ULIKUWA WAP EP 05
Kila nilipomsikiliza kaka Bahati akiongea, hasira zilinishika, nikazidi kuwachukia ndugu wanaoachiwa watoto na marehemu. Nilikumbuka jinsi baba mdogo alivyoonekana kutupenda baba akiwa hai, na namna alivyotubadilikia baada ya msiba. Nafsini mwangu nilitamani nilipe kisasi, si kwa ajili yangu tu, bali kwa ajili ya yatima wote wanaoteswa na ndugu wa wazazi wao. Kaka Bahati amekuwa akinielezea kuhusu maisha yake kwa vipengele, mara nyingi baada ya kula usiku. Zita hulala mapema kidogo, ila mimi napenda kukaa sebuleni baada ya chakula. Licha ya kuzungumzia maisha na historia za nyuma, najifunza mambo mengi sana kwa kuongea na kaka Bahati.
Kwake nimejifunza kupambana na maisha, kuwa mvumilivu, kuthamini watu, kutia bidii katika ,mambo yote na zaidi kusamehe. Nilivyoendelea kuishi naye niligundua kuwa natakiwa kusamehe wote waliowahi kuniumiza katika maisha yangu. Liliokuwa gumu zaidi ni kumsamehe bamdogo Naise, kwani kitendo alichofanya sio tu kiliniumiza, bali pia kiliacha alama mbaya kwenye maisha yangu. Nilimuhadithia kaka Bahati vitu vingi, lakini sikumwambia kuhusu kubakwa kwangu, kwani niliona aibu, mpaka siku moja yeye aliponiambia alifanyiwa jambo baya zaidi ya mimi kubakwa.
“Tukiendelea kuishi kijijini, baba mkubwa alianza kuwa na maisha bora zaidi, nikajua ni mali za wazazi wangu. Kwa mtu wa kijijini, tena miaka hiyo, kununua gari, haikuwa jambo dogo kabisa. Alinunua gari, alianza kulimisha mashamba yake kwa kukodisha vijana wengi ambao baada ya kulima walikuja kula nyumbani. Aliajiri watu wa kupika na ni kama kila siku ilikuwa sherehe. Watoto wa bamkubwa wote walisoma bila shida, na kupatiwa mahitaji yote, isipokuwa mimi na kaka ambao hatukuonekana kama watoto wanaohitaji kuhudumiwa. Mahitaji yetu yote yalipuunzwa, kuanzia elimu mpaka mavazi. Muda ulivyoendelea ndipo tulizidi kuonekana kama watu waliovamia familia za watu, na hivyo tuliishi kama watumwa kabisa.
Niliachishwa shule na kuanza kuchunga mifugo ya bamkubwa huku nikiendelea kumuhudumia kaka yangu, aliyekuwa hawezi hata kunyanyuka bila msaada wa mtu. Kaka yangu ameishi kwa shida mno, kiasi kwamba kuna wakati alitamani ajiue, akidai kuwa ananitesa na yeye akiteseka. Kwangu uwepo wake ulikuwa ni faraja kubwa mno, na hata siku moja sikuwahi kuona ni mateso kumuhudumia.
Siku moja, nilienda kuchunga alfajiri sana kama nilivyozoeshwa. Kuna wakati nilikuwa na vijana wenzangu wakichunga mifugo yao, lakini mara nyingi walianza kuchunga jua limeshachomoza. Mwamzoni niliogopa sana, kwani mazingira ya kule yalinitisha, lakini baadaye nilizoea. Siku hiyo, nikitembea maeneo ambayo hayakuwa mbali sana na nyumbani, nasubiria kuwe na mwanga kidogo ndipo niende mbali, alitokea mwanaume mmoja, tena niliyemfahamu kama rafiki wa baba mkubwa, akaanza kuniuliza maswali kadhaa. Mwanaume huyu alionekana amelala kwenye pombe, kwani kule kijijini hiyo tabia haikuwa ya ajabu. Aliniuliza maswali kadha wa kadha, yasiyo na mbele wala nyuma, kisha akanishika mkono na kuanza kunivutia porini. Nilipiga kelele nyingi sana, nikiamini nitasikiwa. Kaka yangu anasema alisikia hizo kelele, akahisi ni mimi, lakini hakuwa na cha kufanya zaidi ya kupata hofu tu na kusubiri taarifa. Yeye alihisi pengine nimeliwa na mnyama mkali. Yule mwanaume alinichukua na kuanza kuniingia kinyume na maumbile huku akidai ananifundisha maisha. Nililia mno, nikapiga kelele, akiniziba mdomo na kuendelea na kile kitendo, halafu akaniacha hapo na kuondoka.”
Kaka Bahati hakuwa na mke, wala mtoto. Kabla yangu na Zita, aliwahi kuchukua binti mwingine kulea, akawa akimsomesha shule ya bweni, hivyo hatukumkuta kwake. Alimtafutia shule Zita pia, changamoto ikawa kwangu kwani umri wangu ulikuwa mkubwa kidogo na niliishia darasa la tatu tu. Alinitafutia shule nzuri pia, akanitafutia na walimu wa tuisheni wanisaidie kunifundisha. Tulianza maisha mapya mimi na mdogo wangu, kwa kaka Bahati, ambaye alitupenda na kutujali kama watoto wake.
Niliifahamu historia ya kaka Bahati baada ya kuishi naye miezi kadhaa, kwani hakuwa anazungumzia kila kitu mara moja. Yeye alizaliwa kama mtoto wa mwisho kati ya watoto watano kwa baba na mama yake. Waliishi maisha mazuri mno, ya kifahari, baada ya baba yake kuanza kufanya biashara za madini zikakubali. Baba yake hakusoma, wala mama yake, lakini alianza kama kutafuta vibarua kwenye migodi, akawa akipata pesa ndogo sana ya kujikimu.
“Nikiwa mdogo sana, maisha yalikuwa ya shida mno, kiasi cha watoto kukosa chakula. Lakini baba alikuwa mpiganaji asiyechoka. Alikuja kufanikiwa kupata kama mchongo katika madini, ukampatia pesa nyingi mno, akafungua duka lake la kuuza vito vya thamani. Kwahiyo ni kati ya maduka ya sonara ya mwanzo kabisa, kabla biashara haijaenea sana. Biashara ile ilibadili maisha yetu ghafla sana, tukaanza kuishi kifahari, kwenda mpaka nchi za nje miaka hiyo na kusafiri safari za ndani kila mara. Baba yangu hakuwa mchoyo, alisaidia watu wengi sana. Kuna watoto wa ndugu zangu wengi baba aliwasomesha.
Sitasahau siku ambayo tulipata ajali kama familia, miaka ya themanini. Wewe haukuwa umezaliwa wakati huo, lakini ni ajali iliyotangazwa kwenye vyombo vya habari nchini kuwa familia ya tajiri mkubwa yapata ajali maeneo ya mikumi na kuua karibu wanafamilia wote. Mimi, na kaka yangu wa kwanza ndio tulinusurika, lakini kaka aliumia vibaya na mpaka sasa ni mlemavu wa miguu yote. Baba, mama na ndugu zangu wengine wote walifariki, ambao hao ndugu zangu wote walikuwa wa kike.
Katika familia, unajua kuna ndugu unakuwa karibu nao kuliko wengine. Sasa mimi, dada zangu nilikuwa karibu nao sana kuliko huyo kaka yangu. Kaka alikuwa mkali kidogo kwangu, tofauti na dada zangu ambao walinidekeza na kunitetea mara zote. Kusema kweli, katika akili yangu ya utoto, kipindi cha msiba, nilitamani kama walau dada mmoja angebaki, wabadilishane na kaka yangu. Sikuwa mdogo kiasi cha kutoelewa kinachoendelea wakati wa msiba, nilijua kabisa nimepoteza wazazi, na familia yote, nikajua maisha yatabadilika, lakini sikutegemea yangebadilika kiasi kile. Huwezi amini, hata matibabu ya kaka ilifika mahala yakawa shida utadhani sio mtoto wa tajiri mkubwa. Ama kweli, aliyekufa hana thamani tena,” Aliongea kaka Bahati, nikaona kama machozi yakimlenga. Kwa siku hiyo akaishia hapo, hakuendelea tena kuzungumzia mambo ya familia yake.
Maisha niliyoishi na baba mdogo pamoja na maisha ya mtaani yalinifanya niwe muoga na mtu nisiyezoea watu kwa upesi. Lakini tulipoishi na kaka Bahati, taratibu nilianza kubadilika. Alituchukua kutupeleka chakula cha jioni, au kuogelea, alitutambulisha kwa marafiki zake ambao wengine walimcheka na kumwambia kwamba anakoelekea ataanzisha kituo cha kulelea yatima. Lakini nikabaki na maswali mawili kichwani ambayo bado sikuwa na ujasiri kumuuliza, hasa swali kuhusu kuoa. Nilijiuliza, kwanini kaka Bahati hana mke, na pili kwanini hatujawahi kuwaona ndugu zake. Ila pia nikakumbuka kwenye historia yake alisema ilifika mahala hadi matibabu ya kaka yake yalikuwa shida, kana kwamba hakuwa mtoto wa tajiri. Akilini nikahisi pengine ndugu walichukua mali zote na kuwaacha bila kuwajali.
Ni kweli kabisa, siku nyingine Bahati alipoanza kunieleza kuhusu historia ya maisha yake, niligundua ndugu wengi wana roho mbaya kama baba zangu wadogo.
ITAENDELEA..