Notification texts go here Contact Us Buy Now!

NISAMEHE RATIFA SEHEMU YA 21

NISAMEHE RATIFA 21


Akaanza kufanyiwa maandalizi kwa ajili ya uchukuaji video, muda huo, ndugu zake walikuwa pembeni wakifuatilia kila kitu, walionekana kuwa na furaha mno. Dominick hakuacha kuchukua kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo, bado aliendelea na mchakato wake wa kumtengenezea makala msichana huyo. Baada ya kumaliza, akaitwa mbele ya kamera na kuanza kuhojiwa.
Latifa akaanza kusimulia historia ya maisha yake tangu alipofukuzwa mama yake ambayo historia yake alisimuliwa na mzee Issa, alisimulia kila kitu, baada ya kutimuliwa nyumbani kwa mama yake kisa alikuwa na mimba ya mtu mweusi, akakimbilia kwa mwanaume aliyempa ujauzito ule ambaye naye huyo aliamua kumtimua nyumbani kwake.
Ilikuwa simulizi yenye kuhuzinisha, wakati mwingine alipokuwa akisimulia, alitabasamu, kuna kipindi alifika, alibubujikwa na machozi na kuendelea mbele. Hakutaka kuacha kitu, alimzungumzia Ibrahim, jinsi alivyoutesa moyo wake, alivyomuacha mbele ya msichana mmoja wa Kiarabu, aliumia, alikosa raha, akakata tamaa ya kupenda hivyo kurudi nchini Marekani.
Alipofika huko, akasimulia kuhusu Liban, kila alipokuwa akiwazungumzia watu hao wawili, machozi yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake, aliumia mno, aliteseka moyoni mwake mpaka kipindi kingine alitamani kufa, afe ili asiweze kuteseka tena.
“Pole sana Latifa,” alisema mtangazaji aliyekuwa akimhoji.
“Ahsante sana, ila ni maisha, Mungu anaporuhusu jambo fulani litokee, huwa anakupa na mlango wa kutokea,” alisema msichana huyo.
Kipindi hicho kilichukua saa moja, alipomaliza, akasimama na kumfuata mzee Issa, akamkumbatia huku akibubujikwa na machozi mashavuni mwake, alipotoka mikononi mwake, akamfuata bi Semeni na kumkumbatia pia.
“Samahani Latifa,” alisema msichana mmoja, alikuwa mfanyakazi wa hapo.
“Bila samahani.”
“Kuna mtu anakuulizia hapo getini.”
“Nani?”
“Anaitwa Ibrahim, amesema kwamba unamfahamu,” alijibu msichana yule.
Latifa alipolisikia jina hilo, moyo wake ukapiga paaaa, akakunja uso wa hasira, machozi yakaanza kumbubujika tena, kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma kama mkanda wa filamu.
*****
Kwa mara ya kwanza Kituo cha Televisheni cha Global kilitangaza kwa kusema kwamba siku ya Ijumaa kungekuwa na mahojiano maalumu na msichana bilionea mwenye asili ya Kitanzania ambaye alikuwa akiishi nchini Marekani, Latifa Issa kama alivyojulikana.
Kila mtu akatamani kukiangalia kipindi hicho kilichotarajia kuruka majira ya saa tisa alasiri. Watu wakaambiana, wakasambaziana taarifa kwamba msichana huyo bilionea, aliyeleta tumaini kubwa duniani hasa kwa wagonjwa wa kansa angehojiwa moja kwa moja kwenye televisheni.
Kila mtu alitaka kumsikiliza, kila mtu alitaka kusikia historia ya maisha yake kwamba alianzia wapi, alipitia wapi na wapi mpaka kuwa vile alivyokuwa kipindi hicho. Kila kona, stori ilikuwa moja tu kuhusu Latifa, matangazo yakatangazwa sana, watu wakashikwa na hamu kubwa ya kumsikiliza msichana huyo mrembo.
Kati ya watu waliokuwa na hamu ya kumsikiliza Latifa alikuwa Ibrahim, alijua kwamba angeumia hasa mara baada ya kumsikia msichana huyo akizungumzia kile kilichopita, hakutaka kujali sana, alichoamua kipindi hicho ni kumsikiliza tu.
Kwa kuwa alikuwa amekwishamwambia mzee Deo kuhusu Latifa, alichokifanya ni kumwambia kwamba msichana yule aliyekuwa amemkataa alitarajiwa kuhojiwa katika televisheni, hivyo akawa na hamu ya kutaka kumuona.
Siku hiyo ambayo ndiyo ilitakiwa kuonyeshwa kwa kipindi hicho, Ibrahim akaamua kumchukua mzee huyo na kumpeleka nyumbani kwake, hakumuhofia mke wake, alijua kwamba mwanamke huyo alikuwa mkorofi lakini kwenye suala la Latifa, hakutaka kusikia chochote kile.
“Umemleta kufanya nini humu?” aliuliza Nusrat huku akionekana kuwa na hasira, mbaya zaidi akaziba hata pua yake kumaanisha kwamba alikuwa akisikia harufu mbaya.
“Nimemleta, nataka kumuonyeshea yule msichana aliyenipenda, nikaamua kumuacha kwa ajili yako shetani,” alisema Ibrahim kwa kiburi.
“Ndani ya nyumba yangu?”
“Wewe mjinga nini, hebu tupishe, na ole wako ulete za kuleta, ndugu zako watakuta maiti tu humu ndani,” alisema Ibrahim, hata Nusrat alipomwangalia mumewe, alijua kwamba siku hiyo alikuwa tofauti, kama ni ng’ombe basi aliota mapembe.
Ibrahim akamchukua mzee Deo na kwenda kutulia naye kochini, akachukua rimoti ya televisheni na kisha kuiawasha. Mzee Deo alikaa kitini, hakujisikia kuangalia, hakuwa na amani kabisa kwani jinsi alivyokuwa akimwangalia Nusrat ambaye alikaa pembeni kabisa, alionekana kuwa na hasira mno.
Latifa alivyoonyeshwa kwenye televisheni, Ibrahim akajikuta akianza kububujikwa na machozi, moyo wake uliumia, kila alipokuwa akimwangalia msichana yule, akagundua kwamba aliitupa almasi jangwani na kuokota bati.
Msichana huyo mrembo, mwenye muonekano wa fedha akaanza kusimulia historia ya maisha yake. Kila mmoja akabaki kimya akimsikiliza, alianza kusimulia kuanzia mbali, tangu mama yake alipofukuzwa nyumbani kwao, alipokwenda nyumbani kwa mpenzi wake, Deo kisha kumfukuza, alionekana kuumia mno.
Mzee Deo aliposikia historia aliyokuwa akiisimulia Latifa, akashtuka, akaanza kumwangalia Latifa, akasimama kutoka katika kochi lile na kuisogelea televisheni, kila mmoja mule ndani akabaki akimshangaa.
“Ibrahim….” aliita mzee Deo, machozi yakaanza kumtoka.
“Nipo mzee….”
“Latifa ni binti yangu!” alisema mzee Deo huku akionekana kushangaa, Ibrahim akashtuka, si yeye tu, hata Nusratakashtuka.
“Unasemaje?”
“Kumbe Latifa ndiye mtoto wangu aliyezaliwa na Nahra,” alisema mzee Deo.
Hapo ndipo Ibrahim alipoanza kukumbuka mahojiano yale, alikumbuka Latifa alimtaja mtu aliyeitwa Nahra na Deo, wazazi wake waliokuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi mpaka baba yake alipomfukuza mama yake.
Mahojiano yale akayaunganisha na historia aliyowahi kusimuliwa na mzee huyo kwamba zamani alikuwa na mwanamke wa Kihindi, alimpa ujauzito lakini baadaye akafukuzwa nyumbani kwao, na alipokuja kwake, naye alimfukuza ila ni kwa sababu tu alitishiwa kuuawa na ndugu zake Nahra kwa kutumiwa watu waliokuwa na bunduki, na kama asingemfukuza basi angeuawa yeye.
“Ni mtoto wangu! Kumbe Latifa ni mtoto wangu!” alisema mzee Deo huku akijifuta machozi.
Ibrahim alishindwa kuamini, wakati mwingine alifikiri kwamba alikuwa ndotoni, katika kipindi chote alichokuwa akiishi na huyo mzee, alivyokuwa akizungumza naye kumbe alikuwa mzazi wa msichana aliyekuwa amemuacha, Latifa.
Latifa hakuwa na kipindi kirefu katika kituo kile, alichokifanya Ibrahim ni kumwambia kwamba ilikuwa ni lazima kumfuata Latifa huko na kumwambia ukweli kwamba alikuwa na baba yake nyumbani kwake.
“Ngoja nikamlete uzungumze naye,” alisema Latifa.
“Atakubali kuja?”
“Atakuja tu. Subiri,” alisema Ibrahim huku akionekana kuchanganyikiwa, hakutaka kuchelewa, akaondoka kuelekea huko, tena alikuwa akikimbia kwa kasi ajabu.

Jina la Ibrahim lilimchanganya, hakuamini kama kweli aliitwa na msichana yule kwa kuwa alikuwa akihitajika na mtu aliyejitambulisha kwa jina hilo. Huku akionekana kuwa na hasira, akatoka pamoja na ndugu zake kuonana na huyo mtu.
Alipofika, alipomwangalia Ibrahim, akajikuta akiingiwa na huruma, aliyesimama mbele yake alikuwa Ibrahim, yuleyule kijana aliyekuwa amemtesa na kumkataa kipindi cha nyuma, ila hali aliyokuwa nayo, ilimtia huruma mno.
“Ibarhim,” alijikuta akimuita kijana huyo aliyeonekana kupigwa na maisha.
“Latifa…” aliita Ibrahim, tayari machozi yakaanza kumbubujika, hata naye kumbukumbu za nyuma zikaanza kujirudia kichwani mwake.
“Umefuata nini?” aliuliza Latifa huku akiwa amesiamam.
“Kwanza naomba unisamehe kwa yote yaliyotokea, dunia imeniadhibu kwa kile nilichokufanyia,” alisema Ibrahim.
Japokuwa alijiahidi kwamba asingeweza kumsamehe mwanaume huyo lakini hakuwa na jinsi, kwa namna ambavyo alionekana mahali hapo, ilionyesha kabisa kwamba maisha yalimpiga, hivyo hakutaka kumwadhibu tena, alichokifanya ni kuukunjua moyo wake na kumsamehe kwa kila kitu kilichotokea.
“Nimekusamehe Ibrahim, dunia imekufunza,” alisema Latifa.
“Kuna kitu ninahitaji kutoka kwako.”
“Kitu gani?”
“Baba yako anateseka Latifa, kila ulichoambiwa ni kweli kilitokea, ila naye ana historia ya tofauti na hiyo uliyokuwa nayo,” alisema Ibrahim, alikuwa amemsogelea kidogo, kila mtu akashtuka.
“Baba yangu?”
“Ndiyo!”
“Nani?”
“Mzee Deo!”
“Hapana! Baba yangu kashakufa!”
“Una uhakika? Ulionyeshewa kaburi lake? Au hata picha yake unayo”
“Ibrahim, baba yangu! Haiwezekani!”
“Latifa, huu ndiyo muda wa kuusikia ukweli, twende ukamuone baba yako, ameteseka sana, kansa ya mguu ilisababisha kukatwa mguu wake, twende ukamuone, atafurahi kama akikuona,” alisema Ibrahim.
“Baba yangu……” alisema Latifa, sauti ya kilio chake ikaanza kusikika.
“Ni kweli, yupo hai, hana pa kuishi, amekuwa akiteseka miaka yote, alikuwa ombaomba mitaani, alifukuzwa kila sehemu. Nimekuwa nikiishi naye kwa kipindi kirefu pasipo kujua kwamba ni baba yako, historia aliyonisimulia, ni hiyohiyo ambayo umesimulia japokuwa kuna kitu ambacho haukukifahamu, si wewe tu bali hata marehemu mama yako hakukifahamu, nimemsaidia sana mpaka kufikia kipindi hiki. Naomba twende ukamuone, tuwahi, namjua mke wangu, anaweza hata kumuua,” alisema Ibrahim.
“Kumuua! Amuue baba yangu!”
“Ni mwanamke mwenye roho mbaya! Twende Latifa,” alisema Ibrahim, hawakutaka kusubiri, waliposikia kwamba mke wa Ibrahim angeweza kumuua mzee Deo, wote wakaingia ndani ya gari na kuanza kuelekea huko.
Garini, bado Ibrahim aliendelea kumuomba msamaha msichana huyo, alijutia matendo aliyoyafanya, hakuomba msamaha kwa kuwa Latifa alikuwa msichana bilionea, aliomba msamaha kwa kuwa alihitaji kusamehewa kwa yote aliyoyafanya.

itaendelea..

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.