Notification texts go here Contact Us Buy Now!

SIMULIZI - ULIKUWA WAPI SEHEMU YA 04

ULIKUWA WP EP 04


Niliifahamu historia ya kaka Bahati baada ya kuishi naye miezi kadhaa, kwani hakuwa anazungumzia kila kitu mara moja. Yeye alizaliwa kama mtoto wa mwisho kati ya watoto watano kwa baba na mama yake. Waliishi maisha mazuri mno, ya kifahari, baada ya baba yake kuanza kufanya biashara za madini zikakubali. Baba yake hakusoma, wala mama yake, lakini alianza kama kutafuta vibarua kwenye migodi, akawa akipata pesa ndogo sana ya kujikimu.

“Nikiwa mdogo sana, maisha yalikuwa ya shida mno, kiasi cha watoto kukosa chakula. Lakini baba alikuwa mpiganaji asiyechoka. Alikuja kufanikiwa kupata kama mchongo katika madini, ukampatia pesa nyingi mno, akafungua duka lake la kuuza vito vya thamani. Kwahiyo ni kati ya maduka ya sonara ya mwanzo kabisa, kabla biashara haijaenea sana. Biashara ile ilibadili maisha yetu ghafla sana, tukaanza kuishi kifahari, kwenda mpaka nchi za nje miaka hiyo na kusafiri safari za ndani kila mara. Baba yangu hakuwa mchoyo, alisaidia watu wengi sana. Kuna watoto wa ndugu zangu wengi baba aliwasomesha.

Sitasahau siku ambayo tulipata ajali kama familia, miaka ya themanini. Wewe haukuwa umezaliwa wakati huo, lakini ni ajali iliyotangazwa kwenye vyombo vya habari nchini kuwa familia ya tajiri mkubwa yapata ajali maeneo ya mikumi na kuua karibu wanafamilia wote. Mimi, na kaka yangu wa kwanza ndio tulinusurika, lakini kaka aliumia vibaya na mpaka sasa ni mlemavu wa miguu yote. Baba, mama na ndugu zangu wengine wote walifariki, ambao hao ndugu zangu wote walikuwa wa kike.

Katika familia, unajua kuna ndugu unakuwa karibu nao kuliko wengine. Sasa mimi, dada zangu nilikuwa karibu nao sana kuliko huyo kaka yangu. Kaka alikuwa mkali kidogo kwangu, tofauti na dada zangu ambao walinidekeza na kunitetea mara zote. Kusema kweli, katika akili yangu ya utoto, kipindi cha msiba, nilitamani kama walau dada mmoja angebaki, wabadilishane na kaka yangu. Sikuwa mdogo kiasi cha kutoelewa kinachoendelea wakati wa msiba, nilijua kabisa nimepoteza wazazi, na familia yote, nikajua maisha yatabadilika, lakini sikutegemea yangebadilika kiasi kile. Huwezi amini, hata matibabu ya kaka ilifika mahala yakawa shida utadhani sio mtoto wa tajiri mkubwa. Ama kweli, aliyekufa hana thamani tena,” Aliongea kaka Bahati, nikaona kama machozi yakimlenga. Kwa siku hiyo akaishia hapo, hakuendelea tena kuzungumzia mambo ya familia yake.

Maisha niliyoishi na baba mdogo pamoja na maisha ya mtaani yalinifanya niwe muoga na mtu nisiyezoea watu kwa upesi. Lakini tulipoishi na kaka Bahati, taratibu nilianza kubadilika. Alituchukua kutupeleka chakula cha jioni, au kuogelea, alitutambulisha kwa marafiki zake ambao wengine walimcheka na kumwambia kwamba anakoelekea ataanzisha kituo cha kulelea yatima. Lakini nikabaki na maswali mawili kichwani ambayo bado sikuwa na ujasiri kumuuliza, hasa swali kuhusu kuoa. Nilijiuliza, kwanini kaka Bahati hana mke, na pili kwanini hatujawahi kuwaona ndugu zake. Ila pia nikakumbuka kwenye historia yake alisema ilifika mahala hadi matibabu ya kaka yake yalikuwa shida, kana kwamba hakuwa mtoto wa tajiri. Akilini nikahisi pengine ndugu walichukua mali zote na kuwaacha bila kuwajali.
Ni kweli kabisa, siku nyingine Bahati alipoanza kunieleza kuhusu historia ya maisha yake, niligundua ndugu wengi wana roho mbaya kama baba zangu wadogo.

“Tukiwa kwenye msiba, kaka hakuweza kuja kuzika kwani hali yake ilikuwa mbaya sana hospitali. Walijitokeza ndugu ambao hata mimi sijawahi kuwaona au wengine wa mbali kabisa kijijini, na kuanza kuzungumzia habari ya mali. Kila kitu kwangu niliona ni kigeni mno, hivyo sikuwa na cha kusema wala cha kufanya. Cha ajabu watu walionekana kugombania mali mpaka kubishana ila ilipokuja kwenye suala la sisi nani atatulea, walianza kupigiana danadana. Mwisho iliamriwa kuwa tutaishi kwa baba yetu mkubwa aliyeishi Manyara, kabla haujawa mkoa, tena kijijini. Nakumbuka kuna mtoto wake ambaye baba alikuwa akimsomesha shule moja ya bweni, Arusha, na kijana huyo aliendelea kusoma mpaka akamaliza kidato cha nne, akafeli na kushindwa kuendelea. Lakini kwangu mimi ilikuwa mwisho wa masomo yangu.

Niliandikishwa shule huko kijijini ila hata nguo za shule, au viatu sikununuliwa zaidi ya nilivyokuwa navyo. Kaka yangu alipopata nafuu naye aliletwa kule Manyara, lakini alitakiwa kuendelea na matibabu kwa muda. Mara kwa mara vikao vya ndugu vilikaliwa, na kilichozungumziwa ni mali tu na sio malezi, elimu wala afya ya kaka yangu. Kuna siku kaka mwenyewe alijaribu kuuliza kwenye kikao kuhusu afya yake, wakamjibu kwa aibu kwamba kuna pesa zinafuatiliwa, zikipatikana ataenda kutibiwa. Waliishia kumpeleka vituo vya afya vidogo tu pale Manyara kwa muda wa miezi kadhaa kisha wakamtelekeza. Nimemuhudumia kaka mpaka amekuwa mtu mzima wa kuweza kujitegemea. Nashukuru badae kabisa aliweza kuishi kwa kujitegemea, ingawa akiwa na ulemavu wa miguu. Kwa sasa ameoa, ana mtoto mmoja, na huyo ndiye ninamsomesha shule ya wasichana ya Marian.”

itaendelea..

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

إرسال تعليق

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.