ONLY YOU
SEHEMU YA 10
WHATSAPP 0655585220
Kichwa cha Daniel kilichanganyikiwa, hakuamini kama angeweza kumuona msichana mrembo kama alivyokuwa Felista. Alitokea kumpenda, kwa jinsi alivyovaa, alivyokuwa ameumbika kwake alionekana kuwa msichana wa ajabu kabisa.
Wakati mwingine alihisi kama Felista alikuwa ameshushwa, alipendeza machoni mwake na kila alipokumbuka jinsi alivyokuwa, ni kitu kimoja tu ndicho kilichokuja kichwani mwake, ngono.
Alikuwa na namba ya msichana huyo, alikumbuka kwamba alipewa business card hivyo haraka sana akaingiza mkono wake katika mfuko wa suruali na kuitoa kadi ile na kuanza kuiangalia, kadiri alivyokuwa akiitazama ndivyo alivyozidi kumuwaza msichana huyo.
“I must take her,” (ni lazima nimchukue) alijisemea.
“How can I win her? Should I make a call and ask her to meet me or?” (nitampataje? Nimpigie simu na kumbuomba aonane na mimi au?) alijiuliza.
Kichwani mwake hakumfikiria mke wake tena, mtu aliyekuwa ndani ya moyo wake alikuwa msichana huyo tu. Alijua dhahiri kwamba Jackline alikuwa na mtoto mdogo, alihitaji kuonyeshewa mapenzi motomoto lakini kwake akili yake ilibadilika kabisa na kitu pekee alichokihitaji alikuwa Felista tu.
Alijitahidi kukaa kimya siku hiyo, alijifanya kama kutotilia mkazo kuhusu kumpigia simu msichana yule lakini siku iliyofuata, akashindwa kuvumilia, haraka sana akampigia msichana huyo.
“Nimekumbumbuka Felista,” alisema Daniel huku akiangalia nje kupitia katika dirisha la kioo lililokuwa ofisini kwake.
“Naongea na nani?”
“Daniel!”
“Ooh! The big Boss!”
“Hahah! Hakuna buana! Mimi wa kawaida sana!” alijitetea.
“Sawa! Nimefurahi kuiona simu yako,” alisema Felista.
Daniel akatoa tabasamu pana kana kwamba msichana huyo alikuwa mahali hapo. Akabaki akizungumza naye, moyo wake ulikuwa na furaha kubwa kupita kawaida.
Alitokea kumpenda, alitamani kuwa naye, alimfikiria sana na muda huo ulikuwa ni wa kumwambia kwamba alitaka kuonana na kuzungumza naye kwani hakuona kama kungekuwa na msichana mwingine ambaye alitakiwa kuonana naye zaidi ya huyo.
Alizungumza naye kwa kujiamini, alichombeza kwa maneno matatu, alimsifia kwa kumwambia kwamba alikuwa mzuri wa sura, mpole, aliyependeza kwa kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia.
Felista alifurahi, alipenda kusifiwa, alijiona mzuri hivyo alivyoambiwa maneno hayo moyo wake ukaridhika na kuona kabisa kwamba alistahili kwa kile alichokuwa akiambiwa.
“Ningependa kuonana nawe,” alisema Daniel.
“Leo?”
“Ndiyo! Kuna ugumu?”
“Wala hakuna!”
“Basi ningependa nikuone!” alisema.
Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, msichana huyo akakubaliana naye na hivyo kuahidi kuonana sehemu moja maalumu ambayo ilizoelewa kutembelewa na watu waliokuwa kwenye uhusiani wa kimapenzi.
Ilikuwa ni katika bustani ya Las Vegas iliyokuwa Masaki jijini Dar es Salaam. Walikutana mahali hapo na kuanza kuongea. Hawakuwa peke yao, walikuwepo watu wengine ambapo kila mmoja alionekana kuwa bize na mpenzi wake.
Daniel alipomwangalia Felista, msichana huyo alionekana kuwa mzuri zaidi ya jinsi alivyokuwa siku ile aliyokutana nayo. Alimwambia jinsi alivyopendeza, jinsi alivyouteka moyo wake kiasi kwamba hakuwa akijiweza kwa ajili yake.
“Kweli?”
“Ndiyo! Ninakupenda sana Felista! Wewe ni msichana wa kipekee sana moyoni mwangu, ninatamani kuwa nawe,” alisema Daniel huku akimwangalia msichana huyo.
Felista akanyamaza, hakuzungumza kitu, aliuinamisha uso wake chini, akashikwa na aibu za kike. Daniel akamsogelea na kumbusu shavuni mwake.
Kitendo hicho kikausisimua mwili wa msichana huyo, hakuamini kama mtu mwenye pesa kama Daniel angempenda msichana kama yeye ambaye alikuwa ameajiriwa sehemu akifanya kazi zake, tena za kutumwa kila siku.
“Sipendi kutembea na mume wa mtu!” alisema Felista huku akiangalia chini.
“Kwa nini? Tunauma?” aliuliza.
“Kwa sababu hamna malengo!”
“Felista! Nina malengo kwako!”
“Malengo gani? Kunioa? Hivi utaweza kumuacha mkeo kwa ajili yangu?” aliuliza Felista huku akimwangalia mwanaume huyo.
Daniel akabaki kimya, alichokizungumza msichana huyo kilikuwa kweli kabisa lakini hakutaka kuonekana kwamba hakuwa na malengo kwa Felista. Akamwambia mambo mengi lakini kusudi kubwa lilikuwa ni kukubaliwa ombi lake tu.
Kwa jinsi alivyokuwa akizungumza, alivyoonekana, alitia huruma kiasi kwamba ilikuwa vigumu kwa felista kuendeleza msimamo wake wa kumaktaa. Akakubaliana naye na hivyo kumbusu shavuni.
Moyo wake haukutaka kukumbuka kwamba alikuwa na mke nyumbani, tena aliyekuwa na mtoto mdogo kabisa, alikuwa bize na msichana huyo na kwa muda alitakiwa kumsahau mke wake.
Walikaa na kuzungumza mengi kisha kuingia ndani ya gari na kumpeleka msichana huyo nyumbani kwake maeneo ya Kijitonyama. Siku hiyo hawakufanya kitu chochote zaidi ya kubadilishana mate na kuondoka.
Njiani, kichwa chake kilivurugika, alijiahidi kwamba mara baada ya kumuoa Jackline asingeweza kutembea na mwanamke yeyote yule lakini kwa jinsi Felista alivyoonekana, hakuweza kuvumilia hata kidogo.
Ujanja aliokuwa akiutumia ni kwamba alihitaji kumuonyeshea Jackline mapenzi yakeyale, hakutakiwa kumuonyeshea utofauti wowote ule, kama alikuwa akimbusu kila siku alipokuwa akirudi, hata kipindi hicho ambacho moyo wake ulikuwa umechukuliwa na mwanamke mwingine, alitakiwa kufanya vilevile.
Alichangamka, Jackline hakugundua kitu chochote kile, hakubadilika, kama alivyokuwa siku nyingine ndivhyo alivyokuwa hata siku hiyo. Walizungumza mambo mengi lakini kichwa cha Jackline kilikuwa kikimfikiria Felista tu.
Waliachana kwa kipindi kifupi kilichopita lakini tayari mwanaume huyo alionekana kumkumbuka msichana huyo kupita kawaida, akatamani kumpigia simu na kuzungumza naye, alihitaji hata kuisikia sauti yake tu.
Akatafuta njia ya kumkimbia mke wake, apate nafasi ya kukaa peke yake na kumpigia simu ili hata amtakie usiku mwema.
Alichokifanya ni kumwambia mke wake kwamba alitaka kwenda kumfungulia mbwa kutoka kwenye banda lake. Hiyo haikuwa kazi yake, ilikuwa ni ya mlinzi lakini kwa kuwa alimwamini sana mume wake, hakutaka kumuuliza.
Akaelekea huko huku akiwa na simu yake, alipofika, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumpigia simu Felista na kuanza kuongea naye.
“Wewe! Humuogopi mke wako?” aliuliza msichana huyo.
“Hapana! Yupo chumbani!”
“Na wewe upo wapi?”
“Nimekuja kumfungulia mbwa!”
“Ehh! Huna mlinzi!”
“Nimezuga kufanya hivyo ili nije kuongea nawe, japo nikutakie usiku mwema,” alisema Daniel.
“Nashukuru kwa kunijali!”
“Usijali! Nakutakia usiku mwema mpenzi!”
“Na wewe pia!”
“Nakupenda!”
“Nakupenda pia!”
Moyo wake ukaridhika, akajisikia faraja kupita kawaida. Alipomaliza, akamfungulia mbwa na kurudi chumbani. Alipofika, akamsogelea mke wake pale alipokuwa na kumwambia alale kifuani mwake.
“Nakupenda mke wangu!” alisema huku mwanamke huyo akiwa kifuani.
“Nakupenda pia mume wangu,” alisema Jackline huku akifarijika, kwa jinsi walivyokuwa wakiishi na mapenzi aliyokuwa akionyeshewa, ilikuwa ni vigumu kuamini kama mume wake huyo alikuwa akimsaliti.
***
Japokuwa alikuwa na mwanamke mzuri lakini bado macho ya Daniel yalikuwa nje yakimwangalia mwanamke ambaye hakumfikia hata mke wake kwa uzuri. Alichanganyikiwa na kila wakati alipokuwa akimfikiria msichana Felista moyo wake ulikuwa kwenye presha kubwa.
Hakutaka kumuacha msichana huyo, alimpenda na kila wakati alikuwa akimfikiria. Kazi hazikufanyika kama ilivyotakiwa na hivyo kwa sababu ya msichana huyo.
Siku ziliendelea kwenda mbele huku mawasiliano yao yakiendelea kukua. Walikaa kwa wiki moja Daniel akamwambia Felista kwamba alimkumbuka na hivyo walitakiwa kuonana katika Hoteli ya Livingstone iliyokuwa Upanga kwa ajili ya kuzungumza.
Hilo halikuwa tatizo, wakaonana huko, wakazungumza sana katika mgahawa mmoja na baada ya hapo kwenda chumbani kutulia. Wakaanza kushikana huku na kule, baada ya hapo wakajifunika shuka na sauti ya kitanda kuanza kusikika.
Siku hiyo moyo wake ukaridhika, hakufikiria ni kwa kiasi gani moyo wa Jackline ungeumia kama tu angesikia kile kilichokuwa kimetokea.
Baada ya kumaliza, wakarudi tena kwenye mgahawa na kuanza kunywa kahawa kama kawaida. Hapo akakumbuka kwamba hakuwa amempigia simu mke wake kwa zaidi ya saa tatu, akaichukua na kumpigia na kuanza kuongea naye.
Walizungumza huku akimtania kama alivyozoea na kumwambia kwamba angerudi nyumbani mapema kabisa. Mkewe akaridhika na kukata simu.
Baada ya kuzungumza na msichana huyo, akaondoka kurudi nyumbani. Alipofika huko, akapokelewa kama kawaida, akakumbatiwa na kumwagiwa mabusu mfululizo shavuni na mdomoni na kuingia ndani.
Kitu cha kwanza kilikuwa ni kumuona mtoto wake, akacheza naye na baadaye kwenda kuoga. Muda wote Jackline alionekana kuwa na furaha tele, kila alipokuwa akimwangalia mume wake, uso wake ulikuwa na tabasamu pana kama mtu aliyeshinda mamilioni.
“Una furaha sana leo,” alisema Daniel huku akimwangalia mke wake.
“Nahisi baada ya mwaka nitakwenda kupata mtoto wa pili,” alisema Jackline.
“Hicho ndicho kinachokupa furaha?”
“Ndiyo! Napenda sana watoto. Nilishawahi kumwambia Mungu kwamba nitakapoanza kuzaa, nitazaa kama kuku,” alisema Jackline na kuanza kucheka.
Kitandani, walikuwa wakiongea mambo mengi, kila mmoja alionekana kuwa na furaha kupita kawaida jambo lililoashiria kwamba mapenzi yao yalikuwa makubwa kuliko mtu mwingine yeyote yule japokuwa katika upande wa pili, Daniel alichukua uamuzi mbaya wa kumsaliti mke wake huyo.
***
“Shoga upo wapi?” ulikuwa ni ujumbe uliosomeka katika simu ya Jackline.
“Nyumbani! Kuna nini kwani?”
“Mume wako yupo wapi?”
“Kazini!”
“Eeh! Basi inawezekana huyu ninayemuona siyo yeye,” aliandika mwanamke huyo kutoka upande wa pili.
Moyo wa Jackline ukashtuka, hakuwa radhi mawasiliano hayo yaishie hapo, haraka sana akampigia simu mtu huyo na kuanza kuzungumza naye.
Alikuwa mwanamke aliyejulikana kwa jina la Pendo, alikuwa mwanamke mrembo ambaye alikuwa na urafiki wa dhati na Jackline. Walisoma wote kwa kipindi kirefu na kushirikiana kwenye mambo mengi mno.
Wakaanza kuongea. Pendo akamwambia Jackline kile kilichokuwa kikiendelea, alimwambia kuwa alimuona mume wake akiwa na mwanamke mwingine katika Hoteli ya Livingstone iliyokuwa Upanga.
Hilo lilimshtua mno Jackline na kuhisi kwamba inawezekana Upendo alikuwa amechanganya. Mwanamke huyo alimwambia kwamba hakuwa amechanganya ila alikuwa na uhakika kwamba mtu aliyekuwa akimuona mbele yake alikuwa Daniel.
“Hebu mpige picha.”
“Hakuna tatizo!”
Picha zikapigwa na kutumiwa Jackline, alipoziona, moyo wake ukawa kwenye maumivu makali, alikuwa mume wake. Alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake kupita kawaida lakini upande mwingine wa moyo wake ukamtoa hofu na kuhisi kwamba inawezekana msichana yule alikuwa wa kawaida tu.
“Wanaondoka, nadhani wanakwenda chumbani!” alisema Pendo.
“Nakuja!”
Haraka sana Jackline akaondoka nyumbani, alichanganyikiwa, hakuamini alichokuwa amekisikia, aliondoka kwa mwendo wa kasi mpaka katika hoteli hiyo, alilipaki gari lake mbali kabisa na hoteli hiyo, akateremka na kuelekea katika hoteli ile na kuonana na Pendo.
Mwanamke huyo alimwambia kwamba wawili hao waliondoka na kuelekea chumbani kupumzika. Hilo lilimuumiza mno Jackline, alitamani kutoka na kwenda kufumania lakini hakutaka iwe hivyo, hakutaka kugombana na mume wake kisa mwanamke mwingine, akavumilia.
Baada ya saa moja na nusu wawili hao wakatoka. Kila mmoja alionekana kuwa na furaha. Picha aliyokuwa akiiona Jackline ilimuumiza mno, kwa jinsi walivyoonekana, ilionyesha kabisa kwamba walikuwa wapenzi walioshibana na walitoka kufanya mapenzi.
Huku alipokaa kwa kujificha, alikuwa akilia, moyo wake ulikuwa na maumivu makali kupita kawaida. Baada ya dakika kadhaa, akashtukia simu yake ikianza kuita, alipoangalia kioo, alikuwa mume wake.
Kwanza akasita kuipokea, alichukia, moyo wake ulikuwa ukiwaka kwa hasira lakini mwisho wa siku akaona bora apokee na kuzungumza na mume wake huyo.
Hakutaka kuonyesha tofauti yoyote ile, alimuonyeshea furaha kama kawaida, walizungumza kwa dakika kama tano huku kila mmoja akionekana kumfurahia mwenzake.
“Upo wapi my prince?” aliuliza Jackline.
“Ofisini! Ila ndiyo nataka nijiandae nirudi nyumbani! Nimewakumbuka sana,” alisema Daniel bila kujua alikuwa akitazamwa.
“Tumekukumbuka pia! Nakusubiria mume wangu kipenzi,” alisema Jackline na kukata simu.
Alilia mno, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, wakati mwingine alihisi kama alikuwa akiota, hakuamini kama Daniel angeweza kufanya kitu kama kile. Alimwamini mno, alimuonyeshea mapenzi ya kila aina lakini mwisho wa siku akaanza kusalitiwa.
Alihisi kuwa na tatizo sehemu fulani, mtu kama Daniel asingeweza kumsaliti kama kungekuwa na tatizo sehemu fulani, na hili kufahamu tatizo lilipokuwa alitakiwa kuonyesha mapenzi kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Hakutaka kukaa sana mahali hapo, akaondoka huku moyo wake ukiwa umejeruhiwa kupita kawaida. Katika muda ambao Daniela lirudi nyumbani, hakutaka kumuonyeshea tofauti yoyote ile, alimuonyeshea furaha ya ajabu ambayo hakuwahi kumuonyeshea katika kipindi chote.
Furaha ile ilificha maumivu makali yaliyokuwa moyoni mwake, uso ulitabasamu lakini moyo wake ulikuwa ukilia kwa ndani. Alijikaza, alijipa ujasiri wa kutokuyaonyesha maumivu yake mbele ya mume wake.
Usiku walikuwa wakizungumza, wakicheza lakini moyoni mwake hakuwa na furaha hata kidogo. Walifanya kila kitu na hata siku iliyofuatia, akamuaga na kwenda kazini.
Jackline akashindwa kuvumilia, mume wake alipoondoka, akajifungia chumbani na kuanza kulia kwa maumivu makali moyoni mwake. Alijiuliza juu ya kile kilichokuwa kikiendelea, kwa nini mume wake kipenzi aliamua kumsaliti kwa msichana ambaye aliamini kwamba hakuwa mzuri kama yeye zaidi ya makalio makubwa kidogo aliyokuwanayo?
Kila alichokuwa akijiuliza akakosa jibu lakini bado moyo wake ulikuwa na uhakika kwamba kulikuwa na tatizo mahali fulani kwani kwa jinsi alivyokuwa akimfahamu Daniel, namna alivyomuonyeshea mapenzi ya dhati, akilini mwake hakukuingia suala la usaliti hata kidogo.
“Kwa nini lakini? Nahisi kuna kitu, nitafuatilia nijue nini kinaaendelea,” alisema Jackline huku macho yake yakiwa mekundu mno kwa sababu ya kulia sana.
***
Jackline hakutaka kukurupuka, alitakiwa kuwa na ufundi mkubwa katika kumfuatilia mume wake. Alijua kabisa kwamba kama angefanya hayo kwa pupa asingeweza kufanikiwa kwani angeharibu kila kitu na kuonekana mbabaishaji.
Aliwajua wanaume, hawakuwa watu wa kuambiwa tu, walikuwa watu wa kushikwa huku wakiwa na mali mkononi, lakini pia pamoja na hilo alitakiwa kuhakikisha anamdaka huku akiwa na uhakika kwamba huyo alikuwa mpenzi wake vinginevyo angeambiwa kwamba ni rafiki yake tu.
Ili aucheze mchezo huo hakutakiwa kubaki nyumbani hapo, wazo lililokuja ni kwamba aondoke kurudi nyumbani kwa wazazi wake huku akiwa huko ndiyo aanze kucheza mchezo huo kwa lengo la kumtuliza mume wake.
Kumuaga halikuwa tatizo, aliamini kwamba atakapomwambia kuwa anataka kurudi nyumbani kwanza ampeleke mtoto kwa bibi na babu kusingekuwa na maswali mengi.
Usiku mume wake alivyorudi, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumwambia kile alichokuwa amekifikiria. Hilo halikuwa tatizo kwa Daniel, alimruhusu mke wake kumpeleka mtoto kwa babu na bibi yake.
Siku ya kuondoka, alimsindikiza hadi huko ambapo alimwambia kwamba angekaa kwa muda wa mwezi mmoja na kurudi nyumbani.
Kwa jinsi alivyokuwa akizungumza, Daniel hakuweza kugundua maumivu aliyokuwanayo mke wake moyoni mwake. Alitabasamu, walicheka pamoja huku wakitaniana lakini ndani kabisa ya moyo wake kulikuwa na mpasuko mkubwa mno.
Wakati akifikiria kuhusu mpango wake ndipo wazo jingine likamjia kichwani mwake, ilikuwa ni lazima amshirikishe rafiki yake aliyeitwa Pendo kwa lengo la kumpa ushauri juu ya kile alichotakiwa kufanya.
Haraka sana akampigia simu na kuanza kuzungumza. Akaomba kuonana naye na ndani ya dakika kadhaa msichana huyo alikuwa mahali hapo na kuanza kuzungumza.
Alichomwambia Pendo ni kwamba wao wawili walitakiwa kuhakikisha Daniel na Felista wanaachana kwa kuwachezea michezo mingi ambayo ingewafanya wasiwe na amani katika mapenzi yaliyokuwa yakiendelea.
“Ishu si kumuua yeyote, hapa ni lazima tuhakikishe kwamba wanaachana,” alisema Pendo huku akimwangalia Jackline.
“Sawa kabisa. Ni wazo zuri mno! Tunafanyaje sasa?”
“Ni rahisi! Una pesa?”
“Ninazo!”
“Basi tumkodi mwanaume mmoja, awe mzuri wa haja, halafu huyo ndiye ambaye atatumika, lakini pia tumuandae msichana mzuri wa haja, yaani hao ni kwa ajili ya kuwaachanisha wawili hao. Unaonaje?” alisema Pendo na kumalizia kwa swali.
“Wataweza?”
“Kwa nini washindwe! Yaani tujenge chuki kati yao, basi.”
“Sawa.”
Pendo ndiye alikuwa kila kitu, alijua kucheza na mambo kama hayo, katika kipindi ambacho mume wake alikuwa akichepuka na mwanamke mwingine alitumia njia ileile ambayo ndiyo alihitaji hata Jackline aitumie pasipo kushtukiwa.
Haraka sana akampigia simu mwanaume mmoja aliyeitwa kwa jina la Jackson na kumwambia kuhusu dili lililokuwa limewekwa mezani. Mwanaume huyo aliposikia, akafurahia kwani mbali na kupewa pesa, pia alikuwa na uhakika wa kufanya mapenzi na msichana mwingine mrembo.
“Naona unaniletea mpenzi mwingine! Safi sana,” alisema Jackson kwenye simu.
“Hebu tuonane kwanza na mhusika,” alisema Pendo.
Ndani ya saa moja, watatu hao wakakutana katika mgahawa wa Armando uliokuwa Kijitonyama. Jackline mwenyewe alipomuona Jackson akakiri kwamba kweli ingekuwa kazi nyepesi kwa msichana yeyote kudanganyika kutokana na uzuri wa sura aliokuwanao mwanaume huyo.
“Naitwa Jackson, mzee wa kazi,” alisema Jackson huku akimsalimia Jackline, kwa jinsi alivyokuwa akitabasamu, hata uzuri wake ukaongezeka.
“Naitwa Jackline!”
“Ooh! Kwa hiyo sisi ni JJ, safi sana,” alisema Jackson ambaye muda wote alikuwa mtu mwenye uchangamfu mkubwa.
Wakakaa na kuanza kuzungumza. Pendo akaanza kumwambia Jackson kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwamba alitakiwa kumshawishi msichana fulani kimapenzi lakini pia angelipwa kiasi kikubwa cha pesa kama tu angekamilisha kile kilichotakiwa.
“Namba yake?”
“Hiyo si tatizo! Nilifanikiwa kuiiba,” alisema Jackline na kumpa namba ya simu.
“Sawa. Nyie niachieni! Si mnataka aachane na mumeo? Hiyo niachie mimi,” alisema Jackson na kuondoka mahali hapo.
Je, nini kitaendelea?
By Ahmad Mdowe