Notification texts go here Contact Us Buy Now!

NISAMEHE RATIFA SEHEMU YA 17

NISAMEHE RATIFA 17


Serikali haikukataa, ilichokifanya ni kumsikiliza na hatimaye kumdhamini kwenda nchini humo ambapo mara baada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Touba, mara chache alikuwa akipata nafasi ya kwenda katika kambi za wakimbizi na kuzungumza nao, alifanya kila kitu kwa kutengeneza makala kwa njia ya video kwa ajili ya maisha yake ya baadaye.
Aliwazoea wakimbizi, kila alipowaona namna walivyopata tabu, alijikuta akibubujikwa na machozi mashavuni mwake. Picha mbaya za watu waliojeruhiwa vibaya, watu waliokuwa wakiteseka kwa magonjwa mabaya yakiwemo ya zinaa mara baada ya kubakwa na wanajeshi, yalimuumiza mno.
Aliishi huko kwa miaka miwili na ndipo alipoanza kusikia kuhusu Latifa. Alivutiwa naye, msaada alioutoa wa kuisaidia dunia nzima kutokana na magonjwa ya kansa akavutiwa nayo, alichokifanya ni kuanza kumfuatilia msichana huyo.
Latifa alipoanza ziara ya kutembelea nchi mbalimbali Afrika hapo ndipo akaona lingekuwa jambo la maana sana kama angeonana na msichana huyo na kuzungumza naye, kweli alifanikiwa.
Alipomwangalia Latifa, alikuwa msichana mrembo, mwenye mvuto, msichana mwenye macho mazuri, yaliyong’aa mithili ya goroli, lipsi pana, nywele ndefu zilizofika mpaka mgongoni. Moyo wake ukampenda lakini huo haukuwa muda wa mapenzi na alijiahidi kwamba asingeweza kuwa na msichana huyo katika maisha yake yote zaidi ya kufanya naye kazi tu.
Alipopewa sharti la kutokuzungumzia mapenzi, kwake halikuwa tatizo, hakuhisi kama moyo wake ulikuwa kwenye mapenzi na msichana huyo mrembo, alichokifanya ni kukubaliana naye.
Siku iliyofuata ndipo safari ya kuelekea nchini Kongo ilipoanza, walichukua ndege, wakakaa pamoja huku wakizungumza mengi. Japokuwa Latifa tayari alikuwa bilionea lakini hakutaka kujali, alikuwa na nidhamu na fedha zake na hakutaka kutumia kiasi kikubwa cha fedha pasipo kuwa na sababu.
“U mwanamke mrembo sana, umechukua wapi urembo huo?” aliuliza Dominick.
“Umeanza!”
“Nimeanza nini sasa?”
“Nilikwambia nini jana?”
“Daah! Kwani kuna kosa kama nikimsifia Mungu?”
“Hapana! Mambo ya uzuri achana nayo kwanza. Kumbuka, hapa kazi tu,” alisema Latifa, alionekana kubadilika.
“Ooh! Ok! Nilishasahau, hakuna tatizo,” alisema Dominick, akavuta Jarida la Boniventure na kuanza kulisoma.
Ndege iliendelea kukata mawingu, baada ya masaa kumi ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N’Djili uliokuwa katika jiji kubwa la Kinshasa nchini Kongo. Ndege iliposimama, abiria wote wakaanza kuteremka.
Kama ilivyokuwa katika nchi nyingine, watu zaidi ya elfu tano walikuwa wamekusanyika uwanjani hapo tayari kwa kumpokea msichana Latifa. Kila alipofika, aliacha alama kubwa ya umaarufu wake.
Alipendwa kwa kuwa alionekana kuwa msichana mwenye huruma nyingi kuliko wote. Alipofika nje ya jengo la uwanja huo, huku akiwa na Dominick, waandishi wa habari wakaanza kumsogelea na kuanza kumpiga picha mfululizo.
“Mmh! Kumbe maisha ya mastaa yapo hivi!” alisema Dominick, alimwambia Latifa kwa sauti ya chini karibu na sikio.
“Yapo vipi?”
“Hayana raha, kila kona karaha,” alisema Dominick.
Walipofika nje kabisa, tayari mlango wa gari moja likafika uwanjani hapo, lilikuwa lina bendera ya nchi hiyo, lilikuwa la kifahari sana. Mwanaume mmoja aliyevalia suti akawafuata na kuwaambia kwamba walitakiwa kwenda kuingia ndani ya gari lile.
“Ni gari la serikali?” aliuliza Latifa.
“Ndiyo!”
“La nani?”
“Waziri Mkuu!”
“Mmmh! Mwenyewe yupo wapi?”
“Wewe twende, tutaongea mbele ya safari,” alisema mwanaume huyo, walipolifikia gari lile wakaingia ndani na kuanza kuondoka, furaha ambayo watu walikuwa nayo kipindi hicho wakaanza kulikimbiza huku wakishangalia.
“Karibu sana Latifa,” alimkaribisha mwanaume huyo aliyezungumza Kiswahili vizuri kabisa.
“Ahsante sana. Aya, nijibu sasa,” alisema Latifa.
“Nchi hii ipo kwenye matatizo sana,” alisema mwanaume yule.
“Matatizo gani?”
“Watu wanataka waziri mkuu ajiuzulu.”
“Kisa?”
“Machafuko yaliyotokea, yaani watu wana hasira naye, anaishi kwa kujifichaficha tu, kama angeonekana hata pale uwanjani, wangeweza kumuua,” alisema mwanaume yule.
“Nimekuelewa.”
Safari iliendelea mbele, walizungumza mambo mengi huku kila mmoja akimuuliza mwenzake maswali. Kila swali ambalo Latifa aliliuliza lililonekana kuwa muhimu, Dominick aliliandika kwenye notebook yake.
Hawakuchukua muda mrefu wakaingia katika jumba moja kubwa la kifahari, kwa kuliangalia kwa nje tu isingekupa wakati mgumu wa kugundua kwamba mmiliki wa jumba hilo alikuwa mmoja wa watu wenye fedha nyingi.
Gari liliposimamishwa ndani ya eneo la jumba hilo, wote watatu wakateremka. Latifa akabaki akiliangalia jumba lile la kifahari, lilikuwa moja ya majumba makubwa aliyowahi kuingia, kulikuwa na bustani nzuri ya maua, masanamu yaliyonakshiwa kwa unga wa dhahabu, kulikuwa na mbuga ndogo ya wanyama iliyokuwa imezungushiwa fensi huku ndani yake kukiwa na wanyama wachache, kulikuwa na bwawa kubwa la kuogelea, kwa kuliangalia tu, ungegundua kwamba mtu aliyekuwa akiishi ndani ya jumba hilo alikuwa mtu mwenye pesa nyingi.
Wakaingizwa ndani, kulikuwa na makochi makubwa yaliyozungushiwa vyumba vilivyokuwa na rangi ya dhahabu, kadiri Latifa na Dominick walivyokuwa wakiliangalia, bado akili yao iliwaambia kwamba mtu aliyekuwa akilimiliki jumba hilo hakuwa mtu wa mchezo kwenye mambo ya fedha.
Mara mwanaume mmoja akatokea mahali hapo, alikuwa mfupi, mwenye kitambi kikubwa, sura mbaya huku kichwani akiwa amenyoa mtindo wa kijana ujulikanao kama kiduku.
Alikuwa na umri mkubwa, kama miaka sitini lakini kwa kumwangalia, muonekano wake ulikuwa wa ujana zaidi. Alivalia fulana iliyokuwa na picha ya muimbaji wa Marekani, Jay Z, mikononi alivalia saa ya dhahabu. Miguuni, alivalia raba zilizokuwa na chata kubwa ya Nike, kwa muonekano wa harakaharaka usingeweza kugundua kama mwanaume huyo alikuwa mtu mzima.
“Karibuni sana,” aliwakaribisha huku naye akijiweka kochini.
Huyo alikuwa waziri mkuu nchini Kongo, alikuwa miongoni mwa viongozi waliochukiwa mno, machafuko yaliyokuwa yakitokea nchini humo mara kwa mara, yeye ndiye aliyekuwa akisuka mipango huku lengo lake kubwa likiwa ni kuchukua dhahabu na kuwauzia Wazungu.
Wakongo hawakumpenda, waliandamana hadharani kupinga uwepo wake nchini humo, walimchukia sana lakini hawakujua walitakiwa kufanya nini kwani kila uchaguzi mkuu ulipofika, alishinda kwa kishindo kikubwa, ila kwa kuiba kura nyingi.
“U msichana mzuri sana Latifa,” alisema bwana Nelson Savimbi huku uso wake akiupendezesha na tabasamu pana lakini uso haukubadilika, bado ulikuwa mbaya.
“Nashukuru sana.”
Walizungumza mambo mengi, Latifa aliyeonekana kuwa mchangamfu zaidi alimwambia kile kilichokuwa kimemleta nchini Kongo hivyo kuhitaji muda wa siku mbili kwa ajili ya ziara ya kutembelea hospitali za nchini humo na baadhi ya kambi za wakimbizi.
Hilo halikuwa tatizo haa kidogo, alichokifanya bwana Savimbi ni kumruhusu na hivyo kuwasiliana na wahusika na kuwaambia juu ya uwepo wa Latifa nchini humo. Baada ya kuzungumza kwa kipindi kirefu hapo ndipo walipoondoka na kuelekea katika hoteli kubwa ya nyota tano, The Bufalloes iliyokuwa katikati ya Jiji la Kinshasa.
“Nakutakia usiku mwema Latifa,” alisema Dominick.
“Ahsante! Nawe pia,” alisema Latifa na kuingia chumbani kwake.

Usiku hakulala vizuri, kichwa chke kilikuwa kikifikiria juu ya safari yake kubwa ya mafanikio aliyokuwa nayo, ilikuwa safari ndefu ambayo kwa kipindi hicho alijivunia mno kuwa hapo alipokuwa.
Hakuacha kuwakumbuka wanaume waliouumiza moyo wake, wanaume aliotokea kuwachukia kuliko wote katika dunia hii. Hakumpenda Ibrahim hata mara moja, alimchukia Liban, mwanaume wa Kihindi ambaye aliamua kumuacha kwa kuwa tu aliwasikiliza ndugu zake.
Hakutaka kujificha, alikiri kwamba kati ya watu aliokuwa akiwachukia mno basi watu hao walikuwa mstari wa juu kabisa. Usiku huo hakuacha kukumbuka kuhusu mama yake, aliambiwa kwamba mama yake aliitwa Nahra, mwanamke mrembo aliyekuwa mlevi ambaye alifukuzwa na wazazi wake mara baada ya kupewa mimba na mtu mweusi kisha kumfukuza.
Chuki yake ikaongezeka, watu aliokuwa akiwachukia wakaongezeka, pia alimchukia baba yake ambaye hakuwa akimfahamu, sababu kubwa ya kumchukia ni jinsi alivyomfukuza mama yake kisha kuingia kwenye ulevi mkubwa uliompa Ugonjwa wa UKIMWI na mwisho wa siku kufariki.
Mbali na baba yake, aliwachukia babu na bibi yake kwa upande wa mama kwa kitendo chao cha kumfukuza mama yake kisa tu alizaa na baba yake. Moyo wake ulimuuma mno ila wakati mwingine alibaki akimshukuru Mungu kwa kuamini kwamba isingekuwa hivyo, inawezekana leo hii asingekuwa hapo alipokuwa.
Siku iliyofuata, akajiandaa tayari kwa kuanza safari ya kuelekea katika hospitali mbalimbali, alipomaliza kujiandaa, akatoka nje ambapo akakutana na Dominick akiwa tayari nje, alipomuona, tabasamu pana likajengeka usoni mwake.
Hotelini hapo kulikuwa na ulinzi mkubwa, polisi walikuwa wakizunguka huku na kule kuhakikisha kwamba ulinzi unakuwa mkubwa na wa kutosha. Japokuwa Latifa hakupendwa kulindwa na silaha lakini hakuwa na jinsi, alikubaliana na kila kitu.

ITAENDELEA..

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

إرسال تعليق

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.