MOYO ULIOJAA MAUMIVU
SEHEMU YA 02
Akaunti yake benki ilikuwa na kiasi cha shilingi bilioni 3.2, alijenga jumba kubwa lililokuwa Mbezi Beach huku akimiliki biashara nyingi nchini Afrika Mashariki.Maisha yake hayakuwa Tanzania kwa sana, aliishi nchini Ufaransa huku akiendelea na kazi yake ya mitindo ambayo aliifanya kwa zaidi ya miaka mitatu.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa na maswali mengi kuhusu utajiri wa msichana huyu.
Ni miaka michache nyuma wakati akiwa na miaka kumi na tisa, tena huku akichipukia kwenye umaarufu nchini Tanzania aliolewa na mwanaume aliyeitwa Didier Polvat, raia wa Ufaransa aliyekuwa mbunifu wa mavazi duniani huku akimiliki kampuni yake ya Havana Fashion And Modelling ambayo ilifanya kazi dunia nzima kwa kuchukua wanamitindo mbalimbali.
Wawili hao walikutana wakati Didier alipokwenda nchini Tanzania kwa lengo la kutafuta warembo ambao wangeweza kufanya kazi katika kampuni yake. Mara baada ya macho yake kutua kwa Violeth alishtuka, hakuamini kama Tanzania ingekuwa na msichana mrembo kama alivyokuwa.
Alimwangalia kwa matamanio, moyo wake ulimpenda kupita kawaida na hivyo kuomba ukaribu naye. Hilo halikuwa tatizo hasa kwa mtu kama Violeth ambaye alikuwana umaarufu mkubwa Tanzania lakini hakuwa na uwezo wa kujitangaza na kuwa zaidi ya hapo.
Wakaanza kuzungumza, wakaweka ukaribu, Didier hakutaka kukubali, alimuhitaji msichana huyo na hatimaye kumualika jijini Paris nchini Ufaransa kwenda kuhudhuria moja ya maonyesho yake ya mitindo nchini humo.
Violeth alikuwa gumzo kila kona, kila aliyemuona alishtuka, aliwafanya wanaume wote waweweseke kutokana na uzuri wake, alijua kutembea, alijua kuringa, alijua kutoa tabasamu na kubwa zaidi alijua kucheka na kuyafanya meno yake meupe yaonekane vilivyo.
Japokuwa Didier alitokea kumpenda sana Violeth lakini hakutaka kuwa na haraka kumtongoza na kumwambia ukweli wa kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.
Alimwangalia kwa macho yaliyobeba ujumbe mzito lakini hakutaka kumwambia kwa mdomo wake hivyo kuendelea kuyatumia macho yake katika kufikisha kile alichokuwanacho moyoni mwake.
