Notification texts go here Contact Us Buy Now!

ONLY YOU SEHEMU YA 08

ONLY YOU
SEHEM YA 8
WHATSAPP 0655585220
Daniel akaonana na Jackline, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumsogelea msichana huyo, alipomfikia, akamkumbatia na kumpiga mabusu kadhaa mashavuni mwake.
Moyo wake ulikuwa katika amani kubwa, kila alipokuwa na msichana huyo alijihisi kabisa kuwa huru, amani na furaha kubwa moyoni mwake. Alimwangalia Jackline, alionekana kuwa msichana mrembo mno, alimpenda kwa mapenzi ya dhati yaliyokuwa moyoni mwake.
Walikumbatiana kwa dakika nzima na ndipo wakakaa chini na kuanza kuzungumza. Muda mwingi msichana huyo alikuwa akilishika tumbo lake, alifurahi kujiona akiwa mjamzito, kwake, kubeba mimba ya Daniel kilikuwa kitu kikubwa alichokuwa akijivunia nacho.
Walibaki sebuleni huku wakiongea mambo mengi, mama yake Jackline alikuwa akiwaangalia tu, moyo wake uliridhika kupita kawaida. Katika maisha yake alikuwa akipamba kila siku kuhakikisha watoto wake wanakuwa na furaha, kama kitendo cha Jackline kuwa na furaha kuwa na Daniel, kwake ilikuwa ni furaha tele.
“Daniel, nadhani ni muda wa kumwambia baba,” alisema Jackline maneno yaliyomshtua Daniel.
“Kumwambia baba! Kuhusu nini?”
“Hiki kinachoendelea!”
“Mmh! Unahisi ni jambo jema?” aliuliza.
“Ndiyo! Hata kama sitomwambia, jua kwamba kuna siku atajua kuwa mimi ni mjamzito!” alisema Jackline.
“Mh! Atasemaje? Anaweza kuniua!”
“Hawezi!”
“Baba yako si mkorofi?”
“Ni mkorofi kiasi lakini haimaanishi kwamba atakuua, niachie mimi, nitazungumza naye zaidi,” alisema Jackline huku akimwangalia Daniel.
Daniel akashusha pumzi ndefu, moyo wake ulikuwa na hofu tele, aliogopa kupita kawaida na muda wote alikuwa akihisi kuwa mzee Mwamanda angemchukia kwa kile kilichokuwa kimetokea.
Jackline hakuishia hapo, akamwambia pia mama yake kuhusu ule uamuzi aliokuwa amefikia. Mama yake alianza kupinga lakini baada ya kumwambia kwamba ipo siku mzee huyo angejua kwa kuwa mimba hakikuwa kitu cha kujificha, akakubaliana naye na hivyo yeye kutakiwa kumwambia mzee huyo jambo hilo.
Wakaendelea kuzungumza kuhusu mambo mengi, Daniel hakutakiwa kuondoka mahali hapo, alitakiwa kusubiri mpaka mzee huyo atakapofika na kuzungumza naye huku yeye mwenyewe akiwa hapohapo.
Alikuwa na hofu kubwa, alikuwa akitetemeka na wakati mwingine kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka. Alihofu kwa kuwa aliheshimiana na mzee huyo na hakujua ni kitu gani kingetokea kama tu angemwambia kile kilichokuwa kimetokea.
“Unaonekana kuogopa sana,” alisema Jackline huku akimwangalia Daniel.
“Wewe acha tu! Yaani natamani hata kukimbia,” alisema Daniel huku akililazimisha tabasamu kuonekana usoni mwake.
“Hutakiwi kuogopa kitu! Hebu piga moyo konde,” alisema Jackline.
Waliendelea kupiga stori mpaka muda ambao mzee huyo alipofika nyumbani hapo. Hofu ikazidi kuongezeka kwa Daniel, alikuwa akitetemeka, alisalimiana na mzee huyo huku akitamani hata kukimbia.
“Karibi sana dokta,” alisema mzee Mwamanda huku akionekana kuwa na furaha tele.
“Nimekwishakaribia,” alijibu huku tabasamu lake bandia likiwa usoni mwake.
Mzee huyo akaelekea chumbani kwake ambapo akapitiliza mpaka bafuni na kuoga. Muda huo sebuleni hakukuwa na amani, Daniel alikuwa akitetemeka kiasi kwamba alitamani hata kuaga mahali hapo.
Alimwangalia Jackline kwa macho yaliyoonyesha hofu kubwa, alipokumbuka kwamba aliambiwa mzee huyo alikuwa mkorofi, alitamani hata kuondoka mahali hapo.
“Jackline, naomba niondoke,” alisema Daniel huku akimwangalia msichana huyo.
“Hapana! Hili jambo ni lazima tulimalize leo,” alisema msichana huyo.
“Anaweza kukuua!”
“Kama akikuua, basi atuue wote, ila hakuna kuondoka mpaka hili jambo tulikamilishe,” alisema Jackline.
Waliendelea kukaa sebuleni pale mpaka baada ya dakika kadhaa ambapo mzee huyo akarudi sebuleni hapo na kuanza kuongea.
Alionekana kuhisi kitu, haikuwa kawaida kwa Daniel kuwa nyumbani hapo mpaka muda huo, aliona kabisa kulikuwa na jambo lililokuwa likiendelea hapo nyumbani.
Mama yake Jackline hakutaka kunyamaza, huo ndiyo ulikuwa muda wa kumwambia mume wake kile kilichokuwa kimetokea.
Hakutaka kujiuliza mara mbilimbi, akamwambia ukweli wa kila kitu. Mzee mwamanda alikuwa kimya, alimwangalia mke wake alivyokuwa akielezea na muda mwingine alikuwa akiyahamisha macho yake na kumwangalia Daniel ambaye aliuinamisha uso wake chini.
“Mungu nisaidie,” alijikuta akisema Daniel huku akiwa ameinama.
Mama yake Jackline alimwambia mume wake kila kitu, mzee huyo akashusha pumzi nzito, ndita zikaanza kuonekana usoni mwake, alionekana kushtushwa na kusasirishwa kwa kile alichokuwa ameambiwa.
“Dokta...” aliita mzee huyo.
“Naam baba!”
“Ni kweli umempa binti yangu mimba?” aliuliza.
Daniel akanyamaza, swali hilo lilikuwa jepesi kujibika lakini halikutakiwa kujibika kwa pupa. Akanyamaza kwa sekunde kadhaa na kumjibu mzee huyo kwamba kweli alikuwa amempa mimba binti yake.
“Ndiyo mzee!”
“Ulikusudia nini hasa?” aliuliza mzee huyo.
Daniel akanyamaza, hakutakiwa kulijibu swali hilo. Mama yake Jackline alipoona ukimya umetawala akaingilia na kumwambia mume wake kwamba wawili hao walikuwa wakipendana na lingekuwa jambo jema kama wangewaruhusu kuwa wawili na kuishi pamoja.
Mzee huyo hakuzungumza kitu, akasimama na kumsogelea Daniel pale alipokaa na kumuuliza swali moja tu.
“Unadhani nimefurahi kumuona binti yangu akipata mimba kabla ya ndoa?”
Ilikuwa ni rahisi kusikia mapigo ya moyo wa Daniel kwa jinsi yalivyokuwa yakidunda. Kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka huku akizidi kutetemeka.
“Kama kweli umeamua kuwa na binti yangu, usiuumize moyo wake,” alisema mzee huyo, alipomaliza kusema maneno hayo, akaondoka kuelekea chumbani kwake.
Daniel akabaki kimya, alikuwa akisikilizia hatua za mzee huyo jinsi zilivyokuwa zikilia wakati akiondoka kuelekea chumbani kwake.
Mzee huyo alipoondoka kabisa, Daniel akamgeukia Jackline na kumwangalia huku tabasamu likionekana usoni mwake, akajisikia nafuu, mwili ukarudi katika hali ya kawaida.
“Vipi?” aliuliza Jackline huku naye akitoa tabasamu.
“Mh! Unaweza kufa!” alisema Daniel na wote kuanza kucheka.
Waliendelea kukaa mahali hapo huku mama yake Jackline akionekana kuwa na furaha tele, kitendo cha mume wake kukubaliana na Daniel kulimfurahisha kupita kawaida.
Ilipofika majira ya saa mbili usiku Daniel akaaga, akatoka nje, wakati wakiingia ndani ya gari, akaanza kujiskia kizunguzungu, akashindwa kupanda, akaushikilia mlango, kuunyanyua mguu tu akashindwa, hapohapo akaanguka chini.
Jackline akashtuka, haraka sana akachomoka upande aliokuwa na kwenda upande ule wa Daniel. Akamuinua pale alipokuwa huku akimuita.
“Daniel...Daniel...” aliita Jackline, Daniel alikuwa kimya.
Jackline alichanganyikiwa, akaanza kumuita mama yake kwa sauti kubwa, mwanamke huyo akafika nje, akamuona mlinzi akiwa amemshika Daniel pale chini alipoangukia, akauliza tatizo, akaambiwa alianguka ghafla.
Hawakujua kilichokuwa kikiendelea, haraka sana wakampakiza ndani ya gari. Kabla hawajaondoka, mzee Mwamanda akatoka ndani, akaanza kuwaangalia huku akionekana kushangaa.
“Kuna nini?” aliuliza mzee huyo.
“Ameanguka!” alijibu Jackline huku akianza kulia.
“Ameanguka?” aliuliza mzee huyo huku akiwasogelea, akamgusa Daniel, haraka sana akawaambia waondoke kuelekea hositalini kwani hali ya Daniel ilionekana si ya kawaida.
Ndani ya gari Jackline alikuwa akilia huku akiwa amekilaza kichwa cha Daniel mapajani mwake. Hakujua tatizo lilikuwa nini, alishangaa, ilikuwa ni ghafla sana mwanaume huyo kuwa kwenye hali hiyo.
Hakikuwa kifafa, kama kingekuwa chenyewe basi ilikuwa ni lazima kutokwa na mapovu. Kila alipokuwa akijifikiria tatizo lililokuwa limemsibu mpenzi wake, alikosa jibu.
“God! Don’t take him, please” (Mungu! Tafadhali naomba usimchukue) alisema Jackline huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika Hospitali ya St. Marry iliyokuwa hapohapo Mbezi Beach. Haraka sana machela ikaletwa na mwanaume huyo kupakizwa kisha kuanza kusukumwa kuelekea ndani.
Jackline alikuwa akimsindikiza Daniel huku akilia, kwake, wakati mwingine alihisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa mpenzi wake huyo aliyejitolea kumpenda kwa hali na mali.
Alipofikishwa kwenye chumba cha matibabu, akalazwa na wao kutakiwa kusubiri kwa nje. Pale walipokuwa, wazazi wake walikuwa na kazi ya kumbembeleza Jackline aache kulia.
Hakubembelezeka, hakukuwa na kitu kilichokuwa kimemuuma kama kumuona mpenzi wake akiwa kwenye hali hiyo.
“Don’t cry my queen,” (usilie malkia wangu) alisema mzee Mwamanda huku akimbembeleza Jackline.
Madaktari walikuwa wakipishana kuingia ndani ya chumba kile. Mgonjwa alionekana kuwa na tatizo lililokuwa kubwa ambalo lilihitaji uchunguzi wa kina.
Waliendelea kusubiri mahali pale kwa saa mbili, hakukuwa na daktari yeyote ambaye alizungumza nao kwa lolote lile na hata walipokuwa wakiwauliza, hakukuwa na mtu aliyewapa majibu.
Baada ya saa moja, wazazi wake na Daniel wakafika hospitalini hapo kwani walipewa taarifa juu ya kile kilichokuwa kimetokea kwa mtoto wao.
Walipofika tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuulizia hali yake kama alikuwa mzima au la. Walipoambiwa kwamba alikuwa mzima, kidogo mioyo yao ikapoa.
Ilipofika majira ya saa sita usiku, daktari mmoja bingwa hospitalini hapo akawachukua na kuwapeleka katika ofisi yake kwani alikuwa na jambo muhimu alilotaka kuzungumza nao.
“Kuna nini? Amepatwa na nini? Amekufa?” alijikuta akiuliza Jackline huku akiyafuta machozi yake, daktari hakujibu, alibaki kimya huku akisubiri wafike ndani ya ofisi ile na kuwaambia kilichokuwa kikiendelea kwa Daniel.
Je, nini kitaendelea?

By Ahmad Mdowe

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.