MOYO ULIOJAA MAUMIVU
SEHEMU YA 33
Mmoja alikuwa akilia sana lakini mwingine ilikuwa ni maiti tu ambayo ilifungwa vizuri. Maumivu yakazidi kuongezeka kwa Theo, aliiangalia maiti ile ya mtoto wake, hakuamini kama alikuwa amekufa baada ya kuzaliwa.
“Harry mtoto wangu, amka uniangalie baba yako, fumbua macho yako mtoto wangu, nitazame, baba yako nimefika, fumbua macho yako mwanangu,” alisema Theo kwa sauti ya chini huku akiiangalia maiti ya mtoto wake aliyekuwa katika kitanda kidogo.
Maiti ilikuwa kimya, macho yalifumbwa, roho yake haikuwa hapo tena. Moyo wake ulimchoma mno, macho yake yalikuwa mekundu, manesi na daktari ambao walikuwa ndani ya chumba kile, wote walikuwa wakilia, maneno aliyoyaongea Theo yaliwachoma mno, yalionyesha ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alikuwa ameumia.
Akatoka hapo na kusoge kule alipokuwa mtoto wake mwingine, aliyeamua kumpa jina la Rachel, akamwangalia mtoto huyo alikuwa akikunjakunya vidole vyake huku wakati mwingine akilia. Alimwangalia moyo wake ulifurahia lakini bila kuwa na mtoto mwingine, furaha ile haikuwa imekamilika hata kidogo.
Alipotoka hapo akasogea mbele, akafika katika kitanda alichokuwa mke wake, Violeth, alikuwa kimya, alipumilia mashine ya hewa safi. Moyo wake ulimuuma mno, hakujua ni kwa jinsi gani angemwambia kuhusu mtoto wao mmoja aliyekuwa amefariki dunia.
Aliganda tu akimwangalia mke wake huyo alivyokuwa akiutetea uhai wake kitandani pale. Alitamani kumuamsha, ampeleke nyumbani na kumsahaulisha kila kitu, yaani asahau kama alijifungua watoto maoacha wazuri mno.
“Mke wangu! Umepambana, umepigana mno! Wewe ni mwanamke shujaa, una moyo wa chuma, umepigania uhai wa watoto wetu, hata kama mmoja amefariki, ila bado ulipambana....” alisema Theo na kunyamaza, akaendelea kulia kama kawaida.
“Nashukuru kwa kunifanya kuwa baba tena,” alisema Theo na kuifuata maiti ya mtoto wake, akaibeba.