Notification texts go here Contact Us Buy Now!

NISAMEHEE RATIFA SEHEMU YA 14

NISAMEHEE RATIFA EP 14


Vitabu vilimsaidia, alitumia muda wa miezi mitatu na ndipo alipoanza kuona mafanikio ya ile kazi aliyoanza nayo kwa kipindi kirefu, dawa ikaanza kukamilika kitu kilichompa furaha mno kwa kuona sasa alikuwa njiani kutimiza ndoto yake.
Hakutaka kufanya siri, alichokifanya ni kumpigia simu Dk. Dickson Myles kwa ajili ya kufika hapo maabara na kumuonyeshea kile alichokuwa amekitengeneza.
“Unaionaje?” aliuliza Latifa, usoni alikuwa na tabasamu pana.
“Ipo vizuri, umefanyaje mpaka ukapata hii dawa?” aliuliza Dk. Myles huku akionekana kushangaa.
“Ni kazi kubwa na ngumu iliyohitaji mtu ujitoe sana, usijali. Nahitaji unifanyie mipango ili niweze kukamilisha kila kitu,” alisema Latifa.
Hakutaka kumwamini mtu yeyote yule, alitumia muda mwingi sana kutengeneza dawa ile na aliona kama angemwambia mtu yeyote yule namna alivyotengeneza dawa ile basi watu wangeweza kuiga na hivyo kutengeneza haraka na kuisambaza hata kabla hajaisambaza yeye. Hakutaka kuona hilo hivyo alifanya kila kitu kuwa siri kubwa.
Baada ya siku tatu, Dk. Myles akafika na Waziri wa Afya nchini Marekani, Bwana Brian Peterson kwa ajili ya kuiona dawa hiyo. Latifa hakuwa na jinsi, aliamini kwamba huo ndiyo ungekuwa mwanzo wake hivyo akamuonyeshea.
Haikuwa dawa ya vidonge, ilikuwa ni ya kimiminika ambayo ilitakiwa kuhifadhiwa kwenye chupa na mgonjwa alitakiwa kunywa na baada ya mwezi mmoja angepona kabisa na kuwa mzima.
Kilichofanyika ni kumpigia simu dokta mkuu wa Hospitali kubwa ya St. Augustino Medical Center ambaye alifika mahali hapo na kuanza kuiangalia. Alikubaliana nayo kwa asilimia kadhaa na hivyo ilitakiwa kufanyiwa marekebisho hata kabla ya kupitishwa na kuanza kutumika.
Kulikuwa na watu wengi mno nchini Marekani waliokuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya kansa hivyo hata tangazo lilipotolewa kwamba kulihitajika wagonjwa wawili waliosumbuliwa na kansa kwa ajili ya kufanyiwa matibabu, walipatikana kwa haraka sana tena huku wengine wakipanga mstari hospitalini kuhitaji matibabu.
Matibabu yakaanza na hatimaye wagonjwa hao kuruhusiwa kuondoka. Latifa alibaki kimya, kipindi cha mwezi mzima ambacho alitakiwa kusubiri alikuwa na presha tele, alikuwa akimuomba Mungu ili dawa ile ifanye kazi kama ilivyotakiwa na hatimaye aweze kuwa bilionea kwa ajili ya kuiuza dawa hiyo ambayo mpaka katika kipindi hicho alikuwa amekwishaisajili.
Siku zilikatika na hatimaye mwezi kumalizika. Wagonjwa wale waliofanyiwa majaribio wakapigiwa simu na kutakiwa kufika katika hospitali hiyo haraka iwezekanavyo. Wala hawakuchukua masaa mengi, wakafika na hivyo kufanyiwa tena vipimo.
Majibu yalipokamilika, jopo la madaktari sitini wakaitwa kwa ajili ya kuipitia ripoti hiyo ya majibu ya wagonjwa wale. Walikaa katika chumba kile kwa dakika kadhaa, ripoti ilipokamilika ikaletwa na kukabidhiwa Dk. Peterson, akashusha miwani yake na kuiangalia vizuri.
“It is impossible!” (Haiwezekani!) alisema Dk. Peterson kwa mshtuko huku akiangalia majibu ya vipimo.
“What do you see?” (Unaona nini?)
Hakujibu swali hilo, alichokifanya ni kuwapa karatasi ile ya majibu na kila daktari kuanza kuiangalia. Kwa miaka yote hawakuwa wamefanikiwa kupata dawa ya kansa, walikuwa na Masters, PhD, leo hii, msichana mwenye digrii moja tu, tayari alifanikiwa kutengeneza dawa ya kansa, kila mmoja akashtuka.

Malumbano yalikuwa yakisikika kutoka katika nyumba moja nzuri na iliyoonekana kuwa ya kifahari iliyojengwa Sinza Mori. Kelele zile zilizokuwa zikiendelea ziliwafanya majirani kutokutulia, kila waliposubiri zipungue japo kidogo, zilizidi kuongezeka zaidi.
Majirani wakashindwa kuvumilia, walisubiri kwa kipindi kirefu sana kuona kelele hizo zikipungua lakini hazikupungua na hivyo kutoka ndani ya nyumba zao na kuwaamuru wanyamaze lakini hawakunyamaza.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa watu hao kulumbana, maisha yao yalitawaliwa na malumbano ya mara kwa mara, kila siku walikuwa kero kwa majirani ambao mara kadhaa waliamua kuwapeleka katika Ofisi za Serikali ya Mtaa lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote ile.
“Hivi unanijua wewe mwanamke?” aliuliza mwanaume mmoja, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka, mwili wake ulitetemeka kwa hasira.
“Hivi na wewe unanijua? Unaionaje hii ngozi, unaichukulia poa, sasa utaona,” alisema mwanamke huyo.
“Unajua nitakuua wewe malaya!”
“Uniue mimi! Haloo haloo, eti uniue mimi, thubutu,” alisikika mwanamke huyo.
Huyo alikuwa Ibrahim na Nusrat. Ndoa yao ilifikisha mwaka mmoja lakini iliwaka moto. Hakukuwa na furaha ndani ya ndoa, tangu waoane na kuishi pamoja, maisha yao yalitawaliwa na malumbano ya mara kwa mara.
Walipendana kipindi cha uchumba, tu waliahidiana mambo mengi lakini ndani ya ndoa kila kitu kinaonekana kubadilika. Nusrat yule aliyekuwa, msichana yule mrembo alikuwa amebadilika.
Mara kwa mara alikuwa akirudi nyumbani usiku, tena akisindikizwa na wanaume wake, watoto wa Kiarabu walioonekana kuwa na fedha nyingi, alipofika nyumbani, hakutaka kuzungumza na mume wake, moja kwa moja alikuwa akiingia ndani kulala.
Ibrahim aliumia, alivumilia lakini uvumilivu ulifika mwisho, siku hiyo aliamua kulumbana naye, japokuwa walifanya hivyo mara kwa mara lakini siku hiyo ilionekana kuwa tofauti, alikuwa na hasira mno na kila wakati alikunja ngumi.
Nusrat hakuwa msichana aliyetulia hata kidogo, alikuwa mtu aliyehusudu sana starehe kuliko mambo mengine, mara kwa mara wanapokuwa kitandani, Nusrat hakutaka kufanya tendo la ndoa na mumewe jambo lililomuumiza mno Ibrahim
Mbali na hivyo vyote, pajani mwa msichana huyo karibu kabisa na kiuno kulichorwa tattoo moja yenye alama ya kopa ambayo pembeni iliandikwa ‘Nakupenda Nusrat’. Hicho ndicho kilichomkasirisha sana Ibrahim kwani alijua kwamba kulikuwa na mwanaume aliyeichora tattoo hiyo pajani mwa mke wake, hivyo kila siku walipokuwa wakilumbana, ilikuwa ni lazima kuizungumzia tattoo hiyo.
“Hivi haya ndiyo malipo yako? Hivi haya ndiyo malipo unayonipa baada ya kuuacha moyo wangu ukupende kwa mapenzi ya dhati? Nusrat mke wangu! Hivi ndiyo unaamua kunilipa ubaya kwa wema? Hivi hujui kwamba nilimwacha msichana aliyenipenda kwa ajili yako? ” aliuliza Ibrahim. Hapo ndipo kumbukumbu zake za maisha ya nyuma zikaanza kumrudia kwamba aliwahi kumuacha msichana aliyempenda kwa mapenzi ya dhati kwa ajili ya Nusrat ambaye leo hii alikuwa akileta ujinga ndani ya ndoa. Alishikwa na hasira lakini hakujua ni kitu gani alitakiwa kukifanya.
“Kwani nilikulazimisha umuache? Nilikulazimisha? Hebu niache niondoke, nitarudi kesho, najisikia kukesha klabu leo,” alisema Nusrat kwa dharau kubwa, alikuwa kashavalia, alichokifanya ni kuondoka nyumbani hapo kwenda klabu.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake ya kila siku, kila alipokwenda huko, alirudishwa na wanaume wa Kiarabu wenye gari kitu kilichomuongezea maumivu makali Ibrahim mpaka kufikia hatua ya kutamani kumuua msichana huyo.
*****
“You are very bright Latifa, you are very bright,” (Una akili sana Latifa, una akili sana Latifa) yalikuwa ni maneno yaliyosikika kutoka kwa Dk. Myles, hakuwa akiamini kama kweli ile dawa ya Morphimousis aliyokuwa ameitengeneza Latifa iliweza kuwaponya wagonjwa wale waliosumbuliwa kwa kansa.
Dawa ile ikaanza kutangazwa, Wamarekani na watu wa Ulaya ambao asilimia kubwa walikuwa wagonjwa wa magonjwa ya kansa wakamsifia Latifa na kumpa heshima kubwa japokuwa alikuwa na elimu ndogo na umri mdogo wa miaka ishirini na moja tu.
Jina lake likaanza kutangazwa, vituo vya televisheni vyote vikaanza kumtangaza kama mkombozi ambaye aliletwa duniani ili kuwaokoa watu waliokuwa wakiteseka vitandani. Ingawa Latifa alipewa sifa sana na kuonekana mtu sahihi kuletwa duniani lakini kukaanza kuibuka vuguvugu kati ya Tanzania na Marekani.
Latifa alikuwa Mtanzania lakini alisomea nchini Marekani. Nchi hiyo haikutaka kumuachia Latifa kiholela kwamba aelekee nchini Tanzania na kufanya kazi na wakati elimu kubwa aliyokuwa nayo ilitokea nchini mwao.
Latifa akagombaniwa, jina lake likazidi kupenya masikioni mwa watu wengi duniani. Kwa kuwa Marekani lilikuwa taifa kubwa, wakaamua kutumia nguvu zao nyingi kumtangaza Latifa kama Mmarekani na kuipoteza nchi ya Tanzania kiasi kwamba watu wengi duniani walijua kwamba Latifa alikuwa Mmarekani.
Kupitia dawa yake, akaanza kuingiza fedha, maisha yake yakabadilika, kutokana na ongezeko la wagonjwa wa kansa, Latifa akajikuta akiingiza kiasi cha dola milioni mia moja ndani ya wiki moja tu, hizo zilikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni mbili.
Wakati mwingine alijiona kama yupo ndotoni na muda wowote ule angeamka kutoka usingizini, umaarufu alioupata kwa ghafla sana uliyabadilisha maisha yake. Kila siku aliingiza kiasi kikubwa cha fedha, akanunua jumba kubwa na la kifahari lililokuwa Los Angeles hapohapo Marekani.
Ili kuzuia kila kitu kutoka kwa nchi kama Tanzania iliyokuwa ikitangaza kwamba Latifa alikuwa mtu wao, hapo ndipo Wamarekani wakaamua kumuajiri msichana huyo katika hospitali kubwa ya St. Luis Medical Center iliyokuwa hapohapo nchini Marekani katika Jiji la New York.
Japokuwa hakuwa amemaliza masomo yake lakini Latifa akapewa jina la udaktari rasmi na kuanza kuhudumia wagonjwa katika hospitali hiyo. Uwepo wake mahali hapo, ukawafanya wagonjwa wengi kumiminika, hawakuamini kama msichana huyo ndiye yule aliyekuwa amegundua dawa hiyo iliyomaliza matatizo ya watu wengi.
Aliwakumbuka sana Watanzania, alimkumbuka mlezi wake, bi Rachel lakini kila alipotaka kurudi nchini Tanzania, alizuiliwa kwa kupewa majukumu mengi ya kikazi jambo lililoendelea kuzua mtafaruku mkubwa kati ya Marekani na Tanzania.
Ndani ya mwaka mmoja wa mafanikio yake, Latifa akawa daktari mwenye kiasi kikubwa cha fedha, heshima yake ikaongezeka na akawa bilionea kijana kuliko wote duniani huku akimuacha vibaya mmili wa Mtandao wa Kijamii wa WorkSpace, Williams Peters aliyekuwa na umri wa miaka ishirini na mbili.
“Ni kitu gani ambacho huwezi kukisahamu maishani mwako?” aliuliza Larry King, mtangazaji wa Kituo cha Habari cha CNN.
“Ooppss…” alishusha pumzi Latifa na kuendelea:
“Kuna watu wengi wamejeruhiwa, kuna watu wamepewa vidonda ambavyo haviwezi kupona kamwe hata kama utakuja kuwa na maisha ya mafanikio kiasi gani huko mbeleni. Kwangu, siwezi kumsahau mwanaume anayeitwa Ibrahim,” alisema Latifa na kunyamaza.
“Ndiye nani?”
Latifa akanyamaza, akaingia kwenye hali ya mawazo, ghafla akaanza kububujikwa na machozi. Kila kitu kilichotokea katika maisha yake ya nyuma kikaanza kujirudia kichwani mwake.
Chuki kubwa ikamjaa moyoni mwake, hakumpenda Ibrahim, alimnyima furaha kipindi cha nyuma, alimnyanyasa kisa tu alimpenda. Hakudhania kama ingetokea siku yoyote ile angemsamehe mwanaume huyo. Kama kulia, alilia sana, hakutaka kumpenda hata siku moja na hata kile alichomfanyia katika maisha yake, hakutaka kumsamehe hata mara moja.
“Ninamchukia Ibrahim. Ninamchukia mno,” alisema Latifa huku akiyafuta machozi yake.
“Ndiye nani?”
Hapo ndipo Latifa akaanza kusimulia kile kilichokuwa kimetokea katika maisha yake ya nyuma. Alisimulia tangu siku ya kwanza alipokutana na mwanaume huyo alipomfuata shuleni kwao. Moyo wake ukajawa na maumivu makali mno. Alimpenda na kumpa penzi lake, alimthamini lakini baada ya kusafiri na kuelekea Marekani, kila kitu kikabadilika.

“Ni kitu ambacho sitokuja kukisahau. Hata ikitokea siku nikamuona shetani na Ibrahim wapo porini wanataka kuliwa na simba na nina nafasi ya kumuokoa mmoja, nitamuokoa shetani,” alisema Latifa huku akionekana kumaanisha kile alichokisema, moyo wake ulitawaliwa na chuki kubwa dhidi ya Ibrahim, mwanaume aliyeutesa moyo wake hata zaidi ya Liban.

ITAENDELEA

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

إرسال تعليق

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.