Ilikuwa asubuhi ya misukosuko, vurugu na jitimai, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walikimbia bila mpangilio. Kila mmoja akijaribu kuitetea roho yake, wakati askari kutoka Kikosi Maalum cha Polisi wa Kutuliza Ghasia walipokuwa wakitekeleza moja ya majuku yao ya kuzuia fujo katikati ya Jiji.
Wakitumia magari yao ya kazi aina ya Landrover Defender TDI za jeshi la polisi Tanzania, zikiwa na rangi ya blue, bunduki maalum za kurushia mabomu ya moshi zikiwa mikononi mwao. Askari hawa walipita mitaani kifua mbele, wakirusha mabomu ya machozi huku na huku ili kutimiza wajibu wao huo.
Mchoro kuonyesha hali halisi ya mapambano ilivyokuwa
Magari haya yaligawanyika katika pande mbili mengine yalielekea upande wa Mnazi Mmoja. Mengine yakaelekea upande wa Ilala, ili kuwakabili vyema wananchi hawa waliodaiwa kukaidi agizo la serikali lililowakataza kufanyabiashara katikati ya jiji. Askari hawa waliendelea kurusha mabomu kila mahali palipoonekana kuwa na mkusanyiko wa watu kuanzia wawili.
Hali hii ilionekana sawa na mchezo wa kuigiza. Sikufurahishwa na kitendo hiki cha askari kurusha mabomu bila mpangilio, wananchi sasa walikimbia huku na huku mfano wa Pundamilia waishio kwenye mbuga za wanyama za Serengeti, wanapofukuzwa na mnyama mwenye njaa kali Simba.
Hata hivyo kulikuwa na ukaidi wa wazi kutoka kwa raia hawa, ambao walionekana wazi kukaidi amri hii iliyotolewa na polisi kupitia chombo maalum cha kukuza sauti. "Amri ya Jeshi la Polisi, mnatakiwa kutawanyika haraka, vinginevyo tutatumia nguvu kuwatawanya", sauti ilisikika kutoka katika chombo hicho maalum.
Wakati huo mimi nilikuwa nimesimama kwenye ukuta wa Shule ya Msingi Uhuru, karibu na makutano ya Barabara ya Uhuru na Msimbazi, nikifuatilia kwa karibu kasheshe hilo, ambalo kwa kiasi fulani lilibadili sura nzuri ya Jiji la Dar es Salaam, hali ya utulivu ikatoweka na hofu ikachukua sehemu yake. Kumbukumbu za mauaji yaliyosababisha kuwa na wakimbizi wengi katika nchi za Congo, Rwanda na Burundi ikanirudia kichwani.
"Hali hii ikiachwa iendelee hivi kama ilivyo sasa, itatuletea matatizo siku za usoni", nilijisemea moyoni. Nilikumbuka somo la usalama wa ndani, nilifundishwa somo hili na Luteni John John, wakati huo nikiwa mwanafunzi huko Monduli, mkoani Arusha, kuwa askari wanapashwa kufuata taratibu zilizowekwa wakati wa kukabiliana na hali kama hii, kukaidi amri halali.
Kila mahali ambapo askari hao waliona kuna mkusanyiko wa watu, walisogea na kurusha kombora, hali ilikuwa mbaya, karibu kila upande kilio kikubwa kilikuwa ni kuwashwa macho, kutokana na moshi huo kuwaingia machoni. Ili hali hii isikupate lazima ufumbe macho, jambo ambalo ni vigumu kukwepa.
Mimi pia nilikumbwa na kadhia hii, baada ya bomu lililorushwa kuanguka na kulipuka karibu kabisa na mahali nilipokuwa nimesimama. Kutokana na uzoefu wangu katika majanga kama haya, nilifanikiwa kutoka eneo hilo haraka bila kupatwa na madhara makubwa. Kila kikubwa cha watu ilikuwa ni kuwashwa macho, wengine walikimbilia maji ili kusafisha nyuso zao, lakini wakabaki kutetea kile walichoona kinafaa.
Kiasi nilibaini kuwa askari hawa hawakuwa makini katika kutekeleza majukumu yao, nilibaini kuwa iwapo wananchi hawa wakipata silaha zenye ubora kama walizonazo wao huenda wangesalimu amri kutokana na mpangilio wao kuwa mbovu, "Mmmh mfano hali hii ingetokea katika nchi za wenzetu na askari hawa wakafanya mchezo kama hivi, itakuwaje?" nilijiuliza.
"Mabomu haya yanayorushwa hovyo, hivi askari hawa hawaoni kuwa wanaitia hasara serikali", alisema mama mmoja wa makamo alisimama karibu yangu akiyahaha kuyasafisha macho yake.
"Hakuna hasara mama, mabomu haya yamenunuliwa na serikali kwa kazi hii, lakini hayakupaswa kutumika sasa, sioni sababu ya tembo kupigana na sungura, polisi wanatumia nguvu kubwa kupambana na adui ambaye hana silaha yoyote ya hatari, nikisema silaha nina maana hata wembe sidhani kama wamebeba hawa", nilisema.
"Kwanini wasitumie silaha kama hizi kukomesha matukio ya ujambazi yaliyokithiri nchini, au kuwakamata maharamia wanaosumbua wanachi katika maeneo ya mipaka na sehemu ya bahari, ambako kila siku tunasikia meli zinatekwa", alishauri mama huyu.
"Kuhusu suala la ujamnazi ni kweli silaha hizi zingesaidia sana mama, lakini hili na kukabiliana na maharamia wanaoteka meli hapa, polisi hawahusiki, hilo ni jukumu la wanajeshi, majukumu ya polisi ni kukabiliana na raia wakorofi, kama hawa waliogoma kutia amri ya serikali", nilimwambia mama huyu akaonekana kutabasamu.
"Nimejifunza kitu kutoka kwako kijana wangu, kumbe mipakani ni jukumu la wanajeshi? Nimeelewa sasa mwanangu", aliongeza mama huyu aliyekuwa na rafidhi ya mkoa wa Mtwara.
Pamoja na rafidhi yake kuwa ya kimakonde, alionekana mama mwenye busara nyingi, baada ya kumtafakari nikabaini kuwa huenda ni mmoja wa viongozi wa taasisi za wanawake ama mjasiriamali. "Kuwasumbua wananchi kwa kuwapiga mabomu kama hivi wewe kwa mtazamo wako unaona sawa?", aliniuliza.
"Si sawa kabisa, lakini pia lazima uangalia chanzo nini? Serikali imetenga bajeti ya kuagiza silaha kama hizi, kwa ajili ya kazi kama hii, lakini busara ilihitajika kwanza, sijui kama wamefuata njia hizo, pengine inatafutwa sababu ili kupunguza masalia ya silaha hizo", nilimwambia akanikazia macho halafu akacheka.
"Kuwachokoza wananchi ili uwarushie mabomu?, hilo umejaribu kuweka chumvi, sijui, labda kwenye Serikali za Kidikteta", alisema tukacheka huku nikimuaga baada ya hali ya vurugu kutulia kidogo.
Gari langu dogo aina ya VW Golf, lenye muundo wa polisi ambalo wengi hawalijui, nililiegesha ndani ya uzio wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, nilifanya hivyo kuepuka hali hii, ambayo baadhi ya watu huitumia kuwaibia wengine kwa mgongo wa watu wenye msimamo mkali.
Kilichonifikisha katika eneo hili ni kamba maalum niliyokuwa nikihitaji kuinunua, kamba hii ilikuwa na maana kubwa katika kazi zangu za hatari. Nilikuja kuinunua kamba hii baada ya kutokea shambulizi la kushitukiza wakati niliposhuka Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere. Sikujua walionishambulia walikusudia nini. Lakini pia taarifa ya kuteketea kwa jengo la ofisi zetu iliyotolewa na Kanali Emilly, ambayo si kweli iliniongezea tahadhari.
Nilijikuta nikitafakari hili na lile, nikiwaza na kuwazua, nilibaini kuwa kuna tukio la hatari limetokea hivyo, Kanali Emilly alinihitaji haraka ofisi kwake, akalazimika kugeuza lugha, kuwa ofisi zetu tunateketea kwa moto. Hata nilipofuatilia tukio hilo kwenye vyombo vya habari, taarifa hiyo haikuwepo. Hata nilipoongea na Peter Twite, ilionekana hakuna tukio la kuungua jengo la ofisi zetu barabara ya Azikiwe.
Baada ya kupata kitendea kazi kilichonileta eneo hili. Yaani, kamba nyembamba lakini madhubuti kwa ajili ya mambo yangu, nilijiondoa taratibu, nikatembea kwa tahadhari kubwa kuelekea lilipo gari langu, kila mtu karibu yangu alionekana kuwa adui yangu, waswahili wanasema uking'atwa na nyota, ukiguswa na ujani unashtuka, ndiyo hali niliyokuwa nayo, nililikagua gari hilo vizuri, baada ya kujiridhisha nikaingia na kuliodoka taratibu kuelekea Posta, ofisini kwa Kanali Emilly.
ITAENDELEA