SEHEMU YA PILI
Na Nyakasagani Masenza
Jijini Dar es Salaam, kilifanyika kikao cha siri katika nyumba moja ya mfanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya. Mfanyabiashara huyu alifahamika kila pembe la Jiji, akiitwa Mzungu Carlos Dimera, Umbo lake lilitosha kabisa kuogopwa na wapinzani wake. Asili ya mzungu huyu ilikuwa ni Corombia. Kutokana na uwezo wake wa kushawishi, Carlos aliweka matawi kadhaa katika nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Ndiye aliyeitisha kikao hiki kwa siri kubwa.
Kutokana na uwezo wake wa fedha na ushawishi aliokuwa nao kwa baadhi ya viongozi wa serikali kadhaa za Afrika, Carlos Dimera aliweza kuanzisha vikosi kadhaa vya uhalifu ndani ya nchi kadhaa, mojawapo ya vikosi hivyo ni usafirishaji wa shehena kubwa ya dawa za kulevya, kikosi cha wizi kutumia noti bandia na kikosi maalumu cha mauaji dhidi ya watu aliowaita vihelehele. Vihelehele ni wale walioonekana kuingia mambo yake.
Kikao hiki ambacho yeye Carlso Dimera aliwa Mwenyekiti wake, kiliwakutanisha watu wachache, akiwemo mwanamke mmoja tu, Mwana mama huyu aliitwa Hawa Msimbazi, ambaye kutokana na uwezo wake wa kupanga mambo yakawa, wenzake walimfananisha na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Condoliza Rice. Hawa alifananishwa kwa mambo mengi na Mmarekani huyo mwenye asili ya Afrika. Tofauti yao ni kwamba yule alikuwa mtendaji katika Serikali ya Marekani, huyu alikuwa mfanyabiashara wa dawa haramu za kulevya Tanzania.
"Mambo yote yamekamilika kwa asilimia tisini na tisa, vijana wamejipanga vizuri kufanikisha kazi hii, kama itakwenda salama kama tulivyojipanga, nawahakikishia kila mmoja atachagua nchi gani atapenda kuishi pamoja na familia yake", alisema Hamis Nombo, mmoja wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambaye kiutendaji ni mtaalam wa mipango katika kikosi.
"Sijui hata niahidi nini, jambo hili si gumu kama mnavyodhania, mambo yote yamefanyika, kama alivyosema Nombo hii ni nafasi yenu kuamua wapi mtapenda kuishi, baada ya kazi hii kumalizika kila mmoja ataihama nchi hii akatumbue raha huko atakapopenda kwenda", alirudia Dimera.
"Bosi, hakuna sababu ya kuumiza vichwa, vijana wamejipanga vizuri, bahati nzuri ni kwamba muda mfupi uliopita wana spoti wetu wametuletea taarifa kuwa serikali imewatuma vijana wawili kutoka Jeshi la ulinzi kuangalia mambo fulani fulani, watoa taarifa wetu wanasema, vijana hao wametumwa kwa siri, baada ya kuona polisi wanasuasua", alisema Hawa.
"Safi sana, aliyekuita Condoliza Rice hakukosea, kazi unazofanya ni kielelezo kuwa jambo hili litafanikiwa, cha msingi sasa, watume vujana wako waonane na askari hao, ili wapewe ahadi zao kabisa, lakini pia wasiwaendee mikono mitupu, nadhani pia waingizwe kwenye orodha ya malipo yetu na wafahamishwe", alishauri Carlos Dimera.
"Jambo hilo limefanyika hata kabla sijasema katika kikao hiki. Mambo ameleta taarifa. Amesema askari hao ni miongoni mwa Makomandoo mahili sana, wana uwezo mkubwa mno, tayari tumeingia nao mkataba. Wako upande wetu sasa", alisema Hawa Carlos akitabasamu.
"Ni jambo zuri sana Hawa, lazima muelewe kuwa kufanya ishu na watu hatari kama hao lazima tuwe tumejiandaa vizuri pia, tuwe makini nao isije ikawa tunamalizana nao halafu wanaanza kutusumbua", anashauri Nombo.
"Kweli, lakini niwaambie jambo moja, hebu tumalize kazi kwanza, mengineyo yatakuja baadaye", Dimera alishauri.
Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, kila mmoja akitafakari hili na lile, Carlos aligonga meza, akatoa angalizo, "Cha msingi tuwe makini na kila hatua tunayopita na kutoka, ahadi yangu kwenu ni malipo mazuri mara dufu, jiandaeni kuishi vizuri.
"Lakini pia tusimsahau Teacher, maana waswahili wanasema usipoziba ufa utajenga ukuta", alikumbusha Aloyce Jackina, aliyekuwa kimya kwa muda mrefu.
"Hana chochote huyu Teacher, jambo hili likiisha tukafanikiwa kuvuka vikwazo, Teacher atakuwa na nafasi gani?", alihoji Dimera.
"Ni tahadhali tu natoa bosi", aliongeza Jackina.
"Umefanya vizuri, ili tuongeze nguvu na umakini", alisema Hawa.
"Kwa maana hiyo tunaachana baada ya kikao hiki, nawatakia mafanikio mema, tufahamishane kila hatua tutakayokuwa, cha msingi ni kutunza midomo yetu. Tukionana kila mmoja awe na jibu la nchi gani atakwenda kuweka makazi yake ya kudumu" alisema akisimama.
Baada ya kikao hicho, Carlos Dimera alikuwa na kikosi kingine chumba cha pili, watu wawili nadhifu sana walikuwa wakimsubiri. Watu hawa walikuwa wamemaliza kazi waliyotumwa na sasa walikuja kupata maelezo ya kazi nyingine.
"Nimesikia kilio mitaani, watu wanalia, tamaa zao zimewafanya walie, kazi yenu ni nzuri sana, nimefarijika, rafiki yangu mmoja kutoka polisi kituo cha kati amenidokeza kuwa kesi zilizofunguliwa hapo ni waliobiwa kwa mpango wetu, wakati hao bado wanalia na kusaga meno wapo wengine wenye tamaa ya kupata utajiri wa haraka. Wewe Oliver Mapunda hakikisha unaingia Chuo Kikuu Mlimani. Maprofesa pamoja na elimu yao katika dunia, ni wepesi kuingia katika kipindi, wakiingia usifanye makosa", aliagiza Carlos Dimera.
"Naam, nimekusoma bosi", anadakia Oliver Mapunda aliyekuwa kimya akiwa amefunga mikono yake kifuani.
"Kuna wastaafu waliolipwa mapesa yao baada ya kustaafu, wakati bado wanatafakari nini wazifanyie pesa hizo, sisi tunazitaka. Wewe Masta Bolendile, kazi yako ni hiyo, lakini usiishie hapo, tafuta mahusiano ya karibu na watendaji wa mashirika ya umma, hawa wana mapesa mengi, lakini ni wagumu kuzitoa, tukijipanga vizuri tutazichukua".
"Naam bosi", anasema Bolendile.
"Dakika chache zilizopita nimetoka kuzungumza na wenzenu upande wa pili, nimesema baada ya kazi ngumu na nzito iliyo mbele yao, kila mmoja apendekeze nchi gani atapenda kuweka makazi yake ya kudumu, kazi yao ni nzito, kazi ya hatari zaidi ya hii yenu".
"Kazi zote zina hatari bosi", Bolendile aliingilia mazungumzo.
"Sawa, lakini hii kazi yenu tunatumia sayansi na teknolojia zaidi, hata ukikamatwa na polisi haina uzito sana. Lakini 'nga', umekutwa na unga, lazima yatoke mawe ya uhakika. Naamini kila mmoja amepata mgawo wake sawa. Mtaniletea taarifa za kazi hii baadae. Kila mbinu itumike Teacher auawe, iwe kwa risasi, kisu au hata akitumiwa msichana ammalize kwa sumu, Kwaherini". Akafunga kikao na kuondoka.
ITAENDELEA