Notification texts go here Contact Us Buy Now!

NISAMEHEE RATIFA SEHEMU YA 15

*NISAMEHEE RATIFA EP 15*


Mateso yakawa mateso, Ibrahim akawa mtu wa kuhuzunika kila siku, hakuona raha ya ndoa tena, kuna kipindi alikuwa akilala peke yake chumbani, Nusrat hakuwa nyumbani, alikuwa klabu akiponda raha na wanaume wake wa Kiarabu.
Yalikuwa ni maumivu yasiyoelezeka moyoni mwake, rafiki yake mkubwa kitandani akawa mto, kila alipolia, machozi yake yalidondokea kwenye mto, kila alipohitaji faraja ya kukumbatiwa, aliukumbatia mto.
Kila kitu kikabadilika, kuna kipindi alitamani kumuacha Nusrat lakini wakati mwingine alipokuwa akifikiria kwamba msichana huyo alishughulika na vitu vingi katika maisha yake likiwepo suala la kazi, alishindwa kufanya hivyo.
Nusrat aliporudi nyumbani, hakuwa mzungumzaji sana, kila alipofika, alilala popote pale kwani pombe zilimjaa kichwani mwake. Hakuwa na muda wa kuongea na mume wake, alimuona kuwa takataka kwa kuwa alijua kwamba maisha yake yalimtegemea yeye.
Siku zikakatika, Ibrahim alipoona amechoka, ameshindwa kuvumilia, hapo ndipo alipoanza kumtafuta yule mzee ambaye alikuwa akizungumza naye kipindi cha nyuma, mzee ombaomba aliyekuwa akikaa karibu na eneo la Mnazi Mmoja kwa ajili ya kuzungumza naye.
Alipofika huko, mzee yule hakuwepo kitu kilichompa wakati mgumu, akaanza kumtafuta kwa kuulizia. Haikuwa kazi nyepesi, kila alipoulizia, hakukuwa na mtu aliyejua mahali alipokuwa, hakukata tamaa, alizunguka na kuzunguka na mwisho wa siku kufanikiwa kukutana na mtu ambaye alimuelekeza alipokuwa.
“Yule mzee alizidiwa hapa, alipelekwa hospitalini, baada ya hapo hakurudi tena. Ila yupo Magomeni Mapipa, ukifika pale, ulizia kwa mzee Majeed, mzee mwenye ndevu nyingi kama Osama, huwa anaishi nje ya nyumba ya huyo mzee, kibarazani,” alisema kijana muuza maji ambaye alimfahamu fika mzee huyo.
Ibrahim hakutaka kuchelewa, kwa kuwa alikwishapewa maelekezo ya kutosha, hapohapo akaanza kuelekea huko. Njiani alikuwa na mawazo mno, kile kilichokuwa kimetokea, kilimuumiza mno hivyo akatamani kumuona mzee yule ili amshauri juu ya kile kilichokuwa kikiendelea.
Hakuchukua muda mrefu akafika Magomeni Mapipa ambapo baada ya kuulizia kwa mzee Majeed, akaelekezwa na kuelekea huko. Mazingira aliyomkuta nayo mzee yule yalimuumia mno, hakuamini kile alichokuwa akikiona kwamba mzee masikini, aliyekuwa ombaomba alikuwa kibarazani amelala, pale alipokuwa, jua kali la saa saba liliwaka na kumuunguza lakini hakujali, hakuwa na sehemu nyingine zaidi ya hiyo. Ibrahim akahisi kulia.
Japokuwa hakuwa na fedha za kutosha lakini hakutaka kumuona mzee yule akiendelea kuishi katika maisha yale, maisha yaliyojaa umasikini mkubwa ambayo kila alipokuwa akiyafikiria, alijikuta akibubujikwa na machozi tu.
Akampangia chumba katika Mtaa wa Tandale na kumtaka kukaa huko, mara kwa mara alikuwa akielekea huko na kumsaidia kiasi fulani cha fedha ambacho aliamini kabisa kingeweza kumsaidia.
Siku zikaendelea kukatika, baada ya mwezi mmoja, aliporudi ndani ya nyumba ile aliambiwa kwamba mzee yule alikuwa amepelekwa hospitalini, kidonda kile alichokuwa nacho kiliongezeka na kilizidi kuoza japokuwa alikuwa akitumia dawa.
Ibrahim akachanganyikiwa, hakutaka kubaki mahali hapo, kwa kuwa aliifahamu Hospitali ya Mwananyamala sehemu ilipokuwa, akaanza kwenda huko. Njiani, mawazo yake yalikuwa kwa mzee huyo tu, moyoni mwake alihisi kulikuwa na kitu kilichomsukuma kumsaidia mzee yule, hakujua alikuwa na nani na alikuwa na nini, msukumo moyoni mwake ulimwambia ni lazima amsaidie mzee huyo.
Alipofika hospitalini hapo, akaingia mpaka ndani na kupewa maelekezo juu ya mahali alipolazwa mzee huyo, akaelekea huko. Alipofika nje ya chumba kile alicholazwa, akaruhiswa na kuingia ndani.
Mzee yule alikuwa kwenye maumivu makali mno ya mguu wake, kidonda kile kilipelekea mguu ule kuanza kuoza. Ibrahim alipomwangalia, alishindwa kuyazuia machozi yake, yakaanza kububujika mashavuni mwake.
“Wewe ni ndugu yake?” aliuliza daktari.
“Ndiyo! Kuna nini?”
“Hebu nifuate.”
Akaanza kuondoka na daktari yule kuelekea katika ofisi yake ambayo haikuwa mbali na chumba kile. Walipofika, wakaingia ndani na moja kwa moja kutakiwa kukaa kitini.
“Ndugu yako tumemkuta ana tatizo kubwa mguuni mwake,” alisema daktari yule.
“Tatizo gani?”
“Ana kansa ya mguu. Tuliangalia, tukagundua kwamba alichomwa na kitu chenye kutu hivyo kumletea tetenasi. Ugonjwa huu umekuwa ukiua watu wengi sana, kwake, umesababisha mguu kuoza, tukiuacha hivihivi, ni lazima ataoza zaidi kitu kinachoweza kusababisha kifo chake,” alisema daktari yule.
“Ooppss..! Kwa hiyo nini kifanyike?”
“Akatwe mguu! Hicho ndicho kinachotakiwa kufanyika ili kuokoa maisha yake,” alisema daktari yule. Ibrahim akashtuka.
*****
Alihitaji kuwa bilionea, ndivyo alivyokuwa kwa kipindi hicho, maisha yake yalibadilika, Latifa yule wa kipindi cha nyuma hakuwa huyu wa sasa, alikuwa na kila kitu alichokihitaji katika maisha yake.
Jina lake lilikuwa kubwa, alisikika katika kila masikio ya mtu duniani, dawa yake ilileta mapinduzi makubwa na ilisifika kila kona. Latifa alikuwa ni zaidi ya wanamuziki, alikuwa ni zaidi ya wacheza soka na alikuwa ni zaidi ya waigizaji filamu, kila alipopita, aliheshimiwa, watu wengine waliposikia kwamba alitarajia kupita barabara fulani, walikusanyika, yaani wengine walitaka kumuona tu.
Ndugu zao waliokuwa hoi vitandani kwa sababu ya magonjwa ya kansa, walipona na kuwa wazima kabisa, walimshukuru Latifa na hakukuwa na malipo mengine ambayo wangeweza kufanya zaidi ya kumheshimu na kumpenda maisha yao yote.
Latifa hakuishia nchini Marekani, chini ya kivuli cha Umoja wa Mataifa katika Shirika cha Afya Duniani, WHO, akaanza kuzunguka nchi mbalimbali duniani. Hiyo ilimpa heshima, ilimuongezea umaarufu na kila alipokuwa akienda, watu walikusanyika na kutaka kupiga naye picha.
Latifa akawazidi umaarufu hata watu wengine, alipotua nchini Uingereza, kwa heshima kubwa, akaalikwa mpaka bungeni ambapo huko akapewa nafasi ya kuzungumza, kila neno lililotoka mdomoni mwake, lilikuwa lenye kuleta matumaini makubwa kwamba alikuwa kwenye mikakati ya kutengeneza dawa za magonjwa mengi sugu likiwemo UKIMWI.
Hakuishia barani Ulaya, alizidi kuzunguka katika nchi nyingine, alifika mpaka Urusi ambapo huko akapokewa na watu wengi wakiwemo madaktari wakubwa, walioheshimika, madaktari waliokuwa na nyadhifa za kupokelewa na viongozi wakubwa katika nchi nyingine, ila kutokana na kile alichokifanya, wote walikuwa uwanjani kumpokea.
“Ni binti mdogo mno,” kila aliyemuona Latifa alizungumzia juu ya muonekano aliokuwa nao Latifa.
“Nini kinafuata?”
“Nitataka niende na Afrika pia, japokuwa hakuna magonjwa mengi ya kansa, ila natakiwa kwenda kuwaona hata haohao wagonjwa wachache, nitaanzia na Monrovia nchini Liberia,” alisema Latifa.
Taarifa zikatolewa, nao Waafrika ambao kila siku walijiona kutengwa, wakajiandaa kumpokea mtu wao, msichana aliyekuwa maarufu mno duniani kutokana na dawa ya magonjwa ya kansa aliyekuwa ameitengeneza, Latifa.

Waliberia walijipanga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Daniel Oduber Quiros, kila mmoja alikuwa na hamu ya kumuona Dk. Latifa ambaye alitarajiwa kuingia katika uwanja huo muda mchache ujao.
Idadi kubwa ya watu waliokuwa mahali hapo walikuwa na fulana zilizokuwa na picha za msichana huyo huku zikiwa zimeandikwa neno Hero likiwa na maana ya shujaa. Si wote waliokuwa na fulana hizo bali wengine walikuwa na mabango yaliyoandikwa maneno mengi ya kumsifia msichana huyo kutokana na ukombozi aliokuwa ameuleta duniani.

ITAENDELEA..

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.