ulikuwa wap Sehemu Ya Kwanza (1)
Ulikuwa wapi wakati mama yangu anafariki? Ulikuwa wapi nikiomboleza kwa ajili ya baba yangu? ulikuwa wapi nafukuzwa shule kwa ajili ya ada? Ulikuwa wapi nilipoanza kuzurura mtaani? Ulikuwa wapi nauza bikira yangu kwa ajili ya maisha ya mdogo wangu? Ulikuwa wapi miaka yote 22 ya maisha yangu bila wazazi na bila msaada? Nawezaje kuona thamani yako?
Namuuliza maswali hayo baba yangu mdogo, ambaye nakumbuka vizuri siku baba yangu anafariki alimuachia mimi na mdogo wangu, akampa maelekezo ya kututunza na kutusomesha. Siku ya huzuni zaidi kwenye maisha yangu, lakini sikujua ukubwa wa huzuni hiyo, mpaka nilipoanza maisha bila baba, bila mama. Kabla ya kifo cha baba, baba yangu mdogo, Musa, alionesha kutujali na kutupenda. Alikuja nyumbani mara kwa mara, akituletea chokoleti, pipi na zawadi nyingi za kitoto. Wakati huo alifanya kazi benki ya NBC, hivyo uwezo wake haukuwa mdogo. Kulingana na akili ya umri wangu wakati huo, niliona baba mdogo ana hela nyingi sana kwani niliwahi kuambiwa hela zote hupelekwa benki. Nilijua wafanyakazi wa benki wote ni wamiliki wa pesa nyingi zinazopelekwa huko.
Mara nyingi baba alituambia anapeleka hela benki, au anaenda kuchukua hela benki, hivyo nikaiaminisha akili yangu kuwa baba mdogo atakuwa na pesa nyingi sana kuliko baba. Niliwahi kumuuliza mara kadhaa, “Eti bamdogo wewe si una hela nyingi sana? Benki si watu huwa wanaweka hela, nawewe ndio unafanya kazi huko?” Niliamini anamzidi baba pesa, na mara kadhaa nilimwambia hivyo, kwamba baba yetu ana pesa lakini wewe unamzidi pesa.
Baba yangu, marehemu mzee Stephano Wanjiku, alizaliwa kama mtoto wa pekee kwa mama yake, aliyezaa na mkenya miaka ya nyuma, kisha hawakuoana na huyo mwanaume, mama yake ambaye ni bibi yangu akarudi Tanzania, akaolewa na mmasai mmoja, mzee Olengai. Walizaa naye watoto wa tatu, lakini mpaka napata akili mmoja alikuwa ameshafariki, na babu pia mzee Olengai. Bibi yetu tuliishi naye nyumbani kipindi fulani, mpaka baada ya kifo cha baba yangu, ndipo tukahamia kwa baba mdogo.
Baba alifariki kwa ajali ya gari yake, lakini hakufa papo hapo, alikaa hospitali KCMC Moshi kwa muda wa wiki moja, akaruhusiwa kurudi nyumbani lakini wiki iliyofuata alipata mshtuko wa moyo na kufariki. Siku aliyofariki tulikuwa mimi na baba mdogo tumekaa naye sebuleni, mama akiwa jikoni na mdogo wangu amelala chumbani. Baba, kama mtu aliyejua kinachoenda kutokea, alianza kumwambia baba yangu mdogo maneno yaliyoashiria kuondoka kwake, mbele yangu,
“Musa mdogo wangu, wewe ndiye mwanaume ninayekuamini kiasi cha kuweza kukukabidhi familia yangu. Mke wangu bado mdogo ki umri, hivyo ataolewa najua, maana pia ni mrembo sana, lakini siku zote jua hawa ni watoto wako, kabla na hata baada ya mke wangu kuolewa. Simaanishi umnyang’anye, lakini hakikisha unawatunza na wanasoma. Kustawi au kuharibika kwa maisha yao kuko mikononi mwako. Sijafanikiwa kuandika urithi, lakini naamini huna tamaa ya mali hivyo hautamnyang’anya mke wangu mali zake. Mimi naondoka, najua nitakufa tu, lakini naomba unitunzie familia yangu.” Baba aliongea hayo kisha akawa kama amebanwa na kitu kifuani, kabla hata hajatolewa nje kupelekwa hospitali, alifariki.
Sikuwa mkubwa wakati huo, japo mpaka leo nakumbuka maneno ya mwisho ya baba yangu. umri wangu ulipata miaka nane tu, na mdogo wangu miaka mitatu. Baba alikuwa mfanya biashara mkubwa sana miaka hiyo, wa magari kutoka Japan, hivyo alikuwa kati ya matajiri waliotikisa Arusha miaka hiyo. Wakati wa msiba, mama alipoteza fahamu mara kadhaa. Nakumbuka kuna wakati ilibidi apelekwe hospitali. Katika utu uzima wangu ndio nimeelewa kiasi gani mama hakuwa amejiandaa kwa kifo cha baba, au labda baba hakumuandaa.
Baada ya mazishi, akili ya mama ilikuwa kama imechanganyikiwa, kiasi cha kupelekwa hospitali. Mimi na mdogo wangu Zita tulichukuliwa, pamoja na bibi tuliyeishi naye pale nyumbani, tukapelekwa kwa baba mdogo, ambaye hakuwa ameoa wakati huo,na aliishi na mdogo wake pia, wa kiume, bamdogo Naise. Mama alipotoka hospitali, hakurudishwa tena nyumbani, lakini naye aliletwa kuishi nasi kwa baba mdogo Musa.
Ghafla maisha yalianza kubadilika, mama alichukuliwa kama mtoto na sio mke wa baba tena. Bamdogo alimgombeza mama mbele yetu, hakuruhusiwa kufanya chochote bila ruhusa yake huku akimsema kwamba ni mgonjwa wa akili. Nakumbuka mara kadhaa nilikaa na mama chumbani, nikimbembeleza na kumfuta machozi. Mama alianza kudhoofu na mara kwa mara alipelekwa hospitali kwa matibabu ya msukumo wa damu yaani presha. Kuna wakati alizidiwa sana, nikapata wasiwasi kuwa atakufa na yeye. Nakumbuka siku moja, nimetoka shule, nilimkuta mama akiwa na Zita, peke yao nyumbani, huku mama anaumwa sana. Kulingana na maelezo ya mama, alianza kuumwa tangu asubuhi, bamdogo akiwepo pamoja na bibi, lakini bibi alitakiwa kupelekwa kliniki yake hivyo waliondoka baba zangu wadogo wote wawili na bibi, ili bamdogo Naise akakae na bibi kliniki wakati kaka yake akienda kazini. Sikuelewa kwanini hawakwenda pamoja na mama.
Mara ya mwisho mama anaumwa, anapelekwa hospitali na kurudi, kabla ya siku hiyo, bamdogo Musa alisema ugonjwa wa mama ni wa kawaida tu, wameshauzoea kwa sasa, hivyo atapona hata bila dawa tena. Alisema kuanzia siku hiyo hatakuwa akitumia mafuta na muda wake tena kumpeleka hospitali, na ndicho alichofanya siku hiyo. Niliogopa sana kuona hali aliyokuwa nayo mama. Kwa bahati mbaya sana, eneo tuliloishi, Sakina, ni maeneo ya uzunguni kidogo, hivyo hakukuwa na majirani wa karibu wa kuwagongea. Nyumba ziliunganishwa kwa mageti. Nikiwa nimechanganyikiwa sana, bibi alikuja, na huyo mwanae Naise. Nikawakimbilia getini kuwaambia mama anaumwa. Bibi alipata hofu na kumtaka bamdogo Naise ampeleke hospitali, lakini hakukubali badala yake akaondoka akidai ameshamaliza siku nzima na mambo ya hospitali hivyo ana ratiba zake za muhimu zaidi. Bibi aliumwa miguu, hakuwa na uwezo wa kutembea hata mita mia moja.
Sitasahau maumivu niliyopata, mama yangu akikata roho miguuni pangu. Niliona sasa dunia imefika mwisho. Binti wa miaka nane, nilikuwa napewa jukumu la kuwa baba na mama kwa mdogo wangu Zita. Nililia sana, mno yaani, bibi akanikumbatia, akalia namimi, akamfumba mama macho. Sikutaka mama atoke miguuni kwangu, nikiendelea kumuamsha kwa nguvu, huku tukisaidiana na mdogo wangu ambaye akili yake ndogo sana haikuelewa yanayoendelea ulimwenguni. Alianza kulia huku akiuliza kama mama naye watampeleka kule alikoenda baba. Aliomba sana wasimfukie mama kwani baba walimfukia na hakurudi tena.
Tukimzika mama yangu, niliona kila kitu ni kichungu. Sikuona thamani tena ya kuishi, nikataka kujitupia kaburini nizikwe na mama, lakini nilimuhurumia mdogo wangu, na hata hivyo nisingeachiliwa kufanya hivyo. Nililia, kama mtu asiye na msaada wala tumaini lolote. Zita naye alilia sana, akiangalia wanamzika mama. Nilipomuangalia, sikuona mtoto, niliona jukumu kubwa mno ambalo sikujua namna gani naweza kulibeba. Maisha yalinigeuka kwa haraka sana, kupoteza baba na mama ndani ya miezi sita.
Baada ya msiba, tulianza maisha mapya kabisa. Kuna msichana wa kazi aliyeishi pale nyumbani lakini alipewa maagizo ya kuanza kunifundisha kazi. Kila nilipotoka shule, nilitakiwa kufanya kazi za ndani mpaka wakati wa kulala. Nakumbuka miezi miwili iliyofuata tulifunga shule, nikabaki nyumbani. Hapo ndipo nilifanya kazi zilizo ndani na nje ya uwezo wangu. Nilidamshwa alfajiri kila siku, nikatakiwa kusafisha nyumba, kusafisha uwanja, kuandaa chai, kufua, na kazi zote huku dada wa kazi amenisimamia tu bila kunisaidia chochote. Nilichoshangaa, hata dada alishirikiana na baba zangu wadogo kunitumikisha kana kwamba si wajibu wake. Bibi alijaribu kunitetea lakini hata yeye hakuwa na kauli mbele ya watoto wake hao.
Nakumbuka baada ya kufungua shule nilitakiwa kulipiwa ada kwa ajili ya muhula uliofuata. Nilisoma shule moja ya Kimataifa inaitwa Arusha Modern. Nilipopewa barua ya kulipa ada, niliipeleka kwa baba mdogo, lakini sitasahau siku nimempa ile barua. Aliichana mbele yangu, akanitukana sana huku akidai hawezi kutumia pesa yake kunilipia ada wakati anajua ntaishia kubeba mimba tu. Alisema kazi inayonifaa ni kufanya kazi za ndani na sio kusoma. Baba mdogo alisema kwamba ameshatumia gharama kubwa sana kwa ajili yetu hivyo inabidi nifanye kazi, msichana wa kazi aondoke.
“Nina haja gani ya kuendelea kutumia pesa zangu kukusomesha, na pia kumlipa msichana wa kazi wakati wewe uko hapa na mdogo wako mnakula na kulala bure? Wewe mwenyewe unajua baba yako hakuwa na pesa kama zangu, na kwa taarifa yako miaka yote mimi ndiye nilimpatia pesa za kuwatunza. Sasa huu ndio mwisho wa kusoma kwako, utakaa hapa nyumbani na kufanya kazi za humu ndani, huyu binti wa kazi ataondoka.” Alisema maneno hayo baba mdogo, akimaanisha kunikatiza shule. Pia nadhani alichukulia ile kauli niliyokuwa nikimwambia kuwa yeye ana hela kuliko baba, akaamua kunidanganya hivyo. Niliendelea kwenda shule, lakini niliporudi niliongezewa kazi na wakati mwingine kupigwa bila sababu huku akinihakikishia kuwa sitaweza kuendelea kwani nitafukuzwa ada. Kweli ndani ya mwezi mmoja tu nilirudishwa na kuambiwa nisiende tena mpaka nitakapolipiwa.
Nilitegemea dada aondoke siku chache baadaye na asirudi tena. Ni kweli aliondoka, lakini tofauti na matarajio yangu, alirudi baada ya kama mwezi au miezi miwili na kuanza tena kuishi pale. Niligundua baadaye kuwa alirudi akiwa mjamzito. Huyu dada sasa hakuwa dada Selina niliyemzoea kabla. Mara hii alinichukia na kunitesa kwa waziwazi, bila sababu. Nilipochelewa kuamka, aliniamsha hata kwa kunimwagia maji. Alitegemea nifanye kila kitu mwenyewe, mpaka kazi zake binafsi kama kufua nguo za ndani.
Kuna siku niliamka naumwa, nikafanya kazi kwa ugumu sana, lakini dada Selina hakujali hilo kabisa. Siku hiyo nilitapika sana, mpaka bibi ilibidi aseme kwa ukali sana, ndipo jioni baba mdogo aliporudi nikapelekwa hospitali. Wiki hiyo nzima nilikua mgonjwa, lakini ni kwa utetezi wa bibi tu, tena akigombana sana na dada Selina, ndipo nikaruhusiwa kupumzika kwa siku kama tano. Haikupita muda, dada alihamia chumbani kwa bamdogo Musa. Akili ikaanza kuelewa kwamba huyu si dada tena bali ni mama mdogo na ndio sababu hakuendelea kuwa mfanyakazi.
INAENDELEA..