ONLY YOU
SEHEMU YA 7
WHATSAPP 0655585220
Mapenzi yalikuwa motomoto, kila mmoja alimuonyeshea mwenzake jinsi alivyokuwa akimpenda. Japokuwa mara kwa mara Daniel alikuwa akienda nyumbani kwa akina Jackline lakini mzee Mwamanda hakugundua kwamba kijana huyo ndiye aliyemchanganya binti yake na kumuacha Peter.
Kwake alimchukulia kama daktari ambaye mara nyingi alikuwa akifika nyumbani hapo na kumwangalia mtoto wake. Muda ambao Daniel alikuwa akienda ni ule ambao mzee huyo hakuwa nyumbani hapo.
Alikuwa akipigiwa simu na Jackline na kuambiwa kwamba mzee hakuwepo hivyo kwenda huko. Hakukuwa na mtu aliyegundua kitu chochote kile mpaka siku moja ambapo mama yake aliwafuma chumbani kwa Christopher wakiwa wamekumbatiana.
Mwanamke huyo alishtuka, ni kama aliona kitu cha ajabu mbele yake, kile kilichokuwa kimetokea kiliuchanganya kchwa chake na kuhisi kama alikuwa akiota.
Hakuamini kuwaona wawili hao wakiwa wamekumbatiana, alichokuwa akikijua ni kwamba hawakuwa na mazoea ya karibu sasa iweje wafikie hatua ya kukumbatiana kama ilivyokuwa.
Hata kabla hajazungumza kitu chochote, haraka sana Jackline akajitoa mikononi mwa Daniel na kumsogelea mama yake, kwanza akamuomba msamaha kwa kile alichokishuhudia lakini pia akamwambia ukweli kwamba huyo ndiye alikuwa mpenzi wake.
“Unanichanganya! Yaani kujuana juzi tu?” aliuliza mwanamke huyo huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Hatukuanza kuonana juzi!”
“Kumbe lini?”
Jackline akaanza kumwadithia mama yake kila kitu kilichokuwa kimetokea nyuma. Wakati huo Daniel alikuwa kimya, aliangalia chini kwa aibu, akahisi kabisa alivuruga kila kitu mahali hapo.
Jackline alichukua dakika kadhaa kumuhadithia mama yake kilichokuwa kimetokea, mwanamke huyo alikuwa kimya tu. Kwa maelezo ya Jackline yalionyesha ni kwa jinsi gani Daniel alikuwa na mapenzi ya dhati kwa binti yake.
Hakuamini kama kungekuwa na mwanaume ambaye angeweza kujitoa kama ilivyokuwa kwa Daniel ambaye alikuwa radhi kupoteza kila kitu lakini si kumuacha Jackline.
“Daniel! Anachokiongea ni kweli?” aliuliza mama yake huku akimwangalia Daniel.
“Ndiyo mama!”
“Una uhakika kwamba unampenda binti yangu?” aliuliza tena huku akiwa amemkazia macho.
“Ndiyo mama! Ninampenda Jackline!” alijibu Daniel kwa kujiamini kabisa.
Hiyo ilitakiwa kuwa siri, hawakutaka mzee Mwambanda ajue kitu chochote kwa wakati huo kwani miongoni mwa watu ambao walikataa katakata kuona Jackline akiachana na Peter alikuwa yeye.
Mara nyingi wawili hao walikuwa pamoja, walikuwa wakitoka na kwenda sehemu mbalimbali kuyafurahia maisha. Kwao, hakukuonekana kuwa na watu wengine waliokuwa wakipendana kama walivyokuwa.
Walibadilishana mawazo na muda mwingi Jackline alimwambia Daniel kwamba angempenda mpaka kufa kwake.
Uhusiano wao haukuwa siri nyumbani kwa akina Daniel, aliwaambia wazazi wake kwamba Jackline alikuwa mpenzi wa maisha yake na alikuwa tayari kumuoa muda wowote ule ambao msichana huyo angependa.
“Daniel!” aliita baba yake huku akimwangalia.
“Naam!”
“Unanishangaza sana. Unamwamini vipi mtu kama huyo msichana, ni msichana wa maisha mazuri, si ndiyo?” aliuliza baba yake.
“Ndiyo!”
“Unadhani hajawaona watoto wa vibosile wote na kukufuata wewe? Hivi Daniel, una akili kweli?” alihoji baba yake.
“Lakini baba...”
“Daniel! Unatakiwa kukua na kuufahamu vema ulimwengu wa mapenzi.” Alisema mzee huyo.
Hakumwamini kabisa Jackline, kwake, wasichana waliotoka katika familia bora walikuwa watu wa tofauti kabisa, wanaoringa na ambao wanaweza kuchukua uamuzi wowote muda wowote ule.
Hakutaka kumuona kijana wake akipotea, alimwambia wazi kwamba huyo Jackline hakuwa na akili ya kuwaacha watoto wa matajiri na kumfuata yeye wa maisha ya chini.
Kwa Daniel hakutaka kuelewa lolote lile, kwake, aliamini kwamba Jackline alikuwa msichana wake wa maisha yake yote hata kama kungetokea kitu gani, angekuwa na msichana huyo maisha yake yote.
Bado Daniel alikuwa akiendelea na masomo yake chuoni, mapenzi yalichukua sehemu kubwa ya maisha yake lakini hakutaka kabisa kuona akimpoteza msichana mrembo kama Jackline.
Aliwaambia marafiki zake kuhusu msichana huyo na mipango mingi aliyokuwanayo kwake, kila mtu alipomwangalia aliamini kabisa kwamba Daniel alikuwa kwenye penzi la dhati kwani kwa jinsi alivyokuwa akiongea, penzi halikujificha hata kidogo.
Siku zikaendelea kukatika. Baada ya miezi kadhaa Daniel akaanza kujisikia hovyo mwilini mwake, akaanza kusikia maumivu makali ya mgongo huku wakati mwingine akijisikia kizunguzungu.
Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, alichokifanya ni kumwambia mpenzi wake. Jackline aliposikia, moyoni mwake aliumia mno na kumwambia kwamba alitakiwa kwenda kupima.
Hilo halikuwa tatizo, siku iliyofuata akaelekea huko na kupima kawaida, hakukutwa na ugonjwa wowote ule na kuona kwamba inawezekana kulikuwa na tatizo jingine au kama ni ugonjwa ulikuja na kuondoka.
“Ulipima nini?” aliuliza Jackline.
“Maralia, typhord, sina chochote,” alisema Daniel.
“Hivyo tu?”
“Ndiyo!”
“Kingine?”
“Sikupima!”
“Na sasa hivi unajisikiaje?”
“Kidogo afadhali! Nahisi ilikuwa ni ugonjwa wa kupita,” alisema Daniel huku akionekana kudharau alichokuwa akiumwa.
Akapuuzia, hakutaka tena kwenda hospitalini, akajisikia vizuri kabisa hivyo kuendelea na maisha yake kama kawaida. Penzi likawa penzi, wakati mwingine Jackline alikuwa akitoroka nyumbani kwao na kwenda kwa akina Daniel na kulala huko.
Hiyo ilikuwa ni siri kubwa, baba yake hakujua ila mama yake ndiye aliyekuwa akifahamu kila kitu. Hakuwa na cha kufanya, alishindwa kabisa kumzuia binti yake kwenda huko.
Baada ya miezi sita, Jackline akaanza kujisikia tofauti mwilini mwake, akaanza kutapika na mwili kuwa na uchovu mkubwa. Hakutaka kujiuliza hicho kilikuwa kitu gani, jibu lililokuja kichwani mwake ni kwamba alikuwa na mimba.
Hakutaka kubaki na jibu hilo moyoni mwake, ilikuwa ni lazima kwenda kuthibitisha hospitalini, akaenda huko, akapima na kile alichokuwa akikifikiria ndicho ambacho alikutana nacho, akapewa majibu yake, akayachukua na kuangalia, ni kweli alikuwa na mimba.
“Ahsante Mungu,” alijikuta akisema huku akitabasamu. Hakumfikiria baba yake, hakujua ni kwa jinsi gani mwanaume huyo angebadilika na kuwa mbogo, alichokuwa amekiangalia ni kuzaa na mwanaume aliyekuwa
akimpenda, Daniel tu.
***
Moyo wa Peter haukuwa katika hali ya kawaida, bado alikuwa amechanganyikiwa kutokana na kuachwa na msichana Jackline. Alimpenda msichana huyo na kwenye maisha yake hakuona kama angetokea msichana mwingine ambaye angempenda kama ilivyokuwa kwa huyo.
Alichokihitaji sana ni kuonana na mwanaume aliyekuwa amempokonya Jackline kutoka mikononi mwake, alifikiria namna ambayo alitakiwa kuanzia kwani hata kwenda nyumbani kwao alijisikia aibu, hivyo kitu pekee ambacho alikiona kufaa sana ni kumpigia simu ndugu yake na Jackline, Erick.
Simu ikaanza kuita, iliita na kuita lakini haikupokelewa mpaka ilipokatika. Hakutaka kuishia hapo, akapiga tena na tena mpaka simu ilipopokelewa na mwanaume huyo.
Cha kwanza kilikuwa ni kushtaki kwa kile kilichokuwa kimetokea, alimwambia Erick kuwa aliachwa na Jackline kwani aliamua kuwa na mwanaume mwingine kabisa.
Kwa Erick, hakuamini alichokisikia, alihisi kama Peter alikuwa akimdanganya. Alimfahamu kijana huyo, alimpenda mno ndugu yake na muda mwingine alimwambia kwamba kwenye maisha yake hakukuwa na kitu kilichokuwa na nguvu kama mapenzi waliyokuwa wakipendana watu hao.
Mbali na hayo akaanza kuyakumbuka maneno ya dada yake, aliyakumbuka vilivyo jinsi alivyokuwa akimwambia kwamba kwake, Peter alikuwa ni mwanaume wa ndoto ambaye alikuwa tayari kuolewa naye, kuishi naye mpaka siku ambayo Mungu angemchukua katika dunia hii.
Leo, alikuwa akishtakiwa kwamba Jackline alimwacha Peter, haikumuingia akilini mwake na muda mwingi alihisi kama alikuwa akitaniwa.
“Peter! Hivi unachoniambia ni kweli au?” aliuliza Erick huku akiwa amemsikiliza mwanaume huyo kwa muda mrefu alivyokuwa akijielezea.
“Erick! Siwezi kukuficha! Jackline ameniacha,” alisema.
“Hebu tuonane!”
“Sawa.”
Ni ndani ya nusu saa wakaonana maeneo ya Mlimani City ambapo wakaingia katika mgahawa wa Marry Brown na kuanza kunywa kahasa. Hapo ndipo Peter alipoanza kumuhadithia mwanaume huyo kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Erick alikuwa kimya, alimsikiliza Peter kwa umakini kabisa. Kwa jinsi alivyokuwa akiongea, ilikuwa ni rahisi kubaini kwamba mwanaume huyo alikuwa na maumivu makali moyoni mwake.
Aliongea kwa sauti iliyokuwa na uchungu huku macho yake yakimlenga machoni mwake. Alitumia dakika kadhaa, alipomaliza, akanyamaza, akachukua kitambaa chake na kuanza kufuta machozi yaliyoanza kumtiririka.
“Tatizo hasa ni nini?” aliuliza Erick huku akimwangalia Peter.
“Sijajua! Ni maamuzi ya ghafla sana,” alijibu Peter.
“Peter! Dada yangu ana akili sana, hawezi kufanya maamuzi ya kipuuzi ndani ya muda mchache, nahisi kuna kitu, hebu niambie,” alisema Erick.
“Erick! Kama ningekuwa najua chochote, ningekwambia!”
“Unanidanganya! Kama hutaki kuniambia sababu, unadhani mimi nitakusaidia vipi? Hata wakili wako ni lazima umwambie kila kitu kilichotokea ili akusaidie,” alisema Erick.
Peter alipoambiwa hivyo, kwanza akatulia, alichokisema Erick ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe, ili ajue ni wapi pa kumsaidia ilikuwa ni lazima amwambie kila kitu kilichotokea.
Hakuwa na jinsi, akamwambia ukweli sababu ya msichana huyo kumuacha kwamba hakuwa akimjali, akimpa muda wala kumsikiliza.
Erick aliposikia hivyo, kwanza akashusha pumzi ndefu na kumwangalia Peter. Alichokisema kilikuwa sahihi kabisa, alimjua dada yake, alimpenda mtu aliyekuwa akimjali na kumsikiliza, kama peter alishindwa kufanya hivyo basi ilikuwa ni lazima kuachwa kama ilivyokuwa.
“Nikusaidie nini hapo?” aliuliza Erick.
“Nahitaji kumfahamu mtu aliyekuwanaye kwa sasa!” alisema Peter.
“Nitamfahamu vipi?”
“Erick, yule ni ndugu yako, sidhani kama kuna ugumu wowote ule,” alisema Peter.
Huo ndiyo msaada pekee aliokuwa akiuhitaji kutoka kwa Erick, alijua kwamba Jackline alikuwa kwenye uhusiano na mwanaume mwingine, alihitaji kumfahamu kwa sura, alihitaji kukutana naye na kuzungumza pamoja ili kama itawezekana basi amwache Jackline ili awe naye.
Hilo lilikuwa gumu kufanyika kwa Erick, alikataa lakini akabembelezwa sana na mwisho wa siku kukubaliana na Peter na hivyo kuanza kumfuatilia dada yake, hasa kwenye suala la namba ya simu.
Aliamini baada ya kuipata namba hiyo ingekuwa ni rahisi sana kwake kumsaidia Peter, alimfuatilia na siku ambayo aliisahau simu yake, haraka sana akaichukua, akaenda sehemu ya simu zilizotoka, akaliona jina lililoandikwa Hubby, hakutaka kujiuliza, alijua kuwa huyo ndiye mwanaume aliyekuwa akitoka naye kimapenzi, akaichukua namba ile.
Haraka sana akawasiliana na Peter na kumpa namba hiyo. Kwa mwanaume huyo ilikuwa ni furaha tele, hakukuwa na kitu alichokuwa akikihitaji zaidi ya namba hiyo.
Haraka sana akampigia simu na kuanza kuzungumza naye. Aliumia kuongea naye lakini hakuwa na jinsi, alijitambulisha na kumwambia kwamba alihitaji kuonana naye kwani kulikuwa na kitu muhimu alitaka kuzungumza.
“Kuhusu nini?” aliuliza Daniel.
“Naomba tuonane!”
“Sawa, ila ninahitaji kufahamu ni kuhusu ninI!” alisema Daniel.
“Kuhusu Jackline!”
“Amefanyaje?”
“Naomba tuonane na tuzungumze. Cha muhimu ni kwamba hutakiwi kumwambia kama tunaonana,” alisema Peter.
Kwanza Daniel akahisi kitu, aliona kabisa kama kulikuwa na mchezo uliotaka kuchezwa, alianza kwa kukataa lakini kwa kuwa Peter alikuwa na ushawishi mkubwa, hakuwa na jinsi, akakubaliana kuonana naye.
Jioni ya siku hiyo wakaonana katika mgahawa wa The Prince uliokuwa Masaki na kuanza kuongea. Hakutaka kumficha, alimwambia kuhusu uhusiano wake na Jackline ulivyokuwa, alivyompenda na mpaka siku ya mwisho alipoachwa na msichana huyo kuwa na Daniel.
Kwa jinsi alivyokuwa akizungumza ilikuwa ni rahisi kuona ni kwa namna gani Peter alikuwa ameumia moyoni mwake. Daniel alikuwa kimya tu akimsikiliza mwanaume huyo alivyokuwa akiongea kwa hisia kali.
“Nimekusikiliza sana, unataka nikusaidie nini?” aliuliza Daniel baada ya Peter kumaliza kuzungumza.
“Ninahitaji uniachie Jackline wangu,” alisema Peter.
Daniel akashtuka, hakuamini kile alichokisikia kwa mwanaume huyo. Mpaka kufikia hapo akagundua ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alivyokuwa amekufa na kuoza kwa Jackline.
Kwake, kumuacha Jackline lilikuwa suala gumu mno, alimpenda kupita kawaida na kitu ambacho kilimpa furaha ni kwamba msichana huyo alikuwa na ujauzito wake.
“Peter! Hilo ni jambo gumu sana, unazungumzia kitu kigumu kufanyika,” alisema Daniel huku akimwangalia Peter.
“Daniel! Nakuomba, najua unampenda sana Jackline, naomba uniachie msichana wangu, ninampenda, bila yeye siwezi kuishi, naomba unionee huruma, Daniel, naomba unionee huruma,” alisema Peter huku akiikutanisha mikono yake juu ya meza kama kumuomba mwanaume huyo.
“Siwezi kumuacha! Jackline ana mtoto wangu tumboni,” alisema Daniel.
“Daniel! Si tatizo, nitamlea mtoto wako, ila ninaomba sana uniachie Jackline wangu,” alisema Peter huku akiendelea kumuomba mwanaume huyo.
Daniel hakukubali, alijua kabisa kwamba Peter alikuwa akimpenda Jackline lakini hakudhani kabisa kama alikuwa akimpenda msichana huyo kama alivyokuwa akimpenda yeye.
Hawakufikia muafaka japokuwa Peter aliahidi kumgawia kiasi cha shilingi milioni ishirini kama tu angekubaliana naye kuachana na Jackline.
Baada ya kuongea kwa dakika kadhaa, Daniel akaaga na kuondoka mahali hapo huku akimuacha Peter akiwa kwenye maumivu makali.
Alipofika kwenye Bajaj tu kitu cha kwanza kilikuwa ni kumpigia simu Jackline na kumsalimia. Alitamani kumwambia kuhusu kile kilichokuwa kimetokea lakini alisita, hakuona kama kulikuwa na umuhimu wa kufanya kitu kama kile.
“Upo wapi? Kwenye daladala?” alisikika Jackline akiuliza.
“Nipo kwenye Bajaj! Upo nyumbani?”
“Ndiyo mpenzi!”
“Naomba nije nikuone!”
“Nyumbani?”
“Ndiyo! Kwani baba yupo?”
“Hayupo!”
“Basi nakuja!”
Hakutaka kuelekea nyumbani kwao, alichokifanya ni kumwambia dereva Bajaj kwamba safari ilibadilika na hivyo walitakiwa kuelekea Mbezi Beach. Hilo halikuwa tatizo, dereva akakata kona na kuanza kuelekea huko.
Moyo wake ulikuwa na mawazo kuhusu Peter, aliogopa kwa kuona kuwa kama mwanaume yule alikuwa akimpenda Jackline kiasi kile basi kama asingeongeza nguvu ya kumpenda zaidi basi angeweza kupokonywa kitu ambacho hakutaka kabisa kuona kikitokea.
“Nitapambana! Siwezi kushindwa kulilinda penzi langu, nitapambana mpaka mwisho, yaani mpaka namuoa,” alisema Daniel wakati Bajaj ilipokuwa ikikaribia kwao.
JE, nini kitaendelea?
By Ahmad Mdowe