JIJI la Dar es Salaam linatingishika, wezi sugu wanaingiza noti bandia, watu wanaibiwa. Baadhi wanauza majumba, magari na viwanja. Wafanyabiashara hatari wa dawa za kulevya nao wanacharuka, wanatangaza hali ya hatari kwa atakayeonesha kuwaingilia. Patashika linatokea, Dar es Salaam inakumbwa na misukosuko na mauaji ya kutisha.
"Kama unayathamini maisha yako jiweke pembeni". Amri inatolewa, "Vinginevyo yatakupata makubwa". Onyo linatolewa kila pembe ya jiji. Polisi wanagwaya, mauaji ya kutisha yanatokea, tishio linakuwa kubwa zaidi. Rais anapaza sauti, "Lazima hali hiyo ikomeshwe vinginevyo, hatuwezi kuvumilia...".
Mashujaa kadhaa wanajitokeza kuikabiri hali hiyo. Maiti zao ziokotwa kando ya bahari. Teacher anatua uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kukabiliwa na mtihani mkubwa, gari lake linashambuliwa, anaponea chupuchupu. Lakini anaapa kuikabibiri hali hiyo ngumu. SASA ENDELEA.
NOTI BANDIA SEHEMU YA KWANZA
Na Nyakasagani MasenzaNDEGE ndogo ya kukodi ya Kampuni ya ndege za Coastal ilishuka taratibu kwenye uwanja wa ndege wa mjini Musoma, baada ya kuwa angani kwa takribani dakika ishirini na tano hivi ikitoka katika Jiji la Mwanza. Mara baada ya ndege hii kutua kwenye uwanja huu, ulioko karibu kabisa na ukingo wa Ziwa Victoria, eneo maarufu la Makoko, nilikuwa miongoni mwa abiria watatu tuliosafiri kwa ndege hii kutoka Mwanza ambako tulibadilishiwa ndege.
Hii ilitokana na uwanja wa ndege wa Musoma kutokuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa kwa sasa. Baada ya ndege hii kutua, nilitwaa mfuko wangu mdogo uliosheheni vifaa vyangu muhimu vya safari, taratibu nikavuta hatua kutoka ndani ya ndege hii nikiwa tayari kuelekea nje.
Sikuwa na sababu ya kwenda haraka kutokana na hali ya ndege hii kuwa ndogo, hivyo nilisubiri wenzangu watoke kwanza ndipo nami niweze kutoka. Baada ya kukanyaga ardhi ya mji wa Musoma nilitembea taratibu, mkoba wangu begani, nilipita mapokezi na sehemu ya mapumziko ya wageni mashuhuri, nikaelekea kwenye maegesho ya magari ya kukodi nje ya uzio wa uwanja.
Hali ya hewa ya mji wa Musoma ilikuwa ya kuvutia sana, wingu zito lilitanda angani, kuashiria dalili ya mvua. Hali kama hii pia tuliikuta tuliposhuka kwenye uwanja wa Mwanza ambako tulikuta mvua ya kutosha. Kiasi fulani nilivutiwa na hali hii ya ubadiridi hususan kutokana na joto kali nililoliacha Jijini Dar es Salaam.
"Haraka, nipeleke Mkendo tafadhali", nilimwambia dereva teksi, baada tu ya kuingia na kuketi ndani ya gari yake iliyokuwa imeegeshwa karibu na sehemu niliyotoke.
"Sawa mzee", alisema dereva huyo huku akiwasha gari na kufunga mkanda, nami nikafanya hivyo. Wakati anaanza kuondoka aliuliza, "Mkendo ipi?", alihoji dereva huyo huku akiondoa gari taratibu kutoka kwenye maegesho ya uwanja wa ndege.
"Mkendo... Nadhani utaniacha baada ya njia panda ya mtaa wa Iringo", nilimwambia.
"Nadhani dakika tano", alisema huku akiingia kwenye barabara kuu ya Majita, akaongeza mwendo tukaelekea katikati ya mji. Baada ya kuzipita ofisi za Shirika la Umeme Tanzania Tanesco, nilivunja ukimya uliodumu kwa dakika kadhaa.
"Vipi hali ya samaki katika mji huu, wanapatikana?", nilimuuliza, taratibu akageuza shingo kunitazama, kiasi fulani alionekana kushangazwa na swali langu.
"Samaki!... alihoji kwa mshangao.
"Ndio... Mbona kama imekushituawa sana, wanapatikana?".
"Samaki bwana ni wengi sana. tatizo ni bei. Samaki kama Sato wanauzwa kwa bei mbaya sana, viwanda vimeleta shida, minofu ya samaki katika mji huu ni lulu, inasafirishwwa nje ya nchi, wakazi wa hapa tunaachiwa mifupa", alisema kwa utani huku akinitazama usoni akicheka.
"Mifupa ya samaki?", nilimuuliza. Niliwahi kusikia kuwa idadi kubwa ya samaki wanaovuliwa Ziwa Victoria wanapelekwa viwandani na kusafirishwa nje ya nchi, wenyeji wanaambulia mfupa mkubwa wa katikati na kichwa. Maelezo yake yalinifanya nihamasike kuuliza maswali mengine zaidi.
"Hiyo mifupa unayodai kuwa ndiyo inauzwa kwa wananchi, inafaa kuwa chakula?".
"Samahani kaka, wewe ni mgeni katika mji huu?", alihoji kijana huyu ambaye umri wake haukutofautiana sana na wangu.
"Mgeni mwenyeji, ni mzaliwa halisi wa mkoa huu, nimeishi sana mjini hapa, enzi zetu tulipokuwa wadogo samaki walikuwa wengi sana, sato, sangara, nembe ilikuwa usiseme, ukishuka Mwigonero samaki wa kumwaga, nasikia siku hizi hawapatikani ndiyo nashangaa", nilimwambia wakati anaingia kwenye mzunguko wa barabara za Nyerere na kuacha ile ya Sokoni.
"Umewahi kuona mabaki ya samaki yaliyoondolewa minofu ikabaki mifupa, hapa mkoani yanaitwa mapanki. Umewahi kuyaona?", aliniuliza.
"Hapana?".
"Basi labda nikudokeze, mapanki ni sehemu ya samaki waliotolewa minofu kwa ustadi mkubwa na kubaki kichwa na mfupa mkubwa wa katikati, mabaki ambayo huuzwa tema kwa watu wa kipato cha chini, hii inatokana na bei ya samaki kuwa juu sana. Ndiyo hali halisi ndugu yangu, samaki tunawasikia kwenye bomba tu huko viwandani", alifafanua kijana huyu.
"Aisee, sasa nimekupata. Kumbe ndivyo ilivyo...", nilinyamaza kidogo nikitafakari kisha nikamuuliza. "Kwanini serikali isiingilie kati, kuwasaidia wananchi wapate maisha bora, nina maana kuwa yatengwe maeneo ya wavuvi wa samaki kwa ajili ya wananchi wenye kipato cha chini, viwanda navyo vinunue kwa bei ya juu kidogo ili kuweka usawa".
"Nchi hii kaka, wananchi hawana maamuzi, tumewapa wenzetu dhamana wanaitumia kujinufaisha wao na matumbo yao, tatizo pia liko kwetu wabongo, tunajua kulalamika tu lakini hatuna maamzi ya kukataa jambo", alisema, baadaa ya kunyamaza kwa sekunde kadhaa, akageuka kunitazama. Labda hii serikali mpya italeta maisha bora".
"Labda, tusubiri tuone, maana watendaji ni walewale walioshindwa", nilimwambia akacheka.
Baada ya kupita kwenye mzunguko wa Barabara ya Nyerere, tukauacha mtaa wa Sokoni, tukaingia kwenye Barabara ya Nyerere, baada ya kituo cha mafuta cha GAPCO karibu na ilipokuwa karakana ya mabasi ya United. Sambamba na uwanja wa shule ya msingi Mkendo, tukaingia kushoto ulipo mtaa mdogo wa Rutiginga, moja mitaa yenye historia kubwa mjini Musoma. Inasemekana mtaa huu ndiyo wa kwanza kuwa na kinadada wanaouza miili yako. Baada ya kuuacha mtaa huu wa Rutiginga, moja kwa moja tukatokea barabara kuu ya Mkendo.
"Nimelazimika kupita njia hii kukwepa msongamano wa magari eneo la standi ya mabasi, muda huu kunakuwa na foleni kidogo", alisema wakati akisubiri kuingia mtaa wa Mkendo.
"Usijali, mitaa hii naifahamu vizuri pengine zaidi kuliko wewe, hata tungepita barabara ya Uhuru bado ilikuwa sawa tu", nilimwambia akatabasamu wakati akisimama mbele ya studio ya Issa Mkate, nilitoa kiasi cha pesa nikampatia akashukru na kuondoka.
Nilikuwa nimewasili mkoani hapa kwa likizo fupi ya upendeleo, niliyopewa na Mkuu wangu wa kazi, Kanali Benny Emilly, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi. Lakini kabla ya kuondoka Dar es Salaam nilipanga ratiba fupi ya kuonana na watu kadhaa. akiwemo rafiki yangu kipenzi Luteni Kanali Charles Matumbi anayeishi mtaa huu wa Mkendo.
Kwa mjibu wa ratiba yangu mjini Musoma sikuwa tayari kuonana na mtu zaidi na Luteni Kanali Matumbi, nikihofia kuharibu ratiba yangu, kwani nilipanga pia kufika kijijini kwetu Nyamuswa, Wilayani Bunda ambako nilipanga kukutana na mama yangu mzazi niliyempenda sana. Baba yangu niliyempenda sana alikwisha tangulia mbele ya haki. Nimekuwa nikijiuliza maswali maswali mengi kwa nini Baba yetu tuliyempenda alikataa kula chakula hata akadhoofu na kupoteza maisha. Hii ni siri ya Mungu aliyetuumba na kutufanya tuishi kwa muda katika ulimwengu.
Likizo hii fupi ilitolewa na Mkuu wangu wa kazi Kanali Emilly kwa upendeleo, baada ya ofisi yake kupokea hati ya utambulisho wa kimataifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutambua mchango wa utendaji kazi wangu nikiwa mlinzi wa amani wa umoja huo. Baada ya kushiriki kazi za ulinzi wa amani katika mipaka mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania. Kazi niliyofanya kwa uaminifu mkubwa, nikiwa mkuu wa operesheni za kijeshi kwenye baadhi ya mipaka.
Kwa takriban miaka miwili nilihudhuria kozi na masomo mbalimbali ndani na nje ya nchi yetu na kutunukiwa vyeti na shahada mbalimbali, katika ngazi za Ukamanda, Utawala na Ukufunzi katika Shule na Vyuo vya Kijeshi vya ndani na nje ya nchi. Uangalizi wa Amani katika kituo cha SADC Regional Peacekeeping Training Centre, kilichopo Harare Zimbabwe, ambako nilirudi kufundisha kozi fupi za ‘UNITED NATIONAL MILITARY OBSERVARS’ na ‘UNITED NATIONAL STAFF OFFICES’ kwa nyakati tofauti.
Nikiwa nimeshiriki kazi za uangalizi wa amani katika mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea, kwa miezi saba nilifanya kazi hiyo nikipewa dhamana ya mkuu wa operesheni, nikishirikiana na baadhi ya maofisa kutoka katika nchi za Marekani, Norway, Poland, Romania, Kenya, Zambia, Nigeria, India, China na Ukraine. Waliofanya kazi chini yangu kwa nyakati tofauti.
Kutokana na utendaji wangu kama mlinzi wa amani ‘Observer’ wa UN kwenye mpaka wa Ethiopia na Eritrea, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alinitunuku Medali ya amani, ambayo ilimfanya Kanali Emilly afurahishwe sana. Kutokana na utashi wake ameweza kuiongoza Idara hii nyeti kwa ufanisi mkubwa, kutokana na umri wake kufikia wakati wa kustaafu, serikali iliona kuwa bado anaweza kuhimili mikikimikiki ya kazi aliyoizoea wakamuongezea mkataba wa miaka miwili.
Kutokana na uwezo na msimamo wake huo Kanali Emiily amekuwa akishiriki katika kazi za hatari, ambazo zimemjengea heshima. wakati serikali inaangalia nani atakuwa mrithi wa Kanali Emilly, ilimuongezea mkataba wa miaka hiyo miwili, kitendo ambacho kiliungwa mkono na kila mpenda amani duniani.
Baada ya kumaliza kazi na kupewa medali hiyo kama ilivyo kwa wahitimu wengine kutoka mataifa mbali mbali duniani, nilirejea Dar es Salaam nikiwa na matumaini ya kupata hati ya heshima ambayo ni zawadi kwa jeshi na serikali ya Tanzania.
Kama kawaida hati hiyo ilitumwa kwa Jeshi la Tanzania na kupokelewa na Kanali Emilly, ikinielezea kuwa, nimehitimu vizuri na kupata alama B, alama ambayo ni ya juu kutolewa na Chuo hicho, kilichoko kaskazini mwa Jiji la Moscow, nchini Urusi.
Kanali Emilly alifurahishwa sana mimi kupata alama hiyo ya juu, aliniita ofisini kwake na kunikebehi kwa maneno ya utani kiasi kwamba nami niliamini kuwa ndoto zangu zilikuwa ndoto za Kimweri.
Kanali Emilly alitania, "Yawezekana mambo yalikuwa mazito Teacher, sikutarajia, kijana shupavu kama wewe kuchemka, pole sana mwanangu", alisema Kanali Emilly mimi nikimwangalia usoni kwa makini.
"Yawezekana mambo yalikuwa magumu, sikutarajia kupata matokeo ya kushangaza kama unavyosema, nilijipanga vizuri, kama imetokea hivyo sina jinsi", nakumbuka jinsi nilivyomwambia Kanali Emilly akacheka.
"Umejisikiaje kufanya vibaya, Teacher?", alihoji tena.
"Nimejisikia vibaya sana, sidhani kama yupo anayependa kufanya vibaya", nilimwambia.
"Taarifa yako itatoka ubaoni mchana leo, ni taarifa mbaya sana, sina njia nyingine lazima itoke kama ilivyo kawaida", aliniambia huku akionesha tabasamu, lililonishangaza.
"Naomba isiwekwe kwenye ubao", nilijaribu kumshawishi akakataa.
"Hapana, unataka niharibu kazi ili nikufurahishe wewe, sikukutuma kufanya madudu", Kanali Emilly alisema kwa hasira sura yake ilibadilika, nilitoka ndani ya ofisi yake nikitafakari aibu itakayonipata baada ya taarifa hiyo kutolewa.
Nilijiuliza nini nimefanya wakati wa kozi sikupata jibu, nilitembea huku moyo wangu ukisononeka, nikaelekea Kantini, ambako nilikunywa chai na chapati moja tena kwa shida, kisha nikaelekea ofisini kwangu.
Tofauti na jinsi nilivyotarajia, kidogo nipoteze maisha kwa furaha, ubao wa matangazo ulisomeka kuwa nilifaulu vizuri na kupata alama B, alama ambayo ukiipata katika chuo hicho, unatunukiwa cheti cha heshima na Rais wa nchi yako kwa niaba ya Mkuu wa Chuo.
Nilimtafakari Kanali Emilly sikupata jibu, niliporejea mazungumzo yetu ya awali kuwa nimemfedhehesha, nikabaini kuwa Mzee huyu alikuwa akinitania kama ilivyokuwa kawaida yake.
Sikupoteza muda, nilimpigia simu kumfahamisha nilivyofaulu kwa kupata alama B, ambayo tuliipata maofisa wawili, mimi kutoka Tanzania na Meja Charles Katasi wa Jeshi la Uganda.
Kanali Emilly aliniita ofisini kwake na kunifahamisha kuwa, yaliyotokea ni sababu ya furaha aliyokuwa nayo baada ya kupokea hati hiyo. "Unatakiwa Ikulu saa nne ya asubuhi kesho, faili lako limepelekwa kwa Rais, atakubabidhi hati hiyo yeye mwenyewe, maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi watakuwepo, inafurahisha sana Teacher", Kanali Benny alisema huku nikijisikia mwenye furaha ya ajabu kuonana na Rais kesho.
Nilivaa vizuri, nikajipanga pamoja na familia yangu, baada ya kujiweka sawa tulielekea Ikulu, Kanali Emilly na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Jeshi walifika kushuhudia tukio hili la aina yake.
Baada ya Rais kunikabidhi hati yangu ya heshima alisema maneno machache, akitoa maagizo kwa maofisa na makamanda wangu kuhakikisha wanathamini mchango wangu na kuongeza vijana na kuwahamasisha kufuata nyayo zangu.
Kutokana na heshima hiyo, nilipewa nafasi ya kutoa neno la shukrani, baada ya kusema niliitwa kupiga picha za kumbukumbu na Rais, maofisa wa Jeshi, familia yangu, wakiwepo watoto wangu wapendwa, Masey, Changasi na Warioba ambaye alibebwa na Rais.
"Karibu Teacher", mawazo yangu yaliingiliwa na sauti nzito ya Luteni Kanali Matumbi.
"Asante Kamanda", niliitika huku tukashikana mikono, tukakumbatiana kwa furaha.
"Ni Afande Matumbi?", nilimuuliza kwa utani na bashasha.
"Hakika ni mimi, wewe ni Teacher?", yeye pia aliuliza.
"Mwili huu unakula nini Kamanda?", nilimtania.
"Samaki na viazi", alijibu kwa utani.
Luteni Kanali Matumbi alinipokea mkoba wangu, kisha mkono wake wa kushoto akaushika mkono wangu wa kuume, tukatembea kuelekea ndani.
"Umenikumbusha mambo ya zamani Teacher, bahati mbaya sana historia hazijirudii, ingekuwa hivyo tungefanya maandalizi ya kutosha kuzirudia historia", alisema tukacheka.
"Kweli kabisa, unakumbuka opereseni ya kula chakula cha wanafunzi wenzetu kule chuoni Nachingwea", nilimkumbusha.
"Operesheni ipi hiyo Teacher, maana tumefanya mambo mengi?", aliuliza wakati tunaingia kwenye sebule ya nyumba yake.
"Wakati wa mafunzo ya awali kule Fam seven teen Nachingwea, tulianzisha operesheni ya kula chakula cha wenzetu, unamkumbuka yule Bahati kutoka Kigoma?", nilimuuliza.
"Bahati..., Bahatiiii, mbona simkumbuki, alitoka Kigoma?", aliuliza.
"Unamkumbuka bwana, alikuwa kijana mchafu sana, alipenda kuiba mchele stoo wakati wa fatiki na kujipikia vichochoroni", nilimkubusha.
"Bahati... namfahamu sana, alikuwa Kombania C, una kumbukumbu sana Teacher, njaa bwana ni baraa, sikujuwa operesheni ile iliendeshwa na nani?", alisema akitabasamu.
"Niliifanya mimi", nilimwambia tukacheka tena. "Maana Bahati alivunja rekodi kwa kukimbia na kofia ya chuma la moto lililokuwa na ubwabwa.
"Ni kweli alitoka Kigoma".
"Huwezi kuamini, tulijiandaa kama kawaida yetu, baada ya kuwazingira na kuwaachia upenyo ili aweze kukimbia, huku tukiwa tumefunga makaratasi meupe miguuno na upande wa kulia wa mkono mfano wa Military Polisi, tulimkurupusha bwana...", nilisema huku Meja Matumbi akishika tumbo kwa kucheka. "Lakini ilikuwa kama abiria chunga mzigo wako, akakimbia na mzigo, tukaambulia patupu".
"Eheee, alikuwa makini sana katika masuala ya misiso".
"Siwezi kumsahau, tulipomkurupusha tu, kitendo cha haraka, tena bila kuchelewa, alibeba kofia ya chuma, tena likiwa la moto..., aisee alimudu kukimbia nalo", nilimwambia huku tukicheka sana.
Baada ya kucheka sana, huku tukikumbushana mambo yaliyotokea wakati tukiwa chuoni, chakula na vinywaji vililetwa tukaanza kula huku tukiulizana hili na lile.
"Teacher", Luteni Kanali Matumbi aliniita.
"Ndio Kamanda".
"Kulikuwa na uvumi kuwa Rais wa Sudani Omari al Bashir anatafutwa ili akamatwe na kufikishwa kwenye Mahakama ya kimatafa ya uhalifu wa kivita, kujibu tuhuma za mauaji, uvumi huo uliishia wapi, naamini wewe kiasi fulani unafahamu kinachoendelea".
Nilivuta pumuzi nikazishusha, nilitafakari kuhusu swali la Meja Matumbi, nikaamini kuwa hata yeye mizozo na migogoro katika nchi za kiafrika inamsumbua sana akilini.
"Ni kweli, mwaka jana mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC, ilitoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi huyo wa Sudani, niliwahi kumwambia hata Kanali Emilly kuwa ni vigumu mno kwa kiongozi wa nchi kama Bashir kukamatwa na kufikishwa kwenye mahakama hiyo wakati bado anaongoza nchi, ni vigumu sana".
"Hakika ni vigumu Teacher, lakiniiii..., wakidhamiria kabisa kabisa wanaweza kufanikiwa".
"Wampate wapi, ni vigumu sana Bashir kukamatwa", nilisisitiza.
"Kuna ugumu gani, kwani huyu Bashir hafanyi ziara nje ya Sudani... Wanamvizia akitoka tu, wanamtiwa mikononi, sidhani kama inashindikana", alishauri Luteni Kanali Matumbi.
"Wewe unaona rahisi, nikwambie sasa, huyu Mzee pamoja na kuwepo hati ya mahakama ya uhalifu wa kivita, amefanya safari zaidi ya kumi nje ya nchi yake, tena bila woga, ni vigumu mno", nilimwambia akabaki amekodoa macho.
Nilichukuwa glasi ya maji nikanywa kidogo, nilimwangalia kama ana la kusema, nilipoona ananiangalia bila kusema kitu nikatambua kuwa jambo hili limemgusa mno, maana ni mmoja wa maofisa wapenda amani wenye msimamo usioyumbishwa.
"Mbona umenyamaza Mkuu, kama vile umegushwa mno na jambo hili".
"Teacher, kama ungeweza kujua moyo wangu ulivyo, hakika ungeelewa nini natafakari, viongozi wa aina ya Bashir ndiyo wanaochangia machafuko barani Afrika, mtu mmoja anasababisha mauaji ya mamilioni ya watu, haipendezi Teacher", alisema kwa uchungu.
"Ni kweli, lakini utafanyaje, migogoro imekuwa migogoro, watu wanauana kama wanyama, hii yote inatokana na udhaifu wetu, angalia mfano mtu kama Jonas Savimbi, aliumiza watu wengi nchini Angola, amewaachia watu vilema vya maisha, ICC haikuwa na ubavu, iliishia kusema na kulaani tu, mpaka alipouawa. Kwanini walishindwa kumtia mikononi?", nilimwambia.
"Wewe unadhani nini kifanyike kukomesha mauaji ya waafrika, maana kwa takwimu za haraka nchi zaidi ya 30 zinakabiliwa na migogoro mikubwa, inayotishia amani ya dunia, na kati ya nchi hizo zaidi ya ishirini ziko barani Afrika", alihoji.
"Cha kufanya ni kumuomba Mungu, kwa sababu kila siku mataifa makubwa yanatengeneza silaha, na silaha hizi hazitengenezwi kwa ajili ya wanyama, zinatengenezwa kwa ajili yetu, ili uweze kuwa na nguvu kijeshi, lazima uwe na silaha za kisasa, kila taifa linatamba dhidi ya taifa lingine, unadhani amani itapatikana?", nilimuuliza akakuna kichwa.
"Azimio la Umoja wa mataifa la kupiga marufuku mapinduzi ya kijeshi duniani linatekelezwa kweli?", alihoji.
"Hata kama linatekelezwa, mbona halina meno, toka azimio hilo lipitishwe na Umoja wa Mataifa ni nchi ngapi zimepinduliwa na kuongozwa kijeshi, tumeshuhudia baadhi ya nchi Umoja wa Mataifa ukiingilia kati, na sehemu zingine wakisita kufanya hivyo eti ni kuingilia mambo yao ya ndani".
"Kweli Teacher, ni nyingi", Luteni Kanali Matumbi alisema kwa sauti ya upole.
"Aisee, tutafute siku nyingine tutaongea zaidi, muda wangu wa kuwepo hapa Musoma umekwisha, labda tuonane Jumamosi wakati narudi Dar es Salaam, nitajitahidi kuwahi ili tuongee zaidi", nilimuomba Luteni Kanali Matumbi baada ya kuona muda unayoyoma.
"Nilitegemea utalala Musoma, nimekufanyia maandalizi ya kila aina, hebu lala Musoma leo nikutembeze kidogo uone mji", alishauri nikatingisha kichwa kutokubaliana naye.
"Usijali, lazima niondoke leo, nina shauku kubwa ya kumuona mama yangu mzazi, wajuwa tena Afande, baba na mama ni mungu wa dunia, pamoja na kwamba baba alikwisha tangulia mbele ya haki, tafadhali tuonane siku nyingine", nilisema nikisimama kutoka sehemu niliyoketi, maana nilikuwa nimekula na kunywa vizuri.
"Ok, sina jinsi Teacher, nilitegemea kuvuna uhondo zaidi kutoka kwako, basi bwana, ngoja nikutowe", akabeba mkoba wangu tukaelekea nje.
"Usisahau kupita hapa hiyo Jumamosi, nitafanya maandalizi ili usafiri Jumapili", aliongeza, huku nikitingisha kichwa kukubaliana na mawazo yake, japokuwa haitawezekana kurudi hapa kutokana na ratiba yangu niliyojiwekea. Baada ya kuagana na Luteni Kanali Matumbi nilitafuta usafiri wangu binafsi nikaelekea Nyamuswa.
ITAENDELEA