MOYO ULIOJAA MAUMIVU
SEHEMU YA 37
Theo alibaki akimwangalia mke wake pale kitandani alipokuwa. Moyo wake ulimuuma mno, swali alilomuumiza likamfanya kuanza kukumbuka kila kitu kilichotokea. Machozi yalianza kujaa machoni mwake lakini hakutaka kuyaruhusu yatiririke mashavuni mwake kwa kuwa aliamini mke wake angegundua kila kitu.
Violeth aliendelea kumwambia mume wake kuhusu watoto wake, aliamini kwamba alijifungua salama kabisa lakini baada ya kutuliza macho yake usoni mwa Theo, akagundua kulikuwa na kitu kilitokea kwani lisingekuwa jambo jepesi kwa mwanaume ambaye mkewe alijifungua salama kuwa na muonekano ule aliokuwanao.
Akamuuliza tatizo lilikuwa nini, Theo hakutaka kumwambia ukweli, alibaki kimya lakini mke wake huyo hakutaka kunyamaza, alihisi kulikuwa na kitu na alikuwa tayari kuambiwa kwani hali ile ilimtia hofu mno.
“Kuna nini mume wangu?” aliuliza Violeth huku akimwangalia Theo.
“Hakuna kitu!” alijibu Theo kwa kujikaza.
“Mbona macho yako mekundu hivyo? Ulikuwa unalia ama?” aliendelea kuuliza mwanamke huyo.
Theo akashindwa kuvumilia kabisa, machozi yake yakaanza kutiririka mashavuni mwake kitu kilichomshtua mno Violeth ambaye alihisi kulikuwa na jambo fulani ambalo mume wake hakutaka kumwambia.
“Hapana! Kuna tatizo! Kwanza nataka kuwaona wanangu,” alisema Violeth huku akimwangalia mume wake, hakuishia hivyo tu bali akataka kuinuka, haraka sana daktari aliyekuwa pembeni akamsogelea na kumzuia.
“Violeth! Subiri, usiinuke,” alisema daktari kwani alijua kama angeinuka basi angeuchomoa mpira uliokuwa ukipitisha maji kwenda kwenye mishipa yake.
“Niambieni kuhusu wanangu!” alisema Violeth kwa sauti kubwa.
“Subiri kwanza...” alimtuliza daktari.
Ilikuwa vigumu sana kwa Violeth kutulia, alihitaji kitu kimoja tu mahali hapo, kuwaona watoto wake.
Alimwambia daktari kwamba asingeweza kutulia hata kidogo, alifika hospitalini hapo kwa lengo la kujifungua, kazi hiyo ilifanyika hivyo alihitaji kujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.