Notification texts go here Contact Us Buy Now!

BARUA ILIYOWAHI KUNIUMIZA SEHEMU YA 04

Barua iliyowahi Kuniumiza
Mtunzi. Yona Fundi
0675278759

SEHEMU YA NNE.

     Usingizi hakuchelewa ukanipeleka sehemu nyingine. Sehemu ambayo niliyaanza maisha bila ya kuwa na Tina tena. Ijapokuwa niliweza kumsahau Tina lakini nilipitia kipindi kigumu sana mpaka kulisahau penzi lake. Sikuwa mlevi mimi ila niliingia kwenye ulevi wa kupindukia, kitendo kilicho niingizia hasara kubwa kuliko mategemeo yangu. 
Emanuel Shirima, nilifanya kazi kwa nguvu mchana lakini usiku pesa yote ya kazi iliisha kizembe. Nililewa haswa, ulevi ulikaa kichwani mwangu. Pombe ipi nilishindwa kuinywa? Haikuwahi kutokea. Lugha chafu zilijenga urafiki na mdomo wangu. Nilitukana vile nilivyokuwa najiskia. Vilabu vyote vya pombe bubu Mazense Midizini vilinizoea. Nilipigana na walevi wenzangu, pale nilipopishana nao kauli. Na usiombe wa kalitaja jina la Tina wangu. Palikuwa hapatoshi.

 Si kuikumbuka kodi ya chumba na taratibu Mazense Midizini kukanishinda. Mwenye nyumba akaidai kodi yake, hakuchelewa kuniadhiri. Kweli niliadhirika! Vyombo nikaviuza, pesa sikuifanyia jambo la maana. Mpaka nilipokuja kukumbuka shuka wakati kumekucha. 
   Nikaanza kutapatapa na jiji. Ndugu wa kunisaidia hawakuwepo. Vibarua vya ujenzi nikavichapa, hapo ndipo nilipokutana na bosi Muhando, ushupavu wangu akaupenda. Mazoea kati yetu kwenye kazi ya kajenga urafiki. Hatimaye akaamua kuniajili kutoka kibarua na kuwa mfanyakazi wa kudumu katika kitengo kingine kabisa. 
Muhando alinisaidia sana hata kumsahauTina, alichangia kwa maana halisi. Maneno yake yalikuwa dawa sana katika ugonjwa wangu. Sasa sikumkumbuka Tina yule aliyenidekeza nami nikadeka kama mtoto. Nikajiweka mbali na wanawake. Hamu ya kuwa nao ilinitoka kabisa!
  Mwaka wa kwanza ukaisha, si kuzipata habari zake, wa pili pia ukaingia sikuzikamata habari zake, nami sikuzitaka kabisa! Maisha yangu yakaendelea kubadilika haraka. 
      Kitendo cha maisha kuwa katika daraja la kujiweza, kilikuja na mtazamo wa tofauti kwa mama. Akinihitaji kuoa. Swala la kuoa likanikumbusha habari nilizokuwa nimezisahau. 
    Niliwakumbuka wanawake wote niliyowahi kuwa nao. Lakini ilipokuja kwa Tina. Moyo wangu uliuma zaidi. Nilimkumbuka Tina, ni yeye niliyeona anastahiri kuwa mke wangu. Mwanamke ambaye hakuipenda pesa yangu. Tabia yangu ya ukorofi haikufua dafu kwa Tina haraka haraka niliibadili. Ni ajabu lakini ilibaki kuwa kweli, kwangu.
Swala la mama liliendelea kuniumiza sana kichwa. Kila siku nikipambana na kumuahidi mama kuwa nipo karibu kuoa, lakini si kuwa mkweli wa kile nikisemacho.
    Kwa mara ya kwanza nikajikuta naanza kuwa muongo wa yale niliyokuwa nikiyanena.
**********

   Simu ya mama niliyoipokea majuzi, ikawa chachu sana na msukumo wakwenda posta nilipokuwa nikizipokea barua zote alizowahi kunitumia Tina. Sikujua kilinisukuma kitu gani? Ni kama vile kuna jambo lilikuwa likiniongoza. Hakika sikutegema barua yake. Maana karibia miezi sita nyuma, kila nilipoenda kuangalia kama kuna barua kwenye sanduku langu la posta sikuwa nikiona chochote. Na anuani yangu ni yeye pekee ndiye alikuwa akiifahamu.
     Siku hiyo nilipambana na bahasha iliyohifadhi barua iliyoandikwa na Tina, sikuamini kile nilichokuwa na kiona. Miezi mingi ilikuwa imepita bila kuambulia chochote kutoka kwake. Nilitumia muda sana hatimaye kuondoka na barua ile ili nikaisomee nyumbani. 
____________ 

   Mikono yangu iliikamata vyema bahasha, ikipambana kuifungua. Ajabu sasa si kuwa na kitu mkononi. Kumbe nilikuwa nimepitiwa na usingizi; usingizi ulinichukuwa na kunipeleka sehemu nyingine, kabla ya kunirudisha nikiwa na pambana na giza kali kwenye mboni za macho yangu. Mgongo ulionekana kuniuma mno. 
Nilinyanyuka kitandani kivivu, hatimaye nilifanikiwa kuifikia taa, kisha nikaiwasha, chumba kikapokea mwanga wa taa, huku saa ya ukutani ikionesha kuwa ni saa tatu na dakika kadhaa. 
Akili ilichelewa kusoma kwa muda, ilipokaa sawa zoezi la kwanza lilikuwa kwenda kuoga.
  Nilipomaliza kuoga, nguvu ziliniijia, nikachukuwa pesa na kuelekea kwenye banda la chipsi. Nusu saa nilirejea na mfuko wa chipsi, hapo nikaketi na kuanza kuushambulia huku nikiwa na soda ya kopo pembeni. 
  Nilikula haraka haraka maana njaa ilionekana kunichachafya sana. Na hata chakula chenyewe hakikufanikiwa kuipoza njaa yangu. Basi usiku niliuona mrefu, nikiwa na njaa iliyochanganyika na mawazo kibao kwenye kichwa changu. 
 Asubuhi na mapema nilikuwa kazini, nikipambana na majukumu. Niliyaweka mambo vizuri, kila mfanyakazi alionekana kupenda uwepo wangu katika kuyasimamia majukumu. 
   Ilikuwa kawaida yangu licha ya kupewa majukumu makubwa lakini sikuwa nikijivuna. Kila mfanyakazi aliyatimiza majukumu yake vizuri.  

   Ilipita zaidi ya wiki mbili hatimaye bosi Muhando alirejea kutoka Iringa. Hakuna kilichokuwa kimeenda tofauti ofisini, kila kitu kilikuwa sawa. Jambo lile lilimfurahisha sana, likaendelea kuniongezea alama ya uaminifu kwake.

     Wakati wote huo, sikupokea ujumbe wowote kutoka kwenye ile namba, ambayo nilihisi kuwa ni ya Tina. Jambo ambalo lilinifanya kutoendelea kushughulikia habari zozote zilizohusu maisha ya Tina kwa sababu niliona ni kujiumiza tu. Hivyo sikuhitaji kuendelea kuumia kwa sababu yake. 

  Si kuacha kumuelezea bosi mambo yaliyonikuta. Muhando hakuwa na cha kuzungumza sana, zaidi ya kunishauri nikae mbali na Tina, kwa sababu tayari alishakuwa mke wa mtu. 

  Kama kawaida yake, maneno ya Muhando yalikuwa na ukweli ndani yake. Nami niliyatilia maanani sikutaka kuyaacha yaende zake. Na uzuri mambo ya polisi yaliishia juujuu, sikupata muda wa kuyafuatilia tena.
**********
  Mwezi ukapita mambo ya Tina yakawa mbali nami. Lakini simu za mama, bado zilinitesa katika kuyatafuta majibu. Ni mwanamke gani wa kuishi nami? Katika jicho langu nilimkosa. Nilihitaji kutafuta mji mtulivu, ambao kamwe usingenisababishia gonjwa fulani. Mizani ya kichwa changu, bado ilikuwa migumu kuwapa nafasi wanawake kadhaa ambao walijitahidi kuonesha uhitaji wa huduma yangu. Bado niliona wakizihitaji zaidi shilingi zangu na si mapenzi kama ilivyokuwa kwa Tina.
__________
  Siku ya jumamosi, nilirejea nyumbani mapema sana kutokana na uchache wa kazi hiyo ikanifanya niwahi kurudi nyumbani. Pirikapirika ya wiki nzima nayo ilinichosha. Kuipata nafasi ya kurejea nyumbani mapema, ilikuwa ni kama bahati kwangu. 

   Nilipofika nyumbani nilijimwagia maji kisha kitanda kiliupokea mwili wangu. Hazikupita dakika nyingi, simu yangu ilitoa muito wa kuingia ujumbe, haraka nikaiendea simu na kuitoa chaji. Si kuchelewa kufungua ujumbe. Macho ya kapokea, namba isiyojulikana; Ujumbe uliojulikana.

Kwa simulizi zaidi wasiliana nasi kupitia 0675278759
Sikiliza simulizi zetu za sauti kwa kubinya link hii chini

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.