ULIKUWA WAP EP 08
Mshahara wangu wa kwanza haukuwa mwingi lakini kwa kipindi hicho, na kwa maisha niliyoishi, niliuona ni mwingi sana. Nilitoa pesa ya nauli tu na kula milo miwili kwa siku, iliyobaki nikampelekea mzee Magessa kuanza kupunguza deni. Siku hiyo sitaisahau kwa mshangao nilioupata, nilipompa baba Magessa ile pesa. Aliishika bahasha yangu ya pesa baada ya kumpa, akanishikisha mkononi mwangu, tukiwa tumekaa kwa kutazamana ofisini kwake, kisha akaniambia, “Sihitaji unilipe, ila nenda kawafanyie vivyo hivyo wengine wenye mahitaji.”
Nilibaki nimemshangaa kama dakika nzima, nisijue nini cha kumjibu. Sikuamini kwamba kweli anamaanisha nisimlipe hata senti moja. Sikuwahi kufikiri kwamba wema wote ule alionifanyia, alimaanisha kunisaidia tu, bila malipo kabisa. Nilitamani nimbembeleze akubali nimlipe ili nitue mzigo niliokuwa nao, lakini neno alilosema niliona alimaanisha malipo makubwa zaidi ya ambayo ningemlipa. Sikutaka kumpa ahadi yoyote ya kutimiza alichoniambia, lakini machozi yalinitoka huku nikimwambia neno moja tu, ‘Nitafanya hivyo’ halafu nikapokea ile pesa na kuirudisha mfukoni.”
Baada ya hiyo habari ya mzee Magessa ambayo binafsi niliona kama hadithi ya malaika wake, aliendelea kutueleza kwanini tunatakiwa kusamehe kwa kutuelezea maisha yake baada ya hiyo kazi yake ya kwanza. “Nilifanya kazi yangu ya kwanza kwa bidii sana kwani ndiyo ilinitoa kwenye kuombaomba. Lakini kilichonifanya nitie bidii zaidi, ukiacha baba, mzee Magessa, ni uchungu na maumivu niliyosababishiwa na ndugu zangu. Mzee Magessa alipokataa mshahara wangu, nilihifadhi zile pesa, nikasubiri baada ya miezi mitatu huku nikiendelea kuhifadhi pesa kiasi cha kutosha kana kwamba nina deni la kulipa. Nilipopata nafasi ya kuchukua likizo fupi ofisini, nilisafiri kurudi kijijini nilipotoroka, kwa lengo la kwenda kumuona kaka yangu na kumsaidia. Wakati natoroka Manyara nilimuaga kaka, najua alikuja kuwambia na wengine lakini haingedhuru nikiwa tayari nimetoroka.
Namshukuru Mungu, nilimkuta kaka yangu salama na maendeleo yake yalinitia moyo sana. Alianza kufanya shughuli ndogo ndogo za kumpatia kipato, akawa akiendelea na maisha japo ya kimasikini.
Kaka alifurahi mno kuniona, na kuona kuwa maisha yangu yameendelea kulinganisha na wakati tunatengana. Nilianza kufanya mpango wa kumuhamisha pale nyumbani kwani licha ya kuwa alifanya shughuli zake binafsi, lakini alilazimishwa kutumia pesa zake zote kwa matumizi ya nyumbani. Pia siku zote walimfanya kama mtoto mdogo, tena mwenye tatizo, na sio kama mtu mzima. Walimuamulia kila kitu, walimgombeza na kumsimanga na hata watoto wa baba mkubwa aliowazidi sana, yaani umri wangu au wadogo kwangu, nao walimdharau.
Nilifanikiwa kumuhamishia kaka Dar es Salaam, tukaanza kuishi pamoja kwenye chumba nilichopanga. Kipindi chote hicho nilikusudia kulipa kisasi kwa kila aliyenifanyia ubaya, kwa kadiri nitakavyoweza. Ndugu zangu baada ya kuona nainuka walianza kunitafuta. Unajua mali za wizi tena wa urithi huwa hazidumu hata kidogo. Karibu ndugu wote walikuwa sio wenye pesa tena, yaani utadhani baba hakuacha kitu. Jinsi walivyonitafuta ndivyo nilivyozidi kuwachukia. Niliwatukana, nikawajibu hovyo, niliwadharau sana, na hakuna niliyeongea naye kwa adabu. Nilianza kufurahia kila baya lililotokea kwenye maisha yao, na naweza kusema Mungu sio Athumani, yaliwapata mabaya haswaa. Baba mkubwa niliyeishi naye alipata ugonjwa wa kupooza, alifiwa na watoto wake wawili, alikimbiwa na mke wake, yaani tafrani. Wengine hivi ninavyoongea vijana wao wameishia kuwa wavuta bangi, watumia madawa ya kulevya, wengine wamefariki yaani kama wanatembelea laana. Lakini cha ajabu nafsi yangu haikuwa ikiridhika na kila baya lililotokea, ingawa nilifurahia moyoni.
Nakumbuka kuna siku, nikiwa na miaka nane ofisini, nimeshapanda cheo na kuwa na nafasi nzuri zaidi, alikuja jamaa mmoja kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya mafunzo ya uongozi kwa wafanyakazi. Nilihudhiria ile semina ya wiki moja, iliyofanyika hoteli moja hapa Dar. Kitu kilichonisaidia sana kwenye yale mafunzo ni kile alichosema katika mada ya KUJITAMBUA. Yule bwana alizungumza kuhusu nguvu ya msamaha, na namna kutosamehe kunavyoweza kuharibu hata utendaji wako wa kazi. Katika vitu alivyosema ni kuwa, tunapobeba uchungu na visasi tunayaathiri maisha yetu wenyewe, tunachelewesha maendeleo yetu wenyewe, tunawaumiza wapendwa wetu na kujiumiza sisi wenyewe.
Huyu mtu alinifungua kugundua kuwa naishi maisha yasiyo na furaha wala utoshelevu, kwani kila nilipojaribu kupiga hatua, moyoni mwangu nilibeba watu. Kaka yangu Martin alikuwa amejitahidi kunifanya nisamehe, kwani alijua kisasi kinanitesa, lakini alishindwa. Nilifanya kazi kwa bidii lakini sikuwa na maendeleo makubwa. Nilifanya vitu vya kunifurahisha lakini sikuwa na furaha. Sikuwa na namna bora zaidi ya kulipa kisasi zaidi ya kutamani mabaya yawapate, lakini hata yalipowapata, sikuridhika. Niligundua jinsi ambavyo hata mahusiano yamenishinda kwa ajili ya kisasi. Mpaka nakuja kupata hii semina, nilishaisi miaka mingi mno ya uchungu.
(Kaka Martin wakati huo alikuwa ameshajitegemea na kuoa, lakini alihamia mkoani Morogoro).
Niliamua kuanzia wakati huo kujifunza kusamehe, na kwa kiasi kikubwa sana nimefanikiwa, ingawa imenilazimu kuishi bila kuingia kwenye mahusiano kwa kipindi kirefu ili nihakikishe naweza tena kuishi na mwanamke bila kumuumiza.”
Siku hiyo nadhani kaka Bahati alisahau kwamba sisi ni wadogo zake wadogo ambao bado hatuelewi mambo mengi ya maisha bado. Aliongea na sisi kama watu wazima, lakini licha ya umri wetu hasa wa Zita ambaye alikuwa bado mdogo kabisa, mambo aliyotueleza yalitusaidia sote kusamehe. Nadhani alimaanisha kututaka kuachilia mambo maovu tuliyofanyiwa, huku tukiamini Mungu ndiye hulipa kisasi. Nililia siku hiyo, huku nikiiambia nafsi yangu kusamehe na kuachilia. Unajua kama hujawahi kujaribu kumsamehe mtu aliyekukosea sana, huwezi ukaelewa nini ninamaanisha. Nilihitaji kutoa uchungu na machozi, kuwaachilia wale niliowabeba moyoni, hasa baba mdogo Naise. Sikutaka niishi maisha yangu yaliyobaki kwa mateso kwa ajili ya kutosamehe.
Tuliishi na kaka Bahati kwa miaka miwili bila shida yoyote, maisha yenye raha na utoshelevu, huku kipindi cha likizo, yule binti aliyemsomesha akija kusalimia na baadae kwenda kwa wazazi wake Morogoro. Kaka Bahati aliajiriwa kwa miaka kama kumi na kidogo, kisha akaanza kujiajiri, akafungua duka kubwa la kompyuta, akawa akiingiza kompyuta kutoka nje. Hiyo biashara ilimpatia pesa sana, kwani pia alikuwa akitoa huduma za kiteknolojia za kompyuta. Ndani ya miaka hiyo miwili tuliyoishi naye, kaka Bahati alipata mchumba, akatutambulisha kwake, akawa akija pale nyumbani mara kwa mara.
Baadaye alitushauri atutafutie shule ya bweni kwani kwa sasa tuna uwezo wa kuendelea na masomo kama watoto wengine. Wazo hilo kwangu halikuwa baya, kwani niliamini anafanya hivyo kwa nia njema ya kutusaidia kimasomo, lakini niliogopa sana maisha mapya ambayo tungeyaanza shuleni. Kaka Bahati alinitoa wasiwasi kwamba wanafunzi ni watu wema, na walimu pia hivyo hatutapata shida tukiwa shuleni. Tulianza kusoma shule moja mkoani Moshi, ya wasichana, ambayo ilikuwa nzuri tu na hatukupata shida kama nilivyohofia mwanzo.
ITAENDELEA.