Notification texts go here Contact Us Buy Now!

DEREVA TAXI SEHEMU YA KUMI NA MBILI (12)

TAXI DRIVER SEHEMU YA 12
Saa 8:00

Ndiyo, kila mtu wetu wa kazi amekabidhiwa soksi maalumu za kuvaa mikononi, soksi hizo zimetengenezwa kwa mfumo wa pekee sana na endapo mtumiaji akizitumia eidha kwa kufanya mauaji ama vinginevyo, alama za vidole (finger print) zinabaki lakini si za watu walio hai," Alijibu huyo mtu mwenye kitambi kimya kifupi kikatanda eneo hilo kabla ya mtu huyo mwenye kitambi kikubwa kusema tena kwa kuhitimisha. "Huo ni mwanzo wa kuwa hali si shwari na inavyoonekana kuna wanausalama wameingia kazini au kuna yeyote anazo taarifa za mahali walipo wale wazee waliokuwa wakifuatiliwa?" Lakini akauliza mwishoni. "Hadi sasa wazee wale hawajulikani walipo na hata kule walikokuwa wakiishi pia hawapo siku hizi nyumba imekuwa kimya sana kiasi kwamba hadi ukimya huo unaogopesha lakini kati ya hizi nyumba mbili moja pekee ndiyo imefungwa kabisa na moja kunaonekana kuwepo kwa mtu japo haina uhakika sana," Akajibu huyo kijana. "Ngoja taarifa hizi nimfikishie mkuu endapo akinipa muongozo basi lazima nyumba hiyo inayotiliwa mashaka ivamiwe," akasema huyo bwana mwenye kitambi kasha akanyanyuka na yule kijana naye akanyanyuka na kutoka mule ndani. Wakaifuata korido nyembamba na ndefu ambayo iliwatoa hadi nje huko wakaingia kwenye chumba kimoja cha nje na kumkuta binti mmoja hivi ambaye alikuwa akiendelea na kazi zake za uchapaji kwenye kompyuta yake. "Natoka nikirudi utanipa taarifa za kila aliyefika hapa hata kama haja niulizia," akaagiza bwana huyo mwenye kitambi. binti huyo akaitikia kwa kichwa na kuendelea na kazi. Gari yao iliwapeleka hadi Raskazone kwenye lile jumba la yule mzee wa kiarabu aliyekuwa akiificha sura yake muda wote. Walipoingia ndani wakakaribishwa na binti mwembamba mrembo wa kiarabu pia ambaye aliwaingiza hadi ndani. Binti huyo alikuwa amevaa vazi refu jeusi (Baibui) lakini hakuwa amevaa nikabu usoni mwake bali alivaa hijabu tu yenye kuweza kuionesha sura yake ya duara iliyopambwa na macho yaliyopakwa wanja kirembo zaidi huku mboni za macho yake zikiwa na rangi ya buluu yenye kumeremeta. Aliwafikisha watu hao hadi kwenye sebule kubwa na walipofika hapo walikuta kikao cha watu watatu kilichokuwa kikiendelea upenuni mwa sebule ile. Kikao hicho kilikaliwa na mzee yule ambaye hakuwa akipenda sura yake ionekane lakini siku hii alikuwa amevaa mawani ya jua na kofia kubwa ya pama akiwa ameifunika hadi karibu na macho yake kiasi cha kutoweza kumtambua kwa haraka. Kikao kile kilisimama kwa muda baada ya watu wale wawili kuingia pale huku yule binti wa kiarabu mwenye urembo wa haja akiwa amesimama pembeni nyuma ya wale watu wawili.

"Niliwaona tokea nje mkiwa mnakuja, si kwa miadi na huwa sipendi ujio wa namna hii kwangu hata kama kuna jambo la msingi ni lazima ngazi nilizoziweka zifuatwe, hujui mtu wa kumfuata na kumpa habari zinazotakiwa kunifikia mimi James?" Akaongea yule mzee huku akiwa anatazama mezani kanakwamba anaongea na simu. "Najua mkuu!" Alijibu kwa hofu kidogo yule bwana mwenye kitambi ambaye hapo alitambulishwa kama James. "Hii ni nini sasa? Dharau, makusudi au niiweke kwenye tafsiri ipi? Halafu kwa ulivyo na akili ya kipumbavu umekuja na huyu kibaraka wako. Nadhani niliwahi kusema kwenu kuwa mtaishi kwa madaraja kufuatana na kazi yenu na niliweka onyo kali sana kwenu kuwa sitamuacha hai mtu endapo ataleta uzembe. Huu ni uzembe mkubwa sana James lakini kwa kuwa wewe ni mtu muhimu kwangu na upo kwa kazi maalumu ya kuweza kusaidiana na vijana wengine, umeachwa huru lakini huyo kibaraka wako uliyekuja naye,......Sara...!" Akaita huyo mzee kwa sauti kubwa na nzito kiasi baada ya kuongea mlolongo mrefu wa maneno kasha akakamata gilasi ya kinywaji na kuiweka kinywani mwake akaigida yote na kuitupa ile gilasi mezani ikiwa haina kitu. Akachapa vidole vyake kwa mtindo wa pekee sana kiasi cha kufanya sauti ya kama kuvunjika kwa vijiti lakini sauti hiyo iliendana na kishindo cha muanguko wa kijana mtumishi wa mtu yule wa kuitwa James baada ya pigo moja la nguvu lililopigwa shingoni na kuivunjilia mbali shingo hiyo. Sauti ile iliyotoka vidoleni kwa mzee yule haikuwa ikiashiria pigo lile la! Bali ilikuwa ikiashiria kuongezwa kwa kinywaji ambacho kile cha kwenye gilasi alishakimimina tumboni mwake. Sara binti yule mrembo ndiye aliyetekeleza lile pigo na hiyo ni baada ya kuitwa kwa jina lake na yule mzee hiyo kwake ilikuwa ni kama taarifa. Huyu binti ndiye aliyeonekana siku zilizopita usiku akiwa na Hudah ambaye kwa jinsi alivyoonekana alikuwa ni kama mtu kutokea huko bara ulaya kwa jinsi nywele zake alivyokuwa ameziweka. Ukimtazama kwa wasiwasi binti huyo hakika unaweza ukasema ni mpole na mwenye ucheshi wa kuzidi lakini si hivyo, alikuwa na sifa ya ukatili uliofanikiwa kujificha ndani ya urembo alionao. Huyo ndiye binti pendwa na mwenye kujibebea naye sifa kemkem wa mzee Hasheem Mahmood. Mzee ambaye ndiye mwenye kuificha sura yake mara kwa mara, hakupenda kuonekana ama kutambulika sura yake kwa haraka kiasi hicho. Mzee huyo alishawahi kuwa mkuu wa jeshi la polisi huko kisiwani Zanzibar hadi pale alipokuja kustaafu cheo hicho kisha kujiingiza kwenye biashara, alishawahi kuwa mfanyabiashara mkubwa sana ambaye alitambulika Tanzania nzima na alifafanikiwa kumiliki umaarufu mkubwa na pia kupata mafanikio makubwa sana kupitia biashara hiyo aliyokuwa akiifanya. Baada ya kudumu kwenye biashara kwa takribani miaka sita na kupata utajiri mkubwa kutokana na biashara ya usafirishaji wa madini mbalimbali kwa njia za panya na zile chache za halali, akaja kupotea kabisa machoni mwa watu mzee huyo na kutimkia kisiwani Komoro. Kila mmoja alisema vyake kuwa mzee huyo ameamua kwenda kufanya makazi ndani ya kisiwa hicho baada ya kujinufaisha na biashara kubwa aliyokuwa akiifanya lakini kumbe usilolijua ni sawa na usiku wa kiza, siri ilikuwa nafsini mwake wala haikuwa dhahiri kwa watu. Mzee mahmood aliifanya Komoro kuwa kama njia ya kupita akaenda kuishi nchini Somalia kwa karibia robo muongo akijifunza matumizi ya silaha kubwa kubwa za kivita na mbinu za kuweza kufanya biashara kubwa za kupitisha silaha za kivita kwenye mipaka mbalimbali ya nchi hadi kuweza kuuzwa kwenye nchi ambazo zilikuwa zikipambana na vita za wenyewe kwa wenyewe. Huko akafanikiwa kukutana na watu wawili ambao walikuwa ni matajiri wakubwa wanaojihusisha na biashara hizo haramu, mmoja alifahamika kwa jina la Othman Hussein na mwingine aliitwa Abubakar Mahmud. Hawa wakawa ndiwo marafiki zake wakubwa sana na walioweza kumfunza mbinu nyingi za kiharamia. Aliposema anatokea Tanzania tu basi ikawa ni nafasi nzuri kwake kuweza kuchangamana na watu hao kwani ni miaka mingi walikuwa wakitamani kuingia Tanzania na kuweza kuchuma vilivyomo kwa siri bila wazawa kujua lakini waliogopa usalama wa nchi hii ulivyo mahiri wakakosa namna, sasa ujio wa mtu huyo kwao ikawa ni jambo jema sana. 

Baada ya bwana Hasheem kuishi Somalia kwa muda huo, akaondoka na kupelekwa nchini China kwa makusudi maalumu na baada ya miaka mitatu kukatika akarudi Tanzania ndani ya jiji la Tanga kwa siri kubwa bila mtu yeyote kujua kama bwana huyo amerudi nchini. Miezi mitatu ikapita baada ya kurudi nchini kasha akapokea ugeni wa maandishi ambao ulikuwa ukimtaka msaada na huo ulikuja kwa ombi lakini ndani kukiwa na ulazima ama shinikizo. Ujumbe huu ndiyo uliopelekea yeye kuanzisha vikundi vitatu jijini Tanga, kikundi kimoja kikiwa kinahusika na kuwaondoa watu ambao yeye akiambiwa kuwa ni miiba ya kazi yao, basi hutafuta njia ya kuikwangua. Yeye kama yeye akahusika na kuliongoza kundi la mauaji ya mzee Kambo, akiwa na vijana wake anaowaamini lakini bubu, yaani anawatumia kwa malipo maalumu na si kukaa nao pamoja. Pia kazi ya kumuondoa master Dao duniani, kazi hiyo ilifanywa na kundi hilo namba moja likishirikiana na mtu asiye na kundi maalumu kati ya hayo matatu. Aliyefahamika kwa jina la hudah. Kundi namba mbili alilipanga kwa kazi ya kuhakikisha usalama wa kazi yao unazidi kuimarika huku wakihusika kuwandoa duniani wale wote wanaowatumia au kuwaona ni hatari baadaye. Kundi hilo la pili likahusika na mauaji ya madereva Taxi na baadhi ya raia ambao waliingiliana na kazi zao. Kundi la tatu na mwisho hili lilikuwa halina kazi maalumu na hili ndilo lililokuwa likiongozwa na Hudah mwenyewe japo alikuwa na uwezo wa kuingia kwenye kundi lolote na wakati wowote apendao. Kundi hili la tatu halikuwa na watu wengi na ndani yake alikuwepo pia Sarah binti wa mzee Hasheem akiwa kama kiongozi.

Alijua fika kuwa wakati yanatokea hayo yeye hakuwepo hapa Afrika lakini kwa kuwa alikuwa tayari wanaukaribu na watu hao ikawa haina budi kuweza kukubali kuonesha ushirikiano katika kuwasaidia watu hao. Aliambiwa sababu kuu ya msaada huo ambao chimbuko lake lilitokea miaka mitatu ama miwili iliyopita. Kubwa na la msingi ni kufanya kila linalowezekana kuweza kuwafanya watu wawili walioshikiliwa na jeshi la polisi nchini humu baada ya wengine kuuawa wawe huru. Akaambiwa pia watu hao wapo kwenye mahabusu ya siri sana ambayo hakuna mtu yeyote yule anayejua uwepo wa mahabusu hiyo ndani ya gereza la maweni jijini Tanga. Na inasemekana kuwa walihifadhiwa hapo kwenye gereza la maweni ili iwe ngumu kwao kuweza kutoroka kwa wepesi kutokana na ulinzi wa asili wa magereza hayo. Akakubali kuifanya kazi hiyo lakini tangu kupewa kazi hiyo ya uchunguzi wa kujua ni wapi wameweza kuhifadhiwa watu hao, hakufua dafu. Alitumia mbinu nyingi kama kuingiza watu gerezani kwa siri akicheza mchezo mchafu na wakuu wa magereza kwa kutumia cheo chake cha zamani huku akiifanya hiyo kuwa siri kubwa kwake lakini hakuna kilichoambuliwa na badala yake aliambiwa watu hao wapo na walikuwa wakiishi salama kabisa bila shaka lolote na walihifadhiwa sehemu yenye ulinzi mkali sana. Na hata kikao hicho kilichovamiwa na James pamoja na kibaraka wake, kilikuwa kikijadili mbinu mbadala za kuweza kufanya kabla ya kuwaruhusu wenyewe kuweza kuingia katika kazi hiyo. Hapo ilikuwa ni bora kuuwa watanzania mia moja lakini watu wawili Haji Shaiff na Habibu Suleiman wawe hai na warudi nchini kwao wakiwa salama. Hii ni kazi kubwa lakini kwake mzee huyo aliiona ni nyepesi sana kutokana na kuvijua vichochoro vingi na mbinu nyingi za kipolisi sababu zikiwa ni kwamba hata yeye alikuwamo humo kabla ya kustaafu.

Vijana wawili walifika mahala hapo na kuuchukua ule mwili wa yule kijana wakatoka nao huku mabinti wawili wakiingia na kufanya usafi eneo lile kama vile kulimwagika damu kasha Hasheem mzee wa kuficha sura yake akamgeukia James na kumuuliza ujio wake. 

"Kijana uliyeniagiza nimtume Dar es salaam kwa ajili ya kuwafuatilia wale wazee, amepoteza maisha uwanja wa ndege wa jijini hapa na maiti yake kukutwa chooni ikiwa na matundu matatu ya risasi sehemu mbalimbali za mwili wake," Wale wazee wawili waliokuwa wamekaa na mzee Hasheem wakakumbwa na mshtuko lakini Hasheem aligeuza macho yake pembeni na kuyarudisha tena kwa meza ile. "Usalama?" Akauliza. James akajibu. "Usalama upo tena mkubwa sana kwani simu aliyokuwa akiitumia kuwasiliana na mimi nilifanikiwa kuiharibu mapema kabisa mara baada ya kuhisi hatari,"Fantastic boy," Akasifu mzee Hasheem akauliza kama waliokuwa wakifuatiliwa kama wameweza kupatikana, jibu alilopewa ni kwamba wazee wale hadi muda huo hawajulikani walipo na hata makazi yao yapo kimya ispokuwa jingo moja tu ndilo wanalitilia mashaka. "Nilijua tu ni lazima iwe hivyo kwani nawafahamu wale tangu wakiwa kazini, ni wasiri, makini na wanaojua wanafanya nini. Nadhani kwa taarifa hiyo waliyoiacha ni kwamba wapo kazini, sasa mimi nataka kuwaonesha kuwa nimekuwa makini zaidi yao. Tunapeleka mashambulio mawili kwa wakati mmoja, Hudah na Sara watawapa pigo jingine kwa dereva Taxi mwingine au raia huku wewe ukiwa na vijana makini utakao watuma kwenye nyumba mlioitilia shaka," Alisema Hasheem kasha akatulia kimya huku akiwatazama wale wazee wenzake aliokuwa akijadili nao jambo mahala hapo. James akatoka humo ndani na kurudi nje ambako alichukuwa usafiri uliowafikisha hapo wakiwa wawili na sasa mwenyewe, akapotelea mitaani. Huku ndani kikao kile kiliendele mara baada ya Sara pia kutoka mahala hapo.

"Pale tulipokomea nadhani mnakumbuka niliwaeleza nini, ile ilikuwa ni vita kubwa sana mara baada ya lile sekeseke la dereva Taxi Kwisha, Vita hiyo ilipiganwa na watu wenye uweledi mkubwa sana. Nchi ilisimama kwa mara moja, vijana wengi tukawapoteza kwenye mapango ya Amboni mara baada ya kutumwa makomandoo kule wanaoaminika na serikali hii kule mapangoni. Haji Shaiff na Habibu Suleiman wakaweka tishio la kuwataka wanausalama wa nchi hii wawaache waondoke zao na mali zao ambazo walizishikilia kipindi cha sekeseke lililovumbuliwa na dereva Taxi ambaye hakuna aliyemtambua hata jina lake na ndiyo maana hata sasa tunawaangamiza madereva Taxi kwa sababu nao wanahusika kwenye hili. Nchi hii ni ya ajabu sana kwani usishangae hata muokota makopo barabarani akawa ni shushu mbaya sana na ndiyo maana nawaambia vijana wangu mara zote pigeni hata Paka anayewashangaa, hawatakiwi kuamini kiumbe yoyote yule anayeivuta pumzi hii vema. Kitisho kile kiliwatikisa kiasi wakataka kuziachia zile gari ambazo zilikamatwa na silaha pamoja na meli ambayo iliandaliwa maalumu kwa ajili ya kuusafirisha mzigo ule wa silaha ambao ulikuwa ukivushwa tu kwenye bahari ya Hindi. Vijana hao wawili wakawakamata wanawake na watoto kasha wakajirekodi nao wakiwafanyia ukatili wa kutisha. Waliwaingilia kimwili wanawake waliowapenda na kuwachinja pamoja na watoto wale kasha mkanda wa video ule wakautuma kwenye mtandao wa kijamii na mwingine wakiusambaza kwenye vituo vya polisi mbalimbali. Mikanda hiyo ilikuwa ikishinikiza kuachiwa kwa Mali zao kwani hazikuwa za nchi hii bali zilikuwa zikitaka kupita tu. Serikali na watu wake ilivimba si kidogo na kuapa kutowaacha kabisa vijana hao. Pia vijana wale waliwatikisa wakuu wa usalama baada ya kushika sehemu muhimu kama kutishia kuilipua kambi ya jeshi ya Pande, Bandari pamoja na kuharibu kiwanja cha ndege. Kitu kinachonifanya niwe makini zaidi hata sasa ni kuhusu utendaji kazi wake wa kiusalama wa nchi hii. Pamoja na kitisho kile lakini Jeshi halikujibu chochote na badala yake wakatumwa watu wawili tu ambao hawakuwa vijana lakini uwezo wao ulikuwa mkubwa sana. 

ITAENDELEA.

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

إرسال تعليق

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.