ULIKUWA WAP EP 03
Siku mbili baadaye, nilipata nafuu na kutoka hospitalini hapo, ingawa walishauri nikae zaidi lakini pesa niliyolipiwa ilikuwa imeisha na sikuwa tayari kuongeza. Niliondoka na kurudi kule baa, lakini Zita wangu sikumkuta. Wafanyakazi wenzangu walisema alienda kunitafuta alipoona sirudi. Kama sikuchanganyikiwa siku hiyo, sitachanganyikiwa tena. Nililia mno, nikawaza kujiua lakini nikajiuliza endapo Zita atarudi kunitafuta aambiwe nimekufa, atafanyaje. Niliwalaumu wafanyakazi wenzangu kwanini wamemruhusu aondoke, wakajitetea tu, lakini sikuona aliyeongea la maana. Niliondoka hapo kama kichaa, kuanza kuzunguka mtaani, nikimtafuta mdogo wangu, bila mafanikio. Niliacha maagizo kule baa kwamba ikitokea akarudi wasimruhusu aondoke mpaka nirudi. Nikawa kila ikifika jioni, narudi pale kuulizia, ingawa sikuruhusiwa tena kulala pale, isipokuwa kwa uficho.
Wiki mbili zilipita bila kumpata mdogo wangu, nikakonda sana kwa kushindwa kula na kuwa na mawazo. Huyu mtoto kwangu alikuwa ni zaidi ya mdogo, bali kama rafiki wa karibu zaidi, ndugu pekee na kama mtoto wangu wa kumzaa. Nilijihisi nawajibika mno kwa maisha yake. Nilijilaumu kumuacha hata kwa siku moja, lakini nilijipa moyo kuwa kama kuna Mungu duniani, basi sitampoteza mdogo wangu. Nilianza kusali, sala fupi kabisa, “Mungu kama upo, na kama unasikiliza wanadamu, naomba umlinde Zita huko aliko, na unisaidie kumpata.” Nilifanya hivyo kila siku zaidi ya mara tano. Nililia kila nilipomfikiria Zita, huku nikiwa na tumaini dogo sana kwamba kwa kuwa hajafa basi huenda nikampata.
Kuna wakati nilipata mawazo kwamba pengine atagongwa na gari au kupata chochote, lakini nilipingana sana na mawazo hayo mara zote. Uzoefu wangu wa misiba umenifundisha kuwa kufiwa hakuna mazoea. Siku aliyokufa baba, niliumia kana kwamba sina mtu mwingine yeyote duniani. Lakini siku aliyokufa mama, niliumia utadhani sijawahi kufiwa, ni mara ya kwanza. Siku aliyokufa bibi pia niliumia kama mtu aliyepoteza tumaini la maisha kabisa. Kufiwa na ndugu pekee aliyebaki kwenye maisha yangu, Zita, kungepoteza ladha na maana ya kuishi kabisa, na nadhani ningechukua uamuzi wa kujiua siku iyo hiyo.
Baada ya wiki mbili, nakumbuka siku moja nilienda pale baa nilipofanya kazi awali, wakasema hajarudi, nikawa nimekata tamaa kabisa kama atakuja. Nikaanza kuondoka, sijui la kufanya tena, nalia machozi yasiyokauka. Nikiwa njiani, likasimama gari moja, aina ya harrier nyeusi nzuri sana. Alipofungua kioo ambacho kilikuwa tinted, mwanaume mmoja wa miaka kama 35 au zaidi kidogo, aliniuliza habari, nikamjibu na kumuamkia. Akaniuliza nalia nini, sikumjibu bali nikazidi kulia. Yule kaka alishuka kwenye gari, akaanza kunibembeleza, akaniomba sana niende naye kwake, atanisaidia. Kusema kweli nilikuwa na hofu kubwa mno, kuondoka na mtu nisiyemjua, lakini kwa jinsi nilivyokuwa nimejikinai, nilikubali. Nilijisemea moyoni, “Siku zote nayatunza maisha yangu kwa kutokubali kila kitu, lakini hamna faida, kwani sasa hata ndugu yangu pekee nimeshampoteza.”
Nilipanda kwenye gari yake, iliyokuwa na video ndani, imewekwa video ya wimbo fulani ambao ulinikumbusha sana maisha ya nyuma. Wimbo huo uliimbwa na kundi moja la nchi ya Marekani nadhani, wa kingereza, uliitwa LOVE OF MY PAPA, OF MY MAMA, ikimaanisha upendo wa baba yangu, wa mama yangu. Huo wimbo ulirekodiwa kama muvi ya binti mdogo aliyeishi na wazazi wake vizuri sana, lakini wakafariki kwa ajali ya gari siku moja, kisha akaanza kuhangaika mtaani. Alionekana akiomba chakula mtaani, akinyeshewa mvua na kupigwa baridi. Nilishangaa mno kukuta wimbo wa maisha yangu. Nilikuwa nimenyamaza wakati naingia kwenye gari, lakini nikiangalia huo wimbo na video yake, nilianza kulia sana kama mtu aliyepigwa kiasi cha yule kaka kushindwa kuendesha gari. Alipaki pembeni haraka na kuanza kuniuliza nalia nini, nikamwambia kuna vitu nimekumbuka hivyo asinijali.
Tuliendelea na na safari ya mwendo mrefu kidogo, tukakutana na foleni baadhi ya maeneo, baadaye tukafika kwake. Yeye alijitambulisha kwa jina la Bahati, namimi nikamwambia jina langu, Zawadi. Mlinzi alifungua geti, nyumba kubwa na nzuri sana, maeneo ya Salasala jijini Dar es Salaam, tukaingia ndani. Mida hiyo ilikuwa kama saa mbili usiku. Alikuja dada wa kazi, akatusalimia. Kaka Bahati baada tu ya kumjibu akamuulizia, “Yuko wapi mtoto?” “Yuko ndani, ametoka kuoga” Yule dada alijibu. Nilisubiri aulize habari za mke wake, nilisubiri pia nione jinsi mke wake ambavyo angehamaki baada ya kuniona, kwani bado nilikumbuka kwa ufasaha kabisa tukio alilofanya yule mama aliyeniunguza miguu. Nikazidi kuwaza jinsi alivyonisababisha kumpoteza mdogo wangu, nikaanza tena kulia, huku nikijipanga kwa lolote litakalotokea siku hiyo. Yule kaka, Bahati, alinituliza kidogo, akanialika mezani nikale. Muda wote huo sikuwa nimemueleza chochote kuhusu mimi zaidi ya jina langu na wala hakuonesha kuwa na haraka. Tulikaa mezani, akamwambia dada aende kumuhimiza mtoto aje kula.
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka, mbele yangu kulikuwa na chakula ambacho sijawahi kula tangu baba yangu afariki, yaani kuku. Siku zote tukiwa kwa baba mdogo, siku ambazo walipika kuku au nyama, walikula wao tu huku kila kinachobaki kikipelekwa chumbani na kufungiwa kwenye friji yao. Wakati bibi yupo, angalau tulikula nyama mara chache, kwani bibi alipikiwa ndizi zenye nyama au utumbo kila siku, na walipompakulia, alilazimisha na sisi tupakuliwe chakula chake. Baada ya bibi kufariki, sikuwahi tena kula nyama. Nakumbuka kuna siku nilikuwa napika, nikatamani sana nyama walau moja nionje, lakini dada Selina alikuja na kunikuta nikiwa na nyama mdomoni, akanipiga kiasi cha kutothubutu tena siku nyingine. Siku tulizopika nyama au kuku, haikutokea hata siku moja tukaachwa nazo mimi na Zita, kana kwamba ni dawa, haifai kwa watoto. Chakula chetu kikubwa kilikuwa ugali, na maharage au mchicha, na mara chache sana wali. Nilizoea kuwa hayo ndiyo maisha na kwangu haikunisumbua hata kidogo. Kama hiyo ndiyo ingekuwa changamoto pekee, basi nisingewahi kuondoka kwa bamdogo Musa.
Ghafla, nikiwa napakua, alitokea binti mdogo, akasimama mezani tulipokuwa tumekaa kula. Nikasikia kaka Bahati akimhimiza akae ale, kwani alichukua kama dakika nzima amesimama, anashangaa. Nikamuangalia yule binti mdogo kwa makini sana kama mtu ambaye ninaota au nimeona mzimu. Sikuamini, akili haikukubali, nikasema hii ni ndoto nzuri tu naota lakini si kweli. Tukabaki tumeshangaana na mtoto yule sote tukiwa kama tumeona mizuka. Nikajua kuwa Mungu hutuma malaika zake kulinda wapendwa wetu na kujibu maombi yetu. Zita wangu hakuwa yule niliyeachana naye baa siku ile. Hakuwa mchafu, aliyevaa nguo moja kwa zaidi ya wiki. Hakuwa na nywele ndefu zisizochanwa. Hakuwa na harufu ya uchafu kama mimi, bali alisukwa nywele nzuri za uzi zenye shanga, amevaa nguo nzuri ya kulalia na ananukia mafuta mazuri sana. Nilisukuma sahani, nikainuka na kumkumbatia huku nikilia na kumuangalia mara mbilimbili kuhakikisha kwamba ni yeye. Tulikumbatana kama dakika tano nzima, kila mmoja wetu akionesha hisia zake kwa machozi, kaka Bahati akiwa ametuangalia tu.
Baadaye tulikaa mezani, siwezi kusema furaha niliyokuwa nayo ni kubwa kiasi gani. Nilianza kumuhadithia kaka Bahati maisha yetu, kwa kirefu kabisa, lakini baada ya kunielezea alimpata wapi Zita. Kumbe siku ile alipoondoka pale baa kwenda kunitafuta, nayeye alitembea huku akilia sana kama mtu aliyefiwa, baada ya kutafuta masaa kadhaa bila kuniona. Nilitamani kumlaumu Zita kwa kuchukua uamuzi wa kwenda kunitafuta, lakini kwa mtoto wa miaka nane, nadhani akili yake bado haikuweza kufikiri bora zaidi ya hapo. Bahati alimkuta nje ya hoteli aliyokuwa akila chakula, mvua ikimyeshea, mida ya saa nane na nusu mchana.
Nilianza kujiuliza maswali kadhaa, ambayo japokuwa kaka Bahati alijaribu kuyajibu, lakini bado sikuelewa kwanini ni mtu mwema kiasi hiki. Sikuwahi kukutana na mtu mwema, asiye na hila ndani yake, anayetendea wema hata watu asiowajua. Kwake, machozi ya mtoto au binti mdogo yalimuumiza sana. Nilikuja kuelewa ni kwanini baada ya kuishi naye miezi kadhaa, na kujua historia yake. Nikagundua si mimi pekeyangu niliyeumizwa na dunia.
Kaka Bahati hakuwa na mke, wala mtoto. Kabla yangu na Zita, aliwahi kuchukua binti mwingine kulea, akawa akimsomesha shule ya bweni, hivyo hatukumkuta kwake. Alimtafutia shule Zita pia, changamoto ikawa kwangu kwani umri wangu ulikuwa mkubwa kidogo na niliishia darasa la tatu tu. Alinitafutia shule nzuri pia, akanitafutia na walimu wa tuisheni wanisaidie kunifundisha. Tulianza maisha mapya mimi na mdogo wangu, kwa kaka Bahati, ambaye alitupenda na kutujali kama watoto wake.
ITAENDELEA..