ONLY YOU
SEHEM YA 3
WHATSAPP 0655585220
Ilipita miezi mingi tangu siku ya mwisho kumuona, alimkumbuka, alimfanya kwenda hotelini kila siku kwa lengo la kuonana naye lakini hakufanikiwa. Baada ya siku zote hizo kupita, hatimaye akaonana naye mahali hapo kitu kilichomfanya kutokuamini kama alikuwa Jackline aliyekuwa akimfahamu.
Jackline alipomuona Daniel, hakumkumbuka, kwake, mwanaume huyo alionekana kuwa kama watu wengine, alimchukulia kama daktari aliyeambiwa kwamba alikuja kumuona mdogo wake.
“Jackline...” alijikuta akiita huku akimwangalia, akaanza kumsogelea, msichana huyo akashtuka.
“Do we know each other?” (tunafahamiana?) aliuliza huku tabasamu pana la mshangao likiwa usoni mwake.
Daniel hakujibu kitu, alinyamaza huku macho yake yakimwangalia Jackline ambaye naye alianza kuonyesha wasiwasi kwani kila alipojaribu kuvuta picha kama aliwahi kumuona mwanaume huyo sehemu, hakukumbuka.
“You are a superstar, everybody knows you,” (wewe ni maarufu, kila mtu anakufahamu!)
“Mimi?”
“Ndiyo!”
Jackline hakuzungumza kitu, akanyamaza lakini kichwa chake kilikuwa na maswali mengi juu ya mwanaume huyo. Daniel akajifanya kupuuzia na kumjulia hali Christopher huku akimwambia kwamba alihitaji kukiona kidonda chake.
“Wewe ndiye uliyemsaidia jana?” aliuliza Jackline.
“Ndiyo! Alijikata na chupa! Unajisikiaje Columbus?” alimuuliza kwa jina lake la utani alilompa.
“Am fine! Maumivu yamepungua sasa,” alijibu Christopher.
Daniel alikuwa akifikiria namna ya kuendelea kuzungumza na msichana huyo, alimkumbuka, mara ya mwisho kukutana ilikuwa ni miezi tisa iliyopita, hakujua ni kwa namna gani angeanza kuzungumza naye kwani alitamani kumuona kwa muda mrefu sana.
Wakati yeye akifikiria hayo, naye Jackline alikuwa akifikiria yake kichwani. Aliendelea kujiuliza kuhusu mwanaume huyo, alionekana kumfahamu vilivyo lakini hakukumbuka kama aliwahi kumuona sehemu fulani.
Kilichomtisha ni kumwambia kwamba alikuwa supastaa, alijua kwamba alitania kwani hakuwa mtu wa kutoka ndani, sana sana kwenda katika Hoteli ya White Paradise na kuogelea, sasa mwanaume huyo alimjuaje? Kila alipojiuliza, alikosa jibu.
Pale alipokuwa, Jackline alimwangalia, jinsi alivyokuwa akiongea lakini hakupata jibu kama aliwahi kumuona sehemu fulani. Alipomaliza, Daniel akayarudisha macho yake kwa Jackline.
“It has been nine months since the last time I saw you!” (ni miezi tisa sasa tangu mara ya mwisho kukuona) alisema huku akimwangalia.
“Waoo! It is such a long time. Can you remind me where we met?” (Waoo! Ni muda mrefu, unaweza kunikumbusha tulipokutana?) aliuliza msichana huyo.
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yake, akaanza kumwambia Jackline jinsi alivyomuona kwa mara ya kwanza. Alimkumbusha vizuri kabisa na kwa sababu siku ile ilikuwa ya mwisho kwake kwenda hotelini kufurahia maisha na wazazi wake, alikumbuka vizuri.
“Ooh! Nimekukumbuka! Umekua!” alisema Jackline huku akicheka.
“Hahah! Hata wewe umekua, uzuri wako umeongezeka!”
“Ila umejuaje kama naitwa Jackline?”
“Nakumbuka mdogo wako alikuita siku ile, unakumbuka?”
“Ooh!! Yeah! Nakumbuka! Halafu nikaondoka!”
“Yeah! Tena kwa dharau...”
“Jamaniiiiiii...”
“Nakutania! Nimekuwa nikikusubiria kwa miaka tisa sasa...”
“Miaka tisa?”
“Miezi tisa!”
“Ooh! My gosh...umenishtua.”
“Nina zawadi yako nzuri sana!”
“Zawadi! Ya nini?”
“Kukukumbusha siku ile. Nimeandika kitu kizuri kwa ajili yako,” alisema Daniel.
“Hebu nikione!”
“Nitakuonyeshea!”
“Lini?”
“Siku yoyote tu,” alisema Daniel.
Walibaki wakizungumza kwa pamoja huku wakiangaliana mpaka Daniel kusahau kama alifika mahali pale kwa ajili ya kumjulia hali Christopher ambaye aliamua kuachana naye na kuzungumza na dada yake.
“Naweza kupata namba yako niwe nakubipubipu wa kishua?” aliuliza Daniel huku akitabsamu.
“Eti uwe unanibipubipu!”
“Yeah! Kwani vibaya!”
“Si vibaya, ila ukinibipu, na mimi nakubipu!” alisema Jackline na kumpa namba ya simu Daniel kwani kwake alionekana kuwa mwanaume mcheshi, mwenye roho nzuri ambaye hakuwahi kukutana naye kabla.
Daniel akamchukua Christopher na kuondoka naye mahali hapo, wakaelekea nje ambapo sherehe ilianza na watu kuanza kwa kucheza muziki.
Daniel hakutaka kujionyesha sana, akaelekea sehemu iliyokuwa na makochi na kukaa. Moyo wake ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama alifanikiwa kumuona Jackline, kwake, kile kilichokuwa kimetokea kilikuwa kama muujiza mkubwa.
“Halafu wewe unampenda dada yangu? Si ndiyo?” aliuliza Christopher swali lililomfanya Daniel kushtuka, akamwangalia usoni.
“Mimi? Hapana! Unajua yule ni rafiki yangu sana!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
Akili ya Daniel ilikuwa kwa msichana Jackline tu, alimpenda, alihitaji kuwa naye katika maisha yake yote. Alikaa mahali hapo huku akizungumza na Christopher, walitokea kuwa marafiki wakubwa kiasi kwamba mpaka Daniel mwenyewe akawa anashangaa.
Baada ya dakika kadhaa, Jackline akatoka ndani na kuungana na wageni waliofika kwa ajili ya sherehe yake, kila mtu aliyekuwa mahali hapo akaanza kupiga makofi.
Haraka sana Daniel akasimama na kuelekea kule watu walipokuwa, alipofika, macho yake yakatua kwa Jackline. Alivalia gauni refu jekundu lililomfika mpaka miguu, nywele zake alizibana huku akiwa amevalia hereni ndoto.
Miguuni alivalia viatu vya kike vilivyokuwa vimeinuka mpaka juu, kwa kumwangalia tu isingekutia shaka kwamba ulikuwa ukimwangalia mmoja wa wanawake wazuri duniani.
“Jackline, ninakupenda kwa moyo wangu wote,” alisema Daniel, aliongea kwa sauti ya chini huku akimwangalia msichana huyo.
Sherehe iliendelea mpaka ilipokwisha majira ya saa tatu. Watu wakaanza kutawanyika, naye Daniel akaaga. Mzee Mwamanda akamshukuru kijana huyo kwa kuja kwake katika sherehe hiyo lakini pia akamsisitiza kwamba huo hautakiwi kuwa mwisho, muda wowote ambao angejisikia kufika mahali hapo, alikuwa akikaribishwa.
“Haina shida mzee wangu! Nashukuru sana.”
Akaondoka, ndani ya Bajaj kichwa chake kilikuwa kikimfikiria msichana huyo tu, alimpagawisha kiasi kwamba hakuona kama kulikuwa na mwanamke mzuri katika dunia hii zaidi ya Jackline.
Akaichukua simu yake, akafungua sehemu ya ujumbe mfupi na kumwandikia ujumbe uliosomeka ‘Nimeondoka bila kukuaga, nahisi ulikuwa bize, namshukuru Mungu kwa kukuona tena, hakika ulipendeza’ alipomaliza, akautuma, wala hazikuchukua sekunde nyingi, ukajibiwa ‘Lol! Nashukuru pia! Safari njema dokta’.
Alipofika nyumbani, akajilaza kitandani, kichwa chake kilikuwa kwenye mawazo lukuki, bado alikuwa akimfikiria msichana huyo. Aliukumbuka uzuri wake, jinsi alivyokuwa akiongea kwa mapozi, nywele zake alivyokuwa amezinyoa, kwa kifupi kwake alionekana kama malaika.
Alihitaji kumpigia simu na kuzungumza naye, alihofu kwa kuhisi kwamba angekuwa anamsumbua kwa kuwa ilikuwa ni usiku, ila kwa kuwa alipenda sana, hakutaka kujali. Akampigia na baada ya sekunde kadhaa simu kupokelewa na sauti ya msichana huyo kusikika.
“Unajua huwezi kujua ni kwa jinsi gani nina furaha siku ya leo,” alisema Daniel.
“Kivipi?”
“Kukuona! Miezi tisa ni mingi sana, nilikufikiria mno. Ulikimbilia wapi?” aliuliza Daniel.
“Nilikuwa chuoni Afrika Kusini!”
“Ooh! Na umeshamaliza?”
“Ndiyo! Halafu umenikumbusha, hebu niambie ilikuwaje mpaka ukakutana na familia yangu?” aliuliza.
“Ni stori ndefu sana!”
“Ambayo haisimuliki?”
“No! Ambayo haimaliziki! Ila kwa kifupi, ni Mungu tu. Jack, u msichana mrembo sana, unapendeza kwa kila vazi unalovaa, kukutana na wewe ni kama umeikamilisha ndoto yangu,” alisema Daniel kwa sauti ndogo ya mahaba.
“Mmh! Nyie wanaume!”
“Serious! Jack, nikiambiwa nichague kitu kimoja cha kuwa nacho milele yote, hakika ningekuchagua wewe. U msichana mrembo sana, msichana ambaye kila mwanaume angetamani kuwa naye,” alisema.
“Mmh! Aya nashukuru dokta!”
“Niite Danny kama utapenda.”
“Sawa. Nashukuru Dk. Danny!”
Walizungumza mambo mengi, kuanzia saa tano mpaka saa saba usiku bado walikuwa wakizungumza. Daniel hakutaka kusita, hakutaka kumficha msichana huyo, alimwambia kwamba alikuwa akimpenda mno na ndiyo maana kwa kipindi chote hicho alivumilia, alikuwa akimsubiri kwa kuwa aliamini kuwa kuna siku angekutana naye.
Kuambiwa hivyo, Jackline alikutegemea, kwa sauti yake ya upole alimwambia Daniel kwamba alikuwa na mpenzi, kulikuwa na mtu ambaye aliuchukua moyo wake.
“Najua Jackline, msichana mzuri kama wewe hutakiwi kuwa peke yako, tena ungeniambia kwamba hauna mtu, nisingekuamini,” alisema Daniel.
“Ndiyo hivyo! Ila samahani!”
“Usijali! Ila sidhani kama litakuwa jambo baya kama tutaendelea kuwasiliana kwenye simu, kama marafiki,” alisema Daniel kwa sauti ya upole.
“Haina shida! Wewe tu!”
“Sawa,” alisema Daniel na kukata simu.
Ilikuwa ni kama alikuwa akiingia vitani, alijua dhahiri kwamba Jackline alikuwa na mpenzi lakini alihitaji kushinda vita hivyo na kumpata.
Alijua udhaifu wa wanaume wanapokuwa na wanawake kwa kipindi kirefu, alijua jinsi walivyokuwa wakichoka na hata kule kujali kunavyopungua, kwa kuwa alilifahamu hilo, alitaka kumuonyeshea Jackline kwamba yeye alikuwa mwanaume wa kipekee sana, aliyemsikiliza, aliyemchekesha na hata kumfariji.
Alichokifanya ni kumpa Jackline usumbufu, kila wakati alikuwa akimpigia simu na kuzungumza naye, wakati mwingine alikuwa akichati naye huku akimwambia mambo mengi kuhusu maisha.
“Jackline, nikuulize swali?” aliuliza Daniel baada ya wiki ya kwanza kupita tangu waanze kuwasiliana.
“Niulize!”
“Unaijua picha halisi ya mapenzi moyoni mwako?” aliuliza.
“Unamaanisha nini?”
“Yaani nguvu ya mapenzi ilivyokuwa kubwa moyoni mwako!”
“Ndiyo! Naijua.”
“Unakumbuka siku za kwanza ulipokutana na mpenzi wako na kuanza uhusiano?” aliuliza.
“Nakumbuka!”
“Mapenzi yake yalikuwaje?”
“Mmh! We acha, yalikuwa ni balaa...”
“Bila shaka alikuwa akikutafuta kwa siku kila dakika!”
“Exactly” (kabisa)
“Mpaka meseji mia mbili mliziona chache!”
“Yaani we acha tu!”
“Na sasa hivi? Yapo vilevile?”
“Mmh! Hapana kwa kweli!”
“Unahisi kwa nini?”
“Labda tumezoeana!”
“Kwa hiyo mkizoeana mapenzi yanapungua? Kujali kunapungua? Na mawasiliano yanapungua pia?” aliuliza.
“Mh! Maswali magumu hayo,” alisema Jackline huku aitoa tabasamu.
“Jackline! Mapenzi yana nguvu sana, unapoambiwa kwamba mtu anajiua kwa ajili ya mapenzi, usichukulie kawaida, mapenzi yanaleta stress, picha ya mapenzi ni kubwa mno.
“Siku ya kwanza ulipoanza kumpenda mpenzi wako, ile ndiyo picha halisi ya mapenzi, ile ndiyo nguvu ya mapenzi, baada ya kuzoeana, mapenzi yanapungua na mwisho kuondoka kabisa. Sisi ndiyo tunayafanya mapenzi yapungue, ila nguvu ya mapenzi ipo vilevile,” alisema Daniel.
“Inaonekana unafahamu mengi kuhusu mapenzi!”
“Mimi ni masta! Yaani kama chuo cha mapenzi nina PhD,” alisema Daniel na wote kuanza kucheka.
Walizungumza mambo mengi siku hiyo, alichokuwa akikitaka Daniel ni kumteka msichana huyo, alitaka kuwa mtu wa kwanza kumpigia simu asubuhi, na wa mwisho kumpigia simu usiku, alihitaji kuwa mtu wa kwanza kumtakia kula chakula cha mchana na usiku, kwa kifupi, alitaka kumuonyeshea kwamba alikuwa akimjali sana.
Upande wa pili moyo wa Jackline ulianza kubadilika taratibu, kile alichokuwa akikifanya Daniel kilionekana kuanza kumuingia. Kwa siku, Daniel alikuwa akimpigia simu zaidi ya mara kumi, mara kumjulia hali, mara kumtakia chakula chema, mara kumuuliza ni nguo gani alikuwa amevaa siku hiyo, yaani kila kitu alichokuwa akikifanya kilianza kumtenganisha na mpenzi wake.
“Mungu! Naomba unisaidie, sitaki mwanaume yeyote auchukue moyo wangu kutoka kwa Peter,” alisema Jackline.
Je, nini kitaendelea?
By Ahmad Mdowe