NISAMEE RATIFA 18
Wakaondoka na kuelekea katika Hospitali ya Mobutu. Idadi kubwa ya watu ilikuwa hospitalini hapo, waandishi wa habari kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari walikuwa mahali hapo kwa ajili ya Latifa tu.
Gari lile lililombeba yeye na Dominick liliposimama, wakatoka nje, waandishi wakawasogelea na kuanza kuwapiga picha. Latifa aliachia tabasamu pana, akashindwa kuvumilia, akajikuta akibubujikwa na machozi ya furaha, akaanza kuwapungia mikono watu hao.
Alichokikuta ndani ya hospitali hiyo kilimliza, hospitali ilikuwa chafu, huduma mbovu, wagonjwa walirundikana kila chumba, hakukuwa na mpangilio wowote ule. Kila aliyezungumza naye, walimwambia wazi kwamba huduma ilikuwa mbovu hivyo waliiomba serikali iweze kuwasaidia kudumia huduma na si kula hela na kuuza madini kiholela.
“Nitawasaidia kufikisha kilio chenu,” alisema Latifa.
Ziara ya siku mbili ikafanyika kwa mafaniko makubwa, walipomaliza wakaanza safari ya kuelekea nchini Tanzania katika Mkoa wa Kigoma. Walipofika huko, wakachukuliwa na kupelekwa katika Hoteli ya Hiltop na kuchukua vyumba humo. Kama ilivyokuwa sehemu nyingine, hata huko pia watu wengi walitamani kumuona msichana huyo mdogo mwenye mafanikio na hatimaye kuwa bilionea mkubwa akiwa na umri mdogo tu.
Waandishi wa habari na watu wengine walikusanyika katika Hoteli ya Hiltop kwa ajili ya kumuona Latifa ambaye wala hakuwa na hiyana, akaonana na watu hao kwa kukaa nao sehemu fulani kisha kuanza kuzungumza nao, walikuwa kama hamsini hivi.
“Unajisikiaje kuwa Latifa?” aliuliza mwanamke mmoja.
“Najisikia kawaida, ila najiona kuwa na thamani, hiki ndicho nilichokitaka, nitambulike mimi ni nani na nina mchango gani katika jamii,” alijibu Latifa huku akiachia tabasamu.
“Na huyo ni nani? Shemeji yetu?” aliuliza mwandishi mmoja.
“Nani? Huyu? Huyu ni rafiki yangu, anaitwa Dominick, nilikuwa naye tangu Senegal,” alijibu Latifa huku akichia tabasamu pana.
“Mnapendeza kuwa pamoja, kama wapendanao,” alisema mwandishi mwingine, akawasogelea na kuwapiga picha.
Maneno yale kama yakawa yameibua kitu fulani moyoni mwa Latifa, akauhisi moyo wake ukiingiwa na kitu cha tofauti kabisa, kitu alichokuwa nacho kipindi cha nyuma mara baada ya kuisoma barua aliyoandikiwa na Ibrahim.
Alipomwangalia Dominick, mvulana huyu aliachia tabasamu pana, kitu ambacho hata yeye mwenye hakujua kilikuwa nini, akaona kuwa mwanaume mzuri mno, akahisi kuanza kumpenda.
Maswali yaliendelea zaidi, Latifa aliwajibu wote lakini kichwa chake kiliingia katika fikra nyingine kabisa, alikuwa akimfikiria huyo Dominick aliyekuwa bize akiandika. Mara baada ya kumaliza mahojiano, wakaimama na kuelekea ndani.
“Dominick…” aliita Latifa, mwanaume huyo akamsogelea na kusimama karibu yake, walikuwa koridoni katika ghorofa ya tano hotelini.
“Naaam..” aliitikia Dominick huku akimwangalia Latifa, walikuwa karibukaribu mno.
“Au basi…” alisema Latifa, akageuka na kuingia chumbani.
Kichwa chake kikaanza kusumbuka, yule Dominick ambaye alimwambia wazi kwamba hakutaka siku amwambie kwamba alikuwa akimpenda, leo hii alijikuta akianza kumfikiria, mapenzi yakaanza kuchomoza moyoni mwake.
Usiku hakulala, alibaki akimfikiria mwanaume huyo tu. Kitandani, ni mawazojuu ya Dominick ndiyo yalikuwa yakimsumbua kila wakati. Hakujua afanye nini, hakujua kama lingekuwa jambo la kawaida kumwambia mwanaume huyo kwamba alimpenda.
“Dominick…These feelings have to stop right now, I can’t bear them,” (Dominick…hisia hizi zinatakiwa kutoka sasa, siwezi kuzibeba) alisema Latifa huku akibimbirikabimbirika kitandani pale.
Alibaki na mawazo mpaka ilipofika saa nane usiku ndipo alipopatwa na usingizi. Alipoamka asubuhi, akajiandaa na kutoka nje ambapo baada ya kumuona Dominick, akajikuta akishtuka na moyo wake ukidunda kwa nguvu.
“Umeamka salama?” aliuliza Dominick huku akitoa tabasamu lilimvuruga kabisa Latifa.
“Nimeamka salama, wewe?”
“Hata mimi nipo poa.”
Siku hiyo safari ilikuwa ni kwenda katika Hospitali ya Mkoa ya Maweni na hospitali nyingine hapo Kigoma, kote huko, watu walikuwa wakijazana na kumwangalia Latifa, kila aliyemuona hakutaka kuamini kama msichana yule alikuwa Mtanzania kama walivyokuwa.
Wagonjwa wakafarijika, maneno aliyokuwa akiyazungumza msichana huyo yakawatia nguvu na kujiona wakiingiwa na nguvu za kusonga mbele. Baada ya siku nzima ya kuwatembelea wagonjwa, siku iliyofuata ilikuwa ni zamu ya kwenda katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.
Huko, Latifa alijikuta akibubujikwa na machozi, hakuamini kama kulikuwa na watu waliokuwa wakipitia mateso makubwa kama alivyokuwa watu hao. Wengi walikuwa wagonjwa, madaktari walikuwepo kwa ajili ya kuwahudumia lakini kutokana na idadi ya wakimbizi kuwa wengi, hata wale madaktari walionekana kuwa wachache
Siku hiyo napo akashinda hukohuko, baada ya kumaliza kila kitu, wakarudi Kigoma Mjini ambapo wakachukua ndege na kuanza safari ya kwenda Dar es Salaa, sehemu ambayo alizaliwa Latifa, sehemu kulipokuwa na watu wengi aliokuwa akiwachukia.
ITAENDELEA