BARUA ILIYOWAHI KUNIUMIZA
Mtunzi. Yona Fundi
0675278759
SEHEMU YA KWANZA.
Safari ya maisha ni safari ndefu sana ambayo imejawa mabonde pamoja na milima huku ikiambatana na tambalale kwenye sehemu chache ya safari hiyo. Vivyo hivyo ndani ya mapenzi; Mapenzi ya ajabu sana, unaweza ukaniuliza maswali mengi sana kuhusiana na mapenzi lakini majibu ya maswali hayo yanaweza yakauridhisha moyo wako ama ya si uridhishe. Kama ilivyo katika mapenzi basi ni hivyo katika maisha yangu. Iliniwia ngumu sana kuamini hiki ninachokifanya. Si mimi tu kwa upande wangu hata kwa wale watu wangu wa karibu hawakuwahi kuamini kama ningeweza fanya jambo hili.
Kiukweli huko nyuma sikuwahi kuwaza kama na mimi nina kipaji cha kutunga jambo lakini huwezi amini kwasasa ukiwa orodhosha waandishi wazuri katika dunia hii, bila shaka hutonisahau. Kuna wakati niliwahi kujiuliza hivi ni kipi hasa kilichofanya nikavumbua kipaji changu? Hapo ndipo fikra pevu ziliponikumbusha kuwa, mapenzi ndiyo sababu ya kuigundua karama hii. Wanasema shida huvumbua kipaji.
Naam, mapenzi yamenifanya niwe mwandishi mzuri wa hadithi na hata filamu. Na kwenda mbali zaidi hadi kunipatia umaarufu kutokana na kile kinachoitwa upangiliaji wa maneno na kucheza na lugha. Maandishi yangu yamejikuta yakiwa mkombozi wa msomaji ama msikilizaji, yote ni sababu ya mapenzi.
*********
Dhana ya mapenzi ni kubwa mno, huambatana na matukio mengi sana; matukio hayo yanaweza kuwa yenye kuleta furaha ndani yake au huzuni.
Matumizi ya barua za kimapenzi si swala geni masikioni mwako. Kuna nyakati barua hizo hutumika kama kumbukumbu ama kielelezo tosha cha mapenzi, baadhi yake huleta furaha huku nyingine zikibakiza huzuni ndani ya nyoyo zetu pale litokeapo jambo la huzuni ama la furaha ndani ya mahusiano.
Binafsi nimewahi kutumiwa pamoja na kutuma barua nyingi sana, tangu nilipojitoa sadaka ndani ya dimbwi la mapenzi ili kuridhisha matakwa ya moyo wangu. Nilifanya yote hayo ili kuhakikisha nazitendea haki hisia zangu kwa kufuata kilichokuwa kikinituma. Mpendwa msomaji, hapo kabla sikuwahi kuyatambua machungu ya mapenzi na kwenye moyo wangu niliwahi kuapa kutoyaacha, lakini yaliyonikuta yalinipelekea kwa hiyari yangu nijiweke mbali na mapenzi. Ndani ya maisha yangu siwezi isahau barua iliyoandikwa na mkono wa Tina, hakika ilikuwa ni zaidi ya barua.
*********
Tina ni msichana aliyeyabadili maisha yangu kwa namna ya aina yake. Nakumbuka kabla yakuonana na Tina niliwahi kuweka kiapo kwamba; kamwe nisingewahi jihusisha tena na mapenzi kwa maana mapenzi yaliwahi nifanya niione dunia chungu. Usaliti, visa, vituko, migogoro, baina ya wale niliyowahi kuwa nao kabla mboni za macho yangu hazijamwona Tina ilikuwa sababu kubwa haswa ya kujiweka mbali na mapenzi huku nikiamini kuwa katika dunia, mimi Emanueli Shirima, sikuumbwa wala kupewa upendeleo wa kuwa na wapenzi wazuri kama baadhi ya watu wengine wenye furaha katika mapenzi. Kuna wakati nilijikuta nikiamini mapenzi ni pesa, nilitamani sana kuwa na wapenzi wakati huo, lakini si kuwa na pesa, jambo hilo kiukweli lilinipatia wakati mgumu sana. Nikajikuta na wekwa mbali kabisa na dhana ya mapenzi. Kuna wakati nilikuwa nikihakikishiwa kuwa mimi sina mvuto, kitendo kilicho nifanya nijione sina thamani.
Ilikuwa tofauti sana pindi nilipofahamiana na Tina; msichana ambaye na kiri kuwa mboni za macho yangu, hazikuwahi kutazama msichana mwenye mvuto wa namna ile. Umbo lake lenye kuuficha unene kwa mbali na kuuonesha kwa ukaribu huku Mungu akilipendelea urefu wa wastani. Kuachilia mbali ngozi yake ya maji ya kunde vilevile alikuwa na vishimo viwili kwenye mashavu yake; sauti nyororo ambayo kamwe isingelichosha sikio la yeyote ndivyo vigezo vilivyo ongeza alama kwenye ubongo wangu na kunifanya nimuone wa tofauti na wanawake wote waliyowahi kunipiga teke kutokana na ukabwela uliyonizonga.
Ingawa ninajiamini katika swala la maamuzi lakini haikuwa kazi rahisi sana, kama unavyofikiria kuyaachilia yale maamuzi yangu. Unaweza usinimini lakini kama nikikupa nafasi uulize kwa watu wanaomfahamu Emanueli Shirima Kindaki Ndaki, hakuna hata mmoja ambaye atakupa jibu rahisi pale unapotokea kuuliza swali linalohusu kufanya maamuzi magumu.
Nimewahi kubatizwa majina mengi yenye kuudhi na yale yenye kufurahisha huku wengine wakienda mbali na kuniita Msimamo Mkali. Nilikuwa nikiamua jambo huwa ni ngumu sana kulitengua. Nimewahi kusababisha migomo mingi sana kwenye maeneo tofauti tofauti ya kazi. Nimeishi kwa kuamini kile ninachokiamini na hiyo ndiyo siri yangu kubwa.
***********
Ama kwa hakika waswahili hawakukosea pindi waliposema Hakuna mkate mgumu mbele ya chai Kweli Tina aliyalainisha maamuzi yangu kama masihara. Ningekuwa na pesa huenda ningeamini labda Tina alivutika na pesa zangu lakini cha kustaajabisha mfumo wa akili yangu ni kwamba, bado nilikuwa ndani ya uleule ufukara wangu. Bado nilikuwa katika hali ya uvuja jasho wa kufanyakazi kubwa yenye kipato kidogo; kipato nilichokitegemea kwa ajili ya kujikusanyia kodi ya pango katika chumba kimoja kisichofaa kukaliwa na watu ndani ya kitongoji cha Mazense Midizini. Harufu kali ya hewa chafu, ilikuwa kama manukato kwangu kila siku nitokapo na niingiapo ndani ya chumba changu, ambacho hakikuwa mbali sana na majalala bubu katika kitongoji chetu.
Ni kweli jambo la uchafu halikuwa likinipatia tabu sana kwani kila nilipokuwa nikitoka mihangaikoni, mwili mzima ulikuwa na uchovu hivyo nilikuwa nikiulaza kwa ajili ya maandalizi ya siku mpya. Ingawa yote hayo Tina aliyatambua lakini hakupata shaka taratibu tukainza safari ya mapenzi. Alijua kunidekeza, nilideka nitakavyo. Nilijiona mtu kati ya watu. Nani angeweza kuniletea dharau mimi? Mpenzi mzuri, ilikuwa zaidi ya hitaji la pesa. Hata upande wa ufuaji, alijua kuzifua nguo ngumu zilizoishinda mikono yangu. Kero ya kufanya usafi kwenye nyumba ya kupanga ikabaki hadithi kwangu. Chakula cha mama ntilie sikukikumbuka tena. Nani kama Emanuel Shirima? Jibu lilikuwa hakuna. Mtaa mzima walinijua kwa kummiliki Tina mtoto wa Mzee Kobero.
Ukoo uliyosifika kwa kutoa wanawake warembo pale mtaani, huku Tina akiwa mrembo zaidi kati ya watoto wa nne wa Mzee Kobero. Macho ya vijana wengi yalimuangalia yeye pekee, maana ndio ilikuwa karata ambayo haijatwaliwa na wanaume. Dada yake wa kwanza Mariamu aliolewa na mfanyabiashara mmoja wa mafuta mkoani Mwanza, nakumbuka ndoa yake ilifana kupita maelezo. Vivyo hivyo kwa dada yake wa pili kwa jina la Nusura, yeye aliolewa miezi sita nyuma kabla ya mimi kujuana na Tina. Na yeye aliolewa na mfanyabiashara mmoja kutoka huko Zanzibar. Mdogo wake Faudhia bado aliendea kuitafuta elimu katika shule moja ya bweni nje kidogo na mkoa wa Dar es salaam.
Tina baada ya kumaliza kidato cha nne hakufanikiwa kuendelea na kidato cha tano kutokana na kutokidhi vigezo. Wazazi hawakuwa na uwezo wa kumuendeleza kielimu kwa njia nyingine. Ikabidi kazi yake kubwa iwe kumsaidia mama yake kazi kwenye mgahawa wao.
___________
Nilimpenda sana Tina, tabasamu lake halikuwahi kutoka kwenye macho yangu. Sauti yake bembelezi ya kike, ilibaki kwenye mvumo wa masikio yangu. Pale nitembeapo. Ni kama vile ilikuwa sauti ya mtangazaji wa redio mwenye kuongoza kipindi chenye kupendwa sana; sauti ya Tina iliendelea kubaki nami na kuishi nami daima.
________
Mikono yangu ilinitetemeka, baada ya kumbukumbu ya Tina kunipitia. Huku nikiwa na tazama na barua ile.
Je nini kiliendelea?