Notification texts go here Contact Us Buy Now!

SIMULIZI-ULIKUWA WAPI SEHEMU YA 07

ULIKUWA WAPI EP 07


Lakini pia kisasi kilinifanya nisiwe mtu wa marafiki wala wa kusaidia watu. Baba alikuwa na marafiki wengi sana akiwa hai, na alisaidia watu wengi. Kuna rafiki zake baba waliokuwa karibu na sisi kiasi kwamba ungetegemea wangejitolea hata kutulea baada ya wazazi kufariki, lakini niliishia kuwaona msibani. Kuna mmoja, baada ya kuhangaika sana na maisha na kutoroka kijijini, niliwahi kumtafuta na kwenda ofisini kwake, lakini alijifanya hanijui kabisa, na hata baada ya kujitambulisha, alijifanya ana mambo mengi sana na hivyo nimtafute siku nyingine. Nilimtafuta zaidi ya mara tano lakini mara zote alidai hana muda hivyo nije siku nyingine, mpaka nikakata tamaa.
Lakini nakumbuka nikiwa na miaka 20, maisha yamenipiga sana wakati huo, nimetoroka na kumuacha kaka yangu, ingawa alishaweza kujitegemea kwa kiasi kikubwa, nikiwa nimehangaika Dar es Salaam kwa miaka miwili bila msaada wala tumaini lolote, kuna siku nilikutana na mtu akabadili mtazamo wa maisha yangu kwa kiasi, hasa katika suala la kusaidia watu. Kipindi hicho niliamua nitaanza kutafuta mitaji kwa watu nisiowajua, mtu yeyote tu. Nikaona njia rahisi ni kuanza kwenda kanisani. Nilihudhuria kanisa moja kubwa, nikawa kila nikitoka kanisani, nawafuata wanaume au wanawake wanaoonekana na uwezo kifedha kuwaomba msaada. Wakati huo wote, kulala na kula kwangu ilikuwa mtaani. Nilikula kila kitu, bila kujali ni kisafi au kichafu, maadamu ni chakula tu. Sikuangalia mazingira gani nakula au nalala. Maisha kwangu hayakuwa na thamani yoyote zaidi ya kula na kulala. Siku za Jumapili, nilijitahidi kuwa na nguo ambayo naweza kuingia nayo kwenye mikusanyiko ya watu, wasinifukuze, ingawa wengi hawakupenda kukaa karibu na mimi kanisani.

Kila baada ya ibada nilihakikisha nimeongea na watu wawili au watatu, lakini hakuna aliyekuwa na msaada. Wengi wao walinipa jibu moja tu, “Sina hela”. Nilifanya hivyo kwa zaidi ya miezi sita mfululizo, bila kupata msaada wowote kabisa ingawa kanisa lilikuwa kubwa. Nilikariri watu wote wenyeji wa kanisa lile, kwani ilifika mahala nikawa siangalii sana muonekano wa nje, najaribu bahati tu. Siku moja nakumbuka alikuja mgeni kanisani hapo, mwanaume mmoja na familia yake. Wale watu walijitambulisha kuwa wametokea mkoa fulani hapa Tanzania na wamekuja kikazi kwa muda hivyo watakuwa wakisali hapo. Niliogopa kumfuata yule mtu siku ya kwanza baada ya kutoka ibadani, kwani angehisi ni tabia ya watu wa kanisa hilo.

Nilimuacha kama wiki mbili zikapita, nikamfuata wiki ya tatu. Nilimsalimia na tofauti na watu wengi walioonesha kutojali kabisa, yeye alinijibu kama anajibu mtu mwenye thamani kwake. Aliniuliza habari yangu, akaniuliza kama bado nasoma au la. Wakati huo, familia yake ilikuwa ikimsubiri kwenye gari tayari. Nilipomwambia sisomi, aliuliza kwanini au kama nilishamaliza shule. Nilimjibu kwa kujieleza kidogo kuwa sikubahatika kuendelea na shule kutokana na wazazi wangu kufariki nikiwa mdogo.

Yule mwanaume alionekana kuguswa sana na maelezo mafupi niliyompa, kiasi cha yeye mwenyewe kuniomba nimtafute ofisini kwake. Nilifanya hivyo haraka sana na kuonana naye, siku tuliyopanga. Alinikaribisha kwenye ofisi kubwa kama ofisi ya mkurugenzi wa kampuni kubwa sana au kiongozi mkubwa wa serikali. Siku hiyo nilijihisi, kwa mara ya kwanza, kwamba na mimi ni binadamu ninayeweza kuzungumza na watu na kusikilizwa. Mwanaume yule, bwana Magessa, alinisikiliza kwa muda wa karibu saa nzima nikimueleza historia ya maisha yangu huku akinidodosa kwa maswali kadhaa kama mtu anayeonesha umakini kusikiliza ninachomwambia. Baadaye aliniuliza kama nna mpango wowote wa maisha. Tangu nimeamua kuwafata watu, nilikuwa na mpango wa biashara fulani ndogo kichwani mwangu, ili mtu akiuliza anisaidieje, nisimuombe hela ya kula bali mtaji wa biashara. Nilimuelezea biashara yangu, lakini yeye alinishauri kwamba kwa biashara ndogo na inayoanza, na kwa mtu asiye na uzoefu kama mimi, ingenipa shida sana kusimama au ingesimama na baadae ikafa. Alinieleza kuwa bishara inahitaji uzoefu, mtu wa kunishika mkono na jitihada sana, ukiachilia mbali mtaji ambao sitaula.
Baada ya maongezi yetu ya muda na ushauri, bwana Magessa ambaye kwa sasa namuita baba, alinishauri nitafute chuo cha masomo ya uzoefu maalumu kama kompyuta, hoteli, uhazili au kitu chochote, kisha nikimaliza kusoma atanisaidia kutafuta kazi. Kwa wakati huo, ilihitaji kujua kusoma na kuandika tu, na labda kujifunza kiingereza kabla ya kuanza. Aliniahidi kunipatia pesa za matumizi kwa muda wote wa masomo yangu, mpaka nitakapoweza kupata kazi. Lakini aliongeza kusema kuwa atanisaidia, kwa kadiri nitakavyohitaji msaada, ila nikimaliza masomo, nikapata kazi na kuweza kupata kipato kinachonikidhi, basi nitamrudishia pesa yake taratibu.

Siku zote nilienda kanisani, na wakati mwingine nilisikia mchungaji akihubiri kuwa Mungu anatupenda, lakini hilo jambo halikuwahi kuingia akilini mwangu, mpaka siku baba mzee Magessa aliponipa hii habari. Nilikuwa nikijiuliza sana, huyu Mungu wanayedai anatupenda, ni kweli yupo? Na kama yupo, anatupenda sote au ana ubaguzi kwa baadhi ya watu? Kama habagui, maisha yote niliyowahi kupitia na ninayopitia, hayaoni? Au labda hana uwezo wa kunisaidia? Kwangu mafundisho kuhusu upendo wa Mungu, uwezo wake, nguvu au chochote kuhusu Mungu niliona ni uongo na unafiki tu kwani haikuniingia akilini kwanini huyo Mungu wanayemzungumzia ashindwe kunisaidia mimi katika shida zote nilizokuwa nikipitia.

Nililia sana, nilipopewa zile ahadi, huku nikidhani niko ndotoni. Katika maisha yangu yote, hakukuwa na mtu mwema nimewahi kukutana naye kama mzee Magessa. Kama angejitambulisha kama Mungu, hakika ningeamini bila shaka, lakini huku nikiendelea kumshukuru, alianza kuniambia, nimshukuru tu Mungu kwa kuwa ananipenda. Akili yangu hapo ilianza kukubali kuwa itakuwa kweli Mungu ananipenda.

Nilitafuta chuo kimoja, nikasikiliza masharti yao, yaliyonitaka kujiunga na kozi ya kiingereza kwa miezi mitatu kabla ya kuanza masomo. Nilisoma kingereza, halafu nikaanza masomo ya kompyuta na utengenezaji wa kompyuta. Nilisoma kwa mwaka na nusu, yaani miezi 18, huku nikipata msaada wa kila kitu toka kwa mzee Magessa. Alihakikisha sipungukiwi chakula, nauli wala ada ya masomo. Alinipangishia na chumba pia hivyo ikawa mwisho wangu wa kulala mtaani. Nilichokifanya ni kuwa naandika kila pesa aliyonigharimia, ili nitakapofanikiwa, nianze kurejesha. Hakuwahi kukumbushia suala la kulipa, hakuwahi kuonesha kuwa ni mzigo kwake kunihudumia, na wala sikuhitaji kumuomba pesa ya matumizi. Alinipa kiwango kadhaa kwa ajili ya matumizi kila mwezi, akipiga hesabu ya usafiri, na chakula. Alilipa kodi ya chumba changu ya mwaka mzima na ilipoisha alinipa nyingine bila kumuomba. Alilipa ada yote mihula yote, akanisisitiza kumueleza endapo kutatakiwa kulipia gharama nyingine yoyote.

Nilisoma kwa jitihada nyingi mno, huku nikijiona mtu mwenye deni kubwa juu ya mzee Magessa. Kurudi shule ilikuwa ni changamoto kiasi, lakini nilihakikisha nafanya vizuri sana. Nilimaliza masomo yangu na kama alivyoniahidi, alinisaidia kutafuta kazi mahala fulani kama mtaalamu wa ufundi wa kompyuta (computer technician). Unajua miaka hiyo hakukuwa na wataalamu wengi, hivyo hiyo kazi ilinipatia kipato na kunipa heshima kwa watu. Nilianza kupokea mshahara, wangu binafsi, pesa ambayo sikuwahi kukaa na kuota kwamba namimi nitafanya kazi na kulipwa mshahara. Miaka mingi ya utumwa na mateso ilinifanya nijione katika maisha sistahili hata kumfanyia mtu kazi akanilipa mshahara. Niliwahi kuwa nafanya vibarua na kupewa pesa kidogo za kujikimu, lakini wakati mwingine nilifukuzwa kwenye vibarua bila hata sababu za kueleweka, au wenzangu walianza kunifanyia vituko na kuniambia sitakiwi kwenye kazi zao, na mambo mengi ya namna hiyo. Kiufupi nimeishi maisha ya kukataliwa, na ndugu, marafiki hata watu wasionijua, tangu wazazi wangu wafariki, na mzee Magessa ndio alikuwa mtu wa kwanza kunikubali na kunionesha thamani yangu.”-

ITAENDELEA

About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.