mjini. "Wewe ni nani lakini?" akatupa na swali. "Utanijua tu usijali," alijibu Moni. Kimya kikakita tena safari ikawa moto, mwendo aliokuwa akiutumia kijana huyo haukuwa wa kawaida hata kidogo. Kichwani mwake alishamtilia mashaka binti huyo na akilinganisha na matukio yaliyokuwa yakiendelea mjini hapo, akili yake ikawa inahofu juu ya binti huyo kuanzia muonekano hadi maongezi. Walichapa raba hadi walipoingia Pongwe, hapa wakapita kwa kasi kubwa lakini walipokuwa wanakipita kiwanda cha Saruji cha Simba, simu yake ya mkononi ikaita. akaichukua kutoka kwenye kibweta kimoja kilichopo kwenye dash board ya gari yake, akatazama jina la mpigaji akaona Hudah. Akaipokea na kuiweka sikioni huku akiwa makini barabarani.

Nipo Kange hapa, kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani. Nataka kuelekea Masiwani shamba lakini tutatumia njia ya Kange Kasera na ndiyo maana nakusubiri hapa," aliongea mtu huyo ambaye alifahamika kwa jina la Hudah. Tom akajibu hakuna shaka na simu ikakatika. Akajiuliza ni kwanini mtu huyo amsubiri hapo, huwenda alijua kuwa yuko njia hiyo. Alikuwa na hofu kubwa sana na kwa kua alishamfahamu mtu huyo kuwa hakuwa mtu mzuri akawa anafikiria kumpita tu na asijenge ukaribu naye kwani tayari hakuwa na imani thabiti na mtu huyo abadani. "Sielewi nifanye nini?" akasema kwa sauti ndogo ambayo ilimfikia Moni. "Huelewi nini sasa na mbona hiyo simu kama imekupa mashaka?" akauliza Moni huku akimtazama kijana huyo kupitia kioo. Tom akagwaya lakini akajua kuwa bila shaka huo utakuwa ni mtego alitegewa sasa ameuingia bila shida na siku hiyo ilikuwa si yake kuishi. Akapiga breki kali sana na kulisereresha gari lake pembeni na kusimama kwenye kituo cha kusimamia abiria wakisubiri daladala, maeneo ya kiwanda cha Saruji cha Rhino. "Naomba uteremke dada hata pesa yako siihitaji, teremka sielewi mnanichanganya," aliongea Tom kwa kuchanganyikiwa huku akiwa anasugua nywele zake. Moni hakusema kitu alibaki akitabasamu tu na kumtazama huyo kijana kwa kumshangaa kasha akamwambia kuwa hashuki na atakwenda kumchukua na huyo mtu aliyekuwa akiongea naye maana amesikia vizuri sauti kupitia spika za simu yake. Mungu wangu! Tom akatoa macho kama aliyeona mzuka wa hayati babu yake aliyepata kufa angali yeye akiwa bado anatambaa. Niende nikamchukue na huyo mtu, yaani Hudah! Hapana hawa watakuwa wamoja si bure, 'this is my time Tom!' Aliwaza kijana huyo huku bado akiwa ametoa macho lakini hapo hapo akapata ujasiri na kumwambia kuwa hamjui yeye ni nani na kama hamjui basi anaitwa Tom dereva Taxi maarufu na wa siku nyingi na mjini hapo wanamuita mzee wa matukio, atake asitake atashuka tu. "Nilikufananisha siku nyingi sana na nikawa najiuliza wewe ni nani maana ni miaka mingi tangu tupotezane. Ni wewe? Kumbe ni wewe kweli japo siku hizi umekuwa makini na wa tofauti sana," Alisema Moni kwa taratibu mno kama mtu anayetamba hadithi ya kuhuzunisha Tom akapoa, eti, anamjua, anamjua? Kivipi amjue huku yeye akiwa hamjui. Akakataa na si kukataa tu bali aliikataa hadi akili yake pale ilipomwambia akumbuke huwenda kweli wanaweza kuwa waliwahi kuwa pamoja. Alikataa na kutikisa kichwa kushoto kulia na kuchukua chuma kimoja kama nyundo na kumwambia kama hatateremka basi atampiga nacho cha pua. Moni akatabasamu kasha akachomoa bastola na kumnyooshea usoni huku akimtaka awe mpole na kumtaka aendeshe gari na waondoke. Tom akatokwa na macho huku akiwa kagwaya kama mtu aliyekumbwa na ugonjwa wa kupooza mwili. Akiwa anafikiria kuwasha gari, simu yake ikaita tena alipotazama akagundua kuwa ni Hudah. Akanyoosha kidole kwenye kioo cha simu huku akiwa amekumbwa na kigugumizi kizito. "Mwe..mwen...zako anapiga ni....nikupe uongee nae!" Akangea kwa kitetemeshi Tom.
"Hapana hakikisha unaendesha gari hadi alipo, kwanza hapo mjibu ukiwa huna hata mashaka wala wasiwasi pia hakikisha humwambii kama uko na mtu mwingine garini mwako nataka kujua ni nani huyo. Toa mashaka kumbuka," akajibu Moni akiwa amezidi kumuelekezea mtutu wa hunduki kijana huyo. Akapokea hiyo simu ambayo muongeaji wa simu hiyo hakuwa na jipya zaidi ya kumsisitizia kuwahi maana amesimama sana hapo barabarani na hamuoni kutokea. Tom akajibu kuwa ni muda mfupi atakuwa hapo kwani alikuwa karibu mno. Tom akawasha gari na kuliingiza tena barabarani kwa kasi kubwa hadi alipomuona mtu huyo ndipo Moni alipolala chini kabisa ya viti na kutulia. Kijana huyo ambaye muda wote hutembea na brifcas mikononi mwake, akaingia garini humo lakini kitu cha kushangaza siku hiyo hakukaa nyuma na badala yake alikaa pembeni ya dereva. "Habari yako dereva machachari? Kumbe ulikuwa wilayani?" alisalimia Hudah, sauti hiyo ikapenya hadi masikioni mwa Moni. Akaikumbuka sauti hiyo, sauti hiyo ilikuwa ni ile iliyokuwa ikiongea kwa madaha huku ikimkungu'ta risasi mwalimu Dao siku ambayo walivamiwa huko Kauzeni. Akajua sasa yupo kwenye mikono sahihi na hapo anakwenda kuianza kazi yake vizuri. Tom na huyo kijana waliongea mengi baada ya salamu kama marafiki huku wakizidi kuchanja mbuga kuitafuta Masiwani shamba. Walitembea kwa kasi kubwa hadi mahali ambapo hakuna watu wengi wala magari mengi, kijana hudah akaomba gari hiyo isimame huku akitoa bastola kwa siri sana kwenye mkanda wa suruali yake. Gari ikasimama lakini hapohapo mdomo wa bastola nao ukamtazama Tom.

"Unalolote la kuongea labda kuhusiana na mwisho wa maisha yako?" akahoji Hudah. Tom akawa anatetemeka mtindo mmoja tena kupita kiasi. "Kwa nini unataka kuniuwa?" akahoji kwa kitetemeshi. Hudah akamtazama kisha akajibu kuwa si yeye tu, madereva Tax wote waliopoteza maisha hawakupoteza hivihivi ila yeye ndiye aliyekuwa mpotezaji. Macho yakamtoka kijana huyo mara baada ya kupata maneno hayo kutoka kwa kijana huyo. "Kilichopo mbele yako ni kunijibu swali nililokuuliza pekee je, unautetezi au neno lolote la mwisho kwa siku yako hii ya mwisho?"
"Lipo!" Sauti kutokea nyuma ya kiti ikasema. Ikamfanya Hudah kushtuka kwa nguvu mno na alipotaka kugeuka akaambiwa hapo haikuwa mahala pake bali alichotakiwa kukifanya ni kunyoosha mkono wenye silaha juu kama usalama wake. Akataka kuleta ubishi lakini alipata hisia ya chuma cha baridi kikigusa uchogoni mwake. Akawa hana budi zaidi ya kukubali, akapigwa na kitako cha bunduki kwenye upande wa kulia wa kichwa chake, maumivu makali yakamtambaa kichwani akabweka kwa sauti ya maumivu kidogo huku akihisi kimiminika chenye joto kikishuka taratibu kupitia sikioni kuja hadi shavuni mwake, akajua amepasuka. "Teremka chini mikono yako ikiwa juu kwa usalama wako zaidi," aliagiza Moni huku akiichukua ile bastola ya Hudah na kuiweka sitini. Tom yeye alikuwa kimya muda wote huku akimfikiria huyo binti ni nani ambaye kwa harakaharaka bila kupinga ameyaokoa maisha yake. Hudah akaona kama huo Ulikuwa ni mkosi kwake na kichwani alishaweka alama mbaya kabisa ya maamuzi juu ya mtu huyo aliyemuharibia utaratibu wake wa kazi yake. Aliteremka kwa mitego huku mikono yake ikiwa nyuma ya kichwa Moni akiwa nyuma kwa ukaribu zaidi. Tom naye aliteremka kisha akabaki upande wa pili akiwa ameushikilia mlango wa gari yake akitazama nini kinaweza kutokea mahala hapo. Hudah alipoikanyagisha miguu yake chini, akapiga hatua mbili mbele za ghafula kasha akajizungusha kama feni na kuipiga silaha ya Moni halafu hapo hapo akajirudisha tena upande wa pili na kupeleka shambulio kwa binti huyo lakini Moni alifanikiwa kuisoma akili ya haraka ya kijana huyo akainama na kulipisha pigo hilo lipite. Hudah akaruka mbele kwa mtindo wa kupendeza na kugeuka wakitazamana usoni kila mmoja akiwa amejiweka tayari kumvamia mwenzake. Wa kwanza kuanzisha mapambano alikuwa ni hudah, akaja kwa kasi kumfuata Moni, Moni naye akasogea kwa hatua moja kumfuata huyo kijana lakini akiwa na imani kuwa hapotezi umakini. Ngumi kali zilikuwa zikirushwa kutoka kwa Hudah na binti Moni akijitahidi kuzuia na kukwepa hadi pale pigo moja lilipomshinda kuzuia na kuliruhusu liingie kifuani mwake, Moni akapiga yowe la uchungu sana huku akipepesuka na kukishika kifua chake sehemu iliyopata pigo. 

"Nimepata picha sasa, kumbe ni wewe? Nilijua tu ni lazima siku moja tukutane," aliongea Hudah huku akimtazama Moni kwa kumdadisi na kuishusha mikono yake chini kwa wakati huohuo. Sauti na hata mapambano yake yalikuwa ni ya yule binti aliyemkuta Kauzeni wakati akienda kufanya mauaji. Sasa akajua fika alikuwa akipambana na mtu mwenye kutaka kulipiza kisasi cha mzee Dao. Akacheka sana Hudah, alicheka sana na alicheka kwa sababu alijua aina ya mtu aliyekuwa akipambana naye, kwanza ni mtu wa kulia sana wakati wa kushambulia na pia alikuwa si mhimilivu wa maumivu. Akacheka zaidi lakini ghafula kicheko kilikata baada ya kupokea mapigo ya mateke kama matatu hivi kutoka kwa binti huyo. Mawili aliyaotea lakini moja lilimuingia vema kabisa na kukubali kumpeleka chini. Binti huyo akaruka juu na kuja kutua chini mithili ya Mwewe aliyetaka kunyakua kitoweo, Hudah akahama na kumuacha binti huyo atue mwenyewe chini kasha akajizunguusha akiwa palepale chini na kumpiga teke la kiuno ambalo alilikinga japo kwa uchache aliweza kulisikia. Moni akajipindua kama wale wacheza dansi wafanyavyo na kufanikiwa kukwepa mateke kadhaa ambayo Hudah alikuwa akiyarusha. Akajipindua sarakasi ya mbele mtoto huyo wa kike, Hudah akawa anatazamana na mgongo wa binti huyo lakini wakati akiwa anashambulia, ni kama binti huyo alikuwa akicheza na akili yake kwani alishajirusha juu kidogo na lile pigo likapita na kupiga hewa halafu akarudi chini binti huyo na kudunda tena kwa nguvu na kwenda juu zaidi akiwa ametanua mikono na miguu yake mithili ya Nyani arukiavyo tawi la mti ulio mbali kiasi. Hudah akakosa namna ya kufanya kwa haraka, alikuja kushtuka binti huyo anapiga pigo baya sana la masikioni mwake kwa kutumia miguu ile, akazuia lakini haikusaidia, Moni alikunjua mguu mmoja kwa kasi kubwa na kupiga nyuma ya kichwa cha kijana huyo na kumfanya apinduke vibaya huku akiugulia maumivu. Moni akatua chini kasha akajizungusha tena kwa mtindo wa namna yake na kupiga pigo jingine la kumsindikiza ambalo lilimtupa Hudah mbali kidogo hadi akatokwa na mguno wa maumivu na kutulia kimya.

Ni lazima niwatafute wote mlioniulia mtu niliyekuwa nikimtegemea na kwa hili niliapa kuwa sitawaacha hai," aliongea Moni huku akiwa ametulia akimtazama kijana huyo jinsi alivyokuwa kimya. Akiwa hajui hili wala lile, alishangaa kumuona kijana huyo akinyanyuka kwa kasi huku mikononi mwake kukiwa na bastola. Moni akajua kumbe kijana huyo alianguakia mahali ambapo ile silaha yake ilianguka mara baada ya kuikumba. ujanja akakosa, mjanja akawa ni Hudah mahala hapo akaanza kuongea kwa majigambo huku akifuta damu iliyoganda kwenye pembe ya papi za midomo yake. Akaitoa usalama ile bastola kisha akamwambia kuwa katika kazi yao wanaogopa sana shahidi, hivyo kila anayeshuhudia wanachokifanya huyo huwa hana maisha mazuri ya kuishi, ni lazima wamuuwe sasa kwa kuwa yeye amejileta kwenye kifo basi haina budi kumuua. Akajiandaa kumshuti kwa risasi lakini ghafula tu mlipuko mkubwa wa bunduki ulisikika kisha kimya kikatanda huku kila mmoja kati ya moni na Hudah macho yakiwatoka wasielewe nini kimejiri mahala hapo.

_______________________________

ITAENDELEA.

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

إرسال تعليق

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.