Ulikua wapi 06
“Tukiwa kwenye msiba, kaka hakuweza kuja kuzika kwani hali yake ilikuwa mbaya sana hospitali. Walijitokeza ndugu ambao hata mimi sijawahi kuwaona au wengine wa mbali kabisa kijijini, na kuanza kuzungumzia habari ya mali. Kila kitu kwangu niliona ni kigeni mno, hivyo sikuwa na cha kusema wala cha kufanya. Cha ajabu watu walionekana kugombania mali mpaka kubishana ila ilipokuja kwenye suala la sisi nani atatulea, walianza kupigiana danadana. Mwisho iliamriwa kuwa tutaishi kwa baba yetu mkubwa aliyeishi Manyara, kabla haujawa mkoa, tena kijijini. Nakumbuka kuna mtoto wake ambaye baba alikuwa akimsomesha shule moja ya bweni, Arusha, na kijana huyo aliendelea kusoma mpaka akamaliza kidato cha nne, akafeli na kushindwa kuendelea. Lakini kwangu mimi ilikuwa mwisho wa masomo yangu.
Niliandikishwa shule huko kijijini ila hata nguo za shule, au viatu sikununuliwa zaidi ya nilivyokuwa navyo. Kaka yangu alipopata nafuu naye aliletwa kule Manyara, lakini alitakiwa kuendelea na matibabu kwa muda. Mara kwa mara vikao vya ndugu vilikaliwa, na kilichozungumziwa ni mali tu na sio malezi, elimu wala afya ya kaka yangu. Kuna siku kaka mwenyewe alijaribu kuuliza kwenye kikao kuhusu afya yake, wakamjibu kwa aibu kwamba kuna pesa zinafuatiliwa, zikipatikana ataenda kutibiwa. Waliishia kumpeleka vituo vya afya vidogo tu pale Manyara kwa muda wa miezi kadhaa kisha wakamtelekeza. Nimemuhudumia kaka mpaka amekuwa mtu mzima wa kuweza kujitegemea. Nashukuru badae kabisa aliweza kuishi kwa kujitegemea, ingawa akiwa na ulemavu wa miguu. Kwa sasa ameoa, ana mtoto mmoja, na huyo ndiye ninamsomesha shule ya wasichana ya Marian.”
Kila nilipomsikiliza kaka Bahati akiongea, hasira zilinishika, nikazidi kuwachukia ndugu wanaoachiwa watoto na marehemu. Nilikumbuka jinsi baba mdogo alivyoonekana kutupenda baba akiwa hai, na namna alivyotubadilikia baada ya msiba. Nafsini mwangu nilitamani nilipe kisasi, si kwa ajili yangu tu, bali kwa ajili ya yatima wote wanaoteswa na ndugu wa wazazi wao. Kaka Bahati amekuwa akinielezea kuhusu maisha yake kwa vipengele, mara nyingi baada ya kula usiku. Zita hulala mapema kidogo, ila mimi napenda kukaa sebuleni baada ya chakula. Licha ya kuzungumzia maisha na historia za nyuma, najifunza mambo mengi sana kwa kuongea na kaka Bahati.
Kwake nimejifunza kupambana na maisha, kuwa mvumilivu, kuthamini watu, kutia bidii katika ,mambo yote na zaidi kusamehe. Nilivyoendelea kuishi naye niligundua kuwa natakiwa kusamehe wote waliowahi kuniumiza katika maisha yangu. Liliokuwa gumu zaidi ni kumsamehe bamdogo Naise, kwani kitendo alichofanya sio tu kiliniumiza, bali pia kiliacha alama mbaya kwenye maisha yangu. Nilimuhadithia kaka Bahati vitu vingi, lakini sikumwambia kuhusu kubakwa kwangu, kwani niliona aibu, mpaka siku moja yeye aliponiambia alifanyiwa jambo baya zaidi ya mimi kubakwa.
“Tukiendelea kuishi kijijini, baba mkubwa alianza kuwa na maisha bora zaidi, nikajua ni mali za wazazi wangu. Kwa mtu wa kijijini, tena miaka hiyo, kununua gari, haikuwa jambo dogo kabisa. Alinunua gari, alianza kulimisha mashamba yake kwa kukodisha vijana wengi ambao baada ya kulima walikuja kula nyumbani. Aliajiri watu wa kupika na ni kama kila siku ilikuwa sherehe. Watoto wa bamkubwa wote walisoma bila shida, na kupatiwa mahitaji yote, isipokuwa mimi na kaka ambao hatukuonekana kama watoto wanaohitaji kuhudumiwa. Mahitaji yetu yote yalipuunzwa, kuanzia elimu mpaka mavazi. Muda ulivyoendelea ndipo tulizidi kuonekana kama watu waliovamia familia za watu, na hivyo tuliishi kama watumwa kabisa.
Niliachishwa shule na kuanza kuchunga mifugo ya bamkubwa huku nikiendelea kumuhudumia kaka yangu, aliyekuwa hawezi hata kunyanyuka bila msaada wa mtu. Kaka yangu ameishi kwa shida mno, kiasi kwamba kuna wakati alitamani ajiue, akidai kuwa ananitesa na yeye akiteseka. Kwangu uwepo wake ulikuwa ni faraja kubwa mno, na hata siku moja sikuwahi kuona ni mateso kumuhudumia.
Siku moja, nilienda kuchunga alfajiri sana kama nilivyozoeshwa. Kuna wakati nilikuwa na vijana wenzangu wakichunga mifugo yao, lakini mara nyingi walianza kuchunga jua limeshachomoza. Mwamzoni niliogopa sana, kwani mazingira ya kule yalinitisha, lakini baadaye nilizoea. Siku hiyo, nikitembea maeneo ambayo hayakuwa mbali sana na nyumbani, nasubiria kuwe na mwanga kidogo ndipo niende mbali, alitokea mwanaume mmoja, tena niliyemfahamu kama rafiki wa baba mkubwa, akaanza kuniuliza maswali kadhaa. Mwanaume huyu alionekana amelala kwenye pombe, kwani kule kijijini hiyo tabia haikuwa ya ajabu. Aliniuliza maswali kadha wa kadha, yasiyo na mbele wala nyuma, kisha akanishika mkono na kuanza kunivutia porini. Nilipiga kelele nyingi sana, nikiamini nitasikiwa. Kaka yangu anasema alisikia hizo kelele, akahisi ni mimi, lakini hakuwa na cha kufanya zaidi ya kupata hofu tu na kusubiri taarifa. Yeye alihisi pengine nimeliwa na mnyama mkali. Yule mwanaume alinichukua na kuanza kuniingia kinyume na maumbile huku akidai ananifundisha maisha. Nililia mno, nikapiga kelele, akiniziba mdomo na kuendelea na kile kitendo, halafu akaniacha hapo na kuondoka.”
Kaka Bahati amepitia visa vingi sana katika maisha, kiasi cha kwamba karibu kila mara tukiongea, alisema kisa kipya. Umri wake haukuwa mkubwa sana wakati nakutana naye, lakini historia ya maisha yake ni kama ya mtu wa miaka hamsini. Lakini tofauti na ambavyo maisha yamemtenda, yeye ni mtu mpole na mwenye upendo mwingi sana. Hana chuki na mtu, anahurumia watu wa kila aina, na hana kinyongo kwa waliomkosea. Alinifundisha kuwa, unaposhindwa kusamehe aliyekukosea, kinachofanyika si kumuadhibu mkosaji, bali kujiadhibu mwenyewe.
Siku moja tukiwa matembezi ya mwisho wa wiki, mimi, yeye na Zita, kuna maneno alisema nasi, yakanifanya nianze kujilazimisha kusamehe wote walioniumiza. “Nimeishi maisha ya chuki kwa muda mrefu, nikitamani na kusubiri kulipa kisasi kwa wote walioniumiza. Unajua ukiwa umebeba kisasi moyoni, hauishi maisha yako. Yaani kila kazi, shughuli au chochote nilichokuwa nikifanya, kilikuwa kwa ajili ya wale walionikosea. Nilifanya kazi kwa bidii, nikitaraji kupata pesa ili niwakomeshe. Nilitamani kutengeneza jina kubwa, nilitamani hata ningeweza kusomea sheria, kuingia kwenye siasa au kuwa mtu yeyote mkubwa na mwenye mamlaka duniani, lakini si kwa ajili yangu mwenyewe, wala kwa faida yangu, bali ili niwe katika nafasi ya kuwahukumu na kuwalaani walionitesa.”Alizungumza kaka Bahati, halafu akaendelea.
“Mara nyingi ukiwa mtu mwenye kisasi ndani yako, unaweza ukawa mtu unayewafanyia watu ubaya sana, lakini unajihesabia haki daima. Kuna wakati, nilipoanza kuingia kwenye mahusiano, niligundua kuwa nagombana sana na wanawake. Kwanza sikuwa najali kuwa mwaminifu, pia niliwafanya kama watu wasio na thamani huku akili ikiniambia watu wote duniani, ukiacha wazazi na ndugu wa damu, hawana upendo wa dhati. Kwangu wanawake niliona kama watu wa kupita tu kiasi kwamba mtu angenifanyia kosa dogo sana, lingesababisha nimuache. Nimewatesa mabinti wengi bila huruma.
ITAENDE