NISAMEHE RATIFA EP 16
Miongoni mwa watu waliokuwa uwanjani hapo alikuwemo Waziri wa Afya nchini humo, bwana Fredrick Taylor aliyetangulizana na mkewe. Waandishi wa habari kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari nchini humo walikuwepo uwanjani hapo huku wakiwa na vitendea kazi vyao, kikundi cha ngoma za kienyeji kilikuwa tayari huku watoto wawili waliokuwa na maua wakiwa wamewekwa tayari.
Aliyekuwa akisubiriwa hakuwa rais kutoka nchi fulani, alikuwa Latifa, msichana mwenye asili ya Kihindi ambaye mama yake alifukuzwa nyumbani na kutamani kujiua huku baadaye akisaidiwa na kijana toka Mtaa wa Tandale ambaye ndiye aliyemlea Latifa mpaka muda huo.
Baada ya saa moja, ndege binafsi ikaanza kuonekana angani, taarifa zikatolewa kwamba ndege ile iliyotarajiwa kutua ndiyo ambayo ilimbeba Latifa, wapiga picha na watu wengine wakaanza kujiandaa.
Iliposimama, ngazi ikashushwa, ikawa sawasawa na zuria jekundu. Walioanza kuteremka walikuwa watu kadhaa ambao alitangulizana nao na mwisho wa siku kuteremka Latifa mwenyewe.
Alichokiona, akashindwa kuyazuia machozi yake kububujika mashavuni mwake. Msichana yeye, aliyeteswa na mapenzi, msichana ambaye mama yake alikufa kwa Ugonjwa wa UKIMWI baada ya kufanya sana ngono na walevi wa gongo, leo hii alikuwa akipokelewa kishujaa.
“I can’t believe this,” (Siamini hili) alisema huku akionekana kushtuka.
Zaidi ya watu elfu tano walikuwa wamekusanyika ndani ya uwanja huo, walipomuona tu, wakashindwa kuvumilia, wakaanza kupiga makofi na vigelegele vya shangwe. Msichana maarufu kuliko wote duniani alikuwa akiteremka katika ngazi za ndege, alipofika chini, akaanza kusalimiana na bwana Taylor kisha kukabidhiwa maua na watoto wale, kikundi kile cha ngoma za asili kiliendelea kupiga ngoma zile kisha baada ya hapo akachukua nafasi hiyo kupiga picha na baadhi ya watu waliokusanyika uwanjani hapo kisha kupanda ndani ya gari na kuondoka.
Siku iliyofuata ilikuwa ni siku maalumu kwa Latifa kupelekwa katika hospitali ya taifa ya nchi hiyo, huko, akapata nafasi ya kuonana na wagonjwa mbalimbali waliokuwa hoi vitandani. Hakuwaacha, alizungumza nao mengi, aliwafariji na pia kuwatia nguvu kwamba wangepona magonjwa yao.
“Siamini kukuona,” alisema mgonjwa mmoja.
“Kwa nini?”
“Nilisikia mengi kuhusu wewe, nilisikia kuhusu maisha yako, yalinigusa sana, mwisho wa siku nikafikiri kwamba ni mwanamke mtu mzima, kumbe binti mdogo!” alisema mgonjwa huyo huku akimshangaa Latifa.
“Kwani hukuwahi kuniona kabla kwenye televisheni?”
“Sikuwahi! Nimekuwa nikiugua uti wa mgongo kwa mwaka wa tano sasa, siwezi kusimama, siwezi hata kukaa, maisha yangu yote kwa kipindi hicho ni kulala kitandani tu,” alisema mgonjwa huyo maneno yaliyomuumiza mno Latifa.
“Pole sana!”
“Ahsante! Karibu sana katika nchi hii yenye utajiri wa almasi zilizojaa damu,” alisema mgonjwa yule.
“Nashukuru! Ila hautakiwi kuziita almasi zilizojaa damu. Vita vilikwisha, kila kitu kimebaki na kuwa historia, sahau yaliyopita,” alisema Latifa huku akifahamu fika kwamba nchini hiyo ilikuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka kadhaa iliyopita.
Hakuishia hapo, siku hiyo alitaka kuzunguka kote, kila aliyemuona, hakuamini kama siku hiyo alikutana na msichana mwenye jina kubwa, msichana aliyeuwa bilionea mkubwa duniani.
*****
Dunia nzima ilijua uwepo wa Latifa barani Afika, kila mtu alikuwa na hamu ya kumuona msichana huyo mrembo aliyegundua dawa ya magonjwa ya kansa ambayo kwa kipindi hicho ndiyo iliyokuwa ikizungumza katika kila kona.
Watu wengi walitamani kutembelewa na msichana huyo ambaye kwa kipindi hicho alikuwa amemaliza ziara yake ya kutembelea nchini Liberia na alikuwa akijiandaa na safari nyingine ya kuelekea nchini , Kongo, Ivory Coast na sehemu nyingine barani Afrika.
Kila alipopita, Latifa aliacha gumzo kubwa, watu walimzunguka kwa lengo la kuzungumza naye. Kila alipokanyaga, vituo mbalimbali vya televisheni vilimuita na kufanya naye mahojiano, alialikwa katika shule mbalimbali kwa ajili ya kuzungumza na wanafunzi huku wakati mwingine akitembelea kambi za wakimbizi kwa lengo la kuwajulia hali na kuwakumbusha kwamba pamoja na kila kitu kilichokuwa kikitokea, bado alikuwa pamoja naye.
Alipanga kwenda nchini Tanzania, alitamani kuwaona watu aliozoea kuwaona miaka ya nyuma, alitamani kuyaona mazingira ya Tanzania ambayo aliyaacha kipindi cha nyuma. Aliikumbuka nchi hiyo, umasikini mkubwa uliokuwa umeigubika, watu waliokuwa wakifanya kazi usiku na mchana, kila alipowakumbuka, aliuona upendo mkubwa ukiendelea kuongezeka kwa Watanzania wenzake.
“Nitafika Tanzania, nitataka kutembelea sehemu zote nilizowahi kutembelea,” alisema Latifa huku akiwa kwenye Hoteli ya La Revancha iliyokuwa katikati ya Jiji la Dar nchini Senegal.
Pamoja na kutamani kufika nchini Tanzania, bado aliendelea kumkumbuka Ibrahim ambaye kwake alionekana kuwa miongoni mwa watu katili ambao hawakutakiwa kuishi katika dunia hii. Alikumbuka vilivyo kile kilichotokea kipindi cha nyuma, namna alivyotukanwa na kudharauliwa mbele ya macho ya watu, hakika aliuahidi moyo wake kwamba asingeweza kumsamehe Ibrahim.
“Siwezi kumsamehe! Mungu, naomba unisamehe ila kwa Ibrahim, siwezi kumsamehe,” alisema Latifa huku akionekana kuwa na hasira mno.
Ilikuwa ni saa 4:00 usiku, alikuwa amejiandaa kulala tayari kwa kuanza safari ya kuelekea nchini Kongo kisha kwenda Tanzania ambapo angeanzia mkoani Kigoma na kutembelea Hospitali ya Maweni kabla ya kwenda katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.
“Ngriii…ngriiii…ngriiii….” ilisikika simu ya mezani ikiita chumbani humo. Kwa hali ya kichovu Latifa akainuka kutoka kitandani na kuifuata simu hiyo, alipoifikia, akaunyanyua mkono wa simu ile na kuupeleka sikiona.
“Hallo!” aliita.
“Hallo! Samahani, kuna mgeni wako hapa.”
“Mgeni wangu?”
“Ndiyo!”
“Anaitwa nani?”
“Anaitwa Dominick!”
“Mmmh! Sawa! Nakuja.”
Latifa alibaki akishangaa tu, jina la mgeni aliyekuwa akimhitaji lilimtia wasiwasi kwani hakujua alikuwa nani na alihitaji nini kutoka kwake. Hakutaka kujali sana, kwa kuwa alifahamu kwamba alikuwa mtu wa watu, akaamua kuvaa na kushuka mpaka mapokezini ambapo huko akaonyeshewa mwanaume aliyekuwa akimhitaji.
Kwa kumwangalia, alionekana kuwa mwanaume mpole, mtanashati ambaye alivalia shati jeupe, surali nyeusi na tai nyekundu, uso wake ulipendezeshwa na miwani ya macho iliyomfanya kuonekana msomi mwenye masta.
“How are you!” (Habari yako!) alisalimia Latifa.
“Usijali, mimi ni Mbongo mwenzanko,” alisema Dominick huku akiachia tabasamu pana usoni mwake, tabasamu lililomfanya kupendeza vilivyo.
“Hahah! Samahani! Kumbe ni Mtanzania mwenzangu! Nasikia ulikuwa ukinihitaji,” alisema Latifa.
“Yeah! Kuna mengi nataka kuzungumza nawe,” alisema Dominick.
“Yapi hayo?” aliuliza Latifa huku akishtuka.
“Usishtuke, si mapenzi, tunaweza kukaa sehemu?”
“Hakuna tatizo!”
Latifa alijisikia huru, kuwa na Mtanzania mwenzake kulimfanya kujisikia amani moyoni. Walichokifanya ni kusogea pembeni mpaka katika mgahawa uliokuwa hotelini hapo na kisha kutulia.
Kabla ya kuzungumza chochote kile, wakabaki wakiangaliana kwa sekunde kadhaa, macho ya Dominick yalionyesha dhahiri kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake, alionekana kuwa katika dimbwi zito la mahaba.
“Samahani kwa kukusumbua,” alisema Dominick.
“Bila samahani!”
“Kwa jina ninaitwa Domick Simon, nimezaliwa Tanzania ila nilikuja hapa kwa ajili ya masomo yangu ya udaktari katika Chuo cha Touba kilichokuwa katika Mji wa Touba, Mashariki mwa nchi hii. Siku chache zilizopita nilisikia kwamba ungekuja hapa Senegal kwa ajili ya kutembelea wagonjwa katika ziara yako hii iliyo chini ya WHO,” alisema Dominick, Latifa alikuwa kimya akimsikiliza.
“Ndiyo!”
“Nilihitaji kujifunza mengi kutoka kwako, ninahitaji nisafiri nawe sehemu mbalimbali, nadhani kupitia wewe, naweza kupata vitu ambavyo vinaweza kunisaidia sana,” alisema Dominick huku akionekana kuhitaji msaada wa dhati.
“Mmmh!”
“Nini tena?”
“Hakuna tatizo, ila nina sharti moja,” alisema Latifa.
“Usijali Latifa, nitajigharamia kila kitu,” aliingilia Dominick.
“Simaanishi gharama.”
“Unamaanisha nini?”
“Sitaki mwisho wa siku useme kwamba unanipenda, sihitaji mapenzi kwa sasa, ninahitaji kuwa peke yangu,” alisema Latifa huku akimwangalia Dominick usoni.
“Hahaha! Yaani nikuepende wewe? Acha utani Latifa! Hilo sharti si gumu, nimekubaliana nalo,” alisema Dominick.
“Hakuna tatizo! Safari inaanza kesho asubuhi kuelekea Kongo,” alisema Latifa.
“Hakuna tatizo.”
Dickson Simon Magembe, alikuwa mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri sana nchini Tanzania katika mtihani wa kidato cha sita mwaka mmoja uliopita. Uwezo wake mkubwa wa darasani uliomfanya kuongoza Tanzania nzima ukaipelekea serikali ya nchi hiyo kumdhamini kwenda kusoma nchini Marekani katika Jimbo la Los Angeles.
Kwa kuwa alilelewa katika familia iliyopenda kusaidia watu mbalimbali waliokuwa kwenye matatizo, alichokifanya ni kuiambia serikali kwamba hakutaka kwenda kusoma nchini Marekani bali alitaka kupelekwa nchini Senegal ili atakapofika huko, apate muda wa kuwatembelea watu mbalimbali waliokuwa kwenye kambi za wakimbizi ili aweze kuwasaidia.
ITAENDELEA..