TAXI DRIVER SEHEMU YA 20
Ok, bado inasomeka mahala hapo na ni ndani ya nyumba ya ghorofa maana inaoneka kwa juu ni jingo lenye namba BJ 38." akatoa maelekezo kijana huyo huku akisisitiza zaidi kuwa akifika karibu na msikiti wa ijumaa atamuelekeza zaidi. Safari ikawa inazidi kusonga huku ukimya ukichukua nafasi kwa asilimia kubwa. walipokuwa wakiukaribia msikiti huo, radio Call ikaunguruma, maneno kadhaa yasiyoeleweka yakawa yanasikika kasha sauti ikasikika ikisema. "Kiongozi alama fuatiliwaji imepotea machoni mwetu hatuioni kabisa, ni dakika moja tu baada ya kuwa tukitaka kukutaarifu ilipo, ghafula ikapotea machoni mwetu," ilisema sauti hiyo kutoka redioni. "Itakuwaje sasa hii, maana tumekwisha kukaribia eneo la tukio kwa majira haya?" aliuliza Inspekta Musa. "Itakuwa ngumu kujua kiongozi ni nyumba ipi na hata kama mmejua, mtakapovamia bila kujua, madhara yake yanaweza kuwa makubwa kwani mtamfanya adui awatambue ninyi mapema kuliko ninyi kumtambua yeye,"
"Hilo nalifahamu na siwezi kufanya mambo kizembe namna hiyo," Alijibu Inspekta Musa. Ikabidi zoezi hilo la kumfuatilia mtu huyo liishie hapo kwani haikujulikana sababu za mtu huyo kutokuoenekana ni zipi. Huwenda labda kutokana na kuwa tayari ilikuwa ni usiku hivyo akawa amezima simu kwa ajili ya kupumzika. Hayo yote yalikuwa ni mawazo yao ambayo hawakuwa na uhakika nayo kwa asilimia zote.
_____________________________________
Saa 9:25 Asubuhi. Ilimkuta Roi akiwa ametulia maeneo ya Majengo ambako ndiko jingo lake jipya alilokabidhiwa lilipo. Asubuhi hiyo alikuwa mezani akiwa na kikombe cha kahawa akiwa anachoma tumbo huku mkononi mwake akiwa amekamata simu ndogo na mbele yake kulikuwa na kompyuta mpakato akisoma baadhi ya mambo na kujaribu kuyaweka sawa mengine. Baada ya kama nusu saa hivi akawa amesogeza kikombe cha kahawa ile aliyokuwa akiinywa pembeni na kuendelea na kile kilichopo kwenye kompyuta. Pia hakudumu sana akaizima na kutulia kwa sekunde kadhaa huku akikiangalia kile kikombe cha kahawa ambacho kilikuwa na kahawa nyingi tu ndani yake lakini haikuweza kunyweka tena maana ilikuwa imekwisha kupoa tayari. Hilo halikumduwaza sana, akachukua simu yake nyingine na kumpigia mtu amtakae kwa majira hayo. "Cat fika hapa majengo mara moja kuna kazi natakiwa kukupa," akasema Roi mara baada ya kuiweka simu ile sikioni. "Naegesha gari muda si mrefu hapo," alijibu Cat kasha simu ile ikakatwa, sekunde kumi nyingi, gari ndogo nyeupe, ikaingia baada ya maelekezo mahali ambako anaegeshea magari kijana huyo. Roi akatoka ndani mbio na kuelekea mahali ilipo gari hiyo, alipofika alikuta Cat akiwa ameshatoka garini tayari. "Umepajuaje hapa wewe?" akahoji kijana huyo machachari. "Umesahau ahadi yetu ya awali kuwa ulipo nipo," akasema binti huyo huku akielekea ndani ya jingo lile mithili ya mtu mwenye haraka sana. "Inamaana unakuwa nyuma yangu kila muda?" akahoji tena. Cat akasimama na kugeuka akiwa anamuangalia usoni akajibu. "Ndiyo, hata ulivyo kwenda na marehemu SP Asna Mtendele Hotel nilikuwa nyuma yako. Nafikiri ule ndiyo ulikuwa ushahidi wa mwisho kukupa, wajinga walishamlia shabaha, aisee!" Roi akashusha pumzi nyingi sana baada ya kusikia jambo hilo akaanza kuona uhatari wa kufanya kazi moja na mpenzi wake, hakupenda kufuatiliwa katika maisha yake kwa kiasi kikubwa sana. Akajuta kuwa pamoja na Catherine kwenye kazi hiyo. Akamtazama kwa macho ya kuchunguza kama kuna kitu kingine cha ziada aliona na alikuwa akikificha lakini hakung'amua hilo na binti huyo alishageuka na kuelekea ndani hadi sebuleni pale alipokuwa amekaa Roi akipata kahawa, naye akaketi hapo juu ya meza. SP Asna asingekufa, ningetafuta jibu la kumpa huyu mwanamke maana nisingeondoka pale hadi asubuhi. Akajiwazia akimtazana usoni. "Hakuna muda wa kuwa pamoja tena kwenye hili mpenzi," alisema Cat. "Unamaanisha nini? Kuna boya amekupenda na wewe umempenda tayari?" akahoji Roi akiwa anamtazama binti huyo mrembo kwa macho ya kupepesa. "Hakuna kitu unawaza Roi ni kuibiwa tu, kuibiwa na wewe, hivi atakaye kuibia wewe ni nani, kijana mwenye uwezo wa peke yako kwenye anga la kitanda," akasifia Cat.
"Acha kunipaka mafuta kwa mgongo wa chupa mpenzi....nini kimejiri au ni ile ambayo ulinigusia?" akauliza. "Haswaa! Babu amenipigia na kuniambia hadi ikifika jioni ya leo, niwe kitengoni. Yaani nisiwe Morogoro tu bali niwe kitengoni. Amesema kuna kazi kubwa na muhimu ambayo natakiwa kuifanya na nitakwenda kuijua huko huko nikifika," akasema Cat. "Babu huwenda amejua ukiwepo huku hakuna kazi itafanyika?"
"Hapana, Babu anatuaminia sana hasa tukiwa pamoja huwenda kuna kazi kweli," akasema Cat huku akimtazama kijana huyo usoni. "Ok, sawa hayo ni maamuzi ya refalii bwana mchezaji hana ubavu wa kupinga," akasema Roi kasha akanyanyuka lakini hapo hapo Cat naye akanyanyuka kasha akamkumbatia kijana huyo huku akimwambia kuwa ujio wake hapo ni kwa lengo la kwenda kumuaga tu. Hakukuwa na muda wa kupoteza na hata hiyo kazi aliyotaka kumpa ni vema angeisitisha, watu hao wakaanza kushikana hapa na pale, mara kunyonyana ndimi hatimaye wakasahau kuwa hapo ni sebuleni, wakaharibu utaratibu na kuondoa maana ya neno chumba, wakashusha nguo hapo na kuingia kwenye mchezo wao wa kikubwa. Saa moja mbele kila mmoja alikuwa ameridhika na kile alichokifanya au alichofanyiwa na mwenzake, wakaoga na kuagana kila mmoja akimtakia mwenzake kazi njema.
Saa sita juu ya alama, Roi ilimkuta majani mapana nje ya jingo namba 113 ambako ndiko kazi yake ya kumchunguza kijana aliyekuwa akimfuatilia mzee Kichambua itakapoanzia. Hiyo ikiwa ni baada ya kutoka Magomeni Kondoa pia kiuchunguzi na kukuta hakuna cha maana alichoambua kwa mtu anayeitwa Amos Tumbo, akaamua kujaribu na hapo kabla ya kushika jambo jingine. Nyumba hiyo ilikuwa ni ya kawaida sana na ilikuwa imejengwa kwa muundo wa kibiashara. Ilijaa wapangaji wengi sana. Nje ya nyumba hiyo alikuta watoto wa malika mbalimbali wakiwa wanacheza michezo mbalimbali. Hakutaka kuwauliza, aliwapita na kuingia kwenye mlango mdogo ambao ulikuwa ukimpeleka upande wa nyuma ambako kulikuwa na banda la uwani ambako pia kulikuwa na wapangaji. Alipofika huko akawakuta akina dada wawili waliokuwa wamejipara vya kutosha sana wakiwa waketi kishakunaku, akawasalimia nao wakaitikia kwa bashasha huku wakisitisha kile walichokuwa wakikifanya na kumkirimu mgeni. "Karibu kaka tukusaidie!" alizidi kukaribisha dada mmoja mwenye lafudhi ya kipwani pyua. "Asante," akajibu Roi huku akiwa anawatazama kwa zamu mabinti hao kasha akauliza tena. "Samahani ninyi ni wenyeji wa muda mrefu hapa au ni wenyeji wa mtaa huu?"
Mimi hapa hapana, sina muda tangu kufika hapa labda mwenzangu?" Binti mmoja kati ya wale wawili alisema, alikuwa mweupe pee! Ulikuwa si weupe wa asili japo alikuwa nao huo weupe ila kauzidisha na weupe wa dukani hadi ukakithiri na kumchukiza. "Mimi ni mwenyeji wa mtaa huu na mpangaji wa muda kidogo hapa," akasema huyo dada wa pili ambaye alikuwa na rangi ya maji ya kunde, mwembamba kiasi huku akiwa amesuka nywele kwa mtido wa kizamani wa Kilimanjaro ambao ulimtoa kirembo zaidi. "Ok, asante dada nadhani unaweza kunisaidia shida yangu....nilikuwa namuulizia mtu mmoja anafahamika kwa jina la Janga alikuwa ni rafiki yangu mkubwa kidogo kipindi hicho niko shule ya Usagara Sekondari pale," akasema Roi, mguno mdogo ukamtoka yule dada na kuangusha kichwa na macho yake chini. Alivyoonekana ni wazi alikuwa akimfahamu lakini huwenda mtu huyo akawa hayupo au kuna janga limemkuta kama jina lake. "Kiukweli kaka yanguu, mh! Hujawahi kukutana naye muda mrefu eenh?" Akaulizwa Roi na dada yule. Roi akajibu kuwa ni muda mrefu sana hajawahi kuonana naye kama ambavyo alimueleza awali. Akatazama chini kwa muda wa kama sekunde tatu hivi na alipokinyanyua tena kichwa chake, akawa anakisugua kidevu chake kirefu kidogo kwa kidole cha shahada huku akisema. "Nijuavyo mimi mtu huyo alishafariki dunia", akasita baada ya kusema hayo huku akimtazama Roi usoni kama kunamshtuko wowote ambao kijana huyo atauonesha. Roi akawa kama amepatwa na jambo asilolielewa hapo kwa jinsi alivyoduwaa kwa muda na kutikisa kichwa kushoto na kulia kukataa jambo lile, ni kweli aliyekuja kumuulizia ni marehemu aliyepoteza muda wa miaka kadhaa iliyopita sasa hapo alitaka kujidhihirishia kuwa kweli mtu huyo alikufa kwa siku hizo chache au kitambo kingi kama tafiti zao zinavyosema. " Alikufa?" akauliza kwa kushtuka. "Ndiyo, alishakufa huyo", akajibu huyo dada. " Hivi karibuni au?" akauliza swali hilo likiwa kama mtego kwake. "Hivi karibuni!, akasita kuendelea na kugeuka upande wa mlango wa nyumba kubwa ambako kulikuwa na mzee mmoja aliyekuwa amejifunga khanga ya kitenge kiunoni, bila shaka alikuwa katika maandalizi ya kwenda kuoga. Vazi hilo watu wa pwani hulitumia aghalabu mara wakosapo Saluni. "Eti, baba, Janga tangu afe ana muda gani?" akauliza huyo dada baada ya kumgeukia huyo mzee. "Janga huyu mtoto wa aliyekuwa mwenye nyumba hii?"
"Ewaa! Hakika mzee wangu huyo huyo", akadakia Roi akiigiza kuwa alikuwa akimfahamu kabisa mtu huyo tena kwa undani mkubwa sana lakini kumbe sivyo alikuwa akicheza na akili za watu hao pasipo wenyewe kujua kama walikuwa wakichezewa mchezo wa kipelelezi. "Huyo kijana anayemuulizia Janga ni nani kwani Asia maana tusije tukawa tunaropoka tu kumbe kuna jambo baya lipo nyuma ya hili na tukajikuta matatizoni, maana siku hizi wanausalama wanaibuka kila siku....eti, kijana ni nani wewe na huyo Janga ni nani kwako?" akauliza swali moja kwa watu wawili lakini akiwa na maana kuwa kijana aliyepo hapo ndiye aliyepaswa kujibu hilo swali. "Alikuwa ni rafiki yangu mkubwa sana kipindi hicho mimi nasoma shule ya sekondari Usagara", akajibu Roi. Mzee huyo mwenye kitambi kidogo akashuka ngazi ya mwisho aliyokuwa amesimamia na kupiga hatua hadi hapo alipo Roi na kusimama huku akiwa anamtazama kijana huyo usoni. "Janga baada ya baba yake kufariki dunia miaka kama ishirini na moja, ishirini ama kumi na kenda iliyopita, yeye na nduguze wakaingia kwenye mgogoro wa mali na kutaka kugawana mali zote alizoacha marehemu baba yao. Mgogoro huo uliafikiwa kwa kuuza kila kitu na kugawana fedha ambazo yeye binafsi aliamua kuzifanyia ujana hadi zilipokwisha huku wenzake wakifanya ya maana. Alipomaliza akawa tegemezi kwa ndugu zake wakamchoka na kumtimua akahamia mitaani. Akaanza uteja wa kubwia unga na uvutaji bangi hatimaye akawa kibaka mzuri tu. Barabara ya kumi na nne, kumi na tano hadi kumi na sita wakawa wanamjua vizuri tu na si kumjua pekee, ulikuwa ukisikia jina la Janga kama huja jiepusha unakutwa na majanga kweli lakini ya wapi sasa! Ngoma ikavuma kwa mshindo mwishowe wa kupasuka
umefika. Bwana mdogo yule akaangukia pua vijana wenzake wakamkamata na kumsweka kwenye gurudumu la trekta na kumlipua na moto akafa kifo kibaya kabisa na mimi ndiye niliyeinunu nyumba hii. Sasa ni miaka kama si kumi ama nane bahati, tangu kijana huyo kupoteza maisha", aliongea mzee huyo. Roi akainamisha kichwa chini akiwa na masikitiko makubwa sana lakini ubongoni mwake kukiwa na zaidi ya hilo, mengi yaliyokuwa ubongoni mwake ni je, kama Janga alifariki miaka kumi iliyopita, Janga huyu aliye uawa uwanja wa ndege aliyekuwa akimfuatilia Kichambua ni nani? Alikaa kinywa wazi kwa takribani dakika moja nzima akiwa na huzuni nje lakini ndani kukiwa na mchanganuo mkubwa wa kazi yake. "Daah! ama kwa hakika yaliyomkuta ni makubwa, asanteni sana jamani nashukuru sana kwa kuweza kunipa ukweli maana ni muda sana sikuwahi kumtia machoni, asante sana mzee wangu", alishukuru Roi huku akiwa anapiga hatua za taratibu nyuma kutaka kuondoka. Akakaribishwa hapo na mwishoe akatoka nje akachepukia kwenye nyumba ya kwanza na pili kasha akatoa simu mfukoni na kupiga mahali. "Amiri jaribuni kulichimbua hili jambo kinagaubaga, huyo kijana si yeye kunamchezo hatarishi umepangwa madhubuti hapa na sasa naona jinsi mambo yalivyo siriazi, naomba mnipe majibu ya chimbuzi hizo haraka sana",..................."Ndiyo, angalieni itakavyokuwa kisha mnipe majibu ya haraka zaidi",..............."Ok, sawa", akakata simu baada ya kusema hayo kasha akachukua usafiri na kutereza.
Kimya kilitanda hadi walipoingia ndani kwenye nyumba aliyokuwa akiishi Tom hapo Moni alijikalisha kitini na kutulia. yeye aliamini kwa asilimia kubwa kabisa kuwa dereva Taxi huyo hakuwa mtu mbaya na alikuwa na harakati ya kuwatafuta wabaya wanaohusika na mauaji yao kiholela hivyo alijiaminishia usalama mkubwa mno kutoka kwa kijana huyo lakini kwa upande wa Tom yeye alikuwa haamini wala usalama wake hakuupa asilimia kubwa japo binti huyo alikuwa upande wake kutokana na kuweza kumsaidia kutoka kwenye kifo kilichokuwa kikimyemelea huku akisema kuwa anamfahamu. Kila akikumbuka maneno ya binti huyo kuwa anamfahamu, kichwa kilimuuma na kilikuwa kikitaka kujua ni wapi aliwahi kukutana na mtu huyo. Akafungua friji na kutoka na chupa moja ya bia kasha akamsogezea binti huyo. "Unaonekana umlevi sana?" akahoji Moni. "Hapana si hivyo ila zipo hapa kwa ajili ya kupunguza msongo wa mawazo", akajibu Tom. Moni akamtazama kijana huyo kwa jicho la kuibia kasha akainamisha kichwa chini alipokuja kukiinua, akakizungusha kwenye ile sebule yote. "Unaishi mwenyewe kwenye nyumba hii?" akauliza Moni. "ndiyo, ni mwenyewe na hakuna mpangaji hata mmoja. "Ni nyumba yako hii?"
"Hapana nimepanga na ni vyumba viwili na sebule japo nimejenga lakini nimeamua kupanga na nyumba yangu nikaweka wapangaji",
"Kwanini?" Maisha yangu yako hatarini kila wakati hivyo nahofia kuipoteza nyumba yangu niliyoijenga kwa kujiminya, nitahamia kwangu siku moja kila jambo likiwa sawa,"
"Na unaishi mwenyewe humu, hujaoa?"
"Sijaoa ndiyo, na sijafikiria kufanya hivyo kwa sasa bado nina hofu na maisha niishio?"
"Unauhasama na mtu labda au inakuwaje hadi ukawa unaandamwa hivyo?" akazidi kuuliza Moni, Tom akasita kujibu baada ya kuona ni maswali tu na anajibu bila kuwa na hofu kama vile anamfahamu binti huyo. Kusita kwake hakukumfanya akae kimya bali aligeuza kibao cha maswali na kumtaka binti huyo ajitambulishe kwanza ndiyo na yeye aweze kuwa huru kujibu kila amuulizacho.
ITAENDELEA