RIWAYA : KIJIJINI KWA BIBI SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA.
MTUNZI : ALEX KILEO.
________________
ILIPOISHIA...
________________
Kesho yake ilipofika, mama Kayoza na
Kayoza
pamoja na Omari wakaongozana
usiku ule mpaka kwa mchungaji
Wingo, Walipofika, mchungaji na
familia yake, wakawakaribisha ndani,
na baada ya maongezi ya muda
mrefu, mchungaji aliwaambia kuwa,
mama kayoza na Omari warudi
nyumbani, ila Kayoza abakie, kwa
sababu anataka akeshe nae huku
wakimfanyia maombi na familia
yake Mchungaji.
Mama kayoza na Omari
wakajiondokea zao, wakamuacha
kayoza nyumbani kwa mchungaji...
KAMA MCHUNGAJI ANGEJUA
KITAKACHOMTOKEA, WALA ASINGEKUBALI
KUBAKIA NA KAYOZA...
_______________
ENDELEA...
_______________
Baada ya mama kayoza kuondoka, Mchungaji alielekea katika chumba kimojawapo ndani ya nyumba yake na kukaa kwa muda wa dakika chache kisha akarejea tena mahali alipomuacha Kayoza,
"we ni mkristo wa dhehebu gani?" Mchungaji wingo alimuuliza Kayoza baada ya kukaa.
"ni mromani, romani catholic" Kayoza
alijibu huku akijaribu kutabasamu.
"ok, je unaamini katika
ulokole?" Mchungaji Wingo akarusha swali
jingine.
"mi naamini katika dini
yeyote na dhehebu lolote ambalo linafuata matakwa na njia za
Mungu" Kayoza akajibu,
"Umeshawahi kukaa peke yako hata siku moja na kufanya maombi?" Mchungaji Wingo alimuuliza Kayoza huku akimuangalia kwa umakini,
"Hapana" Kayoza alijibu,
"Na kanisani uwa unaenda?" Mchungaji Wingo aliendelea kumuuliza Kayoza,
"Hapana" Kayoza akajibu,
"Sasa unaamini vipi katika dini zinafuata matakwa ya Mungu aliye hai ungali wewe hufuati njia za Mungu?" Mchungaji alimuuliza Kayoza,
"Kuna kipindi uwa Nataka sana kwenda kanisani, ila uwa najikuta napata uvivu mkubwa sana" Kayoza alitoa jibu lililomfanya Mchungaji Wingo atabasamu,
"Wewe unafikiri ni kitu kinapelekea upate uvivu siku ya kwenda kanisani?" Mchungaji Wingo aliuliza tena,
"Mwanzo nilikuwa sijui, ila kwa hizi habari alizonieleza mama, nafikiri ni mzimu ndio ulikuwa unaniletea hali hiyo" Kayoza alijibu na kufanya mchungaji atabasamu tena,
"Mbona mama yako alikuwa anaenda kanisani akiwa chini ya huo mzimu?" Mchungaji Wingo aliuliza,
"Hivi mchungaji unadhani nyumba ya jirani yako unaweza kuitawala kama unavyoitawala nyumba yako?" Kayoza alitoa swali lililomfanya Mchungaji Wingo ashtuke kidogo,
"Unamaanisha nini kusema hivyo?" Mchungaji Wingo aliuliza,
"Mzimu kanifanya mimi kuwa nyumba yake, sasa anaweza kunikontroo atakavyo yeye, kwa hiyo mamlaka anayoweka juu yangu ni lazima yawe yana nguvu kuliko anayoweka juu ya mama yangu" Kayoza alimjibu Mchungaji Wingo,
"Jibu lako zuri sana, ila lina kasoro, hakuna kiumbe kitakachoweza kukutawala hapa duniani kama utamuamini Mungu" Mchungaji Wingo aliongea huku anaangalia mazingira ya sebuleni kwake,
"Kwa maana hiyo mimi simuamini Mungu?" Kayoza aliuliza,
"Hiyo ni Imani iliyopo moyoni kwako, kwa hiyo hilo swali jiulize wewe" Mchungaji Wingo aliongea huku akitabasamu,
"Kwani Mchungaji imani ipo kwenye nyumba za ibada tu?" Kayoza aliuliza,
"Hilo swali nitakujibu siku nyingine. Nikuletee maji ya baridi au ya moto?" Mchungaji Wingo alimuuliza Kayoza huku akitabasamu,
"ila mchungaji mimi sijaomba maji na wala sina kiu" Kayoza alijibu huku akionekana kumshangaa Mchungaji Wingo,
"Sijamaanisha una kiu, na sio kila unachopewa, kuna vitu unapewa bila hata kuomba" Mchungaji Wingo aliongea huku akiondoka na kumuacha Kayoza akimuangalia huku akitabasamu kutokana na maneno ya Mchungaji Wingo.
*******************
Sajenti Minja alitolewa moja kwa moja kutoka katika ofisi za mkuu wake wa jeshi na kuanza kupelekwa katika nyumba moja nzuri ambayo ilionesha haikuwa inakaliwa na mtu au anaekaa pale atakuwa hayupo au ni watu ambao hawapendi kelele, uzuri mwingine ni kwamba ile kambi ni ngeni machoni kwa Sajenti Minja ila si ngeni masikioni mwake kwa maana alishapata habari za kambi hii kutoka kwa wenzake wachache aliokutana nao mafunzoni.
Waliendelea kuisogelea ile nyumba huku kila mmoja akiwa kimya na uzuri wa ile nyumba kwa nje, tayari Sajenti Minja kichwani kwake alishatengeneza fikra za kule ndani ya nyumba kutakuwaje. Aliwaza kutakuwa na kitanda kikubwa, jakuzi, upepo mzuri wa Air condition na kila aina ya chumba kizuri ambacho mwanajeshi kama yeye anastahili kupumzika.
"Mheshimiwa vua viatu" Mwanajeshi aliyeongozana na Sajenti Minja aliongea na kumfanya Sajenti Minja atoke kwenye dimbwi la mawazo,
"Alaah! Kumbe tumefika?" Sajenti Minja aliuliza huku akitabasamu lakini yule Mwanajeshi hakushughulika kumjibu na badala yake alibonyeza namba zilizopo kwenye mlango na mlango ukafunguka, hapo ndipo alipokuta wanajeshi wengine wawili wakiwa mlangoni wakiwasubiri,
"Huyu wa wapi?" Mwanajeshi mmoja kati ya wale wawili aliuliza,
"Mgonjwa wa kifua" Mwanajeshi aliyeongozana na Sajenti Minja alijibu na kufanya Sajenti Minja ajikohoreshe kidogo,
"Kumbe kweli unaumwa? Twende ukapate matibabu upumzike" Mwanajeshi yule mwenye herufi zilizoandikwa MP aliongea na kumfanya mwenzake atabasamu na wakati huo huo yule Mwanajeshi aliyemleta Sajenti Minja aliishia mlangoni na kurudi alipotoka.
Wale wanajeshi wakiwa na Sajenti Minja walivipita vyumba kadhaa na mwisho waliingia katika chumba kimoja kilichoandikwa "BREATH",
"Ebu ruka ruka kichura chura kidogo ili mwili upate joto" MP mmoja alimwambia Sajenti Minja,
"Ni moja ya matibabu au?" Sajenti Minja aliuliza kwa mshangao,
"Ruka bwana, dawa unazotakiwa kunywa zinahitaji joto kubwa la mwili" Yule MP aliongea huku akimuangalia Sajenti Minja.
Sajenti Minja akaanza kuruka kichura chura kwa kasi huku akicheka na kubadilisha mitindo mbalimbali ya kuruka kichura chura.
Baada ya dakika mbili jasho lilianza kumtoka, akaamua asimame,
"Nadhani hapa nipo poa, mwili umeshachemka huu" Sajenti Minja aliongea huku akitabasamu, lakini alikuwa amekosea sana, alishtukia akipigwa kofi zito sana la shingo,
"Endelea kuruka, nani kakupa ruhusu ya kusimama?" MP mmoja aliongea kwa ukali huku akiwa amemkunjia uso Sajenti Minja,
"Kwani ni adhabu hii?, sio lazima niruke" Sajenti Minja nae aliongea kwa ukali huku akiwa amepaniki,
"Tutajua kama ni adhabu au sio adhabu" MP mwingine aliongea na kumpiga ngumi Sajenti Minja iliyompata vizuri usoni. Sajenti Minja alivyoona hivyo akaona imeshakuwa hatari, akaanza kupambana na wale MP, alipambana nao vizuri na akawadhibiti, maana alitoa kichapo cha hatari mpaka wale MP wakawa wanaogopa kumsogelea.
Sajenti Minja akiwa bado anajiamini kwa kichapo alichotoa, alianza kuondoka kibabe, ila hata kabla hajapiga hatua mbili alitokea mwanajeshi mwingine akiwa na bastola,
"Ukileta fujo nakufumua miguu, lala chini na uweke mikono juu" Mwanajeshi aliongea huku akiwa hatanii,
"Kwani kuna tatizo gani, mbona siwaelewi?" Sajenti Minja aliuliza,
"Lala chini ndio uhoji" Mwanajeshi aliongea kwa sauti kubwa na kumfanya Sajenti Minja akubaliane nae, akalala chini na wale MP waliokula kichapo wakamwendea na kumfunga pingu kwa nyuma, kisha wakambeba juu juu mpaka katika chumba kingine na kumuweka juu ya kiti cha chuma na kumfunga na kamba, kisha wakaanza kumpiga kwa hasira walimchakaza haswa.
Baada ya kuridhika na kipigo walichokitoa, ndipo alipoingia yule bwana mkuu wa jeshi aloyekuwa anamuhoji mwanzo kule ofisini, MP wakampigia saluti na kumsogezea kiti kwa kukiweka mbele ya kiti alichokalia Sajenti Minja,
"Umelijua kosa lako?" Yule bwana alimuuliza Sajenti Minja huku akimuangalia kwa huruma, lakini Sajenti Minja hakuweza kujibu kitu,
"Ulichofanya wewe ni kudhalilisha jeshi. Huwezi kuacha kazi kwa kuogopa kitu kwa sura wala muonekano. Ni bora ungeomba muda wa kujipanga tungekuelewa. Alafu ulipoamua kuacha kazi ukaamua utumie na kigezo cha kuumwa, hilo ni kosa pia, unadanganya wakati uliahidi kusimamia ukweli" Yule bwana mkuu wa jeshi aliongea kwa sauti ya upole ila iliyosikika vyema masikioni kwa Sajenti Minja.
Kisha yule bwana akasimama huku akimuangalia Sajenti Minja,
"Mpelekeni sehemu tulivu apoze maumivu" Yule bwana aliongea na kuanza kuondoka huku akiwa haonekani kama ni mtu mwenye kupenda kucheka.
Yule bwana alitembea mpaka alipofika mlango wa kutokea nje ya lile jengo, ndipo aliposikia sauti kubwa ya Sajenti Minja ikipiga kelele kutokana na maumivu aliyokuwa anayapata muda huo,
"Siku zote mwanajeshi mpumbavu utulivu anaostahili ni huo unaoambatana na maumivu" Yule bwana mkubwa aliongea huku akitabasamu na wakati huo huo alikuwa anatoka nje ya lile jengo lililokuwa tulivu kwa nje, ila kwa ndani si sehemu salama kwa wanajeshi wenye makosa.
***************
Baada ya muda kidogo Mchungaji Wingo alirudi huku akiwa na jagi lililojaa maji,
"Muda wa maombi unakaribia, umejiandaaje?" Mchungaji Wingo alimwambia Kayoza,
"Kawaida tu, ila naimani tutafanikiwa" Kayoza alijibu,
"Ni bora umetanguliza Imani mbele, ni jambo jema" Mchungaji aliongea kwa imani,
"Nimekuletea maji hayo unywe, ingawa hujaniagiza ila itabidi unywe" Mchungaji Wingo alimwambia Kayoza,
"Haina shida, nitakunywa tu" Kayoza alijibu huku akiyamimina yale maji katika glass.
Muda wote ambao mchungaji alikuwa anaongea na Kayoza, watoto wake walikuwa wanatayarisha chumba cha kufanyia maombi.
Baada ya maandalizi,
mchungaji Wingo alimkaribisha Kayoza
katika chumba cha maombi, kisha
watoto na mke wa mchungaji Wingo
wakaingia katika chumba cha maombi,
huku kila mmoja akiwa amebeba biblia yake mkononi, hapo ilikuwa yapata saa tano za usiku
usiku.
Baada ya wote kujumuika ndani ya kile chumba, maombi yakaanza rasmi,
Mchungaji Wingo na familia yake
walikemea kwa juhudi zote, mpaka saa
saba usiku, Kayoza alikuwa kama
mwanzo, hakuwa na mabadiliko yoyote, Ila Mchungaji hakukata
tamaa, pia alikuwa anahisi
akishindwa kumtibu Kayoza, heshima
yake inaweza kushuka katika kanisa, kwa hiyo alizidisha maombi .
Ilipofika saa nane za usiku mabadiliko yakaanza kwa Kayoza, alihisi kizunguzungu, hakuna aliyeyaona hayo kabadiliko isipokuwa yeye mwenyewe.
Wakati maombi yanaendelea Mchungaji
akahisi, kuna nguvu nyingine iko kwa
nje, inashindana nae, kwa maana yeye alikuwa na uwezo wa kuona mpaka visivyoonekana. Ile nguvu iliyokuwa inatoka nje ilikuwa haimdhuru ila hakuwa akiitaka iendelee kumuingilia katika maombi yake. Akaamua atoke nje mara moja na akaiacha familia yake inamuombea Kayoza. Ile
kutoka nje, akakutana na watu zaidi ya kumi, wote wako uchi, wamejipaka
majivu usoni.
Mchungaji Wingo
hakupata tabu kuwatambua kuwa
wale ni wachawi. Katika kipindi cha
maisha yake ya uchungaji ameshakutana na hayo mambo mara nyingi tu.
Akaona dawa yao ni ndogo tu, akaanza kukemea, Baada ya kupambana nao kwa
muda wa saa moja, wale wachawi
wakawa wanaelekea kushindwa.
Ila ghafla mambo yakabadilika, Mchungaji Wingo akaanguka chini kisha akapoteza
fahamu. Sasa wale wachawi
wakasogea pale alipolala mchungaji huku wakiruka ruka kwa furaha na kuongea lugha isiyoeleweka. Walimsogelea kwa ajili ya kummaliza kabisa Mchungaji Wingo, ila kila
walipojaribu kurusha makombora
yao, hayakumdhuru
mchungaji.Wakajua sababu ya hayo
mambo ni kutokana na nguvu ya maombi ya familia ya mchungaji
waliyokuwa wanaendelea nayo chumbani.
Wachawi wote wakavamia
katika kile chumba kwa ajili ya kupambana na maombi ya familia ya Mchungaji, ni kitendo cha
dakika kumi tu, familia yote ya
mchungaji ilikuwa imepoteza fahamu ni kutokana na kwamba hawakuwa na imani ya kutosha.
Wachawi wakawabeba kisha wakawalaza nje ya geti pamoja na
mchungaji mwenyewe, kitu kilichowashangaza wachawi ni kuwa
kulikuwa na kijana ambae ni kayoza, toka wale wachawi waanze kuloga,
yeye hakudhurika, ndipo wachawi
wakafanya kosa la mwaka,
wakamweka kayoza katikati yao,
kisha, wakaanza kumloga, bila kutegemea, kayoza akabadilika na
kubeba taswira ya kutisha, wale wachawi mawazo yao yakaona zoezi
lao limefanikiwa, mmoja kati ya wale
wachawi, akamsogelea kayoza ili
ammalize kabisa, ni kitendo bila
kuchelewa, kayoza ndani ya sekunde
kumi alishanyonya damu wachawi
watatu, ndani ya dakika moja
alishamaliza wachawi wote, nao
akawatoa nje, kisha akawalaza
pamoja na familia ya mchungaji,
kisha akarudi katika chumba cha maombi na akapoteza fahamu.
Asubuhi kulipokucha, watu wengi sana walijaa nje ya nyumba ya
Mchungaji Wingo, na wote walikuja kuangalia watu ambao walilala nje ya nyumba ya Mchungaji huku wakiwa na alama za meno shingoni.
Kati ya watu waliolala getini alikuwepo pia Mchungaji mwenyewe na familia yake...
******ITAENDELEA******