Notification texts go here Contact Us Buy Now!

SIMULIZI - ULIKUWA WAPI SEHEMU YA 02

Ulikua wapi? EP 02


Mateso yangu yalizidi sana, lakini nilipata faraja kwa bibi, aliyenitia moyo kuvumilia akiniahidi kuna siku hali itakuwa sawa tena. Pia mdogo wangu Zita, alinifanya nijitie nguvu na kuvumilia lolote ambalo ningefanyiwa. Bibi hakuwa na msaada kabisa kwa mateso yangu zaidi ya kunitia moyo, ukiacha hiyo mara moja nilipoumwa, kwani kila alipojaribu kunitetea nayeye aliishia kufokewa, “Nyamaza mama.” Ilifika mahala nilizoea kuwa mule ndani mimi, bibi na Zita sote ni kama watoto tusioweza kujitetea kwa lolote.

Siku nyingine niliyoumia sana ni siku ambayo na bibi yangu pia alifariki, lakini kilichoniumiza sana ni kukosa msaada dakika kadhaa kabla ya kufariki. Baba mdogo na mke wake, dada Selina, walitoka jioni, na bamdogo Naise hakuwa ameshinda nyumbani siku nzima. Bibi akaanza kuumwa miguu huku akilia sana, mpaka anazimia, nikijaribu kumsaidia bila kujua cha kufanya. Kufika wakati wakubwa wanarudi, hali yake ilikuwa mbaya sana, kiasi kwamba nadhani hata hospitali hakufika. Alifariki bibi yangu, nikaanza kusemwa sana na bamdogo Naise kuwa nina laana, kwanini baba, mama na bibi, wote wafe mbele yangu. Hapo ndipo maisha yaligeuka na kuwa machungu zaidi ya shubiri. Niliishi miaka mitano ya lawama, kazi zilizonizidi umri, chuki na mateso ya kila namna bila faraja yoyote. Siku zilivyoendelea, mdogo wangu akili yake ilianza kukomaa, hivyo tukawa tukisaidiana kazi za ndani na kuzungumza hivyo kidogo nikaanza kupata faraja.

Siku moja usiku, nikiwa na miaka 14, baba mdogo Musa na dada Selina wakiwa wametoka, alikuja bamdogo Naise akiwa amelewa, ingawa si sana. Alianza kunisema kuwa nina laana na hivyo anatakiwa anitoe laana. Alianza kunivua nguo na kunitaka kimapenzi, wakati huo tumekaa chumbani mimi na Zita. Nililia sana, nikimuomba anihurumie, lakini aliniambia nichague aidha amuue mdogo wangu mbele yangu au afanye mapenzi na mimi kwani ni lazima nitoe bikira yangu kwake ili kutoa laana. Aliahidi nisipokubali, angemfanyia hicho kitendo mdogo wangu, na kwa umri wake mdogo, angefanya hivyo mpaka mtoto angekufa. Aliponiambia nichague, ilibidi nikubali ili amuache mdogo wangu. Nililia mno, nikipiga kelele na kuomboleza, akanishika kinywa, akanifunga na nguo. Alimfunga Zita pia ili asipige kelele kisha alianza kunibaka mbele ya Zita. Niliumia, sana, nikalia machozi lakini hakujali hilo. Alipomaliza aliondoka na sikujua alienda wapi kwani hakurudi tena mpaka nimeondoka pale.

Ilikuwa ni kawaida bamdogo Musa na mkewe wakirudi hupitiliza moja kwa moja chumbani, sisi tukiwa tumelala tayari, kwani walikuwa na funguo yao. Nilibaki nalia mpaka wanafika, Zita wakati huo amelia mpaka akapitiwa usingizi. Walifika na kuingia chumbani kwao kulala. Nilitamani ningewambia kuhusu tukio alilofanya bamdogo Naise, lakini sikupata huo ujasiri, nilijua hata ningesema ningeishia kugombezwa tu na wala nisingesaidiwa. Ni kweli, ndivyo ilivyokuwa kwani kesho yake kwa ajili ya kulia sana, nilichelewa kuamka, akaja dada Selina chumbani na kuniamsha kwa maji kama kawaida. Nilipoamka, aliona macho yangu yamevimba sana, na ya mdogo wangu pia, akaanza kutuhoji, nikajieleza huku nalia.

Dada Selina alikaa kimya kama dakika nzima huku akionesha kama hali ya kustuka na huruma kiasi, lakini aliinuka na kwenda chumbani kwao, akamwambia mumewe nadhani, kwani muda mfupi baadaye alikuja bamdogo Musa wakaanza kututukana kuwa tumejilengesha kwa bamdogo Naise halafu tunasingizia kubakwa. Hapo ndipo niliona nyumba ile hainifai tena, nikakusudia kutoroka. Niliwaza ni nini hasa kinanikalisha, kwani hata chakula wakati mwingine tunakosa. Niliamua nitatoroka, nimchukue Zita pia, tukatafute kazi kokote ya kutupatia chakula. Nadhani walihisi kuwa ningetoroka na pengine kumshitaki bamdogo Naise polisi kwani wiki hiyo nzima ni kama dada Selina alibaki akituchunga. Hakuondoka kwenda popote tofauti na kawaida yake. Sikutumwa kwenda dukani kama nilivyozoea awali, lakini pia bamdogo Naise hakurudi tena. Bamdogo Musa akawa akinilaumu kwamba nimemfanya mdogo wake atoroke kwa kumsingizia ametubaka.

Wiki iliyofuata ni kama walianza kuzoea, na kunituma dukani tena. Baadaye wakasahau kabisa na kuondoka tena wakati wa jioni. Nakumbuka ilikuwa siku ya Jumamosi, zimepita wiki tatu kamili tangu nibakwe, walitoka mida ya saa moja usiku, nadhani walienda kwenye sherehe ya harusi. Wakati huo nilishamuandaa Zita siku nyingi kuwa kuna siku tutaondoka hapo nyumbani na kumuonya asiseme. Walipoondoka tu, niliweka nguo zetu kwenye mfuko wa kiroba tulichoweka nguo, na kila kitu, tukala chakula chetu kwa haraka, tukaondoka mida ya saa mbili usiku. Kabla ya kuondoka nilijaribu kuangalia kama naweza kupata pesa kidogo chumbani kwa bamdogo, nikaingia na kupekua maeneo kadhaa nikabahatisha kuona kibunda cha pesa, laki mbili zimefungwa pamoja. Sikuchukua nusu wala sikuwaza kuwa nitaitwa mwizi, nilibeba na kuondoka nazo bila kuhesabu, nikaja kuhesabu kesho yake tukiwa safarini. Sikujua wapi tunaelekea usiku huo, lakini nilikusudia kutoka pale nyumbani na kutorudi kamwe.
Siku hiyo tulilala mtaani, mbali kabisa na eneo la nyumbani, sehemu moja Arusha inaitwa Mbauda. Ili kuwa salama, niliona baada ya kuondoka tupande daladala na kuelekea popote, hivyo tukaenda Mbauda, tukatafuta sehemu moja nje ya duka, tukalala. Kama unavyojua Arusha, baridi ni kali mno. Lakini kati ya nguo chache nilizobeba, nilibeba za kujikinga na baridi zaidi, hasa kwa ajili ya mdogo wangu. Zita alilia mara kadhaa, lakini nilimfariji kuwa tunaachana kabisa na mateso ya kwa bamdogo. Tulilala hapo lakini usiku wazo lilinijia la kuondoka Arusha kabisa hivyo alfajiri sana nikamuamsha Zita, tukaanza kufanya mpango wa tiketi ya kwenda Dar es Salaam. Nilifanya hivi kwani nilishawahi kusikia kuwa Dar es Salaam kuna kazi nyingi, pia nilitaka nihakikishe kuwa hata nikitafutwa sitapatikana. Tulisafiri na kufika Dar, siku hiyo hiyo jioni.

Nimeishi maisha machungu, ya mateso mno Dar es Salaam. nimetafuta kazi mara kadhaa, bila mafanikio. Kuna wakati nilipata kazi za ndani, lakini walinikataa kukaa na mdogo wangu. Baada ya miezi minne ya kulala mtaani, nilifanikiwa kupata kazi ya kuuza baa. Kazi hiyo ilianza vizuri kwani ilitupatia chakula na sehemu ya kulala, ingawa chumba kimoja tulilala wasichana wanne wafanyakazi, pamoja na Zita. Sikujali ni wapi tunalala, ila kulala ndani ya chumba kwangu ilikuwa ni ahueni kubwa. Miezi minne mizima ya kulala mtaani, kuomba omba na kuokota vyakula ilinifanya nitamani kazi yoyote. Kama hujawahi kuishi mtaani unaweza ukawa na ujasiri wa kutukana kila unayemuona akiomba omba. Yale maisha ni magumu asikwambie mtu. Watu wanakuona kama mbwa koko, asiyestahili hata kuongeleshwa na watu, wala hata kuangaliwa akivuka barabara ili asigongwe na gari.

Mara kadhaa tulinusurika kubakwa, tena na wengine watu wenye akili zao kabisa. Kuna wakati ilitubidi kuhama eneo la kulala kwa kulinda usalama wetu, kwani ilitokea uvamizi wa usiku na hivyo kutafuta eneo salama zaidi. Zita alikuwa akilia lakini baadae alizoea kuwa haya ndio maisha. Niliumia sana siku aliyoomba turudi kwa bamdogo, Arusha. Kwangu kuishi mtaani na mateso yale ilikuwa ni sawa kabisa na kuisi kwa baba mdogo Musa, lakini tofauti yake ni kwamba huku mtaani nilikuwa na matumaini kwamba kuna siku ningepata kazi na maisha yakawa mazuri. Kwa bamdogo niliishi bila tumaini la kwamba siku moja nitakuwa huru, au maisha yatabadilika.
Nilipopata kazi, nilianza kuona nafuu ya maisha, lakini tofauti na matarajio yangu, wanaume wengi walianza kunitaka kimapenzi.

Kusema kweli kazi ni kazi lakini kazi ya baa ina changamoto kubwa mno. Nilikataa wanaume mara kadhaa, nikaitwa na meneja na kuonywa kuwa siwatendei haki wateja wake, huku akiahidi nikiendelea na tabia hiyo, nitafukuzwa. Nakumbuka mara ya kwanza nilikubali kuondoka na mwanaume mmoja, ananizidi zaidi ya miaka 25 nafikiri. Tulipofika nyumba ya wageni, nilianza kulia sana huku nikimuomba anisamehe. Akilini nilikumbuka maumivu niliyopata siku bamdogo Naise ananibaka, sikutamani yajirudie. Nililia sana, kiasi cha kumfanya anionee huruma na kuamua kuniacha. Aliondoka hapo bila kunirudisha kazini, ikabidi niondoke usiku huo, nikiulizia ulizia mpaka nikafika kazini ambapo ndipo tulilala pia.

Meneja aliposikia aliniita na kunisema sana, akasema lile jambo likijirudia tena atanifukuza kazi. Tatizo la kazi ya baa, hauna muda kabisa wa kufanya kitu kingine chochote wala kutafuta kazi nyingine. Kuna wakati nilijaribu kuongea na wateja niliowaona wastaarabu, kuhusu kufanya kazi nyumbani kwao. Wengine walinitukana, wakidai kuajiri muuza baa ni kuleta Malaya nyumbani kwako. Wengine walinishitaki kwa meneja, nikagombezwa au kutandikwa vibao, wengine walinikubalia lakini wakaanza kuonesha kunitaka kimapenzi. Nilijitahidi kuongea zaidi na wateja wa kike, lakini unajua baa wateja wengi ni wa kiume ndio huja pekeyao, na kuongea na mtu akiwa na mume wake pembeni mara nyingi ilinifanya niambulie matusi tu.

Siku moja kuna mwanaume, aliyeonekana mstarabu sana, niliongea naye, akanikubalia na kesho yake alikuja saa moja jioni na kunipeleka kwake. Niliamua nitaondoka kwanza mimi halafu nikihakikisha mazingira yanafaa ndipo nimchukue Zita wangu. Niliongea na Zita, akanielewa, nikaenda na yule mwanaume. Niliamini alishaongea na mke wake kuhusu kuniajiri, lakini cha ajabu nilipofika tu, mke wake baada ya kutambulisha aliingia jikoni na kutoka na maji ya moto, akanimwagia miguuni. “Hiki ndicho ninachowafanya mabinti wadogo wanaofakamia ndoa za watu,” alisema, huku akimwaga maji hayo. Nilitoka mbio sana nje, nikilia, nikaacha wakigombana na mume wake, nikaanza kukimbia. Sikuweza kukimbia kwa mwendo mrefu kwani maumivu makali yalianza na kunifanya nishindwe kutembea. Kwa bahati sana yule baba alikuja na kunikuta njiani nikiugulia maumivu, akanipeleka hospitali kwa gari yake, akaacha amenilipia bili yote na kunipa kiasi cha pesa huku akiniomba msamaha. Nililala hospitali, nikimuwaza mdogo wangu sana, kwani sikumzoesha kujitegemea.

ITAENDELEA..




About the Author

Hello,I am Web Designer and Expert facebooktwitteryoutubeinstagramexternal-link

Chapisha Maoni

Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
Oops!
It seems there is something wrong with your internet connection. Please connect to the internet and start browsing again.
AdBlock Detected!
We have detected that you are using adblocking plugin in your browser.
The revenue we earn by the advertisements is used to manage this website, we request you to whitelist our website in your adblocking plugin.
Site is Blocked
Sorry! This site is not available in your country.