Notification texts go here Contact Us Buy Now!

DEREVA TAXI SEHEMU YA KUMI NA NNE (14)

TAXI DRIVER SEHEMU YA 14

Hiyo ya siku hiyo aliona huwenda ndiyo ikawa ni njia moja wapo ya kuwakaribia anaowataka lakini pia ajue ni akina nani hao anaowataka? Kwanza yeye mwenyewe ni nani? Kwanini alikuwa akimtazama Tom kwa macho ya pekee sana je, anamfahamu au ni nini ilikuwa sababu ya kumtazama kijana yule namna ile. Kizunguzungu. "Halafu ni dereva Taxi pia" akajisemea huyo dada na kunyanyuka hapo kasha akaufunga na huo mlango kwa ndani na kujitokomeza chumbani akatulia kimya.

SONGA NAYO
Kulikuwa kuna matukio mawili yaliyotokea kwa wakati mmoja na kila moja lilikuwa na umihimu katika kufuatilia ili kuweza kujua nini afanye na wapi anzie, moja na lililokuwa mbele ya ratiba yake lilikuwa ni la kwenda kukutana na askari mmoja wa jeshi la polisi mwenye cheo cha SP, ambaye alipewa taarifa kuwa kuna baadhi ya matukio ambayo yalipata kufanyiwa uchunguzi naye lakini kabla hata hajachukua maamuzi Roi, anakutana na taarifa mpya kabisa ya tukio jingine la mauaji lililotokea maeneo ya Guzo tende au Tanga pazuri au Sabasaba almaarufu tena likiwa ni la kuuawa kwa dereva Taxi. Akajikuta akipata kigugumizi cha miguu na kushindwa kufanya maamuzi ya haraka ya wapi miguu hiyo ianzie kwenda. Katika hali hiyo ya kutafakari, ikapelekea kuchukua muda mrefu sana kuwepo hapo na ndipo alipokata shauri na kuonelea ni bora kama ataenda kituoni kwanza kwani kupitia huko kuna mengi angeweza kung'amu. Akaingia garini mwake na kuondoka. Dakika tano mbele zikamkuta akiwa anaegesha gari nje ya kituo cha polisi cha Chumbageni. Akatoka na kuingia ndani ya kituo hicho. Muonekano aliokuwa nao ulikuwa ni wa kijana wa kileo kabisa aliyetoka na mavazi ya kileo kiasi kwamba usingeweza kumjua kwa wepesi kama ulishawahi kukutana naye. 

"Habari za hapa?" Akasalimia kijana huyo alipofika kwenye meza kuu ya maulizo. "Nzuri karibu, tukusaidie?" salamu hiyo ilijibiwa na mwanadada mwenye cheo cha Koplo. "Tafadhali nahitaji kuonana na SP Asna," aliongea hitaji lake Roi huku akiwa kama alikuwa akilisoma mahali jina hilo. Yule afande alimtazama huyo kijana kwa sekunde kadhaa kasha akamuuliza kama alikuwa na miadi nae na ni ya namna gani. Roi akajibu kuwa yeye ni Inspekta Raphii wa kituo cha Polisi Korogwe na yupo hapo kwa miadi ya kawaida tu na si vinginevyo. Alijibu hivyo sambamba na kuonesha kitambulisho kilichokuwa kikimtambulisha hivyo. "Ok, ni huyo hapo anayetoka ofisini imekuwa ni bahati kwako,.....Afande Asna, kuna mgeni wako hapa dada," alisema huyo binti wa hapo mapokezi huku akimuelekea huyo aliyekuwa akimpa taarifa hiyo. Kabla hata huyo anayeitwa afande Asna hajanyanyua kinywa chake, Roi akawa ameshamfikia karibu kabisa na alipo yeye, ni wazi afande huyo alipatwa na mshangao juu ya ugeni huo lakini haikuwa tatizo kwa kijana huyo. Mshangao huo ulikwenda pia kwa yule Koplo na akajiuliza kama kulikuwa na ufahamianaji juu ya watu hao.

Naitwa Inspekta Raphii Nkinda," akaonesha kitambulisho kasha akasema. "Tafadhali nahitaji kuongea na wewe mawili matatu"
"Kuhusiana na nini kiongozi?" akahoji SP Asna. "Usihofu, ni kuhusiana na hivi vifo vinavyoendelea hapa mjini na hili ni agizo la kiuchunguzi kutoka makao makuu hivyo usishangae kuona maafisa wa jeshi la polisi wakigongana kwenye hili," Akajibu Roi kasha akamtazama huyo binti usoni kwa uzuri zaidi. Alikuwa ni mrembo si hapa, sura alipewa hasa maana ilipambwa na macho mazuri, pua mdomo pamoja na mashavu yenye vishimo kimtindo au waweza viita 'Dimpoz' vishimo hivyo. Roi akameza mate kidogo kabla ya huyo binti kujibu 'Ok'. Walitoka nje hadi ndani ya gari moja Toyota Deffender ya polisi wakajifungia mlango na kupandisha vioo.

"Naitwa Roi" Jina hili likamfanya SP Asna atoe macho na kuufanya urembo wake uzidi kung'aa haswa. Jina hili analifahamu sana na kipindi kijana huyu anapambana na maharamia wa uuzaji wa silaha yeye alikuwa bado ni mdogo sana kwenye jeshi la polisi na alikuwa kwenye kituo cha wilaya ya Muheza akiwa na cheo cha Konstebo wa Polisi (PC). "Ulishawahi kulisikia mahali jina hili?" Akaweka ulizo Roi huku akiwa bado macho yake yaliyompa shida askari huyo kumtazama yakiwa surani mwa binti huyo. "Nalifahamu hilo jina na mwenye jina hilo nazijua sifa zake tu," akajibu SP Asna. "Asante, nipo hapa kwa ajili ya kinachoendelea hapa mjini, nipo kwa siri sana kwani haitakiwi mtu yeyote yule kufahamu hilo, najua wewe si mbaya na niko hapa kwa kazi maalumu pia ambayo kama utaifanya iwe tofauti nawe nitakufanya uwe wa tofauti pia sitajali," Akabadili muonekano kabisa kijana huyo huku akiwa si yule aliyeingia awali garini humo. "Taarifa ni kwamba," akaendelea. "wewe ulihusika na uchunguzi wa kifo cha aliyewahi kuwa jaji wa mahakama ya rufani mkoani hapa na pia dereva Taxi aliyeuawa usiku mmoja na jaji huyo?"
"Ndiyo," Alijibu Asna. "Ripoti zinasemaje kwenye uchunguzi wako?" Akauliza Roi. "Hakuna cha kuweza kumkaribia aliyefanya hayo kwani nilipomuhoji mke wa jaji huyo, alisema tu ni usiku wakiwa wamelala ndipo mumewe akaamka na kutoka nje na hakumwambia anakwenda kufanya nini, baada ya hapo ni ukimya mkubwa uliopoteza saa zima hadi akakutwa na hofu hapohapo kitandani na usingizi kumtenga kabisa akaamua kunyanyuka na kuchungulia dirishani ndipo akaona mumewe akiwa chini kitu kama kimiminika kikiwa kimejenga kifereji cha muda, akakurupuka na kutoka ndani, alipofika akakutana na kisanga hicho na kujikuta akipiga yowe moja na kutokujua nini kilifuata baada ya hapo," Alijibu SP Asna. "Ulimuhoji zaidi?" Roi akauliza tena.
"Ndiyo, niliendelea kumuhoji lakini hakukua na jipya maana anasema hata marafiki wa mumewe hakuwahi kuwaona wala hawajui hivyo mengi ya mumewe huwa ni siri,"
"Bila shaka majibu hayo aliyokupa ni kutokana na maswali uliyopata kumuuliza?"
"Ndiyo, alijibu kila nililomuuliza kwa ufupi ni kwamba alinipa ushirikiano mzuri tu," alijibu SP Asna. "Vipi kuhusu uchunguzi wa kitaalamu kutoka kwa madaktari na ule wa kipolisi?" Akauliza Roi akizidi kuchimba. "Kwa kweli uchunguzi wa kidakitari ni wa kawaida sana kwani ripoti inasema kuwa hakuna kilichomuua zaidi ya risasi mbili za kichwani na zote zilipita sehemu moja na hakukutwa alama zozote za vidole (finger print) Uchunguzi wa kipolisi haukugundua hilo lakini tuliporudi kwetu na kuchimbua zaidi ni kwamba muuaji ametumia risasi zinazotumiwa na Barreta Pistol na ni kwa vifo vyote viwili. Hakukuwa na alama za vidole kama tukio lile la uwanja wa ndege lilivyotukia...!"
Hilo la uwanja wa ndege likoje na utofauti wake ni upi tukiacha hili?" Akadakia Roi huku akiwa makini zaidi. "Kuna kijana tulimkuta ameuawa na maiti yake kutelekezwa chooni lakini pembeni tulimkuta na bastola ndogo aina hiyohiyo kama niliyokutajia ikiwa kiunoni mwake, tukaichukua na kwenda kuifanyia uchunguzi lakini pia kuna moja ilifikishwa hapa kituoni ikitakiwa kufanyiwa uchunguzi kama huo na inasemekana ni ya kijana huyohuyo. Tumekuta alama za vidole lakini zinazochanganya sana," 
"Kabla ya alama za vidole, ni nani aliileta hiyo nyingine ichunguzwe?"
"Mkuu hakuweka wazi alitoa agizo tu," akajibu SP Asna. Roi akajua hiyo ilitoka kwa Kichambua, taarifa hizo alizipata, hapo alitaka kujua kama hata hilo liko bayana kwa wengine?

"Naomba kuipata hiyo ripoti ya uchunguzi wa huko uwanja wa ndege hivi punde kama unayo," akaagiza Roi. "Kwa sasa Upelelezi uko mikoni mwa Inspeka Musa lakini ipo moja ambayo niliihifadhi mahali, wacha nikupe," Akasema huyo dada kasha akatoka garini na kuelekea ndani ya kituo hicho. Roi akatazama nje na kuyazunguusha macho yake, hakukuwa na kipya alichokiona baada ya kama dakika mbili, Asna alitoka akiwa na kimkoba chake cha mkononi akaingia na kukifungua akampa hiyo karatasi maalumu ya plastiki ambayo ilikuwa na alama hizo za vidole. 

"Vipi kuhusu ajali iliyotokea leo?" Akauliza Roi. "Hapa si ajali, mambo ni hayohayo na mauaji ni hayohayo pia," Alijibu SP Asna huku akionekana kutazama saa yake ya mkononi mara kwa mara Roi akamtazama akagundua kuwa binti huyo kulikuwa na miadi mahali au vinginevyo. "Asante kwa kunipa ushirikiano nadhani nitapata jambo kupitia hizi ripoti, vipi uko kazini bado au unakwenda nyumbani?" Akasema Roi kasha akachomekea mwishoni. "Naelekea nyumbani mida hii, hapa ni kesho tena, siku yangu imekwisha," alijibu namna hiyo huku akiwa ameukamata mlango wa gari tayari kushuka lakini akashangaa mkono wa Roi ukiwa kwenye mkono wake huku kidole gumba kikiwa kinachezea malaika/vinyweleo vilivyolala mkononi mwake. "Naomba nikupe lifti kama huto jali," Akachombeza pasipo kubandua macho yake machoni mwa binti huyo. Nguvu zilimwisha afande Asna akajikuta akijiweka sawa kitini na kuuliza. "Unajua ninakoelekea kwani?"
"Kama huwezi kuniambia unakoelekea hata kwangu nitakupeleka," akazidi kumvunja mifupa binti wa watu Roi. "Unavituko wewe, haya twende," Akajibu mtoto huyo baada ya kumaliza kucheka kicheko kidogo cha aibu. Wakatoka humo garini na kuingia kwenye gari iliyokuja na kijana huyo maeneo hayo wakaondoka na kuliingiza barabarani. Maneno ya hapa na pale yakawafikisha Komesho. Gari ikaingia kulia kama inayokwenda Majengo Magomeni, ilipofika mwisho wa shule mbele kidogo almaarufu kwa Zaharani, Roi akaegesha kushoto. "Unaishi mtaa huu na siyo kwenye nyumba za askari?" Akauliza Roi huku akifungua waleti yake na kutoka na kadi kazi. "Yaa, nipo mtaa huu kiongozi, nyumba za askari zimejaa na unajua kuwa sina muda mrefu tangu kufika hapa," akajibu. "Ok, si mbaya ila umakini unahitajika, askari makini kama wewe unayefuatilia mambo mazito na changamano la wana wa uswahilini ni shida sana, kamata hii kama tulivyokubaliana jioni ya leo tukutane Mtendele Hotel kwa ajili ya kuchangamsha akili," Alisema Roi akiwa anamkabidhi kadi kazi binti huyo ambaye aliipokea na kutoka garini, mwendo wake wa maringo kama vile si askari ambaye ukakamavu upo ndani yake. Umbo lenye mbinuko kwa nyuma unaolisimanga vazi la jeshi la polisi kwa jinsi lilivyombana, likamfanya Roi apige ngumi usukani wa gari na kuiwasha muda huohuo akanyoosha barabara hadi Majengo kona, akakunja kulia na kuikama barabara ya Mwanzange kuja soko kubwa la Mgandini. Moyoni akajiahidi kuwa lazima Chui atambe kwa Mbawala jioni ama usiku wa siku hiyo, alishammezea mate afande Asna na tamani la kumla lilimkaa mtimani mwake.

____________________________________

Tom alichanganyikiwa sana juu ya mauaji hayo yaliyokuwa yakitokea kila siku na alikuwa na mengi ya kufanya siku hiyo lakini aliamua kuyaweka kando na kuamua kudili na jambo hili pekee. Hakuwa mpambanaji wa kutisha sana lakini mbinu za kijanja alikuwa nazo kama kujua kuvizia, kurusha ngumi kwa kujaribu lakini mbinu kubwa ambayo Mungu alimpendelea ni mbio alikuwa na uwezo mkubwa wa kukimbia kuliko wanariadha maarufu duniani na hilo ndilo lililomfanya ajiamini hata kuingia sehemu zenye kutisha. Majira hayo ya saa kumi na mbili magharibi, kijana huyo alikuwa na gari yake maeneo ya makorora ambako ndiko makazi yake yalipo lakini hakuwa nyumbani bali alikuwa mahali ambapo mara nyingi hukutana na mtu wa kuitwa Hudah. Kwa nini Hudah? Yeye binafsi aliamini hakuna mtu wa kwanza anayehusika na mauaji zaidi ya Hudah kwani mara zote alizowahi kukutana naye alikuwa ni mtu mwenye maongezi tata yenye kutilia shaka. Alikuwa maeneo ya Makorora sokoni akaja hadi Mti mkavu alipokuwa anapita hapo kuna kitu aliona kwenye duka moja la vyakula la hapo kabla hajafika kwenye makutano ya barabara ya Makorora, Sahare na ile ya kwenda mjini. Kuna kijana alimuona na alimfananisha na mtu aliyekuwa akimtafuta, hakutaka kudharau hisia zake, akasogeza gari yake karibu kabisa na duka lile halafu akaliacha likiwa bado linaunguruma akashuka na kwenda pale dukani. "Aloo mgosi eenh! Hebu nipatie soda 'take away' ya baridii! Nikate kiu nahisi joto sana," akasema Tom huku akitoa sarafu ya shilingi mia tano lakini kwa kupitia ujanja ujanja akimtazama kijana aliyemtilia shaka. Hakuwa amekosea, alikuwa ni mwenyewe lakini kijana huyo hakuonekana kumchangamkia Tom. Haikuwa tabu mzee wa mashamsham akaona bora aanze yeye. Akamsalimia kwa bashasha za kipwani na makeke ya hali ya juu kiasi kwamba yule kijana ilikuwa ni ngumu kukataa kujibu salamu ile, akajibu kwa sura ya tabasamu vizuri tu, wakaongea kidogo hadi pale kijana huyo alipoaga. "Uko na usafiri?" Akauliza Hudah. "Hiyo hapo bosi wangu siwezi kuacha hiyo ndiyo ofisi yangu bwana," akajibu Tom. "Basi nichukue ukanitupe barabara ya Ishirini kuna jamaa yangu pale nakwenda kumcheki," akasema Hudah. Tom akamtoa shaka na kutangulia garini. Sekunde kumi na tano, safari ikawa imeanza, wakaondoka kwa mwendo wa wastani lakini wenye kuwahi, punde wakawa eneo husika Hudah akashuka baada ya kulipa shilingi Elfu mbili kasha akaomba kukutana na dereva Taxi huyo siku inayofuata. Tom akakubali dili hilo na kuondoka lakini alivuka mtaa mmoja tu yaani kutoka ishirini hadi kumi na tisa, akaja akasimama barabara ya kumi na nane, akaliingiza gari chobingo kasha akashuka na kurudi alikotoka kwa mwendo wa haraka nusu kukimbia nusu kutembea hadi alipomshusha Hudah. Akazunguuka nyuma ya nyumba moja ambayo kwa mbele kulikuwa na fundi viatu pamoja na kijiwe cha Kahawa na Tangawizi hasa nyakati kama hizo za kuzama kwa jua. Alikuwa akienda kwa tahadhari kuu mno na alipofika kwenye nyumba ya nyuma akasikia sauti ya mlango uliokuwa ukifunguliwa na alipochungulia, akawaona vijana wawili waliokata mwili na misuli yao kututumka ni kama walikuwa wakitoka kufanya mazoezi. Walivaa fulana za kukata mikono ambazo walizikata wenyewe kienyeji na kufanya roho mbaya ya kukataa kumpelekea fundi cherehani ridhiki. Mh! Akagumia kasha akavuta hatua na kutoka eneo hilo. Alichokiona ndicho alichokikusudia kukiona sasa kazi ilikuwa ni moja tu ya kujua Hudah ni nani na kwanini anamhusisha na mauaji yanayoibuka kila mawio na machweo.

Usiku wa saa tano kama na nusu hivi, ulimkuta Hudah na wale jamaa kwenye gari ndogo wakielekea maeneo ya bandarini. 

ITAENDELEA.

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.