Barua iliyowahi Kuniumiza
Mtunzi. Yona Fundi
0675278759
SEHEMU YA MWISHO.
Hawakuchelewa kunitupia lawama; lawama ambazo siku zijua nini haswa chanzo chake. Nilitumia muda mwingi kunyamazisha vilio vyao, huku nikijihisi mtu mwenye hatia. Bila hata ya kufahamu ni vipi mimi nilikuwa nikihusishwa na taarifa za Tina kufariki? Kichwa changu kilionekana kuwa kizito, mwili wangu ulipenywa na baridi kali. Nikiwa siamini kile nilichokuwa nikikisikia. Amefariki vipi Tina? Na mbona amefariki ilihali sijui hata barua yake ilikuwa imeandikwa nini?
Nilijilaumu kwa kuwa mzembe hadi kusababisha Barua ya Tina, kupotea pasina kuisoma. Nilihisi huenda itakuwa imebeba ukweli wa sababu ya kifo cha Tina, kwa maana Tina hakuwa Tina tena.
Miezi miwili kabla ya kuwa eneo lile, mwili wa Tina walishauzika. Hilo nililifahamu wakati nikiendeleza kubembeleza vilio vya baba na mama yake na Tina.
Baada ya wimbi la simanzi kutawala eneo lile. Hakuna nilichoona naweza kukifanya kwa muda ule. Nilihitaji kuwapa muda zaidi Baba na Mama Tina, kabla ya kufahamu juu ya shutuma zangu na hata uwepo wa barua hiyo ya Tina.
Nilitumia muda huo, kuwasiliana na Bosi Muhando kumwelezea hali niliyokutana nayo eneo lile. Bosi Muhando alinisihi niwe jasiri katika kupambana na hali ile. Akanitaka kuwapatia nafasi wazazi wake Tina, iliniweze kufahamu ukweli juu ya kifo cha Tina.
**********
Baada ya muda mama yake na Tina alijitoa pale alipokuwa na kuingia ndani, alipotoka ndani alikuwa na bahasha kisha akanipatia bila kusema nami. Bahasha ya kaki, mikono yangu ikipambana kufungua bahasha ile. Ujasiri ukiwa umenishika. Kimya kikiwa kimetanda kati yetu.
Dakika kadhaa nilianza kupambana na maandishi yaliyoandikwa na Tina.
*********
Barua ilisomeka;
Kwako Emanuel Shirima, natumaini u mzima wa afya. Sina shaka sana na hili. Ni miezi mingi sana imepita na sasa inakaribia mwaka tangu nilipopoteza mawasiliano nawe. Huku ukiwa umefahamu fika kuwa nimeolewa sasa. Najua kitendo cha kupata taarifa ya kuwa nimeolewa Emmanuel kilikutesa sana. Laiti ningekuwa na uwezo wa kuzirudisha nyakati nyuma moja kati ya makosa ambayo kamwe nisingetamani kuyafanya nikupotezana na wewe Emmanuel.
Nipo kwenye dunia ya mateso na maumivu. Neno furaha limekuwa msamiati adimu ndani ya ubongo wangu. Ni vigumu mtu kulijua hili. Maana sura nzuri niliyonayo, imeficha msiba na majuto yaliyoweka kambi ya kudumu ndani ya moyo wangu.
Kwa muda mrefu sana, mwili wangu hautamani dunia kwa sababu ya mateso niliyokupatia Emmanuel.
Najua uliteseka kwa sababu nafahamu ni jinsi gani ulivyokuwa ukinipenda. Hata hivyo najua umetumia nguvu zako nyingi kwajili ya kurudisha penzi letu lililopotea. Siwezi kukuhukumu Emmanuel, kwa lipi haswa? Hakika mimi ndiye sababu ya kulizika penzi letu. Tabu ya maisha ilinifanya nikusaliti Emmanuel. Hali duni iliyokuwa ikiendelea kutusurubu siku hadi siku kwenye familia yetu, sikutaka niendelee kuwatesa wazazi wangu. Katika hali ile ya kunitafutia chakula na mahitaji yangu. Hilo likaidhinisha ndoa yangu kwa mtu ambaye sikudhani kama angelikuwa ana roho ya kinyama kiasi kile. Uwezo wake ulificha makucha yake, mwanzoni akionesha ana mapenzi ya dhati nami.
Kuna wakati nikikaa huwa nahisi hata ardhi na mbingu kwa pamoja vinanizomea, na kuna kipindi huwa mawazo yananijia, huenda haya maumivu niyapatayo leo ndani ya maisha yangu, ni malipo juu ya ule unyama na ukatili nilokutendea.
Huwezi amini Emmanuel mwaka mmoja tu ulitosha mimi kuifurahia ndoa yangu. Siku zilizofuata vibao vikali nikawa na vipokea pasipo na makosa. Mwanaume akaona hiyo haitoshi akaniweka mbali kabisa na wazazi ilikuendelea kuninyanyasa vile alivyokuwa akijisikia.
Niliendelea kuvumilia, nikijuawazi mateso yale yote niliyokuwa nikiyapokea ni kama malipo ya kukutendea ubaya Emmanuel wangu.
Mungu akanipiga kofi zaidi, mwanaume akaniletea magonjwa ndani. Hali yangu ya kiafya ikaanza kubadilika siku hadi siku. Nilijitahidi sana kukutafuta Emmanuel walau nikuombe msamaha kwa kile nilichokutendea, ili moyo wangu ulioendelea kuteseka na gonjwa la usaliti upate kufarijika.
Hiyo ikanilazimu, kutafuta mahali ulipokuwa ukifanyia kazi. Namba ya mawasiliano yako niliipata. Lakini sikuona umuhimu wa kuitumia katika kuyafikisha haya.
Maandishi pekee kupitia mkono wangu yalinipa faraja, nikayaandika haya nikitegemea msamaha kutoka kwako. Ili hata siku ambayo na ingia kaburini niende huku nikitambua Emmanuel umenisamehe kwa mabaya yote niliyokutendea.
Najua nimebakiza siku chache za kuishi hapa duniani. Naomba hii barua itumike kama toba yangu kwako. Maandishi ya hii barua yaulegeze moyo wako, ili hata nikipatwa na mauti, kwa Mungu niweze samehewa.
Sina mengi zaidi ya kukuomba msamaha Emmanuel. Ni mimi Wako umpendaye Tina Kobero.
*******
Yalikuwa maandishi ya mwisho ya Tina, ambayo yaliuumiza sana moyo wangu na kunitesa vilivyo, kitendo kilicho pelekea mpaka hivi sasa kuwa moja kati ya waandishi bora ulimwenguni.
Naweza sema licha ya kunifikisha hapa, lakini hii ni barua iliyowahi kuniumiza katika maisha yangu, kwa maana kitendo cha kutoka Morogoro nikiwa nimefahamu ukweli wa kifo cha Tina ambacho kilichangiwa na mwanaume wake, licha ya kumpatia magonjwa hata hivyo, alifariki kutokana na vipigo vikali alivyokuwa akipatiwa na mumewe.
Niliamua kujivika upelelezi na hata nikafanikisha kumkamata mume wa Tina, nikiambatanisha vielelezo vyote mbele ya sheria. Nashukuru Mungu, kesi hiyo ilikamilika ingawa nilipitia vikwazo vingi sana katika kuifuatilia kesi ile, nikisaidiwa na bosi wangu Muhando.
Hatimaye tulifanikiwa kumfunga kifungo cha maisha mume wa Tina.
Hiyo haikutosha kuniacha na kizazaaza, maisha ya Tina yaliendelea kunitafuna siku hadi siku. Nikipambana na ahadi niliyomuahidi mama yangu. Japo ilichelewa sana hatimaye nilimpata mwanamke ambaye niliridhika nae na kuona yeye pekee anaweza kukikalia kiti alichokuwa amekikalia Tina, ndani ya moyo wangu.
Namshukuru Mungu ulipita mwaka mmoja baada ya kufuatilia kesi ya Tina. Ndipo nilipofanikiwa kumpata mwanamke ambaye yeye alikuwa akijihusisha na maswala ya uandishi wa habari. Kwa kiasi kikubwa alichangia sana kunifikisha hapa, huku nikizitoa chuki zilizozikwa kwenye moyo wangu dhidi ya wanawake. Ambao wote niliamini kwamba hawana mapenzi ya dhati na hata kufikia kulitekeleza wazo la mama la kuoa mwanamke mwingine tofauti na Tina. Nashukuru Mungu, hata mwanamke huyo niliyempata, bado alikuwa na tabia kama zile alizokuwanazo Tina. Ambazo niliona ingelikuwa nadra wanawake wengi kuwanazo.
Mwaka mmoja baadae nilifanikiwa kumpata mtoto wa kike. Ilipofika kwenye suala la kumpa jina; jina la Tina niliona linafaa sana. Kuanzia hapo taratibu nikaanza kujishungulisha na mambo ya uandishi, ili kuwa kama masihara lakini misukosuko ya mapenzi ikinifanya niwe mwandishi mzuri pasipo mategemeo yangu.
Nikiandika mikasa kadhaa wa kadhaa niliyopitia kwenye mapenzi, kabla sijaamua kuandika mkasa huu wa barua iliyowahi kuniumiza, katika hali ya ajabu zaidi ilinipatia tunzo ya mwandishi bora wa mwaka.
Kuanzia hapo ikanitengenezea fursa nyingine ya kuandaa miswada mbalimbali ya filamu nchini.Umaarufu ukaanza kuninyemelea taratibu.
Ukweli ni ngumu sana kuificha harufu, kila mmoja ikamnukia. Jina la Emmanuel Shirima likawa kubwa zaidi. Bwana na bibi Kobero maisha yao nikayaweka katika mirija iliyofaa kwao, kwa hilo nika wafurahisha zaidi. Kama ilivyo kwa bwana na bibi Kobero maisha ya mama yangu nayo yalighubikwa na furaha tele ndani yake.
*********MWISHO.**********
Unaweza tazama filamu yetu mpya kwa kubofya link hii chini.