Niliendesha gari taratibu kuelekea kwenye ofisi zetu zilizoko Barabara ya Azikiwe. Kichwa changu kilishika hili na lile, nilijiuliza maswali mengi ambayo hata hivyo nilikosa maelezo yake. Nilijilaumu kwa kutozima simu yangu ya mkononi nilipokuwa kijijini kwetu Nyamuswa, ningefanya hivyo, pengine sasa ningekuwa nafaidi samaki, kuku wa kienyeji na maziwa ya mtindi.
Kutoka Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, nilipokuwa nimeegesha gari, nilipita kwenye Barabara za Shauri Moyo na Uhuru nikaibukia kwenye taa za kuongoza magari za Karume, ambapo nilisimama kusubiri ruhusa ya taa hizi. Nilipoingia kwenye Barabara ya Rashid Kawawa, niliongeza mwendo kidogo ili kuwafanya madereva wa magari ya nyuma yangu yasipate usumbufu. Nilipolipita eneo la Msimbazi Centre, niliiacha barabara hii nikaingia kulia halafu kulia tena nikaupita Uwanja wa mpira wa Kaunda, unaomilikiwa na Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam.
Shambulizi la usiku uwanja wa ndege liliniongezea hofu na umakini katika kufanya maamuzi, nilijiweka tayari kwa lolote, kila mtu alionekana kuwa adui yangu, nilijiuliza maswali mengi, ningekuwa wapi muda huu iwapo shambulizi lile lingefanikiwa, sikujua sababu za watu hao kufanya shambulizi hilo lililolenga kuniondolea maisha, moyo wangu haukuwa na amani tena, nililitilia shaka kila gari lililoonekana kuwa nyuma au mbele yangu.
Ilikuwa vigumu sana kwa mtu asiye na uwezo wa ziada kama wangu kulibaini gari ninaloendesha, nililazimika kutumia gari hii Toyota Brevis ya rafiki yangu Tigani, ili kukwepa shambulizi lingine, japokuwa dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia hakuna jambo la siri, lolote laweza kutokea.
Shambulizi hilo lilinithibitishia kuwa watu hawa hawana mchezo na wamejipanga vizuri katika mipango yao ya kazi, nilimtafuta Luteni Fred Libaba kwenye simu yake, baada ya kumpata nilimuuliza mahali alipo akanijulisha kuwa yuko Wizara ya Mambo ya Nje kwa kazi maalum nikamtaka asirudi ofisini mpaka nitakapomjulisha ili baadaye tuonane juu kwa juu nje ya ofisi.
**********************
Wakati huo, kikao cha dharura kilifanyika nyumbani kwa mzungu Carlos Dimera. Kikosi maalumu cha matapeli wa kisasa kabisa kikiongozwa na mzungu huyu kilikutana kwa siri kujadili hatua za kuchukua baada ya shambulizi la kumuua Teacher kutofanikiwa.
"Nani aliongoza mpango wa mashambulizi ya usiku kule uwanja wa ndege?" akiwa amechukizwa sana Carlos Dimera aliuliza baada ya wajumbe wote muhimu kufika kwenye kikao hiki.
Tofauti na kikao cha awali kilichofanyika juzi, ambapo Carlos alifanya mazungumza na washiriki pande mbili, kila upande aliupangia majukumu yake, safari hii aliwakutanisha wote, kilikuwa kikao cha pamoja, kikiwahusisha wataalam wa wizi madini feki, watakatishaji wa noti bandia na wasafirishaji wa dawa za kulevya.
"Bosi Carlos... Vijana walijipanga vizuri mno, tulikuwa na asilimia zaidi ya mia kumaliza kazi hii, kwa hili tusitafute mchawi, lazima ufahamu katika mawindo, kuna kuwindwa pia, ndicho kilichotokea usiku. Lakini tukuhakikishie kuwa kutenda kosa siyo kosa, kosa ni kulirudia hilo kosa, leo itakuwa mwisho wa maisha ya Teacher, popote atakapoonekana amekwisha", alisema Nombo.
"Sitaki kusikiliza hadithi za Abunuasi hapa, natoa nafasi ya mwisho, kama Nombo alivyosema kazi hii iishe leo mapema ili tupate uhuru wa kufanya mambo yetu, tukionana kesho tusizungumzie habari ya Teacher tena, nimetenga kiasi cha pesa kwa ajili ya sherehe kubwa, mkimaliza kazi hii vizuri tukutane tupongezane kwa kazi nzuri", Carlos Dimeta alieleza.
"Pamoja na kikao hiki cha dharura, Nyati, Simba na Chui wako katika mawindo, tunawasiliana kila baada ya dakika tano au kumi, kama unavyowajua vijana hawa bosi, jua la kesho Teacher hawezi kuliona kabisa, hasa nikimfikiria Nyati alivyo Teacher amekwisha", alieleza Jackina.
Baada ya mpango huu kuwekwa sawa, mjadala mwingine ulianza, walibuni mbinu nyingi za kuchukua pesa kwa wafanyabiashara matajiri na baadhi ya wastaafu walioorodheshwa bila kusababisha madhara. Mbinu hii ilipangwa na Carlos mwenyewe, mzungu huyu alikuwa na mbinu nyingi na kuwafanya washiriki wa mtandao huu kutegemea zaidi mawazo yake.
Pamoja na kumiliki pesa nyingi, ambazo walifanikiwa kuziiba kwenye mabenki kadhaa ya Dar es Salaam. Pia waliweza kusafiri ndani na nje ya nchi wakitumia hati bandia na mbinu hizi na zile kujipatia pesa.
Carlos Dimera alikuwa karibu na baadhi ya viongozi wa serikali. Nchini Tanzania, alikuja nchini kwa mgongo wa mwekezaji aliyekuja kujenga kiwanda cha kutengeneza tembe maalumu za kope za urembo wa akina dada. Kutokana na ukarimu wake alifahamiana na kila mtu. Machoni mzungu huyu alionekana kama rafiki wa kila mtu, lakini moyoni alikuwa adui mkubwa wa maendeleo ya taifa.
Kumbukumbu zilionyesha kuwa mzungu Carlos Dimera alikuwa amefukuzwa kutoka katika baadhi nchi za Afrika ambako alibainika kufadhili vikundi vya wahalifu. Nchi ya mwisho kutimuliwa ilikuwa Rwanda, ambako aliishi kwa zaidi ya miaka mitatu, akitokea Kampala, nchini Uganda baada ya kutiliwa shaka. Alipoingia Dar es Salaam Tanzania hakuwa mgeni katika nchi ya Afrika Mashariki, kwani alimudu kuongea kwa ufasaha lugha ya kiswahili hivyo haraka aliweza kuunda mtandao wake na kuanza kazi rasmi.
Maofisa kadhaa wa idara za serikali, waliokuwa na dhamana ya kusimamia pesa za umma waliibiwa kwa mbinu hizi na zile, baadhi waliona aibu kuripoti taarifa hizo polisi wakihofia kufukuzwa kazi wengine wakijipeleka polisi wenyewe wakidanganya wamevamiwa na majambazi.
Baada ya kuingia Jijini Dar es Salaam, haraka Carlos aliweza kujenga hekalu au jumba kubwa la kisasa kando ya bahari na kuiomba serikali imruhusu kuweka walinzi wake binafsi, baada ya kupata kibali, aliweka ulinzi mkali kuzunguka jumba hili, akiwatumia askari wa kukodi kutoka kitengo maalum cha ujasusi cha Havana, nchini Cuba.
Vinywaji na vyakula vya aina mbalimbali vililetwa, wajumbe walikula, wakanywa na kusaza, wakiifurahia faida ya kazi yao, kila mmoja alionekana mwenye furaha kupita kiasi, wakimuomba mungu awasaidie kufanikisha jukumu lililokuwa mbele yao.
Pamoja na wajumbe hawa, Carlos Dimera, alikuwa na vijana wengine watatu ambao huonekana kwa nadra sana. hawa waliokuwa wamehitimu vizuri mafunzo ya ujasusi sehemu mbalimbali duniani, vijana hawa pia aliwatumia kwa nadra sana, hususan pale Simba, Chui na Nyati wanapokuwa wameshindwa kutimiza moja ya majukumu yao. Simba, Chui na Nyati walikuwa mfano wa mbwa mwitu, kazi yao kubwa ilikuwa kuteka au kuua watu pale wanapoagizwa kufanya vile.
Kufukuzwa kwa Carlos katika baadhi ya nchi hizo haikumfanya kuvunja mitandao yake huko, kazi ziliendelea kama kawaida kwani ndiye aliyeanzisha utapeli wa noti za bandia, pia ndiye muasisi wa kutegesha vyura, mijusi na wadudu kwenye baadhi ya ofisi za serikali na hivyo kuwafanya watumishi wa ofisi hizo, Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakurugenzi kuzikimbia ofisi zao wakiamini kurogwa na wakati huo huo vijana wa Carlos Dimera wanageuka kuwa waganga hodari wa tiba na kufanikiwa kujipatia mapesa mengi kutoka kwa vigogo hao.
"Bosi, nakuhakikishia vijana wako tayari kwa kazi, tumefanya mengi kupitia ubunifu wa kichwa chako, ili tusonge mbele lazima mtu afe, mtu huyo anajiita Kapteni Teacher, kama alipona katika shambulizi la jana, leo hawezi kuchomoka, vijana wameapa", alisema Hawa kwa kujiamini.
Mwana mama huyu alikuwa katili na kipenzi cha Carlos Dimera, alikuwa na sifa kadhaa za kumfanya awe kipenzi cha mzungu huyu, moja ya sifa hizo ni ukatili pia alikuwa na uwezo wa kubadili jambo, akalisimamia kwa nguvu zake zote hata likawa sheria au kanuni.
"Sikilizeni, nimepata ujumbe wa maandishi kutoka kwa wanaspoti wetu, kama mtakumbuka wiki iliyopita tuliweza kuchukua kiasi kikubwa cha pesa kwa watu wawili, mmoja ni Waziri mstaafu huko Mikocheni, mwingine ni mfanyabiashara wa Sinza". Carlos Dimera aliwaeleza.
"Naam bosi, kilikuwa kibarua kigumu mno, lakini tuliweza kufanikiwa, kuna nini bosi?" alihoji Jackina aliyekuwa kiongozi wa operesheni hiyo.
"Wahusika wametoa taarifa polisi. Lakini sina tatizo na jeshi la polisi, hawa ni watu wetu wanachukua mshahara hapa, mbaya ni kwamba malalamiko yamepelekwa idara ya usalama inayosimamiwa na wanajeshi, Hawa amesema tuna watu wetu huko lakini haitoshi, wanajeshi ni kigeugeu. Jaribio la jana lilikusudia kumuua Teacher na kutoa onyo, baada ya jaribio hilo kushindwa naamini adui yetu atajipanga vizuri zaidi, akionekana popote ua kwanza", alisema Carlos Dimera.
Baada ya kutafakari kwa sekunde kadhaa, Jakina akasimama, "Taarifa kutoka kwa wana mtandao wetu ni kwamba idara hii inawategemea sana maofisa wake wawili. Huyu Kapteni Teacher na mwingine anaitwa Fred, huyu ni afisa wa cheo cha Luteni.
"Safi sana Jackina, ndiyo sababu nakuamini sana, naamini kazi yako itafanyika vizuri, ukitoka hapa pita kwa mhasibu akuongezee nguvu, ikiwezekana Teacher na huyu Fred wasilione jua la kesho. Lakini jitahidi kuwahadharisha vijana wako wasiende kichwa kichwa kwa watu kama hawa", Carlos Dimera alishauri.
"Kuhusu hilo ondoa shaka bosi, hivi tunavyoongea vijana wako nyuma yake, tumewahadharisha wasiwe na papara, kazi hizi hazitaki papara, subiri wakati ufike, utasikia", alisema Jackina kwa kujiamini.
"Naamini kuwa wote mmeinjoy vizuri, haya ndiyo maisha, nani kati yenu atapenda kurudi kijijini, aanze maisha ya kijijini, unaamka alfajiri na jembe mkononi, mazao baada ya miezi sita, unavuna, bado kuna usumbufu kibao, ikiwemo kukopwa mazao na usilipwe kwa wakati au hata usilipwe kabisa", alihoji Nombo.
Baada ya kupanga mipango ikapangika, kikao kilivunjwa, huku Carlos akisisitiza kupewa taarifa ya kifo cha Teacher mapema iwezekanavyo.
ITAENDELEA