NISAMEHE RATIFA 13
“Ni vizuri kusaidia watu wasiojiweza,” alisema Nusrat.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki baina ya mzee masikini, ombaomba na Ibrahim. Mara kwa mara alikuwa akimfuata na kuzungumza naye mambo mengi ambayo kwa Ibrahim, yalimsisimua sana.
“Kwa hiyo ikawaje mpaka ukawa ombaomba?” aliuliza Ibrahim, alitegesha masikio yake kumsikiliza mzee yule ambaye pasipo kutegemea, akaanza kububujikwa na machozi, swali aliloulizwa, likazifanya kumbukumbu zake kurudi nyuma, akaanza kulia.
“Duniani kuna watu wabaya sana, duniani hapa, kuna watu wenye roho mbaya sana,” alisema mzee yule masikini.
“Kwa nini?”
“Nimepitia maisha magumu sana, sina kitu, nimepoteza kila kitu maishani mwangu,” alisema mzee yule.
Sauti yake ilikuwa ya chini sana, alizungumza huku akionekana kuwa na maumivu makubwa ya moyo. Kila alipoongea kidogo, alinyamaza, akameza fundo la mate na kuendelea.
Mzee huyo alimuhadithia Ibrahim mambo mengi huku akimbariki kwa kila kitu atakachokifanya katika maisha yake ya mbele. Ibrahim aliporidhika, akamuaga mzee yule tayari kwa kuondoka. Akajikuta akishikwa mkono, akageuka na kumwangalia mzee yule.
“Katika kila ukifanyacho, kumbuka kitu kimoja,” alisema mzee yule, alikuwa amemkazia macho Ibrahim.
“Kitu gani?”
“Usimfanye mwanamke akalia.”
“Nisimfanye mwanamke akalia?”
“Ndiyo! Kila chozi la mwanamke linalodondoka, huwa na laana nzito sana,” alisema mzee huyo.
“Kivipi?”
“Nipo hapa kwa sababu ya chozi la mwanamke, nipo hapa kwa kuwa nilimfanya mwanamke kulia. Hakika ningejua kama haya yangetokea, hakika ningemfanya kuwa na furaha milele, nisingeruhusu kuliona chozi lake,” alisema mzee yule, akanyamaza, akakiinamisha kichwa chake chini, akaanza kulia tena.
“Nyamaza sana mzee. Lakini kwa nini unaniambia hivi?”
“Ni kwa sababu wewe ni rafiki yangu, sipendi upate majanga kama niliyoyapata mimi, ninatamani uje kuwa na furaha kubwa maishani mwako,” alisema mzee yule.
“Maneno yako yananitisha.”
“Si kwamba nakutisha, ila ninakwambia njia za kufanikiwa, njia za kuiepuka laana maishani mwako,” alisema mzee yule.
“Usijali mzee, nitakuwa nikija mara kwa mara,” alisema Ibrahim na kuondoka. Moyoni mwake hakuweza kukumbuka chochote kuhusu Latifa japokuwa maneno yale yaliutesa sana moyo wake.
****
Usiku hakulala, muda wote macho yake yalikuwa wazi huku akiangalia juu tu. Kichwa chake kilikuwa na mawazo lukuki, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea nyumbani kwa mpenzi wake mara baada ya kwenda kutambulishwa.
Mpaka asubuhi inaingia, Latifa hakuwa amepata hata lepe la usingizi, usiku mzima alikuwa na mawazo tu. Hakutaka kuendelea kukaa nchini India, akajiandaa, akawasiliana na ofisi za kampuni ya ndege ya Indian Airlines na kuhitaji kuwekewa tiketi moja ya kwenda nchini Tanzania, hilo halikuwa tatizo.
“Kwa nini nina mkosi hivi? Kwa nini yote haya yananitokea mimi tu?” alijiuliza lakini hakupata jibu, bado alijiona kuwa na mkosi mkubwa maishani mwake.
Ilipofika saa kumi jioni, tena huku akiwa hajaingiza kitu chochote mdomoni, akaondoka hotelini hapo kuelekea uwanja wa ndege na ilipofika saa kumi na mbili jioni, akapanda ndege na kuanza kuelekea nchini Tanzania huku akiwa na majonzi makubwa moyoni mwake.
Kama kulia alilia sana lakini hakubadilisha kitu, kila kitu kilichokuwa kimetokea, kilitokea na hivyo alitakiwa kusahau kila kitu. Alipofika jijini Dar es Salaam, Latifa akapokelewa kwa shangwe kwa kuwa alifanikiwa sana katika elimu yake.
Alikuwa msichana mwenye uwezo mkubwa mno, alijijengea heshima kubwa chuoni kutokana na uwezo wake kuwa mkubwa, kila mtu akajivunia kuwa na mtu kama yeye hasa katika familia ya bi Rachel.
Siku zikaendelea kwenda mbele mpaka pale alipotakiwa kurudi tena chuoni nchini Marekani, akarudi zake. Chuoni huko, hakukutana tena na Liban, mwanaume huyo alikuwa amehama chuo na kuelekea katika Chuo cha Mumbai nchini India, hakurudi tena nchini Marekani.
Uzuri wa Latifa ukaendelea kuwa gumzo, hakujua ni nani aliwaambia watu kile kilichotokea, baada ya wiki kadhaa tu, kila mmoja alifahamu kilichoendelea nchini India na hivyo kumpa pole sana.
Hakutaka kujali tena, kila kitu kilichotokea maishani mwake alikichukulia kama changamoto. Japokuwa kwake ilikuwa ngumu kumsahau Liban lakini hakuwa na jinsi, baada ya miezi miwili tu, kumbukumbu juu ya Liban zikaanza kupotea kichwani mwake.
Uwezo wake wa darasani ulikuwa uleule, watu walimshangaa sana, darasani hakuwa mtu wa kawaida hata mara moja. Wanafunzi wengi walimfuata na kuanza kufundishwa naye, Latifa alikuwa tofauti huku wanachuo wengine wakisema kwamba msichana huyo alikuwa na uwezo mkubwa zaidi ya maprofesa chuoni hapo.
“Naomba kuuliza swali,” alisema Latifa, walikuwa darasani walipokuwa wakisoma.
“Uliza,” alisema profesa huku akiiweka vizuri miwani yake, kila mtu alimheshimu Latifa, hivyo kila alipoinuka na kutaka kuzungumza kitu, watu wote walikuwa kimya.
“Bila shaka mtu wa kwanza kutengeneza gari, alifikiria kuhusu gari tu na wala hakufikiria kwamba kuna mtu angekuja na kutengeneza ndege, si ndiyo?” aliuliza Latifa.
“Ndiyo!” alijibu profesa.
“Hivi kwa nini huyu mtu aliyekuja na kugundua ndege hakufikiria kutengeneza gari lenye miguu kumi badala ya minne?” aliuliza Latifa.
“Unamaanisha nini?”
“Nataka kufahamu tu.”
“Mmmh! Sijui kwa nini hakufikiria hilo.”
“Sawa. Lakini, kama Alexander Bell aligundua simu ya mezani, kwa nini mtu aliyegundua simu ya mkononi asigegundua simu za aina nyingine zinazotumia waya?” aliuliza Latifa.
“Napo sijui.”
“Kuna chochote unachojifunza kutokana na maswali yangu?”
“Hapana. Unamaanisha nini?”
“Kama jopo la madaktari duniani walikaa kwa ajili ya kutafuta dawa za kuua kansa iliyokomaa, wakakosa, hivi hatuwezi kuwa kama mtu aliyegundua ndege na simu za mkononi? Yaani namaanisha kwa kwenda mbele na kufikiria kitu kingine zaidi?” aliuliza Latifa.
“Unamaanisha nini?”
“Najua umeshajua ninachokimaanisha. Ninataka kutengeneza dawa za kuteketeza kansa katika dunia hii,” alisema Latifa kwa kujiamini.
“Unasemaje?” aliuliza profesa huku akiishusha miwani yake na kumwangalia vizuri Latifa.
“Ninataka kutengeneza dawa ya kansa, hiyo dawa itaitwa Morphimousis, nikwambie kitu profesa? Itakwenda kuokoa maisha ya watu wengi, niamini. Hii ndiyo nafasi ya kuwa bilionea ili yule Ibrahim na Liban wanitafute,” alisema Latifa, ghafla machozi yakaanza kumbubujika.
Huo ndiyo ulikuwa uamuzi aliokuwa ameuchukua, alikuwa akisomea masomo ya udaktari hivyo lengo lake kubwa kwa wakati huo lilikuwa ni kuwa daktari mkubwa ambaye angeweka historia katika dunia hii kwa kuweza kukumbukwa katika maisha yake yote, kabla na baada ya kifo.
Darasani alikuwa na akili mno, hakuwa msomaji sana lakini kila ulipokuwa ukija mtihani, kama kawaidayake alikuwa akiongoza kama kawaida yake. Latifa aliendelea kunawili kila siku lakini kwa kipindi hicho, hakutaka kuwa na mwanaume yeyote yule, alitaka kubaki peke yake mpaka atakapokufa.
Siku zilikatika, hapo ndipo alipoamua kuanza kusoma kwa juhudi hata kama alikuwa genius, alitaka kujifunza mambo mengi kuhusu mwili wa binadamu, ni kwa namna gani ulikuwa ukishambuliwa na magonjwa ya kansa na kwa namna gani angeweza kuyadhibiti magonjwa hayo.
Hilo likamfanya kushinda maabara kila siku, likamfanya kutafuta dawa nyingine ambazo alikwenda nazo humo kisha kuanza kuangalia ni kwa jinsi gani angeweza kutengeneza dawa moja ambayo ingekuwa yenye ubora mkubwa sana.
“Dawa zinapatikana kwenye miti, huko ndipo kwenyewe,” alisema Dk. Warren, alikuwa dokta mwenye uwezo mkubwa aliyeweka historia kwa kutengeneza dawa za magonjwa ya mifupa.
“Naweza nikapata wapi hiyo miti?”
“Nenda Amazon.”
“Unamaanisha msitu wa Brazil?”
“Ndiyo!”
Aliamua kwa moyo mmoja kufanya kile alichotaka kukifanya, kwenda nchini Brazil halikuwa tatizo, akajipanga na kisha kuelekea huko. Msitu ulikuwa unatisha sana lakini hakuwa na jinsi, alitakiwa kuingia na kuutafuta mti mmoja ulioitwa Mendozo, mti pekee uliokuwa na uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali, mti pekee ambao magome yake yalitumika kuwatibu Wabrazil.
Alipofika huko, tena huku akiwa na watu watano wenye silaha kali wakaanza kuzunguka msituni kwa malipo makubwa. Ilikuwa kazi kubwa, ya hatari na yenye kuchosha lakini hakutaka kukata tamaa, mbele yake aliyaona mafanikio makubwa, hivyo alitaka kupambana zaidi mpaka anaupata huo mti.
Walizunguka kwa kupumzika kwa kipindi cha wiki nzima na ndipo walipofanikiwa kuupata mti huo, wakachukua magome na kisha kurudi Rio De Janeiro huku kila mmoja akiwa na furaha.
Alipofika hotelini tu, kitu cha kwanza ni kuchukua magome yale na kuanza kuyafanyia kazi, alitaka kujua ni vitu gani vilikuwepo ndani ya miti ile ili mwisho wa siku na yeye aweze kuvitengeneza vitu hivyo au vinavuofanana na hivyo na mwisho wa siku kutengeneza dawa kali na yenye nguvu. Akafanikiwa katika hilo na kurudi nchini Marekani huku akiwa na sample.
“Nakwenda kuwa bilionea,” alisema Latifa, mwili ulichoka sana, alikuwa safarini kurudi nchini Marekani. Moyo wake ukafarijika mno.
Uhusiano wa kimapenzi uliwapa furaha kila mmoja, mipango yao ya ndoa iliendelea kupangwa na siku ya harusi ikawekwa tayari kwa ajili ya harusi hiyo ambayo ilionekana kufana hata kabla ya kufika.
Kila mmoja akawa na kimuemue cha kutaka kuoana, wageni wakaitwa kutoka Uarabuni tayari kwa kuhudhuria harusi hiyo kati ya Nusrat na Ibrahim. Hakukuwa na tatizo lolote lile, kila mmoja, hasa ndugu wa Nusrat walimpenda sana Ibrahim kwani ndiye alikuwa mtu pekee aliyechaguliwa na ndugu yao.
Baada ya wiki moja, hatimaye Ibrahim alivalia kanzu kubwa na kwenda ukweni kuoa. Huko, akajipatia mke wake na hatimaye maisha ya furaha kama mke na mume kuanza. Hakukuwa na mtu aliyefikiria jambo lolote lile baya, kila mmoja aliona kwamba ndoa kuwa furaha tupu pasipo kujua kwamba wakati mwingine, wanandoa hujuta sababu ya kuwafanya kuoa au kuolewa.Hawakujua hilo.
*****
Latifa akawa mtu wa kushinda maabara tu kwa ajili ya kuifanyia kazi dawa yake. Ilikuwa ni kazi kubwa lakini hakutaka kushindwa, kadiri alivyokuwa akiwafikiria wanaume walioutesa moyo wake na kumfanya kulia, hakutaka kukata tamaa kwa kuamini kwamba ni lazima angefanikiwa tu.
Siku ziliendelea kukatika, ndoto yake kubwa kwa wakati huo ilikuwa ni kuwa bilionea mkubwa baada ya kuuza dawa ya magonjwa ya kansa yaliyowatesa watu wengi duniani, hasa Wamarekani na watu wa Ulaya nzima.
Hakutaka kurudi nchini Tanzania, alikuwa bize akitengeneza dawa hiyo kwa kutumia vifaa maalumu. Wakati mwingine hakula chakula chochote kile, alishindakuanzia asubuhi mpaka usiku pasipo kuingiza chochote tumboni mwake, si kwamba hakusikia njaa, alisikia njaa lakini hakutaka kula mpaka ile hatua ambayo alitamani kuifikia kwa siku husika aifikie.
ITAENDELEA..