Notification texts go here Contact Us Buy Now!

ONLY YOU SEHEMU YA 09

ONLY YOU
SEHEMU YA 9
WHATSAPP 0655585220
Ilipofika majira ya saa sita usiku, daktari mmoja bingwa hospitalini hapo akawachukua na kuwapeleka katika ofisi yake kwani alikuwa na jambo muhimu alilotaka kuzungumza nao.
“Kuna nini? Amepatwa na nini? Amekufa?” alijikuta akiuliza Jackline huku akiyafuta machozi yake, daktari hakujibu, alibaki kimya huku akisubiri wafike ndani ya ofisi ile na kuwaambia kilichokuwa kikiendelea kwa Daniel.
***
Kabla daktari hakujibu kile kilichokuwa kikiendelea kwa Daniel, akabaki kimya, macho yake alikuwa akiwaangalia watu hao kama walikuwa na utayari wa kusikia kile kilichokuwa kimetokea.
Kichwa chake kilikuwa kikifikiria mengi, hakujua kama huo ungekuwa muda sahihi wa kuwaambia au haukuwa muda sahihi. Alibaki kimya kwa muda na kuanza kuzungumza.
“Ndugu yenu tumemkuta akiwa na tatizo kubwa,” alisema daktari huyo, huo haukuwa muda wa kuficha, ilikuwa ni lazima aseme ukweli kile kilichokuwa kikiendelea.
“Tatizo gani?” aliuliza mzee Mwamanda
“Ndugu yenu ana ugonjwa wa kansa ya damu,” alisema daktari huku akiwaangalia kila mmoja.
Walishtuka, hawakuamini kile walichokisikia, walimwangalia daktari mara mbilimbili, jibu lake lilionekana kutokuwa sawa na wakati mwingine walihisi kama walikuwa wakitaniwa.
Waliuliza mara nyingi lakini jibu lake lilikuwa lilelile kwamba Daniel alikuwa na ugonjwa wa kansa ya damu ambao kwa kitaalamu ulijulikana kama Eukemia.
Jackline akashindwa kuvumilia, hapohapo akaanza kulia, aliumia moyoni mwake, aliya jua magonjwa ya kansa, yalikuwa hatari ambayo yalipoteza maisha ya watu wengi duniani.
Hakutegemea kabisa kupokea jibu kama hilo. Kansa ya damu haukuwa na dawa, ulikuwa ni ugonjwa wa kutisha zaidi ya Ukimwi na kila mmoja aliyekuwa akiupata, mwisho wake ulikuwa ni kifo tu.
“Haiwezekani! Dokta, haiwezekani,” alisema alisema Jackline na kuanza kulia.
Huo ndiyo ukweli ulivyokuwa, majibu hayakubadilika, majibu yalisomeka kwamba Daniel alikuwa na ugonjwa wa kansa ya damu.
Walizungumza mengi na daktari na kuwaambia maneno ya kuwafariji kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa wa Daniel kupona kama tu wangechukua matibabu ya haraka.
Haikuwa kansa iliyokuwa imekomaa, ilikuwa imeanza na kama wangewahi tiba kwa haraka hata kabla ya miezi mitatu kukatika basi angeweza kupona kabisa.
Walizungumza mengi, walipomaliza, wakatoka na kwenda kumuona Daniel katika chumba alichokuwemo. Walipofika humo, Jackline akashindwa kuvumilia, akamsogelea mpenzi wake pale kitandani na kumkumbatia huku akilia.
Maneno ya daktari yakaanza kujirudia kichwani mwake, aliumia, alikuwa tayari kupoteza kila kitu katika maisha yake lakini si kumpoteza Daniel. Kwake, mwanaume huyo alikuwa kila kitu, furaha yake, tumaini lake na ni mtu ambaye alikaa vilivyo moyoni mwake.
“Jackline, usilie mpenzi,” alisema Daniel kwa sauti ya chini akbisa.
“Ninaumia mno! Why Mungu anafanya hivi?” aliuliza huku akilia.
“Yote ni MungU! Tumshukuru kwa kila jambo,” alisema Daniel kwa maneno ya kishujaa.
Kilichofuata ni kuanza matibabu. Kwanza akahamishwa katika hospitali hiyo na kupelekwa katika Hospitali ya Living Water iliyokuwa Upanga jijini Dar es Salaam.
Ilikuwa ni hospitali ya kisasa, ynye gharama kubwa mno. Kwa familia ya Daniel haikuweza kupambana na gharama kubwa bali mtu aliyeahidi kumsaidia alikuwa ni mzee Mwamanda.
Kila siku Jackline alikuwa akienda hospitalini hapo na wakati mwingine kulala hukohuko. Hakutaka kumuacha Daniel, alikuwa na hofu kwa kuhisi kwamba angeweza kufa hivyo alitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha anakuwa naye karibu mno kwa kipindi hicho.
Mzee Mwamanda alitamani kuona Daniel akirudi katika hali yake ya kawaida. Alijua dhahiri kwamba kijana huyo alikuwa akipendwa sana na binti, na kitu kizuri ni kwamba alikuwa na baba wa mjukuu wake, hivyo kumpoteza yeye kilikuwa ni kitu kibaya mno.
Alichokifanya ni kuanza kuhangaikia matibabu yeye mwenyewe, ilikuwa ni lazima ahakikishe kwamba Daniel anapona kwani ndiyo ingekuwa furaha kwa binti yake, hivyo kaka baba hakutakiwa kulala usingizi.
Aliwasiliana na madaktari wengine na kuwaelezea kilichokuwa kikiendelea, wao wakamwambia kwamba alitakiwa kumsafirisha na kumpeleka nchini India katika hospitali ya Ganga ambapo kulikuwa na matibabu makubwa na mazuri zaidi.
Hakutaka kulichukulia jambo hilo kipeke yake, akamuita mkewe na kumwambia, akakubaliana naye, haikutosha, akamuita Jackline, naye akakubaliana naye na kuonyesha furaha aliyokuwanayo moyoni mwake, akamkumbatia baba yake na kumpiga mabusu mfululizo.
Baada ya hapo akawasiliana na wazazi wa Daniel na kuwaambia. Aliwaweka wazi kwamba hakutaka kuona kijana huyo akifariki kwani tayari alikuwa kama mwanafamilia hivyo ilikuwa ni lazima apambane kuhakikisha anayaokoa maisha yake.
Kwa wazazi hao ilikuwa ni furaha tele, wakakubaliana naye na wa mwisho kuambiwa alikuwa Daniel mwenyewe ambaye bila kupepesa macho alimwambia mzee huyo alikuwa tayari, si kwa India tu, popote pale alikuwa tayari kwenda kutibiwa.
Harakati za safari zikaanza kufanyika. Zilifanyika kwa kasi kubwa kwani ilikuwa ni lazima kuyaokoa maisha ya mwanaume huyo aliyekuwa muhimu mno.
Ndani ya siku mbili tayari walikuwa ndani ya ndege na kuanza kuelekea nchini India. Ndani ya ndege kila mmoja alionekana kuwa na furaha mno, Jackline alikuwa pembeni ya mpenzi wake, muda wote alikuwa akimwangalia, wakati mwingine alikuwa akitabasamu lakini wakati mwingine alionekana kuwa na huzuni kubwa.
Katika vitu ambavyo hakutaka kabisa kuona vikitokea ni kumpoteza mpenzi wake huyo. Ndege iliendelea kukata mawingu na baada ya saa kumi na sita ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Coimbatore.
Gari la wagonjwa kutoka katika Hospitali ya Ganga lilikuwa mahali hapo, baada ya abiria kuteremka, na wao wakateremka na kwenda kwenye magari maalumu yaliyofika mahali hapo kwa ajili ya kuwachukua.
Safari ikaanza na kuelekea katika hospitali hiyo. Njiani bado Jackline alikuwa akizungumza na mpenzi wake, alimtia moyo kwa kumwambia kwamba angepona na kuwa kama zamani.
Hawakutumia muda mwingi wakafika katika hospitali hiyo na hivyo Daniel kuchukuliwa na kuingizwa katika chumba cha mapumziko kabla ya kupewa matibabu.
Jopo la madaktari wanne wakakutana katika chumba cha mkutano na kuanza kuzungumza kuhusu ugonjwa uliokuwa ukimsumbua Daniel. Mikononi mwao walikuwa na ripoti ya Daniel ambayo ilitoka nchini Tanzania.
“Ni ugonjwa mbaya lakini kwa sababu ndiyo kwanza upo katika hatua ya kwanza, ninaamini tutafanikiwa,” alisema D. Patesh.
“Kweli! Ila kabla ya yote ni lazima kwanza tuchukue vipimo vingine kwa sababu ugonjwa mkubwa kama huu huwa unakuja na baadhi ya magonjwa, ni lazima tufanye uchunguzi wa damu yake kwa undani zaidi,” alisema daktari mwingine, wakakubaliana na hivyo kuanza kufanya uchunguzi kuhusu hali ya Daniel.
“Mungu atakuponya,” yalikuwa ni maneno machache yaliyokuwa yakisikika kichwani mwa Jackline.
***
Matibabu yalikuwa makubwa, yaliendelea kufanyika nchini India. Kila siku walikuwa ni watu wa kumuomba Mungu kuhakikisha kwamba Daniel anapona na kurudi katika hali yake kama kawaida.
Siku ziliendelea kukatika, madaktari hawakuchoka, kila siku kulikuwa na kazi ya kuhakikisha mwanaume huyo anarudiwa na afya yake kama ilivyokuwa zamani. Walibadilishana zamu, waliingia kwa zamu ndani ya chumba hicho na kuendelea kumtibu.
Walimpa dawa zenye nguvu, ilikuwa ni lazima kuiteketeza kansa hiyo hata kabla haijaanza kusambaa mwilini mwake. Hilo lilifanyika kwa nguvu kubwa na hatimaye baada ya mwezi akaruhusiwa kurudi nyumbani huku akipewa dawa ambazo alitakiwa kuzitumia kwa miezi sita.
“Baada ya hapo?” aliuliza mzee Mwamanda.
“Atakuwa mzima wa afya, cha kumshukuru Mungu ni kwamba tumeiwahi, vinginevyo mambo yangekuwa mabaya zaidi,” alijibu daktari.
Daniel akawa na furaha, alimshukuru mzee Mwamanda, alimuona mwanaume huyo kuwa na moyo wa kipekee, si kwa sababu alikuwa na uhusiano na mtoto wake na kumpa mimba, ila kujitoa kwa kiasi kikubwa namna ile ilikuwa ni upendo wa dhati.
Alikuwa na biashara zake, aliacha kila kitu kwa ajili yake, kila alipokuwa akifikiria hilo, aliona kabisa kwamba mzee huyo alistahili kumshukuru kwa yote aliyokuwa amemfanyia.
Siku moja kabla ya safari alikesha na Jackline katika chumba alichokuwa amelazwa, kila alipomwangalia msichana huyo, alikuwa mrembo mno, alimpenda kuliko kitu chochote kile katika dunia hii.
Hakuacha kumbusu, hakuacha kumshukuru kwa kuuruhusu moyo wake kumpenda. Alimtafuta mno, alilitafuta penzi la msichana huyo na hatimaye alifanikiwa kulipata, kubwa zaidi ni kwamba alimchukua kutoka kwa mwanaume mwingine kabisa.
Siku ya safari ilipowadia, wakapanda ndege na kurudi nchini Tanzania. Huko, waliendelea kupendana na hatimaye kuanza mipango mipya ya kuishi pamoja, hakukuwa na kitu walichokitamani kama hicho.
Wazazi waliposhirikishwa, hakukuwa na tatizo, wakakubaliana nao na hatimaye watu hao wawili kufunga ndoa takatifu kanisani. Wakawa mume na mke na baada ya miezi ya kujifungua ilipokamilika, Jackline akajifungua mtoto wa kike hospitali.
“Mke wangu!” aliita Daniel huku akionekana kuwa na furaha kupita kawaida.
“Ndiyo mpenzi!”
“Ninashukuru kwa zawadi hii, hakika ni zawadi kubwa ambayo nisingeweza kuipata sehemu yoyote ile,” alisema Daniel huku uso wake ukionyesha ni kwa jinsi gani moyoni mwake alikuwa na furaha kupita kawaida.
Maisha yakawa matamu, ya furaha, walionyesheana mapenzi kemkem, mtoto yule akawaunganisha na kuifanya mioyo yao kupendana kupita kawaida.
Daniel akawekwa katika kampuni moja ya mzee Mwamanda ambayo ilikuwa ikihusika na uchukuaji mizigo kutoka bandarini na kuisambaza sehemu nyingi jijini Dar es Salaam na nje ya nchi.
Alikuwa bosi, aliheshimika japokuwa alikuwa na umri mdogo. Alinyenyekewa, alipendwa na kuheshimiwa kila alipokuwa akipita.
Ofisi yake haikuwa bandarini, ilikuwa Posta Mpya katika Jengo la Mkapa. Ilikuwa moja ya ofisi nzuri ambapo ndani yake ilikuwa imezungukwa na vioo huku kiyoyozi kikipiga muda wote aliokuwa ofisini humo.
Mezani kulikuwa na kompyuta yake na pembeni kulikuwa na picha kadhaa za familia yake, kila alipokuwa akiziangalia, moyo wake ulikuwa na hamu ya kufanya kazi zaidi kwani aliamini kuwa kitu pekee kitakachoifanya familia yake kuishi maisha mazuri ni kufanya kazi kwa bidii tu.
“Samahani bosi,” alisema sekretari kupitia simu yake ya mezani.
“Ndiyo!”
“Kuna mgeni anakuulizia!”
“Nani? Adul?”
“Hapana! Amejitambulisha kwa jina la Felista!”
“Oh! Mwambie aingie!” alisema.
Ni ndani ya sekunde kadhaa mlango wa ofisi yake ukafunguliwa na msichana huyo kuingia. Alikuwa mweupe, mrefu kidogo, kifua saa sita, alipendeza kwa kuvaa sketi fupi ambayo iliiacha miguu yake wazi kwa kiasi kikubwa.
Alikuwa mzuri wa sura, hata kama hakuwa akiongea lolote, kwa mbali tabasamu lake lilikuwa likionekana. Alipoingia, Daniel alipomuona, kwanza akashtuka lakini akapiga moyo konde baada ya macho yake kuziona picha akiwa na familia yake.
“Karibu!” alimkaribisha huku akisimama, wakapeana mikono.
“Ahsante!” aliitikia msichana huyo na kukaa kwenye kochi.
Harufu yote ndani ya ofisi ikabadilika, harufu ya manukato ikatawala kila kona humo ndani. Pale alipokaa, Felista aliikunja miguu yake kwa staili ya nne, mapaja yakawa wazi lakini Daniel hakuonekana kushtuka kabisa.
Felista akaanza kumwambia kuhusu jambo lililomfanya kufika mahali hapo, alimwambia kwamba alikuwa na shida, alikuwa mfanyabiashara, alihitaji kupokea mizigo kutoka nchini Marekani lakini kwa bahati mbaya hakuwa na kampuni ambayo ingemuwezesha kusafirisha mizigo hiyo mpaka kulipokuwa na ofisi yake.
Hilo halikuwa tatizo kwa Daniel, hiyo ilikuwa kazi yake, ilikuwa ni pesa ambayo ilijileta. Akamwambia kwamba hakukuwa na shida, kama alihitaji msaada, kampuni yake ilijitolea kumsaidia kwa malipo ya kawaida kabisa.
Felista akafurahi, wakakubaliana kuhusu malipo, na baada ya hapo, akampa business namba yake na msichana huyo kusimama kwa lengo la kuondoka.
“Tutawasiliana bosi!” alisema Felista.
“Usijali!”
Akageuka na kuanza kuelekea mlangoni. Hapo ndipo kidogo Daniel akashtuka, alipomwangalia msichana huyo kwa nyuma, alijazia kidogo, umbo lake lilijigawa vilivyo, yaani ilikuwa ni sawa na kumuona mrembo wa Tanzania.
Hipsi zilipangwa na kupangika, kiwowo kidogo, miguu yake ilikuwa imejaa kidogo. Daniel akashindwa kuvumilia, akamfuata na kumfungulia mlango, kwa tabasamu pana, Felista akashukuru, akatoka, akamsindikiza kidogo na kisha kuondoka.
“Mmh! Mungu unajua kuumba,” alijisemea wakati msichana huyo akiifuata lifti kwa lengo la kuingia na kuondoka. Akashusha pumzi nzito na kurudi ofisini kwake.
Je, nini kitaendelea?

By Ahmad Mdowe

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.